NYONGEZA
Mlo wa Jioni wa Bwana—Maadhimisho Yanayomletea Mungu Heshima
WAKRISTO wanaamriwa waadhimishe Ukumbusho wa Kifo cha Kristo. Maadhimisho hayo yanaitwa pia “mlo wa jioni wa Bwana.” (1 Wakorintho 11:20) Maadhimisho hayo yana umuhimu gani? Yanapaswa kufanywa wakati gani na jinsi gani?
Yesu Kristo alianzisha maadhimisho hayo usiku wa Pasaka ya Kiyahudi mwaka wa 33 W.K. Pasaka ilikuwa maadhimisho yaliyofanywa mara moja tu kila mwaka, siku ya 14 ya mwezi wa Nisani katika kalenda ya Kiyahudi. Ili kukadiria tarehe hiyo, inaonekana kwamba Wayahudi walisubiri hadi sikusare (Machi 21) ya wakati wa majira ya kuchipua. Hiyo ndiyo siku ambayo mchana na usiku zinalingana. Mwezi wa Nisani ulianza wakati mwezi mpya ulipoonekana kwa mara ya kwanza karibu na Machi 21. Maadhimisho ya Pasaka yalifanywa siku 14 baadaye, baada ya jua kutua.
Yesu aliadhimisha Pasaka pamoja na mitume wake, kisha baada ya kumfukuza Yuda Iskariote, akaanzisha Mlo wa Jioni wa Bwana. Mlo huo ulichukua mahali pa Pasaka ya Kiyahudi na hivyo unapaswa kuadhimishwa mara moja tu kwa mwaka.
Injili ya Mathayo inasema: “Yesu alichukua mkate na, baada ya kutoa baraka, akaumega, akawapa wanafunzi, akasema: ‘Chukueni, mle. Huu unamaanisha mwili wangu.’ Pia, akachukua kikombe na, akiisha kushukuru, akawapa, akisema: ‘Kinyweeni, ninyi nyote; kwa maana hii inamaanisha “damu yangu ya agano,” ambayo itamwagwa kwa ajili ya wengi kwa msamaha wa dhambi.’”—Mathayo 26:26-28.
Watu fulani huamini kwamba Yesu aligeuza mkate kuwa mwili wake na divai kuwa damu yake. Hata hivyo, mwili wa Yesu ulikuwa kamili alipowapa mkate huo. Je, kweli mitume wa Yesu walikuwa wakila mwili halisi na kunywa damu yake? Hapana, kwa kuwa kufanya hivyo kungekuwa kuvunja sheria ya Mungu iliyokataza kunywa damu. (Mwanzo 9:3, 4; Mambo ya Walawi 17:10) Kulingana na Luka 22:20, Yesu alisema: “Kikombe hiki kinamaanisha agano jipya kwa msingi wa damu yangu, ambayo itamwagwa kwa ajili yenu.” Je, kikombe hicho kilikuwa “agano jipya” kihalisi? Hilo halingewezekana kwa kuwa agano ni makubaliano wala si kitu halisi.
Hivyo, mkate na divai ni mifano tu. Mkate huwakilisha mwili mkamilifu wa Kristo. Yesu alitumia mkate uliobaki baada ya mlo wa Pasaka. Mkate huo uliokwa bila chachu, au hamira. (Kutoka 12:8) Mara nyingi Biblia hutumia chachu kuwakilisha dhambi au kuharibika. Kwa hiyo, mkate unawakilisha mwili mkamilifu ambao Yesu alidhabihu. Haukuwa na dhambi yoyote.—Mathayo 16:11, 12; 1 Wakorintho 5:6, 7; 1 Petro 2:22; 1 Yohana 2:1, 2.
Divai nyekundu inawakilisha damu ya Yesu. Damu hiyo inafanya agano jipya liwe halali. Yesu alisema kwamba damu yake ilimwagwa “kwa msamaha wa dhambi.” Hivyo, wanadamu wanaweza kuwa safi machoni pa Mungu na kuwa katika agano jipya pamoja na Yehova. (Waebrania 9:14; 10:16, 17) Agano au mkataba huo huwawezesha wale Wakristo waaminifu 144,000 kwenda mbinguni. Watakuwa wafalme na makuhani mbinguni na kuwaletea wanadamu wote baraka.— Mwanzo 22:18; Yeremia 31:31-33; 1 Petro 2:9; Ufunuo 5:9, 10; 14:1-3.
Ni nani wanaopaswa kula mkate na kunywa divai wakati wa Ukumbusho? Ni wale tu walio katika agano jipya, yaani, wale walio na tumaini la kwenda mbinguni. Roho takatifu ya Mungu huwasadikisha kwamba wamechaguliwa kuwa wafalme mbinguni. (Waroma 8:16) Wako pia katika agano la Ufalme pamoja na Yesu.— Luka 22:29.
Namna gani wale walio na tumaini la kuishi milele katika Paradiso duniani? Wanatii amri ya Yesu kwa kuhudhuria Mlo wa Jioni wa Bwana, lakini wao huwa watazamaji wenye heshima wala hawashiriki mifano. Mara moja kila mwaka, Mashahidi wa Yehova huadhimisha Mlo wa Jioni wa Bwana mnamo Nisani 14 baada ya jua kutua. Ingawa ni watu wachache tu ulimwenguni wanaodai kuwa na tumaini la kwenda mbinguni, maadhimisho hayo yanathaminiwa na Wakristo wote. Ni pindi ambayo wote wanaweza kufikiria juu ya upendo usio na kifani wa Yehova Mungu na Yesu Kristo.—Yohana 3:16.