Mambo ya Walawi
13 Yehova akaendelea kuwaambia Musa na Haruni: 2 “Ikiwa mtu ana uvimbe kwenye ngozi yake, au upele, au kigaga, au doa ambalo linaweza kuwa ugonjwa wa ukoma,*+ anapaswa kupelekwa kwa kuhani Haruni au kwa mmoja wa wanawe, makuhani.+ 3 Kuhani atachunguza sehemu iliyoathiriwa ya ngozi. Ikiwa nywele za sehemu hiyo zimebadilika kuwa nyeupe na ugonjwa umepenya chini ya ngozi, huo ni ugonjwa wa ukoma. Kuhani atauchunguza na kutangaza kwamba mtu huyo si safi. 4 Lakini ikiwa ana doa jeupe kwenye ngozi na inaonekana halijapenya chini ya ngozi na nywele hazijabadilika kuwa nyeupe, basi kuhani atamtenga mtu huyo kwa siku saba.+ 5 Kisha kuhani atamchunguza siku ya saba, na ugonjwa huo ukionekana kwamba hauendelei, nao haujaenea kwenye ngozi, atamtenga kwa siku nyingine saba.
6 “Kuhani anapaswa kumchunguza tena siku ya saba, na ikiwa ugonjwa huo umefifia na haujaenea katika ngozi, kuhani atatangaza kwamba mtu huyo ni safi;+ kilikuwa kigaga tu. Kisha mtu huyo atafua mavazi yake na kuwa safi. 7 Lakini ikiwa ni wazi kwamba kigaga hicho kimeenea* kwenye ngozi baada ya mtu huyo kwenda kwa kuhani kuthibitisha utakaso wake, basi atafika tena* mbele ya kuhani. 8 Kuhani atachunguza kigaga hicho, na ikiwa kimeenea kwenye ngozi, atatangaza kwamba mtu huyo si safi. Huo ni ukoma.+
9 “Mtu akishikwa na ukoma, ni lazima apelekwe kwa kuhani, 10 kisha kuhani atamchunguza.+ Ikiwa ana uvimbe mweupe kwenye ngozi na nywele za sehemu hiyo zimebadilika kuwa nyeupe na uvimbe huo umebadilika kuwa kidonda kibichi,+ 11 huo ni ukoma wa muda mrefu, kuhani atatangaza kwamba mtu huyo si safi. Hapaswi kumtenga,*+ kwa kuwa si safi. 12 Lakini ikiwa ukoma umeenea kwenye ngozi yote na kufunika mwili mzima kuanzia kichwani mpaka miguuni, kwa kadiri ambayo kuhani anaona, 13 na kuhani amemchunguza na kuona kwamba ukoma umefunika ngozi yake yote, atatangaza kwamba mtu huyo ni safi.* Ngozi yote imekuwa nyeupe, yeye ni safi. 14 Lakini akipata kidonda kibichi, hatakuwa safi. 15 Kuhani akikiona kidonda hicho kibichi, atatangaza kwamba mtu huyo si safi.+ Kidonda hicho kibichi si safi. Ni ukoma.+ 16 Lakini kidonda hicho kikibadilika tena na kuwa cheupe, mtu huyo ataenda kwa kuhani. 17 Kuhani atamchunguza,+ na ikiwa kimebadilika kuwa cheupe, kuhani atamtangaza kuwa safi mtu huyo aliyeambukizwa.
