Chukar—Mgeni Katika Paradiso
MIMI na rafiki zangu tulikuwa tunatarajia kwa hamu kutembelea kisiwa cha Hawaii kinachoitwa Maui. Hasa tulitaka kuona kuchomoza kwa jua tukiwa juu ya mlima wa volkano Haleakala, ambao uko mita 3,055 juu ya usawa wa bahari. Tulikuwa tumeambiwa kwamba hilo ni tukio la pekee. Kwa kuwa tulikuwa tunaishi Kapalua, tulihitaji kuamka saa nane usiku na kuelekea upande ule mwingine wa kisiwa. Kisha tulihitaji kupanda mlima huo mrefu kwa gari. Tulifikiri hiyo ilikuwa mapema sana na kwamba tungejikuta peke yetu barabarani. Haikuwa hivyo! Tulikuwa katika msafara wa magari mengi yaliyokuwa yakielekea kwenye kilele cha mlima huo. Tulipofika juu ya mlima, kulikuwa na baridi sana. Lakini tulikuwa na blanketi za kujikinga.
Mamia ya watu walikuwa wakingoja kwa subira jua lichomoze saa 12 hivi. Kila mtu alikuwa na hamu ya kuona jambo hilo lenye kuvutia, nazo kamera zilikuwa zimetayarishwa ili kupiga picha. Lakini tulihuzunika sana mawingu mazito yalipotanda juu ya mlima huo nasi hatukuweza kupiga picha zozote! Lakini mara nyingi kunakuwa na uwezekano wa mawingu kutanda juu ya milima iliyo karibu na Bahari ya Pasifiki. Kwa hiyo, hatungefanya jambo lolote isipokuwa kungoja hadi mawingu hayo yapite huku tukipigwa na joto la jua linapochomoza. Kisha jambo tusilotarajia likafanyika! Mbele yetu mandhari yenye kuvutia sana ya bonde la mlima huo lenye vijia vingi ndani yake ilianza kuonekana. Hivyo hatukuvunjika moyo sana.
Ghafula tukasikia sauti ya kushangaza, mlio kama wa kuku akiita vifaranga ukimalizia kwa “chuKAR, chuKAR.” Kisha tukaona mahali kelele hizo zilikuwa zikitoka. Kulikuwa na ndege maridadi wa jamii ya kware anayeitwa chukar, ambaye asili yake ni mabara ya Asia na Ulaya na jina lake la Kilatini ni Alectoris chukar. Ndege huyo hukaa ardhini katika majira ya kuzaliana, ambapo yeye hulalia mayai yake. Hakujaribu kuruka badala yake alikimbia.
Ndege huyo alifikaje kwenye kisiwa maridadi cha Maui? Inaonekana kwamba chukar waliletwa katika kisiwa hicho. Katika bara la Amerika Kaskazini, wao hufugwa na kuachiliwa ili wawindwe. Tulifurahi sana kwamba angalau tulikuwa tumemwona kwa ukaribu ndege huyo mwenye haya.—Tumetumiwa makala hii.