Imekuwaje Kwa Asili ya Kibinadamu?
“KWA nini muda huu wetu una ukatili kwa watoto? Kwa nini kuna ukatili kwa wanyama? Kwa nini kuna jeuri? . . . Kwa nini watu hufanya uvamizi-haramu? Kwa nini watu huanza kutumia dawa za kulevya? . . . Kwa nini, ukiisha kuwa na kila kitu, watu fulani hugeukia mambo hayo ya msingi ambayo hudhoofisha utamaduni wote?”
MASWALI hayo yaliulizwa kwa sauti kubwa na waziri mkuu wa Uingereza. Labda wewe umeuliza maswali kama hayo mara nyingi. Je! umepata majibu yoyote yanayoridhisha?
Akilenga shabaha ya maswali yake, waziri mkuu huyo alisema: “Kwa miaka kadhaa nilipokuwa mchanga na katika siasa nikiwa na matumaini yangu yote na ndoto na tamaa za kutazamia makuu, ilionekana kwangu na kwa wengi wa marika wangu kwamba kama tungepata muda ambapo tungekuwa na nyumba nzuri, elimu nzuri, kiwango kizuri cha maisha, hapo kila kitu kingekuwa tayari na sisi tuwe na wakati ujao ulio mzuri na rahisi zaidi. Sasa twajua kwamba sivyo ilivyo. Sisi twakumbana na matatizo halisi ya asili ya kibinadamu.”—Italiki ni zetu.
Asili ya kibinadamu yaweza kufasiliwa kuwa “mielekeo na tabia za msingi za wanadamu zenye ujumla wa hali nyingi.” Kwa wazi, mielekeo na tabia zenye kuhitilafiana zaweza kusababisha matatizo ya kibinafsi, ya kitaifa, au hata ya kimataifa. Lakini ni kwa kadiri gani hasa asili ya kibinadamu yalaumika kwa maelekeo hatari ya leo katika jeuri, uvamizi-haramu, ulanguzi wa dawa za kulevya, na mambo kama hayo?
Je! asili ya kibinadamu ndiyo tu ya kulaumika kwa hali ambazo zatisha ‘kudhoofisha utamaduni wote’? Au kuna mambo mengine tupaswayo kufikiria ili kufafanua kwa nini watu huelekea kwa urahisi kwenye mazoea ya ubinafsi yenye kushusha tabia, hali wangeweza kujitahidi sana kufikia mafuatio ya juu zaidi yenye ubora mwingi? Acheni tuone.