Utiaji-Damu Mishipani Wafikiriwa Tena
KATIKA kipindi hiki cha kusikitisha cha UKIMWI, tisho kubwa zaidi la afya ya mgonjwa akiwa hospitalini laweza kuwa katika chumba cha upasuaji. “Hakuna njia iwezekanayo tuwezayo kufanya ugavi wa damu uwe bila viini vya magonjwa kabisa,” asema Dakt. Richard Spence, ambaye kwa zaidi ya mwongo mmoja ameongoza Kitovu cha Upasuaji Bila Damu katika Cooper Hospital-University Medical Center katika Camden, New Jersey, Marekani.
Basi haishangazi kwamba kitovu hicho cha kitiba hutibu Mashahidi wa Yehova wengi, ambao kukataa kwao kutiwa damu mishipani kwa msingi wa Biblia kwajulikana sana. (Mambo ya Walawi 17:11; Matendo 15:28, 29) Hata hivyo, wagonjwa kadhaa ambao si Mashahidi pia huenda huko kutibiwa, wakihangaishwa na hatari ziwezekanazo za kutiwa damu mishipani, ambazo zinatia ndani kuambukizwa mchochota wa ini, UKIMWI, na maradhi mengineyo. “Kuongezeka kwa UKIMWI kumeonyesha uhitaji wa kuchuja damu,” yasema Courier-Post Weekly Report on Science and Medicine. “Lakini viini fulani vyaweza kupita mfumo wa mchujo kwa sababu mtu fulani aweza kuwa na virusi kabla ya kugunduliwa wakati wa kupima.”
Kwa sababu ya hatari kama hizo, Kitovu cha Upasuaji Bila Damu hutumia vibadala vya utiaji-damu mishipani, kutia ndani kutumia chombo cha kuzungushia damu ya mgonjwa nje ya mwili—njia ambayo Mashahidi fulani waweza kuikubali chini ya hali fulani.a Tiba nyingine inahusu matumizi ya dawa ambazo zinachochea kuongezeka kwa damu ya mgonjwa. Kuongezea hilo, vibadala vya damu vilivyotengenezwa mara kwa mara hutumiwa kusaidia kupata oksijeni bila uhitaji wa kutia damu. “Mashahidi wa Yehova wanataka utunzaji bora zaidi wa kitiba,” asema Dakt. Spence, “lakini wanataka vibadala wala si utiaji damu mishipani.”
Mashahidi wa Yehova ni wenye shukrani kwa ushirikiano na msaada ambao wamepokea kutoka kwa madaktari wanaoheshimu masadikisho yao ya kidini. Kama tokeo, kwelikweli wamepokea “utunzaji bora zaidi wa kitiba” nao wamedumisha dhamiri safi mbele ya Yehova Mungu.—2 Timotheo 1:3.
[Maelezo ya Chini]
a Mazungumzo zaidi ya njia hiyo na mambo yanayohusika katika kufanya uamuzi wa kibinafsi kulingana na dhamiri yako mwenyewe yanaonyeshwa katika Mnara wa Mlinzi wa Machi 1, 1989, kurasa 30-31.