UFALME
Kimsingi ni serikali ya kifalme; pia eneo na vikundi vya watu walio chini ya utawala wa mfalme, au mara chache zaidi, chini ya mfalme wa kike au malkia. Mara nyingi ufalme ulikuwa ni urithi. Mtawala mwenye enzi kuu aweza kuwa na vyeo vingine kama vile Farao au Kaisari.
Falme za nyakati za kale, kama vile leo, zilikuwa na nembo za kifalme. Kwa kawaida kulikuwa na jiji kuu au mahali pa makao ya mfalme, mahakama ya kifalme, jeshi lililo tayari (japo pengine likiwa limepunguzwa sana katika idadi nyakati za amani). Neno “ufalme,” kama linavyotumiwa katika Biblia, likiwa peke yake halifunui jambo lolote lililo dhahiri kuhusiana na muundo wa kiserikali, ukubwa wa eneo, au mamlaka ya mfalme. Falme zilitofautiana katika ukubwa na uvutano kuanzia zile mamlaka zenye nguvu za ulimwengu kama vile Misri, Ashuru, Babiloni, Umedi-Uajemi, Ugiriki, na Roma, kurudi chini hadi falme-majiji zilizo ndogo kama vile zile zilizokuwa Kanaani wakati Waisraeli walipopigana kutwaa ushindi. (Yos 12:7-24) Huenda pia muundo wa kiserikali ulitofautiana sana kutoka ufalme mmoja hadi ufalme mwingine.
Ufalme wa kwanza wa historia ya kibinadamu, ule wa Nimrodi, yaonekana hapo awali ulikuwa ufalme-jiji, baadaye ukapanua milki yake ikatia ndani majiji mengine, msingi wake ukiwa katika Babeli. (Mwa 10:9-11) Salemu, ambalo juu yake Mfalme-Kuhani Melkizedeki alitawala katika ufalme wa kwanza ulio na kibali cha Mungu, ni wazi pia lilikuwa ufalme-jiji. (Mwa 14:18-20; linganisha Ebr 7:1-17.) Falme kubwa zaidi zilihusisha eneo zima, kama vile falme za Edomu, Moabu, na Amoni. Zile milki kuu, zilizotawala maeneo makubwa na zenye falme tanzu nyingine, yaelekea kwa ujumla zilianza na kusitawi kutokana na nchi-majiji madogo au vikundi vya kikabila ambavyo hatimaye viliungana chini ya kiongozi mmoja mbabe. Nyakati nyingine miseto hiyo ilikuwa ya muda, mara nyingi ikiundwa kwa ajili ya vita dhidi ya adui yao mmoja. (Mwa 14:1-5; Yos 9:1, 2; 10:5) Mara nyingi falme za vibaraka zilifurahia kiwango kikubwa cha uhuru wa kuwa dola, au uhuru wa kujitawala, japo zilikuwa chini ya mapenzi na madai za ile mamlaka yenye kupiga ubwana.—2Fa 17:3, 4; 2Nya 36:4, 10.
Matumizi Yaliyo Mapana. Katika matumizi ya Kimaandiko neno “ufalme” laweza kurejelea sehemu fulani hususa za serikali ya kifalme. Laweza kurejelea milki ya eneo la nchi ambayo juu yake enzi kuu inadhihirishwa. Kwa hivyo, milki ya kifalme ilitia ndani si jiji kuu tu bali pia milki nzima, ikihusisha falme zozote za cheo cha chini au zilizo matanzu.—1Fa 4:21; Est 3:6, 8.
Huenda neno “ufalme” kwa njia ya kijumla likarejelea serikali ya kibinadamu yeyote au zote, iwe inaongozwa kihalisi na mfalme au sivyo.—Ezr 1:2; Mt 4:8.
Huenda likamaanisha ufalme, cheo cha kifalme au daraka la mfalme (Lu 17:21), pamoja na ile adhama, nguvu, na mamlaka yenye kuambatanishwa. (1Nya 11:10; 14:2; Lu 19:12, 15; Ufu 11:15; 17:12, 13, 17) Huenda watoto wa mfalme wakarejelewa kuwa ‘uzao wa ufalme.’—2Fa 11:1.
Ufalme wa Israeli. Agano la Sheria lililopewa taifa la Israeli kupitia Musa, lilikuwa na uandalizi kwa ajili ya utawala wa ufalme. (Kum 17:14, 15) Mtu aliyeongoza ufalme huo alipewa mamlaka na kupewa adhama ya kifalme, si kwa ajili ya kujitukuza binafsi, bali ili atumikie kwa ajili ya kumstahi Mungu na kufaidi ndugu zake Waisraeli. (Kum 17:19, 20; linganisha 1Sa 15:17.) Hata hivyo, baada ya muda wakati Waisraeli walipoomba wapewe mfalme, nabii Samweli alionya kuhusu madai ambayo mtawala kama huyo angetoa kwa watu. (1Sa 8) Inaelekea wafalme wa Israeli walikuwa wenye kukaribiwa na kufikilika na raia zao zaidi ya ilivyokuwa na wafalme wa zile falme nyingi za kale za upande wa Mashariki.—2Sa 19:8; 1Fa 20:39; 1Nya 15:25-29.
