Hofu—Ni Rafiki au Adui?
“Nafikiria jinsi ninavyotaka kufa. Sitaki kupigwa risasi, lakini nikipigwa, nataka nipigwe risasi hapa kichwani, ili nife papo hapo.”
RIPOTA mmoja wa Los Angeles Times alisikia maneno hayo kutoka kwa msichana mwenye umri wa miaka 14. Alikuwa akipata maoni ya wanafunzi kuhusu mauaji ya majuzi—vijana wakiua watu wazima na vijana wengine. Ripoti hiyo iliitwa: “Ulimwengu wa Hofu.”
Bila shaka unajua kwamba wengi wanaishi kwa hofu. Hofu ya nini? Ni vigumu kutaja hofu moja hususa. Ona kama unaweza kupata katika sanduku lifuatalo mambo ambayo marafiki wako au watu wengi katika eneo lenu wanahofu. Sanduku hili limetoka katika Newsweek la Novemba 22, 1993, nalo laonyesha matokeo ya mahoji ya “watoto 758 wenye umri wa kati ya miaka 10 na 17, pamoja na wazazi wao.”
Vijana hao wangalihojiwa sasa, wangalitaja sababu nyingine zaidi za kutokeza hofu, kama vile matetemeko ya dunia. Baada ya tetemeko lenye msiba mkubwa katika Los Angeles katika Januari 1994, Time liliripoti: “Miongoni mwa dalili za mkazo wa akili wa baada ya kupatwa na msiba mna ugonjwa wa kumbukumbu za misiba iliyopita zisizoweza kudhibitiwa, ndoto za kuogofya, kutahadhari kupita kiasi na hasira inayotokana na kutoweza kudhibiti maisha yako mwenyewe.” Mfanya biashara mmoja aliyekuwa ameamua kuhama eneo la tetemeko alisema: “Uharibifu si kitu. Ni woga-mkuu ulio mbaya. Waenda kulala katika chumba cha chini ukiwa umevalia viatu. Hupati usingizi. Kila usiku, unaketi tu hapo ukingojea tetemeko litokee. Ni hali mbaya sana.”
“Mfululizo wa Misiba Wawatia Wajapani Wasiwasi” ndicho kilikuwa kichwa cha ripoti moja kutoka Tokyo ya Aprili 11, 1995. Ripoti hiyo ilisema: “Lile shambulizi la gesi ya neva . . . hasa lilikuwa pigo kubwa kwa Wajapani kwa sababu lilikuja likiwa sehemu ya mfululizo wa matukio ambayo kwa ujumla yalitokeza chanzo cha wasiwasi mpya kuhusu wakati ujao. . . . Watu hawahisi usalama tena wakiwa katika barabara ambazo zamani zilijulikana sana kuwa salama mchana au usiku.” Na si wazee-wazee tu ambao wana hofu. “Profesa Ishikawa [wa Chuo Kikuu cha Seijo] alisema hangaiko hilo . . . lilionekana hasa miongoni mwa vijana, ambao mara nyingi hawajui vizuri jinsi wakati ujao utakavyokuwa.”
Uthibitisho waonyesha kwamba “pindi moja tu ya ogofyo kubwa yaweza kubadili utendaji wa kikemikali wa ubongo, ikifanya watu wawe wenye kusisimka upesi zaidi hata miongo mingi baadaye.” Wanasayansi wanajaribu kuelewa jinsi ubongo hufasiri hali ya kuhofisha—jinsi tunavyochanganua mambo mbalimbali na kuitikia kwa hofu. Profesa Joseph LeDoux aliandika: “Kwa kugundua njia za neva zinazotokeza hali zinazofanya kiumbe kijue hofu, twatumaini kufafanua utendaji wa ujumla wa kumbukumbu hiyo.”
Lakini wengi wetu hawajali sana chanzo cha kikemikali au neva kinachosababisha hofu. Kwa kufaa twaweza kupendezwa na majibu ya maswali kama, Kwa nini tunaogopa? Tuitikieje? Je, hofu yoyote ni nzuri?
Labda unakubali kwamba nyakati nyingine hofu inaweza kukusaidia. Kwa mfano, wazia ni wakati wa giza ukaribiapo nyumba yako. Mlango u wazi kabisa, ingawa uliufunga kabisa. Kupitia dirishani unaona kama kuna vitu vyeusi-vyeusi vikisonga-songa. Unashtuka, ukishuku sana kwamba kuna kitu. Labda mwizi au mtu aliye na kisu yumo humo.
Hofu yako ya kiasili juu ya hali hizo yaweza kukusaidia usitumbukie hatari bila kujua. Hofu inaweza kukusaidia kutahadhari au kupata msaada kabla ufikie hali iwezayo kukudhuru. Kuna mifano mingi kama hiyo: ishara inayokuonya juu ya umeme wenye nguvu nyingi; tangazo la redio juu ya dhoruba inayoelekea eneo lenu kwa kasi; kelele kali ya vyuma kutoka kwa gari lako unapoliendesha katika barabara yenye magari mengi mno.
Katika visa vingine hofu fulani yaweza kuwa rafiki. Inaweza kutusaidia kujilinda au kutenda kwa hekima. Hata hivyo, unajua vizuri kwamba ile hofu ya kila wakati na yenye kudumu si rafiki kamwe. Ni adui. Inaweza kutokeza hali ya kupumua kwa kasi, mipigo ya haraka na nguvu ya moyo, kudhoofika, kutetemeka, kujihisi kutapika, na kutopenda eneo lako.
Unaweza kupata kuwa jambo la kupendeza kwamba Biblia ilisema kihususa kwamba wakati wetu ungekuwa na matendo yenye kuhofisha duniani na pia kuwa na hofu kuu. Kwa nini iwe hivyo, nayo iathirije maisha yako na mawazo yako? Pia, kwa nini inaweza kusemwa kwamba kutokana na maoni ya Biblia, kuna hofu ya kila siku ambayo hasa ni yenye kusaidia na ni nzuri? Ebu tuone.
[Sanduku katika ukurasa wa 3]
Wakiulizwa ni mambo yapi yanayowahangaisha zaidi na familia zao, watu wazima na watoto husema wanahofu:
WATOTO WAZAZI
56% Uhalifu wa jeuri dhidi ya washiriki wa familia 73%
53% Mtu mzima kupoteza kazi 60%
43% Kutoweza kununua chakula 47%
51% Kutoweza kugharamia daktari 61%
47% Kutoweza kugharamia makao 50%
38% Mshiriki wa familia kuwa na tatizo la dawa ya kulevya 57%
38% Familia yao haitaishi pamoja 33%
Chanzo: Newsweek, Novemba 22, 1993