Maisha na Huduma ya Yesu
Kuvunja Masuke Siku ya Sabato
BAADA YA muda mfupi Yesu na wanafunzi wake wanaondoka Yerusalemu kurudi Galilaya. Ni wakati wa masika, na mashambani kuna masuke ya nafaka. Wanafunzi wana njaa. Kwa hiyo wanavunja masuke na kuyala. Lakini kwa kuwa ni Sabato, vitendo vyao havipiti bila kuonwa.
Viongozi wa kidini katika Yerusalemu walikuwa wamejaribu kumwua Yesu muda mfupi tu kabla ya hapo ikisemekana kwamba yeye alikuwa amekosa-kosa kufuata Sabato. Sasa, Mafarisayo wanaleta shtaka. “Tazama! Wanafunzi wako wanafanya neno ambalo si halali kulifanya siku ya sabato,” wao wanashtaki.
Mafarisayo wanadai kwamba kuvunja masuke na kuzifikicha zile punje mikononi, ili kuzila ni kuvuna na kuzipiga-piga. Lakini fasiri yao kali-kali juu ya kile ambacho ni kazi imefanya Sabato iwe mzigo, hali ilikusudiwa iwe wakati wa furaha, wenye kujenga kiroho. Kwa hiyo Yesu anapinga kwa kutumia mifano ya Kimaandiko kuonyesha kwamba Yehova Mungu hakukusudia kamwe sheria Yake ya Sabato itumiwe vikali-vikali hivyo bila sababu.
Walipokuwa na njaa, Yesu anasema, Daudi na watu wake walisimama kwenye hema takatifu, wakaila mikate ya wonyesho. Hata ingawa mikate hiyo ilikuwa tayari imekwisha kuondolewa mbele za Yehova na badala yake ikawekwa mipya, kwa kawaida ni makuhani waliowekewa waile. Hata hivyo, chini ya hali hizo, Daudi na watu wake hawakulaaniwa kwa sababu ya kuila.
Akitoa mfano mwingine, Yesu anasema: “Hamkusoma katika torati kwamba siku ya sabato makuhani hekaluni huinajisi sabato wasipate hatia? ” Ndiyo, hata katika siku ya Sabato makuhani wanaendelea kuchinja wanyama na kufanya kazi nyingine hekaluni wanapotayarisha dhabihu za wanyama! “Lakini nawaambieni,” Yesu anasema, “kwamba hapa yupo aliye mkuu kuliko hekalu.”
Akiwaonya Mafarisayo kwa upole, Yesu anaendelea: “Kama mngalijua maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka, msingaliwalaumu wasio na hatia.” Halafu anamalizia hivi: “Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato.” Yesu alimaanisha nini kwa kusema hivyo?
Yesu alikuwa akiutaja utawala wake wa Ufalme wenye amani wa miaka elfu moja. Kwa muda wa miaka 6,000 wanadamu wametoa jasho la utumwa wakiwa chini ya Shetani Ibilisi, wakawa wa kawaida na kupatwa na jeuri na vita. Kwa upande mwingine, ule utawala wa sabato kuu ya Kristo utakuwa wakati wa pumziko la kutokuwa na taabu na uonevu kama huo. Mathayo 12:1-8; Mambo ya Walawi 24:5-9; 1 Samweli 21:1-6; Hesabu 28:9; Hosea 6:6.
◆ Ni shtaka gani linalofanywa dhidi ya wanafunzi wa Yesu, naye Yesu analijibuje?
◆ Yesu anatambulisha kwamba Mafarisayo wanakosea katika jambo gani?
◆ Ni kwa njia gani Yesu ndiye “Bwana wa sabato”?