18 “Mtu akishikwa na jipu kisha lipone, 19 na uvimbe mweupe au doa lenye mchanganyiko wa rangi nyekundu na nyeupe litokee mahali palipokuwa na jipu hilo, ni lazima aende kwa kuhani. 20 Kuhani atachunguza doa hilo,+ na akiona kwamba limepenya chini ya ngozi na nywele za sehemu hiyo zimebadilika kuwa nyeupe, atatangaza kwamba mtu huyo si safi. Ni ugonjwa wa ukoma uliotokea mahali palipokuwa na jipu. 21 Lakini kuhani akichunguza na kuona kwamba hakuna nywele nyeupe sehemu hiyo na doa halijapenya chini ya ngozi, nalo limeanza kupona, atamtenga kwa siku saba.+ 22 Na ikiwa limeenea kwenye ngozi, kuhani atatangaza kwamba mtu huyo si safi. Ni ugonjwa. 23 Lakini doa hilo likibaki palepale na halijaenea, ni uvimbe tu wa jipu, kuhani atamtangaza kuwa safi.+
24 “Au ikiwa mtu ana kovu lililosababishwa na moto na kovu hilo bichi likigeuka rangi na kuwa doa lenye mchanganyiko wa rangi nyekundu na nyeupe au nyeupe tu, 25 kuhani atalichunguza doa hilo. Ikiwa nywele zimebadilika na kuwa nyeupe katika doa hilo na inaonekana limepenya chini ya ngozi, ni ukoma uliotokea kwenye kovu, basi kuhani atatangaza kwamba mtu huyo si safi. Ni ugonjwa wa ukoma. 26 Lakini kuhani akichunguza doa hilo na kuona halina nywele nyeupe, halijapenya chini ya ngozi, na limeanza kupona, atamtenga mtu huyo kwa siku saba.+ 27 Kuhani atamchunguza siku ya saba, na ikiwa limeenea kwenye ngozi, atatangaza kwamba mtu huyo si safi. Ni ugonjwa wa ukoma. 28 Lakini doa hilo likibaki vilevile na lisipoenea kwenye ngozi, na ikiwa limeanza kupona, ni uvimbe tu wa lile kovu, kuhani atatangaza kwamba mtu huyo ni safi, kwa sababu ni mwasho wa kovu hilo.
29 “Mwanamume au mwanamke akipata kidonda kichwani au kwenye kidevu, 30 kuhani atachunguza kidonda hicho.+ Akiona kwamba kimepenya chini ya ngozi na nywele za sehemu hiyo ni za manjano na ni chache, kuhani atatangaza kwamba mtu huyo si safi; ni ugonjwa unaoathiri ngozi ya kichwa au kidevu. Ni ukoma wa kichwa au wa kidevu. 31 Lakini kuhani akiona kwamba kidonda hicho hakijapenya chini ya ngozi na sehemu hiyo haina nywele nyeusi, anapaswa kumtenga mtu huyo kwa siku saba.+ 32 Kuhani atachunguza kidonda hicho siku ya saba, ikiwa hakijaenea au hakina nywele za manjano na hakijapenya chini ya ngozi, 33 mtu huyo anapaswa kunyolewa, lakini hatanyolewa sehemu yenye kidonda. Kisha kuhani atamtenga mtu huyo kwa siku saba.
34 “Kuhani atakichunguza tena kidonda hicho siku ya saba, na ikiwa kidonda hicho kilicho kichwani na kwenye kidevu hakijaenea au kupenya chini ya ngozi, kuhani anapaswa kutangaza kwamba mtu huyo ni safi, atafua mavazi yake na kuwa safi. 35 Lakini ikiwa kidonda kimeenea kwenye ngozi baada ya mtu huyo kutangazwa kuwa safi, 36 kuhani atamchunguza, ikiwa kidonda hicho kimeenea kwenye ngozi, kuhani hahitaji kuchunguza ikiwa kuna nywele za manjano; mtu huyo si safi. 37 Lakini akimchunguza na kuona kwamba hakijaenea na nywele nyeusi zimeota sehemu iliyokuwa na kidonda, mtu huyo amepona. Yeye ni safi, kuhani atamtangaza kuwa safi.+
38 “Mwanamume au mwanamke akiwa na madoa meupe kwenye ngozi, 39 kuhani atayachunguza.+ Ikiwa madoa hayo si meupe sana, ni vipele visivyo na madhara vilivyotokea kwenye ngozi. Mtu huyo ni safi.
