KIGIRIKI
Lugha ya jamii-lugha za India-Ulaya. (Chimbuko la Kiebrania ni jamii ya Shemu, ambayo ni jamii-lugha nyingine.) Awali, Maandiko ya Kikristo yaliandikwa katika Kigiriki (isipokuwa Injili ya Mathayo, iliyoandikwa kwanza katika Kiebrania) na ni katika lugha hiyo pia kwamba tafsiri kamili ilitokezwa ya Maandiko ya Kiebrania, yaani, Septuajinti ya Kigiriki. Ni lugha yenye kunyambulika, inayotokeza unamna-namna katika usemi kupitia mashina, viambishi awali, na viishio.
Koine. Kuanzia karibu mwaka 300 K.W.K. hadi karibu mwaka 500 W.K. ndiyo iliyokuwa enzi ya Koine, au Kigiriki cha kawaida, mchanganyiko wa Kigiriki chenye lahaja tofauti hasa ile ya Kiattika ikiwa ndiyo yenye ushawishi zaidi. Koine ikawa ndiyo lugha ya kimataifa. Ilikuwa na mvuto wenye kutokeza zaidi kuliko lugha nyinginezo za wakati huo, kwa kuwa ilijulikana karibu kila mahali. Koine inamaanisha lugha ya kawaida, au lahaja inayotumiwa na wote. Jambo la kwamba matumizi ya Koine yalienea sana linaonyeshwa na uhakika wa kwamba amri za magavana wa kifalme na za seneti ya Roma zilitafsiriwa katika Koine ili zisambazwe kotekote katika Milki ya Roma. Basi, shtaka lililobandikwa juu ya kichwa cha Yesu Kristo alipotundikwa liliandikwa si katika Kilatini rasmi tu na Kiebrania bali pia katika Kigiriki (Koine).—Mt 27:37; Yoh 19:19, 20.
Msomi mmoja anaeleza hivi kuhusu matumizi ya Kigiriki katika nchi ya Israeli: “Ingawa sehemu kubwa ya Wayahudi waliukataa utamaduni wa Kiyunani pamoja na njia zake, hawakuweza kuepuka kushirikiana na Wagiriki na matumizi ya lugha ya Kigiriki. . . . Walimu Wapalestina walipendelea tafsiri ya Maandiko ya Kigiriki, wakiyaona kuwa chombo cha kuwasilisha kweli kwa Watu wa Mataifa.” (Hellenism, cha N. Bentwich, 1919, ukur. 115) Bila shaka, Septuajinti ya Kigiriki ilikusudiwa kwanza kabisa iwanufaishe Wayahudi, hasa wale waliokuwa Watawanyika, ambao sasa hawakuzungumza Kiebrania sanifu lakini wenye kufahamiana na Kigiriki. Maneno yenye asili ya Kigiriki yakaja kuchukua nafasi ya maneno ya Kiebrania cha kale yanayohusisha ibada ya Kiyahudi. Neno sy·na·go·ge′, linalomaanisha “kukutana pamoja,” ni mfano wa maneno ya Kigiriki yaliyotumiwa na Wayahudi.
Koine ilitumiwa na waandikaji Wakristo walioongozwa na roho. Kwa kuwa waandikaji Wakristo walioongozwa na roho walihangaikia sana kuwasilisha ujumbe wao kwa njia inayoeleweka kwa watu wote, walitumia Koine badala ya Kigiriki rasimi. Waandikaji wote hao walikuwa Wayahudi. Ingawa walikuwa wa jamii ya Shemu, hangaiko lao halikuwa uenezaji wa utamaduni wa jamii ya Shemu, bali ile kweli kuhusu Ukristo halisi, na kwa kutumia lugha ya Kigiriki, wangeweza kuwafikia watu wengi zaidi. Wangeweza kutimiza vizuri utume wao wa ‘kufanya wanafunzi kutoka kwa watu wa mataifa yote.’ (Mt 28:19, 20) Pia, Koine ilikuwa chombo bora cha kuelezea mawazo tanzu ambayo walitamani kuwasilisha.
Kupitia ujumbe wao uliokwezwa, waandikaji Wakristo walioongozwa na roho waliipa Koine nguvu, adhama, na uchangamshi. Maneno ya Kigiriki yakawa na maana iliyo wazi zaidi, iliyo kamili zaidi, na iliyo ya kiroho zaidi katika ule muktadha mbalimbali wa Maandiko yaliyoongozwa na roho.
