Bunduki—Ulimwengu Bila Hizo
TANGU mwanzo wa historia ya kibinadamu, binadamu amegeukia jeuri katika mishughuliko yake pamoja na binadamu mwenzake. Uuaji ulitokea katika familia ya kwanza Kaini alipomwua Abeli ndugu yake. Uuaji huo umeendelea tangu hapo—ndani ya familia, ndani ya makabila, na kati ya mataifa. Kwa kadiri silaha zilivyozidi kuwa zenye nguvu, ndivyo mihanga walivyozidi kuwa wengi. Mawe na marungu yaliacha kutumiwa na nafasi hiyo ikachukuliwa na mikuki na mishale, nayo ikaondoka na mahali payo pakachukuliwa na bunduki na makombora. Uharibifu wa mamia ukawa wa maelfu; leo maelfu hayo yamekuwa ni mamilioni. Si wakati wa vita tu bali pia wakati wa amani. Si kwa kufanywa na askari-jeshi bali pia na raia walio faraghani. Si kwa kufanywa na watu wazima tu bali pia na watoto. Je! ongezeko la jeuri litakuja kwisha wakati wowote? Ikiwa jambo hilo lategemea watu, matazamio ni ya gizagiza.—2 Timotheo 3:1-5, 13.
Kristo Yesu alitabiri kwamba huu ungekuwa wakati ambapo mataifa yangeinuka dhidi ya mataifa mengine katika vita vya kuogofya, vikifutilia mbali uhai wa mamilioni. Magonjwa ya kipuku na matetemeko ya dunia yangeua wengi mahali pengi. Binadamu angekuwa akichafuza dunia kwa kadiri ambayo uwezo wayo wa kutegemeza uhai wenyewe ungetishwa—sasa wanasayansi wengi wanatamka hofu hiyo. Lakini upendo wa binadamu kwa fedha husababisha aendelee kujisukuma katika hekaheka yake ya uchafuzi, nayo itakwisha wakati tu Yehova Mungu mwenyewe aingilia mambo ili “kuwaangamiza wale wanaoangamiza dunia.”—Ufunuo 11:18, HNWW.
Wengi hudhihaki maonyo hayo na kutimiza kwa njia hiyo sehemu nyingine ya ishara iliyotabiriwa ya siku za mwisho: “Awali ya yote jueni kwamba siku za mwisho watakuja watu ambao mienendo yao inatawaliwa na tamaa zao mbaya. Watawadhihaki ninyi na kusema: ‘Aliahidi kwamba atakuja! Je, sasa yuko wapi? Mambo ni yaleyale tangu babu zetu walipokufa; hali ya vitu ni ileile kama ilivyokuwa mwanzo wa ulimwengu!’”—2 Petro 3:3, 4, HNWW.
Lakini wingu hili lenye giza linalokaa-kaa juu ya ainabinadamu lina tazamio fulani zuri. Yesu alitabiri kwamba kwenye kuwapo kwake, “mataifa duniani yatakuwa na dhiki kwa sababu ya wasiwasi kutokana na mshindo wa mawimbi ya bahari. Watu watazirai kwa sababu ya woga, wakitazamia mambo yatakayoupata ulimwengu.” Lakini alisema pia ungekuwa wakati wa ‘kusimama [wima, NW] na kuinua vichwa vyenu juu, kwa maana ukombozi wenu umekaribia.’—Luka 21:25-28, HNWW.
Mataifa yamo katika dhiki, matungamo ya watu yana msukosuko, na watu mmoja mmoja wamo katika hofu ya mambo yanayokuja juu ya dunia, lakini ni wakati wa kukombolewa kwa wale wanaongojea Ufalme wa Mungu unaokuja na Utawala wa Miaka Elfu wa Kristo Yesu. Huo utakuwa wakati wa kutimizwa kwa ahadi ya Yehova Mungu ya ‘mbingu mpya na dunia mpya ambamo uadilifu utakaa.’—2 Petro 3:13, NW.
