Mti Utakaokuduwaza
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI EKUADO
KUFIKIA katikati ya mwezi wa Desemba pwani ya Ekuado haikuwa imepata mvua ya msimu. Majani hayakung’aa sana kwa sababu ya vumbi lililotapakaa kwenye vilima. Mawingu mazito ya kijivu yalitanda angani na kufanya siku iwe na utusitusi, huku kikundi fulani cha wasafiri kikiwa barabarani kuelekea magharibi kwenye Bahari ya Pasifiki. Ghafula, wote walikazia macho mti mmoja pembeni mwa barabara. Gari lilisimama ghafula. Waliona mti upi?
Mti wa guayacan uliochanua maua tele! Baada ya kukimya kwa kitambo walisema hivi kwa mshangao: “Ni maridadi kama nini! Je, umewahi kuona rangi nyangavu kama hizi? Nimeona miti mingi yenye kuchanua maua ya rangi nyekundu-nyeupe, zambarau, nyekundu, au ya machungwa, lakini umaridadi wa mti huu wapita yote!”
Baada ya kustaajabia umaridadi wake wa rangi nyangavu ya dhahabu, hatimaye waliendelea na safari. Kumbe hawakujua kwamba kulikuwa na miti zaidi. Baada ya kusafiri kwa muda, waliona mti mwingine wa guayacan ukiwa umechanua maua kemkemu kisha mwingine. Ilionekana ni kana kwamba vilima vilifunikwa kwa maua yenye rangi nyangavu ya dhahabu! Huu ulikuwa msimu wa kila mwaka wa mti wa guayacan kuchanua maua—wakati ambapo misitu isiyovutia hufunikwa na rangi zenye kuvutia sana.
Hata hivyo, mti huo maridadi wenye kuchanua maua hupatikana katika nchi nyingine pia. Kwa kweli, mti huo hukua kiasili katika sehemu nyingi za Amerika Kusini na Kati. Pia huitwa araguanay, guayacan amarillo, tarumbeta ya dhahabu, na mti wa tarumbeta, ikirejezea maua yake yenye umbo la tarumbeta na rangi ya dhahabu. Jina lake la kisayansi ni Tabebuia chrysantha.
Mti wa guayacan pia huwa na mbao laini ambazo zimetumiwa kwa miaka mingi kutengenezea fanicha za hali ya juu. Kuadimika kwa mti huu kumelazimu nchi fulani kutunga sheria za kuulinda. Hilo huhakikisha kwamba wenyeji na wageni wanaendelea kufurahia umaridadi wake wa pekee unapochanua, ijapokuwa huchanua kwa siku chache tu mara moja kwa mwaka.
Bila shaka mti wa guayacan humtukuza daima msanii mkuu kuliko wote—Muumba wetu Mtukufu, msanifu wa dunia hii ya kustaajabisha tunamoishi.