Mandhari Kutoka Bara Lililoahidiwa
Njoo Uzuru Bahari ya Galilaya!
NI MAHALI kuchache kukumbukwapo kwa urahisi na wasomaji wa Biblia kama Bahari ya Galilaya. Lakini je, ungeweza kufunga macho yako na kuona akilini bahari hiyo yenye maji yasiyo na chumvi, ukiweza kuona sehemu mbalimbali kuu, kama vile mahali ambako Mto Yordani huingia na kutokea au zilipo Kapernaumu na Tiberia?
Chukua wakati kujifunza picha iliyo chini iliyochukuliwa kutoka angani, ukilinganisha nambari zilizo kando. Wewe waweza kutambulisha sehemu ngapi zenye nambari? Kadiri uzijuavyo, ndivyo Biblia yako itakavyokuwa hai na yenye maana. Kwa kusudi hilo, njoo ufanye ziara fupi, yenye kuarifu.
Picha hii iliyochukuliwa kutoka angani ni kuelekea kaskazini-mashariki. Acheni tuanze na #1. Hiyo ni sehemu gani ya bahari? Naam, ncha ya kusini, ambako Yordani hutokea, ukielekea chini kati ya Samaria na Gileadi kutiririka kuingia Bahari ya Chumvi. Kueleka kushoto unaona ncha hiyo ya bahari kwa ukaribu zaidi, inayoonyeshwa pia katika 1993 Calendar of Jehovah’s Witnesses.
Bahari ya Galilaya imo ndani sana katika Bonde la Ufa, karibu meta 200 chini ya Bahari ya Mediterania. Unapochunguza picha hiyo iliyochukuliwa kutoka angani, tazama milima inayoinuka kutoka ufuo wayo wa mashariki (karibu na #7). Vilima na milima inainuka pia kutoka ufuo ulio karibu zaidi, au wa magharibi, hilo likikazia kwamba bahari hiyo imo katika kibonde, bahari ikiwa na urefu wa karibu kilometa 21 na upana ufikao upeo wa kilometa 12. Fuo zilikuwa na nafasi kwa ajili ya vijiji na hata majiji, kama vile Tiberia (#2). Kumbuka kwamba umati kutoka Tiberia ulivuka bahari hiyo katika mashua hadi mahali ambako Yesu alikuwa amewalisha 5,000 kimuujiza.—Yohana 6:1, 10, 17, 23.
Usongapo kando ya mwambao kuelekea kaskazini kutoka Tiberia, wapita mkoa wenye rutuba wa Genesareti (#3).a Yesu alitoa yale Mahubiri ya Mlimani katika eneo hilo, na yaelekea kwamba kwenye ufuo ulio karibu, ndiko alimwita Petro na wengine watatu wawe “wavuvi wa watu,” kama ionyeshwavyo hapa. (Mathayo 4:18-22) Ukiendelea kusafiri, wafikia Kapernaumu (#4), lililokuwa kitovu cha utendaji mbalimbali wa Yesu, hata likarejezewa kuwa ‘jiji la kwake.’ (Mathayo 4:13-17; 9:1, 9-11; Luka 4:16, 23, 31, 38-41) Ukiendelea kuelekea mashariki kuzunguka bahari, wavuka (#5) mahali Yordani wa juu zaidi hutiririka kuingia baharini (chini). Kisha wafikia eneo la Bethsaida (#6).
Hata twaweza kutumia sehemu hizo chache kutoa kielezi juu ya jinsi ujuzi wako kuhusu Bahari ya Galilaya waweza kukusaidia ufuate, na kuona akilini, masimulizi ya Biblia. Baada ya Yesu kuwalisha wale 5,000 katika eneo la Bethsaida na umati ukajaribu kumfanya mfalme, yeye aliwatuma mitume kwa mashua kuelekea Kapernaumu. Katika safari yao, pepo za dhoruba zilikuja chini kutoka milimani kwa ghafula na kuumua mawimbi, hilo likiogofya mitume. Lakini Yesu aliwajia akitembea juu ya bahari, akatuliza dhoruba hiyo, na kuwawezesha kushuka Genesareti wakiwa salama. (Mathayo 14:13-34) Wale waliotoka Tiberia walivuka kwenda Kapernaumu tena.—Yohana 6:15, 23, 24.
Ukiendelea kuzunguka upande wa mashariki wa bahari, wapita ile ambayo yaelekea iliitwa “nchi ya Wagerasi [au, Wagadarene].” Kumbuka kwamba hapa Yesu aliondosha roho waovu kutoka kwa wanaume wawili. Hao roho waliingia kikatili katika kundi kubwa la nguruwe, lililotelemka kwa kasi gengeni likaingia baharini. Baadaye mmoja wa wanaume hao alitoa ushahidi katika majiji ya karibu ya Dekapoli yenye kusema Kigiriki. Yesu aliwasili na pia kuondoka eneo hilo kwa mashua akivuka Bahari ya Galilaya.—Mathayo 8:28–9:1; Marko 5:1-21.
Umalizapo ziara yako kuelekea ncha ya chini zaidi ya bahari, wapitia karibu na mahali ambapo mto mkuu (uitwao Yarmuk) huleta maji mengi kwenye Mto Yordani wa chini zaidi.
Biblia haitaji mahali hususa ambapo mambo fulani yalitukia karibu na Bahari ya Galilaya, kama vile kule kutokea kwa Yesu baada ya ufufuo wakati Petro na wale mitume wengine walipokuwa wakivua samaki (chini). Je! wewe wafikiri ilikuwa karibu na Kapernaumu? Kwa vyovyote, ujuzi wako kuhusu bahari hiyo ya maana wakusaidia uone akilini uwezekano huo.
[Maelezo ya Chini]
a Ona makala “Genesareti—‘Nzuri Ajabu na Yenye Kupendeza’” katika Mnara wa Mlinzi la Januari 1, 1992.
[Picha katika ukurasa wa 24]
1
2
3
4
5
6
7
N
S
E
W
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24, 25]
Garo Nalbandian
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.