Alfabeti. Alfabeti zote zilizopo leo za Ulaya zinatokana na alfabeti ya Kigiriki kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja. Hata hivyo, Wagiriki hawakujibunia alfabeti yao; waliiazima kutoka kwa jamii ya Shemu. Hilo linaonekana wazi kutokana na uhakika wa kwamba herufi za alfabeti ya Kigiriki (za karibu na karne ya saba K.W.K.) zilifanana na herufi za Kiebrania (za karibu na karne ya nane K.W.K.). Pia, walikuwa na mpangilio huohuo wa kijumla, ila kukiwa tofauti chache tu. Kuongezea hayo, matamshi ya majina ya baadhi ya herufi yanafanana sana; kwa mfano: al′pha (Kigiriki) na ʼa′leph (Kiebrania); be′ta (Kigiriki) na behth (Kiebrania); del′ta (Kigiriki) na da′leth (Kiebrania); na mengine mengi. Koine ilikuwa na herufi 24. Katika kuitumia alfabeti ya jamii ya Shemu ifaane na lugha ya Kigiriki, Wagiriki waliiboresha kwa kuchukua herufi za ziada kwa ajili ya konsonanti linganifu ambazo hawakuwa nazo (ʼa′leph, heʼ, chehth, ʽa′yin, waw, na yohdh) nao wakazitumia kuwakilisha sauti za vokali au irabu a, e (fupi), e (ndefu), o, y, na i.
Msamiati. Msamiati wa Kigiriki ni mpana na ni mwafaka. Mwandikaji Mgiriki huwa na maneno mengi yanayomwezesha kutofautisha mambo kinagaubaga na kuwasilisha maana iliyo barabara kama atakavyo. Kwa mfano, lugha ya Kigiriki hutofautisha kati ya ujuzi wa kawaida, gno′sis (1Ti 6:20), na ujuzi wenye kina, e·pi′gno·sis (1Ti 2:4), na kati ya al′los (Yoh 14:16), linalomaanisha “-ingine” ya aina moja, na neno he′te·ros, linalomaanisha “-ingine” ya aina tofauti. (Gal 1:6) Semi nyingi katika lugha nyinginezo zimeshirikisha maneno ya Kigiriki na vilevile mizizi ya kimsingi inayohusisha maneno ya Kigiriki, na kutokeza lugha iliyo sahihi na hususa zaidi katika usemi.
Nomino. Nomino huambishwa kulingana na kauli, jinsia, na idadi. Maneno yanayohusiana, kama vile viwakilishi nafsi na vivumishi, huambishwa ili yapatane na visabiki vyake au vitu vinavyorejelewa.
Kauli. Kwa ujumla inaonekana Koine ilikuwa na kauli tano. (Wasomi fulani huziongeza hadi kuwa nane.) Kwa kawaida Kiingereza hakina badiliko katika maumbo ya nomino ila katika kauli ya vimilikishi na katika idadi. (Hata hivyo, viwakilishi nafsi hubadilikabadilika zaidi.) Lakini katika Koine, kila kauli huhitaji muundo tofauti au kiishio tofauti, na kwa njia hiyo kuifanya kuwa lugha tata zaidi kuliko Kiingereza.
Kibainishi. Katika lugha ya Kiingereza kuna kibainishi kilicho dhahiri (“the”) na vibainishi visivyo dhahiri (“a,” “an”). Koine ina kibainishi kimoja tu ὁ (ho), ambacho kwa njia fulani kinalingana na kibainishi kilicho dhahiri “the” katika Kiingereza. Ingawa kibainishi kilicho dhahiri “the” cha Kiingereza hakinyambuliki, kibainishi cha Kigiriki hunyambulika kulingana na kauli, jinsia, na idadi, na nomino hali kadhalika.
Kibainishi cha Kigiriki hakitumiwi tu kubainisha nomino, kama ilivyo katika Kiingereza, bali pia hutumiwa pamoja na nomino-vitenzi, vivumishi, vielezi, virai, vishazi, na hata sentensi nzimanzima. Matumizi ya kibainishi pamoja na kivumishi yanapatikana katika Kigiriki kwenye Yohana 10:11, ambamo tafsiri ya neno kwa neno ni: “Mimi ni mchungaji yule mwema [mmoja].” Maneno hayo yana uzito kuliko kusema tu “Mimi ndiye mchungaji mwema.” Ni kama kuandika neno “mwema” katika italiki ili kulitia mkazo.
