Kutoka
26 “Utatengeneza hema la ibada+ kwa vitambaa kumi vya kitani bora kilichosokotwa, pia kwa nyuzi za bluu, sufu ya zambarau, na kitambaa cha rangi nyekundu. Utavitarizi+ kwa michoro+ ya makerubi. 2 Kila kitambaa cha hema la ibada kitakuwa na urefu wa mikono 28* na upana wa mikono 4. Vitambaa vyote vitakuwa na ukubwa uleule.+ 3 Vitambaa vitano vya hema la ibada vitaunganishwa pamoja na kuwa kitambaa kimoja kirefu, na vitambaa vile vingine vitano vitaunganishwa pamoja na kuwa kitambaa kimoja kirefu. 4 Utatengeneza vitanzi vya nyuzi za bluu kwenye upindo wa kitambaa cha mwisho, nawe utafanya vivyo hivyo kwenye upindo wa kitambaa kile kingine mahali ambapo vitaunganishwa. 5 Utatengeneza vitanzi 50 kwenye kitambaa kimoja na vitanzi vingine 50 kwenye upindo wa kitambaa cha pili ili vitanzi hivyo vielekeane vitakapounganishwa. 6 Nawe utatengeneza vibanio 50 vya dhahabu na kuunganisha vitambaa hivyo pamoja kwa vibanio hivyo, ili hema la ibada liwe na kitambaa kimoja kizima.+
7 “Pia utatengeneza vitambaa vya manyoya ya mbuzi+ vya kufunika hema hilo. Utatengeneza vitambaa 11 vya hema.+ 8 Kila kitambaa kitakuwa na urefu wa mikono 30 na upana wa mikono 4. Vitambaa vyote 11 vitakuwa na ukubwa uleule. 9 Utaunganisha vitambaa vitano pamoja na vitambaa sita pamoja, na kitambaa cha sita utakikunja upande wa mbele wa hema. 10 Kisha utatengeneza vitanzi 50 kwenye upindo wa kitambaa cha kwanza, kwenye kipande cha mwisho kabisa, na vitanzi 50 kwenye upindo wa kitambaa cha pili, mahali vitakapounganishwa. 11 Nawe utatengeneza vibanio 50 vya shaba na kuvitia kwenye vitanzi na kuunganisha vitambaa hivyo pamoja, ili hema liwe na kitambaa kimoja kizima. 12 Sehemu inayobaki ya vitambaa vya hema itaning’inia. Nusu inayobaki ya kitambaa cha hema itaning’inia upande wa nyuma wa hema. 13 Sehemu inayobaki ya vitambaa hivyo itaning’inia pande zote za hema kwa urefu wa mkono mmoja kila upande, ili kulifunika hema.
14 “Utatengeneza pia kifuniko kingine cha hema kwa kutumia ngozi za kondoo dume zilizotiwa rangi nyekundu na juu yake kifuniko cha ngozi za sili.+
15 “Utatengeneza viunzi vya mbao+ za mshita vilivyo wima kwa ajili ya hema hilo.+ 16 Kila kiunzi kitakuwa na urefu wa mikono kumi na upana wa mkono mmoja na nusu. 17 Kila kiunzi kitakuwa na ndimi mbili* zilizounganishwa pamoja. Hivyo ndivyo utakavyotengeneza viunzi vyote vya hema la ibada. 18 Utatengeneza viunzi 20 kwa ajili ya upande wa kusini wa hema la ibada.
19 “Utatengeneza vikalio 40 vya fedha+ chini ya vile viunzi 20: vikalio viwili chini ya kiunzi kimoja pamoja na ndimi zake mbili, na vikalio viwili chini ya kila kiunzi kinachofuata pamoja na ndimi zake mbili.+ 20 Utatengeneza viunzi 20 upande wa pili wa hema, upande wa kaskazini 21 pamoja na vikalio vyake 40 vya fedha, vikalio viwili chini ya kiunzi kimoja na vikalio viwili chini ya kila kiunzi kinachofuata. 22 Utatengeneza viunzi sita sehemu ya nyuma ya hema la ibada, upande wa magharibi.+ 23 Nawe utatengeneza viunzi viwili viwe mihimili miwili ya pembeni upande wa nyuma wa hema la ibada. 24 Katika pembe zote mbili kutakuwa na viunzi viwili kuanzia sehemu ya chini mpaka sehemu ya juu, kwenye pete ya kwanza. Hivyo ndivyo utakavyotengeneza viunzi vyote viwili; vitakuwa mihimili miwili ya pembeni. 25 Kutakuwa na viunzi vinane na vikalio vyake 16 vya fedha, vikalio viwili chini ya kiunzi kimoja na vikalio viwili chini ya kila kiunzi kinachofuata.
26 “Utatengeneza fito za mshita, fito tano kwa ajili viunzi vya upande mmoja wa hema la ibada,+ 27 na fito tano kwa ajili ya viunzi vya upande wa pili wa hema la ibada, na fito tano kwa ajili ya viunzi vya sehemu ya nyuma ya hema la ibada, upande wa magharibi. 28 Ufito ulio katikati ya viunzi utatoka mwisho mmoja mpaka mwingine.
29 “Nawe utavifunika viunzi hivyo kwa dhahabu+ na kutengeneza pete za dhahabu ili zishikilie fito, na fito hizo utazifunika kwa dhahabu. 30 Utatengeneza hema la ibada kwa kufuata ramani ambayo nilikupa mlimani.+
31 “Utatengeneza pazia+ la nyuzi za bluu, sufu ya zambarau, kitambaa cha rangi nyekundu, na kitani bora kilichosokotwa. Utalitarizi kwa michoro ya makerubi. 32 Utalining’iniza kwenye nguzo nne za mshita zilizofunikwa kwa dhahabu. Kulabu zake zitakuwa za dhahabu. Nguzo hizo zitakaa juu ya vikalio vinne vya fedha. 33 Utalining’iniza pazia hilo chini ya vibanio na kuleta sanduku la Ushahidi+ humo, nyuma ya pazia. Pazia hilo litatenganisha Patakatifu+ na Patakatifu Zaidi.+ 34 Utaweka kile kifuniko juu ya sanduku la Ushahidi ndani ya Patakatifu Zaidi.
35 “Utaiweka ile meza nje ya pazia, na kinara cha taa+ kitaelekeana na meza hiyo upande wa kusini wa hema la ibada; utaiweka meza upande wa kaskazini. 36 Kwa ajili ya mlango wa hema, utatengeneza pazia la nyuzi za bluu, sufu ya zambarau, kitambaa cha rangi nyekundu, na kitani bora kilichosokotwa na kufumwa.+ 37 Utatengeneza nguzo tano za mshita na kuzifunika kwa dhahabu kwa ajili ya pazia hilo. Kulabu zake zitakuwa za dhahabu, nawe utazitengenezea vikalio vitano vya shaba.