Sura 40
Somo la Rehema
YESU huenda bado akawa katika Naini, ambako hivi majuzi alifufua mwana wa mjane, au labda yeye anatembelea jiji fulani la karibu. Farisayo mmoja jina lake Simoni anatamani amtazame kwa ukaribu mtu huyo anayefanya maajabu kama hayo. Kwa hiyo yeye amwalika Yesu akale chakula pamoja naye.
Akiiona pindi hiyo kuwa fursa ya kuhudumia watu waliopo, Yesu anakubali mwaliko huo, kama vile yeye amekwisha kukubali mialiko kula pamoja na wakusanya kodi na watenda dhambi. Hata hivyo, anapoingia nyumba ya Simoni, Yesu hapokewi kwa uchangamfu kama ilivyo kawaida kuwapokea wageni.
Nyayo zilizovishwa sapatu zinapata joto na mavumbi kama tokeo la kusafiri katika barabara zenye mavumbi, na ni kitendo kilicho desturi ya ukaribishaji-wageni kuosha nyayo za wageni kwa maji baridi. Lakini nyayo za Yesu hazioshwi anapofika. Wala yeye hapokei busu la kumkaribisha, ambalo ni kawaida ya mapokezi. Naye hapewi yale mafuta ya ukaribishaji-wageni yaliyo desturi kumpa mgeni kwa ajili ya nywele zake.
Wakati mlo unapoendelea, wageni wakiwa wangali wanaegemea meza, mwanamke mmoja asiyealikwa anaingia chumbani humo. Yeye anajulikana katika jiji hilo kuwa anaishi maisha ya ukosefu wa adili. Inaelekea yeye amesikia mafundisho ya Yesu, kutia na mwaliko wake wa kwamba ‘wote wale waliolemewa na mizigo waje kwake wapate burudisho.’ Na kwa kuvutwa sana moyoni na mambo ambayo ameona na kusikia, sasa mwanamke huyo amemtafuta Yesu.
Mwanamke huyo akuja nyuma ya Yesu mezani na kupiga magoti kwenye nyayo zake. Huku machozi yake yakiangukia nyayo za Yesu, mwanamke huyo ayapangusa kwa nywele zake. Pia achukua mafuta yenye manukato kutoka kwa chupa yake, na anapobusu kwa wororo nyayo za Yesu, yeye azimiminia mafuta yale. Simoni anatazama kwa kutokubali jambo hilo. “Mtu huyu kama angekuwa nabii,” yeye anawaza, “angemtambua mwanamke huyu amgusaye, ni nani, naye ni wa namna gani, ya kwamba ni mwenye dhambi.”
Akifahamu kufikiri kwa Simoni, Yesu anasema: “Simoni, nina neno nitakalo kukuambia.”
“Mwalimu, nena,” yeye anajibu.
“Mtu mmoja mkopeshaji alikuwa na wadeni wawili,” Yesu anaanza. “Mmoja amwia dinari mia tano, na wa pili hamsini. Nao walipokuwa hawana cha kumlipa, aliwasamehe wote wawili. Katika hao wawili ni yupi atakayempenda zaidi?”
“Nadhani,” Simoni anasema, labda akiwa na hali ya kutojali swali lile kwa kuwa laonekana ni kama halifai kisa kilichopo, “ni yule ambaye alimsamehe nyingi.”
“Umeamua haki,” Yesu anajibu. Na ndipo akigeukia mwanamke yule, yeye amwambia Simoni hivi: “Wamwona mwanamke huyu? Niliingia nyumbani kwako, hukunipa maji kwa miguu yangu; bali huyu amenidondoshea machozi miguu yangu, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake. Wewe hukunibusu; lakini huyu tangu nilipoingia hakuacha kunibusu sana miguu yangu. Hukunipaka kichwa changu mafuta; bali huyo amenipaka miguu yangu marhamu.”
Hivyo mwanamke huyo ametoa wonyesho wazi wa toba ya kutoka moyoni kwa ajili ya ukosefu wake wa adili wa wakati uliopita. Kwa hiyo Yesu amalizia, akisema: “Kwa ajili ya hayo nakuambia, Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana; lakini asamehewaye kidogo, huyo hupenda kidogo.”
Yesu hatolei udhuru au haachilii tu kwa vyovyote ukosefu wa adili. Bali, kisa hicho kinafunua ufahamu wake wenye huruma juu ya wale wanaofanya makosa maishani kisha wadhihirisha kwamba wanasikitikia makosa hayo na kwa hiyo wanamjia Kristo wapate kitulizo. Akimwandalia mwanamke huyo burudisho la kweli, Yesu anasema: “Umesamehewa dhambi zako. . . . Imani yako imekuokoa, enenda zako kwa amani.” Luka 7:36-50; Mathayo 11:28-30.
▪ Yesu anapokewaje na Simoni mkaribishaji wake?
▪ Ni nani anayetafuta Yesu, na kwa sababu gani?
▪ Yesu anaandaa kielezi gani, naye akitumiaje?