Japo ufalme wa Israeli ulianza na mfalme kutoka mstari wa Benyamini, baada ya hapo Yuda lilikuja kuwa kabila la kifalme, kupatana na unabii wa Yakobo akiwa mahututi kitandani. (1Sa 10:20-25; Mwa 49:10) Nasaba ya kifalme ilianzishwa katika mstari wa Daudi. (2Sa 2:4; 5:3, 4; 7:12, 13) Ufalme huo ‘uliporaruliwa’ kutoka kwa Rehoboamu, mwana wa Sulemani, makabila kumi yalifanyiza ufalme wa kaskazini, huku Yehova Mungu akibaki na kabila moja, Benyamini, ili liendelee kuwa pamoja na Yuda, “ili Daudi mtumishi wangu aendelee kuwa na taa sikuzote mbele zangu katika Yerusalemu, jiji ambalo nimejichagulia ili kuweka jina langu humo.” (1Fa 11:31, 35, 36; 12:18-24) Japo ufalme huo wa Yuda ulianguka kwa Wababiloni katika 607 K.W.K., haki ya kisheria ya kutawala hatimaye ilipitishwa kwa mrithi aliye na haki, Yesu Kristo, “mwana wa Daudi.” (Mt 1:1-16; Lu 1:31, 32; linganisha Eze 21:26, 27.) Ufalme wake ulikuwa uwe usio na mwisho.—Isa 9:6, 7; Lu 1:33.
Tengenezo la kifalme lilisitawi katika Israeli ili lisimamie katika kutekeleza masilahi ya ufalme huo. Lilijumlishwa na jopo la washauri wenye kuaminika na mawaziri wa nchi (1Fa 4:1-6; 1Nya 27:32-34), na vilevile idara mbalimbali za serikali zenye waangalizi wa kusimamia utekelezaji katika nchi za dola hiyo, kusimamia uchumi, na kuandaa mahitaji ya mahakama ya kifalme.—1Fa 4:7; 1Nya 27:25-31.
Ingawa wafalme wa Israeli katika mstari wa Daudi wangeweza kutoa maagizo hususa, mamlaka halisi ya kutunga sheria ilitegemea Mungu. (Kum 4:1, 2; Isa 33:22) Mfalme alikuwa na daraka katika mambo yote kumwelekea Mwenye Enzi kuu na Bwana halisi, Yehova. Ukosaji na upotovu kwa upande wa mfalme ungeleta adhabu za kimungu. (1Sa 13:13, 14; 15:20-24) Nyakati nyingine Yehova aliwasiliana na mfalme mwenyewe (1Fa 3:5; 11:11); nyakati nyingine alimpa maagizo na shauri au karipio kupitia manabii waliowekwa rasmi. (2Sa 7:4, 5; 12:1-14) Pia mfalme angeweza kupata shauri lenye hekima la baraza la wanaume wazee. (1Fa 12:6, 7) Hata hivyo, utekelezaji wa maagizo au karipio, haukutegemea manabii au wanaume wazee, bali Yehova.
Wakati mfalme na watu waliposhikamana kwa uaminifu na agano la Sheria walilopewa na Mungu, taifa la Israeli lilifurahia kiwango fulani cha uhuru wa kibinafsi, ufanisi wa kimwili, na upatano wa kitaifa usiopatikana katika falme nyinginezo. (1Fa 4:20, 25) Wakati wa ile miaka ya Sulemani kumtii Yehova, ufalme wa Israeli ulipata sifa na heshima iliyoenea sana, ukiwa na falme tanzu nyingi na kufaidika na rasilimali za nchi nyingi.—1Fa 4:21, 30, 34.
Ufalme wa Yehova Mungu ni wa enzi kuu ya ulimwengu mzima, ingawa kwa muda ulidhihirishwa kwa njia yenye kuonekana kwa muda kupitia ufalme wa Israeli. (1Nya 29:11, 12) Ufalme wake ni wa kudumu na hauwezi kubadilishwa, si kitu kama vikundi vya watu na falme za jamii ya wanadamu zitaukiri au la, nayo dunia yote ni sehemu ya milki ambayo ni haki yake. (Zb 103:19; 145:11-13; Isa 14:26, 27) Kwa msingi wa Yeye kuwa muumba, Yehova hufanya mapenzi yake mbinguni na duniani akiwa mwenye enzi kuu, kulingana na makusudi yake mwenyewe, akiwa hawajibiki kwa yeyote (Yer 18:3-10; Da 4:25, 34, 35), lakini sikuzote akiwa anatenda kwa kupatana na viwango vyake mwenyewe vya uadilifu.—Mal 3:6; Ebr 6:17, 18; Yak 1:17.