40 “Ikiwa mwanamume atapata upara kichwani, yeye ni safi. 41 Akipata upara sehemu ya mbele ya kichwa, yeye ni safi. 42 Lakini mtu akipata kidonda chenye mchanganyiko wa rangi nyekundu na nyeupe kwenye upara au paji la uso, ni ukoma unaotokea kwenye upara au paji lake la uso. 43 Kuhani atamchunguza, na ikiwa kidonda kilicho kwenye upara au paji lake la uso kina uvimbe wenye mchanganyiko wa rangi nyekundu na nyeupe, na ngozi yake inaonekana ni kama ina ukoma, 44 mtu huyo ana ukoma. Yeye si safi, kuhani anapaswa kutangaza kwamba mtu huyo si safi kwa sababu ya ugonjwa aliopata kichwani. 45 Mtu mwenye ukoma anapaswa kuvaa mavazi yaliyoraruka, hapaswi kutunza nywele za kichwa chake, naye anapaswa kufunika masharubu yake na kusema hivi kwa sauti: ‘Mimi si safi, mimi si safi!’ 46 Kwa muda wote atakaokuwa na ugonjwa huo hatakuwa safi. Kwa kuwa yeye si safi, ataishi akiwa ametengwa. Ataishi nje ya kambi.+
47 “Vazi likiathiriwa na ugonjwa wa ukoma, iwe ni vazi la sufu au la kitani, 48 iwe ni ndani ya mtande au ndani ya mshindio wa kitani au wa sufu, au ndani ya ngozi au ndani ya chochote kilichotengenezwa kwa ngozi, 49 na ikiwa vazi, ngozi, mtande, mshindio, au kitu chochote cha ngozi kina doa lenye mchanganyiko wa rangi ya manjano na kijani au doa jekundu, huo ni ugonjwa wa ukoma, kuhani anapaswa kuonyeshwa vazi hilo. 50 Kuhani atachunguza ugonjwa huo, naye anapaswa kulitenga vazi hilo lenye ugonjwa kwa siku saba.+ 51 Atakapolichunguza siku ya saba na kuona kwamba ugonjwa huo umeenea ndani ya vazi, ndani ya mtande, ndani ya mshindio, au ndani ya ngozi (haidhuru ngozi hiyo inatumiwa kwa kusudi gani), huo ni ukoma hatari, vazi hilo si safi.+ 52 Anapaswa kuliteketeza vazi hilo au mtande au mshindio wa sufu au wa kitani au kitu chochote cha ngozi kilichoathiriwa na ugonjwa huo, kwa sababu huo ni ukoma hatari. Ugonjwa huo unapaswa kuteketezwa.
53 “Lakini kuhani akichunguza na kuona kwamba ugonjwa haujaenea ndani ya vazi au ndani ya mtande au ndani ya mshindio au ndani ya kitu chochote cha ngozi, 54 ataamuru kitu kilichoathiriwa kioshwe, naye atakitenga kwa siku saba zaidi. 55 Baada ya kitu hicho kuoshwa kabisa, kuhani atakikagua. Ikiwa doa hilo halijabadilika, hata ikiwa ugonjwa haujaenea, kitu hicho si safi. Mnapaswa kukiteketeza kwa sababu kimeliwa na ukoma, iwe kimeliwa chini au ndani.
56 “Baada ya kitu hicho kuoshwa kabisa, kuhani atakikagua na akiona kwamba doa hilo limefifia, atararua sehemu iliyoathiriwa ya vazi au ngozi au mtande au mshindio. 57 Hata hivyo, doa hilo likitokea sehemu nyingine ya vazi au ndani ya mtande au ndani ya mshindio au ndani ya kitu chochote cha ngozi, ugonjwa huo unaenea, nanyi mnapaswa kuteketeza kitu chochote kilichoathiriwa.+ 58 Lakini ikiwa vazi au mtande au mshindio au kitu chochote cha ngozi hakina doa baada ya kuoshwa, kitu hicho kinapaswa kuoshwa mara ya pili, nacho kitakuwa safi.
59 “Hiyo ndiyo sheria kuhusu ugonjwa wa ukoma ulioathiri vazi la sufu au la kitani, au mtande au mshindio, au kitu chochote cha ngozi; itatumiwa kutangaza vitu hivyo kuwa safi au si safi.”