SURA YA 34
Yesu Achagua Mitume Kumi na Wawili
MITUME 12
Ni mwaka mmoja na nusu hivi tangu Yohana Mbatizaji alipomtambulisha Yesu kuwa Mwanakondoo wa Mungu. Yesu anapoanza huduma yake, wanaume kadhaa wanyoofu wanakuwa wanafunzi wake, kama vile Andrea, Simoni Petro, Yohana na labda Yakobo (ndugu ya Yohana), Filipo, na Bartholomayo (ambaye pia anaitwa Nathanaeli). Baada ya muda, watu wengine wengi wanajiunga nao kumfuata Kristo.—Yohana 1:45-47.
Sasa Yesu yuko tayari kuwachagua mitume wake. Hawa watashirikiana naye kwa ukaribu na watapokea mazoezi ya pekee. Lakini kabla ya kuwachagua, Yesu anaenda mlimani, labda mlima ulio karibu na Bahari ya Galilaya mwendo mfupi kutoka Kapernaumu. Anasali usiku kucha, inaelekea anamwomba Mungu ampe hekima na ambariki. Siku inayofuata, anawaita wanafunzi wake na kuchagua 12 kati yao wawe mitume.
Yesu anawachagua wale wanaume sita waliotajwa mwanzoni, na pia Mathayo, ambaye Yesu alimwita akiwa kwenye ofisi ya kodi. Wale wengine watano ni Yuda (ambaye pia anaitwa Thadayo na “mwana wa Yakobo”), Simoni Mkananayo, Tomasi, Yakobo mwana wa Alfayo, na Yuda Iskariote.—Mathayo 10:2-4; Luka 6:16.
Kufikia sasa hawa 12 wamesafiri pamoja na Yesu, naye anawajua vizuri. Baadhi yao ni watu wake wa ukoo. Inaelekea kwamba Yakobo na Yohana ambao ni ndugu, ni binamu za Yesu. Na ikiwa, kama wengine wanavyofikiria, Alfayo ni ndugu ya Yosefu, baba mlezi wa Yesu, basi mwana wa Alfayo, mtume Yakobo, ni binamu ya Yesu.
Bila shaka, si vigumu kwa Yesu kukumbuka majina ya mitume wake. Lakini je, wewe unaweza kuyakumbuka? Njia moja inayoweza kutusaidia ni kukumbuka kwamba wawili wanaitwa Simoni, wawili wanaitwa Yakobo, na wawili wanaitwa Yuda. Simoni (Petro) ana ndugu anayeitwa Andrea, na Yakobo (mwana wa Zebedayo) ana ndugu anayeitwa Yohana. Hiyo ni njia rahisi ya kukumbuka majina ya mitume wanane. Wale wengine wanne, wanatia ndani mkusanya kodi (Mathayo), yule ambaye baadaye anakuwa na shaka (Tomasi), yule aliyeitwa akiwa chini ya mti (Nathanaeli), na rafiki ya Nathanaeli (Filipo).
Mitume kumi na mmoja wanatoka Galilaya, eneo la nyumbani la Yesu. Nathanaeli anatoka Kana. Filipo, Petro, na Andrea wanatoka Bethsaida. Hata hivyo, baadaye Petro na Andrea wanahamia Kapernaumu, ambako inaonekana Mathayo aliishi. Pia, Yakobo na Yohana wanaishi Kapernaumu au karibu na huko, na biashara yao ya uvuvi iko hapo karibu. Inaonekana Yuda Iskariote ambaye baadaye anamsaliti Yesu ndiye mtume pekee anayetoka Yudea.