Mfano unaoonyesha kibainishi kikiwa kimetumiwa katika kishazi kizima katika Kigiriki unapatikana kwenye andiko la Waroma 8:26, ambamo kibainishi kisicho na jinsia kinatangulia maneno “kuhusu tunalohitaji kusali.” Tafsiri ya neno kwa neno ingekuwa “lile kuhusu tunalohitaji kusali.” (Int) Ili kuwasilisha maana katika Kiingereza au Kiswahili, ni muhimu kuongeza neno “tatizo.” Kibainishi kinaangazia mambo, hivi kwamba tatizo hilo linatokezwa wazi liwe suala dhahiri. Hivyo, tafsiri “Kwa maana lile tatizo kuhusu tunalohitaji kusali hatujui” (NW) inatoa kwa usahihi zaidi wazo la mwandikaji.
Vitenzi. Vitenzi vya Kigiriki huundwa kutokana na mizizi ya vitenzi hasa kupitia mashina na viishio, au viambishi na viambishi tamati. Vinaungwa kulingana na kauli za kitenzi, dhamira, njeo, nafsi, na idadi. Katika Kigiriki vitenzi vinaibua changamoto iliyo kubwa katika utafiti kuliko nomino. Uelewaji mzuri wa Koine katika miaka ya karibuni, hasa kuhusiana na vitenzi vyake, umewawezesha watafsiri kuwasilisha maana ya Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo kwa njia nzuri kuliko ilivyokuwa katika tafsiri za zamani. Baadhi ya mambo yenye kupendeza zaidi kuhusiana na vitenzi vya Kigiriki na ushawishi wavyo katika kuielewa Biblia, yanazungumziwa katika mafungu yanayofuata.
Kauli ya Kitenzi. Lugha ya Kiingereza ina sauti mbili tu katika vitenzi vyake, yaani, kauli ya kutenda na kauli ya kutendewa, lakini Kigiriki pia kina “kauli ya katikati” iliyo tofauti kabisa. Katika kitenzi hicho, kiima hushiriki katika matokeo ya tendo au, nyakati nyingine hutokeza tendo lenyewe. Kauli hiyo hukazia kupendezwa kwa mhusika katika tendo la kitenzi hicho.
Kauli hiyo ya katikati ilitumiwa pia kutilia mkazo. Ilitimiza kusudi kama lile ambalo italiki hutimiza katika Kiingereza au Kiswahili. Paulo alisema hivi baada ya kuambiwa kwamba vifungo na dhiki vilikuwa vikimngojea akifika Yerusalemu: “Hata hivyo, siifanyi nafsi yangu kuwa kitu chenye thamani sana kwangu, kama tu ningepata kumaliza mwendo wangu na huduma niliyopokea kutoka kwa Bwana Yesu.” (Mdo 20:22-24) Hapa kitenzi poi·ou′mai kinachotafsiri “siifanyi,” kiko katika kauli ya katikati. Paulo hasemi kwamba hathamini uhai wake, bali kwamba kutimizwa kwa huduma yake ni jambo la muhimu zaidi. Huo ndio mkataa wake, haidhuru ni nini maoni ya wengine.
Kauli ya katikati inatumiwa katika andiko la Wafilipi 1:27: “Ila tu jiendesheni [au, “endeleeni kama raia”] kwa namna inayostahili habari njema juu ya Kristo.” Katika andiko hilo kitenzi po·li·teu′o·mai, kiko katika kauli ya katikati, po·li·teu′e·sthe, “endeleeni kama raia,” yaani, shirikini katika utendaji wa raia, mkishiriki kutangaza habari njema. Kwa kawaida raia wa Roma walijishughulisha sana katika mambo ya Serikali, kwa kuwa uraia wa Roma ulithaminiwa sana, hasa katika miji ambamo wakaaji wake walikuwa wamepewa uraia na Roma, kama ilivyokuwa katika Filipi. Kwa hiyo, hapa Paulo anawaambia Wakristo wasiwe wasiotenda, kana kwamba wao ni Wakristo wa jina tu, bali kwamba ni lazima washiriki katika utendaji wa Kikristo. Hilo linapatana na maneno aliyowaambia baadaye: “Lakini sisi, uraia wetu uko mbinguni.”—Flp 3:20.
