Maswali Kutoka Kwa Wasomaji
● Mtume Paulo alikuwa na maana gani katika 2 Wakorintho 2:15, 16 alipojitaja mwenyewe na wenzake kuwa “harufu”?
Mtume Paulo aliandika hivi: “Sisi tu manukato ya Kristo, mbele za Mungu, katika wao wanaookolewa, na katika wao wanaopotea; katika hao wa pili harufu ya mauti iletayo mauti; katika hao wa kwanza harufu ya uzima iletayo uzima.”—2 Kor. 2:15, 16.
Tunaweza kuyafahamu maneno hayo vizuri zaidi tukifikiria mambo yaliyotukia wakati wa maandamano ya ushindi ya Warumi. Wakati jeshi lenye ushindi liliporudi na kupita katika mji wa Rumi kwa kuandamana, ubani ulichomwa (ukafukizwa) juu ya madhabahu za mahekalu na kueneza harufu nzuri hewani. Manukato ya ubani huo yalikuwa na maana mbalimbali kwa watu mbalimbali. Harufu hiyo ilikuwa nzuri kwa askari walioshinda vitani, ikawa na maana ya kwamba wangepata vyeo vyenye heshima, madaraka makubwa zaidi na mali. Lakini kwa mateka wasiosamehewa waliokusanywa pamoja waandamane katika barabara, ubani huo wenye kuchomwa uliwakumbusha kwamba wangeuawa baada ya maandamano. Vivyo hivyo, ujumbe uliohubiriwa na mtume Paulo pamoja na wenzake ulikuwa kama harufu yenye kuwapendeza walioukubali lakini ukawa harufu mbaya sana kwa walioukataa.