Maua ya Kiroho Yalikua Katika Brewery Gulch
ZAMANI za kale utendaji wa kivolkeno uliyeyusha shaba, fedha, na dhahabu ndani sana ardhini. Msongo wa mvuke ukalazimisha kiasi kikubwa sana cha madini hayo kupitia mianya na kuyaweka katika kile ambacho sasa kinaitwa Milima ya Mule iliyoko kusini mwa Arizona, Marekani. Katika 1877, Jack Dunn, mpelelezi wa jeshi aliyekuwa ameajiriwa katika Fort Huachuca iliyokuwa karibu, alikuwa akitafuta maji naye akagundua uthibitisho wa kwamba kuna madini yenye utajiri mwingi sana. Yeye alimchukua mchimba-madini, George Warren, ili wachimbe madini hayo.
George Warren akatangaza umilikaji wa kihalali wa sehemu nyingi lakini kwa kukosa kufuatia haki hakumwambia mwenzake Jack Dunn. Umilikaji huo wote ungemfanya Warren awe tajiri sana, lakini akaupoteza wote kwa sababu alipokuwa amelewa kwa kunywa pombe kali, kwa ujinga alichezea kamari umilikaji wake kwenye mbio za farasi, akisema kwamba anaweza kukimbia kwa kasi kuliko farasi. Bila shaka alipoteza kila kitu. Mali hizo hatimaye zikawa Queen Mine. Katika miaka ambayo imepita, uchimbaji mkubwa umetwaa karibu tani milioni nne za shaba na kiasi kikubwa sana cha dhahabu na fedha kutoka Milima ya Mule kabla ya machimbo hayo kufungwa katika 1975.
Kuchimba mawe magumu kwahitaji wachimbaji wenye nguvu. Hao walitoka Ireland, Italia, Serbia, Uingereza na Ujerumani. Kwa sababu ya programu za kuwachochea kufanya kazi zilizotolewa na machimbo mengi, wachimbaji wa mawe magumu ni wachimbaji wenye bidii. Kwa sababu wachimbaji hao walikuwa maelfu ya kilometa kutoka kwa familia zao, wao wakawa pia wachimbaji wanywao pombe kupindukia—hivyo mpika-pombe Mjerumani akajenga kiwanda cha kupika pombe karibu na machimbo hayo. Viwanda vya kupika pombe hupika bia inayohitaji kutengenezwa kidogo tu kabla ya kunywewa. Wengi hupendelea kuinywa ikiwa baridi, katika mazingira ya kirafiki pamoja na kitumbuizo kidogo. Basi, katika barabara iliyo karibu na kiwanda cha kupika pombe, baa nyingi sana zilijengwa. Hizo zikajawa na wachimbaji mawe magumu wenye bidii wanywao pombe kupindukia. Kulikuwa na vitumbuizo, yaani, ukahaba na kamari pamoja na alkoholi—mchanganyiko ambao ungetokeza hali za hatari sana. Barabara hiyo ikaitwa Brewery Gulch nayo ikajipa sifa ya kuwa hatari zaidi ya Tombstone, mji wenye sifa mbaya sana uliokuwa umbali wa kilometa 40 tu kufuata barabara.
Hatimaye, wachimbaji wengi walioa na kujenga nyumba za kulea familia zao. Wachimbaji waliotoka Uingereza walijenga nyumba ambazo wachimbaji Waingereza wa karne ya 19 wangeishi; Waserbia, walijenga nyumba za wachimbaji wa Serbia; Wajerumani, walijenga Kijerumani; Waitalia, walijenga Kiitalia; na watu wa Ireland, walijenga Kiireland. Jiji la awali, Bisbee la kale lilijengwa kando ya bonde lenye kusimama wima sana, hivyo nyumba zao zilijengwa zikining’inia kwenye kuta za bonde, mahali popote ambapo nafasi ingepatikana kwenye mawe. Mkusanyo huo wa kipekee hatimaye ukawa makazi ya zaidi ya watu 20,000, wengi wao wakiwa wachimbaji na familia zao, na sasa jiji hilo huvutia watalii kutoka ulimwenguni kote. Mji huo uliitwa Bisbee kwa heshima ya mtu aliyeweka rasilimali nyingi sana katika machimbo hayo lakini yeye hakupata kamwe kuja kwenye mji huo wenye jina lake.
Kadiri mji ulivyozidi kukua, ndivyo idadi ya baa ilivyozidi kuongezeka kwenye Brewery Gulch. Pindi moja zaidi ya baa 30 zilikuwa zikifanya kazi katika eneo la barabara mbili, na eneo jingine ambalo makahaba walifanya kazi zao lilisitawi mbele kidogo ya mahali hapo pa pombe.
Familia chache za Mashahidi zilipohamia Bisbee karibu 1950. Kuhubiri kwao kulitokeza kufanyizwa kwa kutaniko la Mashahidi wa Yehova, ambalo lilikua likawa na washiriki 12 kufikia 1957. Walihitaji mahali pa kukutania, hivyo wakakodisha jumba ambalo wangeweza kugharamia, sehemu ya mbele ya duka kwenye Brewery Gulch, ng’ambo ya barabara kutoka baa ya St. Elmo’s. Walipata matatizo machache kutoka kwa watu waliopenda kwenda kwenye sehemu za ukosefu wa adili zilizowazingira. Pindi kwa pindi mlevi alienda huko jioni wakati wa mkutano halafu angeketi tu nyuma na kusikiliza—wengine hata walitoa mchango kabla ya kuondoka.