Njeo. Jambo jingine lililo muhimu na tofauti kabisa katika Kigiriki, linalochangia iwe lugha mwafaka ni matumizi yake ya njeo za vitenzi. Vitenzi na njeo zake huhusisha mambo mawili: aina ya kitendo (ndilo jambo muhimu sana) na wakati wa kitendo (silo jambo muhimu sana). Kuna vipengele vitatu muhimu vya kuona kitendo katika lugha ya Kigiriki, kila kimoja kikiwa na sifa za kuvumisha: (1) kitendo kikiendelea (“kuendelea kufanywa”), kinachowakilishwa hasa na njeo inayoonyesha hali ya kuendelea, mkazo mkuu ukiwa ni kitendo kinachoendelea au ambacho kimazoea au kikawaida hurudiliwa; (2) kitendo kikiwa kimekamilika (“kimesha tendwa”), njeo kuu hapa ikiwa ni kamilifu; (3) kitendo cha mara moja, au kwa punje ya wakati (“kutendwa”), kinachowakilishwa na njeo ya aorist. Bila shaka, kuna njeo nyinginezo, kama njeo isiyokamilika, iliyokamilika, na ya wakati ujao.
Ili kuonyesha tofauti iliyoko katika njeo za Kigiriki: Kwenye 1 Yohana 2:1, mtume Yohana anasema hivi: “Kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba” (UV). Kitenzi cha Kigiriki kinachotafsiriwa “dhambi” kinatumia njeo ya aorist, hivyo wakati wa hicho kitendo ni kitambo kidogo, punje ya wakati. Hapa njeo hii ya aorist inaonyesha kitendo kimoja cha dhambi, kwa upande mwingine, kitenzi cha wakati uliopo kingeonyesha hali ya kuwa mwenye dhambi au kuendelea kutenda dhambi. Kwa hiyo, Yohana hazungumzii mtu fulani anayeendeleza zoea la kufanya dhambi, bali juu ya mtu, ‘anayetenda dhambi’ moja (Linganisha Mt 4:9, ambapo njeo ya aorist inaonyesha kwamba Ibilisi hakumwomba Yesu ampe ibada daima au kwa kuendelea, bali “tendo [moja] la ibada.”)
Lakini, ikiwa andiko la 1 Yohana 3:6, 9 litasomwa bila kukumbuka uhakika wa kwamba kitenzi kinachotumiwa kiko katika njeo ya wakati uliopo, Yohana ataonekana kuwa anapinga maneno yake yaliyotajwa hapo juu. Tafsiri ya Union Version inasema hivi: “Kila akaaye ndani yake hatendi dhambi,” na, “Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi.” Tafsiri hii inakosa kuwasilisha katika Kiswahili tendo linaloendelea linaloonyeshwa na njeo ya wakati uliopo ya vitenzi vya Kigiriki vilivyotumiwa. Tafsiri fulani za kisasa, huzingatia tendo linaloendelea, na badala ya hapa kusema, “hatendi dhambi,” wametafsiri vitenzi hivyo ifaavyo: “hana mazoea ya kufanya dhambi,” haendelei kufanya dhambi (NW); “hazoei dhambi,” “hafanyi mazoea ya dhambi” (CB); “hana desturi ya kufanya dhambi,” “haendelei kufanya dhambi” (TEV). Yesu aliwaamuru hivi wafuasi wake kwenye Mathayo 6:33: “Basi endeleeni kuutafuta kwanza ufalme,” kuonyesha jitihada yenye kuendelea, badala tu ya kusema “utafuteni kwanza ufalme” (UV).
