Wakolosai
3 Hata hivyo, ikiwa nyinyi mlifufuliwa pamoja na Kristo, endeleeni kutafuta sana mambo yaliyo juu, ambako Kristo ameketi kwenye mkono wa kuume wa Mungu. 2 Wekeni akili zenu zikiwa zimekazwa juu ya mambo yaliyo juu, si juu ya mambo yaliyo juu ya dunia. 3 Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika muungano na Mungu. 4 Wakati Kristo, aliye uhai wetu, afanywapo dhahiri, ndipo nyinyi pia mtafanywa dhahiri pamoja naye katika utukufu.
5 Kwa hiyo, fisheni viungo vya mwili wenu vilivyo juu ya dunia kwa habari ya uasherati, ukosefu wa usafi, hamu ya ngono, tamaa yenye kuumiza, na tamaa, ambako ni ibada ya sanamu. 6 Kwa sababu ya mambo hayo hasira ya kisasi ya Mungu inakuja. 7 Katika mambo hayohayo nyinyi, pia, wakati mmoja mlitembea mlipokuwa na kawaida ya kuishi katika hayo. 8 Lakini sasa kwa kweli yawekeni mbali nanyi hayo, hasira ya kisasi, hasira, ubaya, usemi wenye kuudhi, na maongezi yenye aibu kutoka katika kinywa chenu. 9 Msiwe mkiambiana uwongo. Uvueni utu wa zamani pamoja na mazoea ya huo, 10 na mjivike wenyewe utu mpya, ambao kupitia ujuzi sahihi unafanywa kuwa mpya kulingana na mfano wa Yule aliyeuumba, 11 hapo hakuna Mgiriki wala Myahudi, tohara wala kutotahiriwa, mtoka-ugenini, Msikithe, mtumwa, mtu huru, bali Kristo ni yote na katika yote.
12 Basi, kama wachaguliwa wa Mungu, watakatifu na wapendwa, jivikeni wenyewe shauku nyororo za huruma, fadhili, hali ya akili ya kujishusha chini, upole, na ustahimilivu. 13 Endeleeni kuchukuliana mtu na mwenzake na kusameheana kwa hiari mtu na mwenzake ikiwa yeyote ana sababu ya kulalamika dhidi ya mwingine. Kama vile Yehova alivyowasamehe nyinyi kwa hiari, fanyeni hivyo nyinyi pia. 14 Lakini, zaidi ya mambo haya yote, jivikeni wenyewe upendo, kwa maana huo ni kifungo kikamilifu cha muungano.
15 Pia, acheni amani ya Kristo idhibiti mioyoni mwenu, kwa maana nyinyi, kwa kweli, mliitiwa hiyo katika mwili mmoja. Na jionyesheni wenyewe kuwa wenye shukrani. 16 Acheni neno la Kristo likae katika nyinyi kwa utajiri katika hekima yote. Fulizeni kufundisha na kuonyana kwa upole kwa zaburi, sifa kwa Mungu, nyimbo za kiroho kwa upendezi, kuimba katika mioyo yenu kwa Yehova. 17 Na lolote lile mfanyalo katika neno au katika kazi, fanyeni kila jambo katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kupitia yeye.
18 Nyinyi wake, iweni katika ujitiisho kwa waume zenu, kama inavyofaa katika Bwana. 19 Nyinyi waume, fulizeni kuwapenda wake zenu na msiwakasirikie kwa uchungu. 20 Nyinyi watoto, iweni watiifu kwa wazazi wenu katika kila jambo, kwa maana hilo ni lenye kupendeza vema katika Bwana. 21 Nyinyi akina baba, msiwe mkichochea watoto wenu wakasirike, ili wasishuke moyo. 22 Nyinyi watumwa, iweni watiifu katika kila jambo kwa wale ambao ni mabwana-wakubwa wenu katika maana ya kimwili, si kwa matendo ya utumishi wa macho, kama wapendeza-wanadamu, bali kwa weupe wa moyo, kwa kumhofu Yehova. 23 Lolote mnalofanya, lifanyeni kwa nafsi yote kama kwa Yehova, na si kwa wanadamu, 24 kwa maana mwajua kwamba ni kutoka kwa Yehova nyinyi mtapokea thawabu ipasayo ya urithi. Tumikieni kama watumwa kwa ajili ya Bwana-mkubwa, Kristo. 25 Hakika yule anayetenda kosa atapokea malipo kwa lile alilotenda kimakosa, na hakuna ubaguzi wowote.