Na hakuna bunduki! Hakuna yoyote itakayohitajiwa kwa vita. “Avikomesha vita hata mwisho wa dunia; avunja uta, akata mkuki, achoma moto magari [magari ya vita, Rotherham].”—Zaburi 46:9.
Hakuna zozote zitakazohitajiwa kwa ulinzi wa kibinafsi. “Wataketi kila mtu chini ya mzabibu wake, na chini ya mtini wake; wala hapana mtu atakayewatia hofu; kwa kuwa kinywa cha BWANA [Yehova, NW] wa majeshi kimesema hivi.”—Mika 4:4.
Ni wanyoofu peke yao, wala si waovu wowote, watakuwako. “Wanyofu watakaa katika nchi [dunia, NW], na wakamilifu watadumu ndani yake. Bali waovu watatengwa na nchi [dunia, NW], nao wafanyao hila watang’olewa.” (Mithali 2:21, 22) Ndipo “wasikivu wenyewe watamiliki dunia, nao kweli watapata upendezo mzuri sana wao katika wingi wa amani.”—Zaburi 37:11, NW.
Machoni pa Mungu jeuri huharibu dunia. Katika siku ya Noa dunia ‘iliharibika mbele za Mungu, dunia ikajaa dhuluma [jeuri, NW].’ (Mwanzo 6:11-13) Kwa sababu hiyo, Yehova alimaliza ulimwengu huo kwa Gharika ya tufe lote. Yesu alifananisha mwisho wa ulimwengu huu wa sasa wenye jeuri wakati wa kuwapo kwake na mwisho wa huo wa kale: “Kwa maana kama vile walikuwa katika siku hizo kabla ya gharika, wakila na wakinywa, wanaume wakioa na wanawake wakipewa katika ndoa, mpaka siku ambayo Noa aliingia katika safina; na wao hawakujali mpaka gharika ikaja na kufagilia mbali wote, hivyo ndivyo kuwapo kwa Mwana wa binadamu kutakuwa.”—Mathayo 24:38, 39, NW.
Katika ulimwengu mpya wa Mungu kila mtu aliye hai atatimiza Marko 12:31: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.” Na Isaya 11:9: “Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua BWANA [Yehova, NW], kama vile maji yanavyoifunika bahari.” Kitakachotimizwa pia katika ulimwengu mpya huo wa uadilifu kitakuwa zile hali tukufu zisimuliwazo kwenye Ufunuo 21:1, 4, HNWW: “Nikaona mbingu mpya na dunia mpya. Mbingu ile ya kwanza na dunia ile ya kwanza vilikuwa vimetoweka, nayo bahari pia haikuwako tena. Yeye atafuta machozi yao yote; maana hakutakuwako tena na kifo, wala uchungu, wala kilio, wala maumivu; maana ile hali ya kale imepita!” Kwa uhakika, wakati huo hakuna jamii zozote za kibinadamu zenye utele wa bunduki!
Hakuna lolote la mabadiliko haya ya maana kwa ajili ya baraka ya binadamu litaletwa na wanamapinduzi walio na bunduki zao zenye kutoa-toa mioto zikifyeka wapinzani. Bali, yataletwa na Yehova Mungu kupitia Ufalme wake chini ya Kristo Yesu. Hivyo basi Isaya 9:6, 7, NW, husema: “Kumekuwa na mtoto ambaye amezaliwa kwetu sisi, kumekuwa na mwana ambaye amepewa kwetu sisi; na utawala wa kimwana-mfalme utakuja kuwa juu ya bega lake. Na jina lake ataitwa Mshauri wa Ajabu, Mungu Mweza, Baba wa Milele, Mwana-Mfalme wa Amani. Kwa wingi wa utawala wa kimwana-mfalme na kwa amani kutakuwa hakuna mwisho, juu ya kiti cha ufalme cha Daudi na juu ya ufalme wake ili kuusimamisha kwa imara na kuuendeleza kwa njia ya haki na kwa njia ya uadilifu, kutoka sasa na kuendelea na hadi wakati usio dhahiri. Bidii ya Yehova wa majeshi itafanya hili.”