Hali kadhalika, katika makatazo, njeo ya wakati uliopo na ya aorist zinatofautiana kabisa. Katazo katika njeo ya wakati uliopo linamaanisha mengi zaidi ya kutofanya jambo fulani. Linamaanisha kukoma kulifanya. Yesu Kristo, akiwa njiani kuelekea Golgotha, hakuwaambia wanawake waliokuwa wakimfuata, “msilie” tu, bali, badala yake, kwa kuwa tayari walikuwa wanalia, aliwaambia, “acheni kunililia.” (Lu 23:28) Hali kadhalika, Yesu aliwaambia hivi wale waliokuwa wakiuza njiwa hekaluni: “Acheni kuifanya nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara!” (Yoh 2:16) Katika Mahubiri ya Mlimani alisema: “Acheni kuhangaika” juu ya nafsi zenu kuhusu kile mtakachokula, mtakachokunywa, au mtakachovaa. (Mt 6:25) Kwa upande mwingine, njeo ya aorist katika makatazo ilikuwa amri ya kutofanya jambo fulani wakati wowote ule. Yesu anaonyeshwa akiwa anawaambia wasikilizaji wake hivi: “Kwa hiyo, msihangaike kamwe [yaani, msihangaike wakati wowote] juu ya kesho.” (Mt 6:34) Hapa njeo ya aorist inatumiwa ili kuonyesha kwamba wanafunzi hawapaswi kuhangaika wakati wowote ule.
Mfano mwingine unaoonyesha kwa nini ni muhimu kufikiria njeo za Kigiriki wakati wa kutafsiri unapatikana katika Waebrania 11:17. Watafsiri fulani hupuuza maana ya pekee iliyo katika njeo ya kitenzi. Inapomrejelea Abrahamu, tafsiri ya Verbum Bible ya Kiswahili inasema hivi: “Alimtoa Isaka mwana wake wa pekee.” Neno la Kigiriki linalotafsiriwa “alimtoa” liko katika njeo isiyo kamilifu, ambalo linaweza kumaanisha kwamba tendo lilikusudiwa au kujaribiwa, lakini halikutimizwa. Hivyo, kulingana na jinsi hali zilivyokuwa kihalisi, kitenzi cha Kigiriki kinatafsiriwa kwa usahihi zaidi kuwa “alijaribu kumtoa.” Vivyo hivyo, andiko la Luka 1:59, linapozungumzia kuhusu wakati wa kumtahiri mwana wa Zekaria na Elisabeti, njeo isiyo timilifu iliyotumiwa inaonyesha kwamba badala ya kutafsiriwa, “Wakamwita Zakaria, jina la baba yake” (KJ), mstari huo unapaswa kusema, “Walitaka kumwita [mtoto huyo] kwa jina la baba yake, Zekaria.” (NW). Hilo linapatana na jambo ambalo lilitokea hasa, yaani, kwamba alipewa jina Yohana, kulingana na maagizo ya malaika Gabrieli.—Lu 1:13.
Kutohoa. Hii inarejelea tahajia za maneno ya Kigiriki kwa kutumia alfabeti nyingine. Katika visa vingi, ni kubadilisha herufi na herufi nyingine, b badala ya β, g badala ya γ, na kadhalika. Ndivyo ilivyo pia na vokali za Kigiriki, a badala ya α, e badala ya ε, e badala ya η, i badala ya ι, o badala ya ο, y badala ya υ, na o badala ya ω.
Vokali-pacha. Kanuni iliyo hapo juu ya herufi moja kuchukua nafasi ya nyingine inatumika pia katika vokali-pacha nyingi: ai badala ya αι, ei badala ya ει, oi badala ya οι. Herufi ya Kigiriki y′psi·lon (υ) haifuati kanuni hiyo katika hali zifuatazo: αυ ni au, bali si ay; ευ ni eu, bali si ey; ου ni ou, bali si oy; υι ni ui, bali si yi; ηυ ni eu, bali si ey.
Hata hivyo, kuna nyakati ambapo zile ambazo huenda zikaonwa mwanzoni kuwa vokali-pacha zinakuwa na alama ya kutofautisha matamshi ya vokali ( ͏̈) ikiwa juu ya herufi ya pili, kwa mfano, αϋ, εϋ, οϋ, ηϋ, ωϋ, αϊ, οϊ. Alama za matamshi juu ya i·o′ta (ϊ) au y′psi·lon (ϋ) zinaonyesha kwamba kwa kweli haifanyizi vokali-pacha pamoja na vokali inayoitangulia. Hivyo, neno y′psi·lon likiwa na alama ya matamshi linatoholewa kuwa y, bali si u. Mifano iliyo hapo juu ingefuatana hivi, ay, ey, oy, ey, oy, ai, oi.
