30 “Sasa wananicheka+
—Wanaume wenye umri mdogo kuliko mimi,
Ambao baba zao ningekataa
Kuwaweka pamoja na mbwa waliolinda kondoo wangu.
2 Nguvu za mikono yao zilikuwa na faida gani kwangu?
Nguvu zao zimekwisha.
3 Wamedhoofika kwa sababu ya umaskini na njaa;
Wanaguguna ardhi iliyokauka
Ambayo ilikuwa tayari imeharibiwa na kuachwa ukiwa.
4 Wanakusanya mmea wenye chumvi kutoka vichakani;
Chakula chao ni mizizi ya miretemu.
5 Wanafukuzwa kutoka katika jamii;+
Watu wanawapigia kelele kama wanavyompigia kelele mwizi.
6 Wanaishi kwenye miteremko ya mabonde,
Kwenye mashimo ardhini na katika miamba.
7 Wanalia kwa sauti kutoka vichakani
Na kujikunyata pamoja katikati ya upupu.
8 Kama wana wa watu wapumbavu na wasio na jina,
Wamefukuzwa kutoka nchini.
9 Lakini sasa wananidhihaki hata katika nyimbo zao;+
Nimekuwa kitu cha kudharauliwa nao.+
10 Wananichukia na kukaa mbali nami;+
Hawasiti kunitemea mate usoni.+
11 Kwa sababu Mungu amenidhoofisha na kuninyenyekeza,
Wanafanya watakavyo mbele zangu.
12 Wanainuka upande wangu wa kulia kama umati;
Wananikimbiza
Na kuweka vizuizi vya maangamizi kwenye njia yangu.
13 Wanaharibu barabara zangu
Na kuzidisha msiba wangu,+
Na hakuna yeyote anayewazuia.
14 Wanakuja kana kwamba wanapita kwenye ufa mpana ukutani;
Wanamiminika ndani katikati ya magofu.
15 Hofu inanilemea;
Heshima yangu inapeperushwa mbali kama upepo,
Na wokovu wangu unatoweka kama wingu.
16 Sasa uhai wangu unatoweka taratibu;+
Siku za mateso+ zinashikamana nami.
17 Maumivu yanatoboa mifupa yangu usiku;+
Na maumivu yanayonitafuna hayaishi kamwe.+
18 Kwa nguvu nyingi vazi langu limechakazwa;
Hunikaba kama ukosi wa vazi langu.
19 Mungu ameniangusha chini kwenye matope;
Nimebaki mavumbi na majivu tu.
20 Ninakulilia unisaidie, lakini hunijibu;+
Ninasimama, lakini unaniangalia tu.
21 Umenigeukia kwa ukatili;+
Kwa nguvu zote za mkono wako, unanishambulia.
22 Unaniinua juu na kunipeperusha katika upepo;
Kisha unanitupa huku na huku katika dhoruba.
23 Kwa maana ninajua kwamba utanishusha katika kifo,
Katika nyumba ambamo watu wote walio hai watakutana.
24 Lakini hakuna yeyote anayeweza kumshambulia mtu anayetaabika+
Anapolilia msaada wakati wa msiba.
25 Je, sijawalilia wale ambao wamekabili nyakati ngumu?
Je, sijawahuzunikia maskini?+
26 Ingawa nilitumaini mema, mabaya yalikuja;
Nilitarajia nuru, lakini giza likaja.
27 Msukosuko uliokuwa ndani yangu haukukoma;
Siku za mateso zilinikabili.
28 Ninatembeatembea kwa huzuni;+ hakuna mwangaza wa jua.
Ninasimama na kulilia msaada katika kusanyiko.
29 Nimekuwa ndugu ya mbwamwitu
Na rafiki ya mabinti wa mbuni.+
30 Ngozi yangu imekuwa nyeusi na imebambuka;+
Mifupa yangu inaungua kwa sababu ya joto.
31 Kinubi changu kinatumika kwa ajili ya maombolezo tu,
Na zumari yangu kwa ajili ya sauti ya kilio.