Baadaye kutaniko lilinunua ardhi kwa ajili ya Jumba la Ufalme—kilometa 11 kutoka Brewery Gulch na mazingira yayo ya kukosa adili. Hilo jumba lilijengwa na kuwekwa wakfu 1958. Jengo hilo limerekebishwa na kupanuliwa mara tatu nalo bado latumikia kutaniko hilo vizuri.
Machimbo hayo yalipofungwa 1975, karibu mji nao ufungwe. Wachimbaji na familia zao walihamia miji ambamo kungali kulikuwa na machimbo. Wakazi waliobaki sanasana walikuwa wachimbaji waliostaafu pamoja na familia zao.
Ile Brewery Gulch iliyokuwa maarufu sana sasa ni kivutio tu cha watalii. Ni baa moja tu inayofanya kazi huko, na jengo la kiwanda cha kupika pombe sasa ni mkahawa wa familia fulani. Lile eneo la makahaba limeharibiwa, ingawa mtu bado aweza kuona ishara zalo katika nyua zinazozingira baadhi ya nyumba katika eneo hilo. Nyua hizo zimetengenezwa kwa springi na fremu za vitanda zenye kutu. Ile Brewery Gulch ambayo wakati mmoja ilikuwa yenye kukosa adili sana sasa ni kitu cha kipekee cha kuvutia wadadisi.
Kwa wakati huu kutaniko lina watangazaji 48 nalo linakua. Kuhubiri nyumba hadi nyumba kwapendeza sana. Mashahidi hukutana na wachimbaji waliostaafu ambao awali walitoka Ireland, Italia, Serbia, Uingereza na Ujerumani na vilevile wasanii wengi, ambao baadhi yao huonyesha kazi zao katika sebule zao.
Sehemu ya huo ukuzi ni kwa sababu mwanamke mmoja ambaye alikuwa akipenda kwenda kwenye baa moja yenye makelele mengi iliyobaki katika Brewery Gulch, iliyoitwa St. Elmo’s, hafanyi hivyo tena. Anaitwa Julie. Julie hakuwa akienda tu huko, bali alikuwa mmojawapo wateja wenye makelele zaidi. Alikuwa akishiriki aina zote za vitumbuizo vya ukosefu wa adili, kutia ndani mapigano ya mara kwa mara, hata na wanaume. Julie alivutiwa na ujumbe wa Mashahidi wa Yehova kwa sababu ya tofauti kubwa ya watu ambao walikuja mlangoni pake. Julie alilazimika kufanya mabadiliko makubwa sana, na hilo lilichukua miaka kadhaa, lakini sasa yeye ni Shahidi aliyebatizwa anayetenda. Mume wake pamoja na watoto watatu pia huhudhuria mikutano kwa ukawaida nao wanafanya maendeleo.
Bisbee ulikuja kuwa mji kwa sababu ya madini yaliyowekwa huko zamani za kale. Watu hawayatafuti tena, lakini wengi wanatafuta hazina ya kweli, ujuzi wa Mungu wa pekee, Yehova, na Ufalme wake. Mazingira yaliyozingira Jumba la Ufalme la kwanza kwenye Brewery Gulch yalikuwa ya ukosefu mbaya sana wa adili, lakini maua ya kiroho yalisitawishwa katika jumba hilo. Kati ya wale watangazaji 12 wa kwanza waliokutanikia jumba hilo la zamani, 7 walikuwa mapainia wa kawaida. Kulikuwa na watoto saba pia. Yaonekana kwamba mazingira mazuri ya kiroho yaliyoonyeshwa na kikundi hicho kidogo chenye bidii katika jumba hilo yalishinda mazingira yasiyo ya adili yaliyokuwa nje.
Watoto sita kati yao waliingia katika aina fulani ya utumishi wa wakati wote wakitumikia wakiwa Mashahidi wa Yehova. John Griffin alihudhuria Watchtower Bible School of Gilead. Ingawa haendelei na utumishi wa mishonari, angali anamtumikia Yehova akiwa mzee katika nchi aliyopelekwa, Kosta Rika. Dada yake, Carolyn (sasa anaitwa Jasso), ni painia wa kawaida katika Sierra Vista, Arizona. Nancy Pugh pia alienda Gileadi, akatumikia akiwa mishonari katika Chile, na angali huko, ingawa haendelei na umishonari. Ndugu yake, Peter, alifanya upainia akaenda Hispania ili kutumikia penye uhitaji zaidi. Susan na Bethany Smith walikuwa wamekuwa mapainia wa kawaida Bisbee kwa jumla ya miaka 50 wote wawili na wangali wanatumikia huko.
Kwa kweli Neno la Mungu “lina nguvu,” hata kufikia hatua ya kukuza maua ya kiroho Brewery Gulch. (Waebrania 4:12)—Imechangwa.
[Picha katika ukurasa wa 23]
Awali Jumba la Ufalme lilikuwa kwenye orofa ya juu ya jengo hili