Vokali fulani (α, η, ω) zina chembe i·o′ta· (ι) (inayoitwa i·o′ta ndisiduni) inayoandikwa chini yazo. Katika kutohoa miundo hii ya Kigiriki, i·o′ta (au i) haitiwi chini ya mstari, bali kando na baada ya herufi ambayo inatokea chini yake. Hivyo ᾳ ni ai, ῃ ni ei, na ῳ ni oi.
Alama za kimatamshi za mkazo. Kigiriki kina aina tatu za mikazo ya kimatamshi: zinazoitwa acute (΄), circumflex (<u34F><u311>), na grave (‵). Katika Kigiriki zinakuwa juu ya vokali za silabi zinazotilia mkazo. Hata hivyo, katika tafsiri zilizotoholewa katika kitabu hiki, alama ya mkazo inakuja mwishoni mwa silabi iliyotiwa mkazo na ni alama moja tu inayotumiwa kwa ajili ya aina zote tatu za mikazo ya kimatamshi ya Kigiriki. Kwa hiyo, λόγος imetiwa alama lo′gos; ζῶον ingekuwa zo′on.
Silabi. Ili kusaidia katika matamshi, ama nukta au alama ya kimatamshi ya mkazo hutumiwa katika maneno yaliyotoholewa ili kutenganisha silabi zote. Neno la Kigiriki huwa na silabi nyingi zinazolingana na vokali au vokali-pacha lililo nazo. Hivyo, neno λόγος (lo′gos) lina vokali mbili na hivyo ni silabi mbili. Vokali mbili za vokali-pacha zipo katika silabi moja, wala si mbili. Neno πνεύμα (pneu′ma) lina vokali-pacha moja (eu) na vokali nyingine moja (a) na hivyo lina silabi mbili.
Katika kugawanya silabi, kanuni mbili zifuatazo zimefuatwa: (1) Konsonanti moja inapokuwa katikati ya neno, inaunganishwa pamoja na vokali inayofuata katika silabi ya pili. Kwa hiyo, neno πατήρ lingekuwa pa·ter′. (2) Nyakati nyingine muunganisho wa konsonanti hutokea katikati ya neno la Kigiriki. Ikiwa muunganisho huohuo wa konsonanti unaweza kutumiwa kuanza neno la Kigiriki, basi unaweza pia kutumiwa kuanza silabi. Kwa mfano, neno κόσμος lingegawanywa kuwa ko′smos. Herufi sm zinawekwa pamoja na vokali ya pili. Hii ni kwa sababu maneno mengi ya Kigiriki kama vile—Smyr′na—huanza na konsonanti hizohizo mbili. Hata hivyo, muunganisho fulani wa konsonanti unapopatikana katikati ya neno na hakuna neno la Kigiriki linaloanza na muunganisho kama huo, zinatenganishwa. Hivyo, neno βύσσος linatoholewa kuwa bys′sos, kwa kuwa herufi ss hazianzi neno lolote la Kigiriki.
Alama za kupumulia. Vokali mwanzoni mwa neno inahitaji alama ya kupumulia iliyo “laini” (᾿) au alama ya kupumulia yenye “kukwaruza” (῾). Alama ya kupumulia iliyo “laini”(᾿) inaweza kupuuzwa wakati wa kutohoa; alama ya kupumulia yenye “kukwaruza” inahitaji herufi h iongezwe mwanzoni mwa neno. Herufi ya kwanza ikifanywa iwe kubwa, alama hizo za kupumulia zinalitangulia neno lenyewe. Katika hali hiyo, Ἰ inakuwa I, ilhali Ἱ inatoholewa kuwa Hi. Maneno yanapoanza na herufi ndogo, alama hizo za kupumulia huwa juu ya herufi ya kwanza au ikiwa ni katika vokali-pacha, juu ya herufi ya pili. Kwa hiyo, αἰών linakuwa ai·on′, ilhali ἁγνός ni ha·gnos′ na αἱρέομαι ni hai·re′o·mai.
Kwa kuongezea, herufi ya Kigiriki rho (ρ), inayotoholewa kuwa r, nyakati zote huhitaji alama ya kupumulia yenye “kukwaruza” (῾) mwanzoni mwa neno. Hivyo ῥαββεί linakuwa rhab·bei′.