Marko
16 Kwa hiyo siku ya sabato ilipokuwa imepita, Maria Magdalene, na Maria mama ya Yakobo, na Salome wakanunua manukato kusudi waje kumpaka. 2 Na mapema sana siku ya kwanza ya juma wakaja kwenye kaburi la ukumbusho, jua lilipokuwa limechomoza. 3 Nao walikuwa wakisemezana mtu na mwenzake: “Nani atakayetubingirishia hilo jiwe kutoka kwenye mlango wa kaburi la ukumbusho?” 4 Lakini walipotazama juu, wakaona kwamba jiwe lilikuwa limebingirishwa mbali, ijapokuwa lilikuwa kubwa sana. 5 Walipoingia ndani ya kaburi la ukumbusho, wakaona mwanamume kijana ameketi upande wa kuume akiwa amevalia kanzu nyeupe, nao wakafadhaika. 6 Yeye akawaambia: “Acheni kufadhaika. Mnamtafuta Yesu Mnazareti, aliyetundikwa mtini. Yeye alifufuliwa hayupo hapa. Oneni! Mahali walipomlaza. 7 Lakini nendeni, mkawaambie wanafunzi wake na Petro, ‘Yeye anawatangulia kuingia Galilaya; huko mtamwona yeye, kama vile alivyowaambia nyinyi.’” 8 Kwa hiyo walipotoka wakakimbia kutoka kwenye kaburi la ukumbusho, kwa maana kutetemeka na hisia-moyo yenye nguvu zilikuwa zimewashika kabisa. Nao hawakuambia mtu jambo lolote, kwa maana walikuwa katika hofu.
UMALIZIO MREFU
Hati-mkono nyingine za kale (ACD) na tafsiri (VgSyc,p) huongeza umalizio mrefu unaofuata, lakini ambao אBSysArm huondoa:
9 Baada ya yeye kufufuliwa mapema siku ya kwanza ya juma akaonekana kwanza kwa Maria Magdalene, ambaye kutoka kwake alikuwa amefukuza roho waovu saba. 10 Maria Magdalene akaenda akaripoti kwa wale waliokuwa wamekuwa pamoja na Yesu, kwa kuwa walikuwa wakiomboleza na kutoa machozi. 11 Lakini wao, waliposikia alikuwa amekuja kwenye uhai na alikuwa ametazamwa na Maria Magdalene, hawakuamini. 12 Zaidi ya hayo, baada ya mambo hayo alionekana katika umbo jingine kwa wawili wao wakitembea, walipokuwa wakienda mashambani; 13 nao wakarudi wakaripoti kwa wale wengine. Wala hawakuwaamini. 14 Lakini baadaye akaonekana kwa wale kumi na mmoja wenyewe walipokuwa wakiegama kwenye meza, naye akashutumu ukosefu wao wa imani na ugumu wa moyo, kwa sababu hawakuamini wale waliokuwa wamemwona sasa akiwa amefufuliwa kutoka kwa wafu. 15 Naye akawaambia: “Nendeni mkaingie katika ulimwengu wote na kuhubiri habari njema kwa viumbe vyote. 16 Yeye aaminiye na kubatizwa ataokolewa, lakini yeye ambaye hataamini atahukumiwa adhabu. 17 Zaidi ya hilo, ishara hizi zitaandamana na wale wanaoamini: Kwa utumizi wa jina langu watatoa roho waovu, watasema kwa lugha, 18 na kwa mikono yao watainua nyoka, na wakinywa kitu chochote cha kufisha hakitawaumiza hata kidogo. Wataweka mikono yao juu ya watu wagonjwa, na hawa watapata kupona.”
19 Kwa hiyo, basi, Bwana Yesu, alipokuwa amekwisha kusema nao, akachukuliwa juu hadi mbinguni na kuketi kwenye mkono wa kuume wa Mungu. 20 Basi, wao wakatoka kwenda na kuhubiri kila mahali, huku Bwana akifanya kazi pamoja nao na kutegemeza huo ujumbe kupitia ishara zenye kuandamana.
UMALIZIO MFUPI
Hati na tafsiri fulani za mwisho-mwisho zina umalizio mfupi baada ya Marko 16:8, kama ifuatavyo:
Lakini mambo yale yote yaliyokuwa yameamriwa wakayasimulia kwa ufupi kwa wale waliomzunguka Petro. Zaidi, baada ya mambo hayo, Yesu mwenyewe akapeleka kupitia wao kutoka mashariki hadi magharibi mbiu iliyo takatifu na isiyofisidika ya wokovu udumuo milele.