Fahari ya Uumbaji wa Yehova
“Mali Nyingi ya Bahari”
WAKATI wa machweo ya jua, upepo mtulivu husukuma maji kwenye uso wa bahari, nayo mawimbi huupiga ufuo wa bahari. Sauti yenye kutuliza ya mawimbi hayo huwavutia sana watu wengi ambao huenda kwenye ufuo ili kupata pumziko na utulivu.a
Fuo kama hizo zenye urefu wa maelfu ya kilometa, hupatikana katika kanda za pwani duniani pote. Mipaka hiyo ya mchanga ambayo hubadilika daima hudhibiti maji ya bahari. Hivyo ndivyo Muumba alivyopanga mambo. Akizungumza juu yake mwenyewe, Mungu anatangaza kwamba ‘ameweka mchanga kuwa mpaka wa bahari.’ Anaongeza kusema: “Ingawa mawimbi yake husukasuka, bado hayawezi kushinda; na ingawa huchafuka, bado hayawezi kuuvuka.”—Yeremia 5:22; Ayubu 38:8; Zaburi 33:7.
Kwa kweli, katika mfumo wa jua, sayari yetu ndiyo tu ambayo sehemu yake kubwa imefunikwa na maji. Zaidi ya asilimia 70 ya sayari yetu imefunikwa na maji. Yehova alipokuwa akitayarisha dunia iwe makao ya wanadamu, aliagiza hivi: “Maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, nayo nchi kavu ionekane.” Na “ikawa hivyo.” Masimulizi hayo yanaongeza kusema: “Mungu akaanza kuiita hiyo nchi kavu Dunia, lakini mkusanyiko wa maji akauita Bahari. Kisha Mungu akaona ya kuwa ilikuwa vyema.” (Mwanzo 1:9, 10) Bahari ina manufaa gani?
Maji ya bahari hutegemeza uhai katika njia nyingi zenye kutokeza. Kwa mfano, maji yana uwezo wa kuhifadhi joto. Hivyo, bahari huhifadhi kiasi kikubwa cha joto, jambo ambalo husaidia kusawazisha hali ya hewa wakati wa baridi kali.
Maji pia yana uwezo mwingine wa kutegemeza uhai. Yanaweza kuyeyusha kwa urahisi vitu vingi zaidi kuliko umajimaji mwingine wowote. Kwa kuwa taratibu nyingi zinazohusu uhai huwezekana kupitia utendanaji wa kemikali, maji ni ya lazima ili kuyeyusha kemikali hizo na kuungana na molekuli zao ili kufanyiza mchanganyiko fulani. Michanganyiko mingi ya kemikali ambayo hupatikana katika chembe-chembe zilizo hai huwa na maji. Kitabu The Sea kinasema: “Vitu vyote vilivyo hai vinahitaji maji—ambayo mwishowe lazima yatoke baharini, kwa ajili ya mimea na wanyama wanaoishi katika nchi kavu.”
Bahari zilizo duniani pia hufanya kazi muhimu ya kusafisha angahewa. Mimea midogo ya baharini hufyonza kaboni monoksidi na kutoa oksijeni. Kulingana na mtafiti mmoja, “mimea midogo ya baharini huongeza asilimia 70 ya oksijeni kila mwaka kwenye angahewa.”
Pia bahari zinaweza kutokeza dawa za asili za kutibu magonjwa. Kwa miaka mingi, sehemu fulani za samaki zimetumiwa kama dawa. Wanadamu wametumia mafuta ya ini la chewa kwa muda mrefu. Hivi karibuni, kemikali za samaki na viumbe wengine wa baharini zimetumiwa kutibu ugonjwa wa pumu na kupigana na virusi na kansa.
Jitihada zimefanywa ili kukadiria manufaa ya kiuchumi ya vitu vinavyotoka baharini. Ingawa hatuwezi kufikia mikataa iliyo sahihi, watafiti wamekadiria kwamba karibu thuluthi mbili za chakula na bidhaa nyingine zinazotokana na mimea na wanyama hutoka baharini. Jambo hilo huthibitisha ukweli wa kwamba bahari ziliumbwa kwa kusudi fulani, yaani, kutimizia mahitaji ya viumbe na kutegemeza uhai. Kwa kweli, kusudi hilo linapatana na kile ambacho Biblia hukiita “mali nyingi ya bahari”!—Kumbukumbu la Torati 33:19.
Yehova anatukuzwa kuwa Mbuni Mkuu na Mfanyi wa mali hiyo. Nehemia alichochewa kumsifu kwa maneno yafuatayo: “Wewe peke yako ndiye Yehova; wewe mwenyewe umezifanya mbingu, . . . bahari na vyote vilivyomo; nawe unavihifadhi vyote hai.”—Nehemia 9:6.
[Maelezo ya Chini]
a Ona Kalenda ya Mashahidi wa Yehova ya 2004, Septemba/Oktoba.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]
Maji, Upepo, na Mawimbi
Maji na upepo hufanyiza mawimbi makubwa ambayo hupiga miamba kwa kishindo, kama haya ya California, Marekani. Sikuzote, mawimbi yamekuwa sehemu yenye kushangaza ya bahari, yakionyesha nguvu zake. Pia hutukumbusha nguvu kubwa sana na za kushangaza za Muumba. Yehova ndiye ‘anayeyakanyaga mawimbi makubwa ya bahari.’ “Kwa uwezo wake ameichochea bahari, naye kwa uelewaji wake amemvunja vipande-vipande yule mshambuliaji.” (Ayubu 9:8; 26:12) Kwa kweli, “juu ya sauti ya maji mengi, mashuu [“mawimbi,” Union Version] makubwa ya bahari, Yehova ni mwenye fahari katika kilele.”—Zaburi 93:4.
Mchanga Wenye Maumbo Mbalimbali
Pindi kwa pindi, ufuo wa bahari ni sehemu yenye mchanga wenye maumbo mbalimbali yenye kuvutia, kama rundo hili la mchanga kwenye pwani ya Namibia, kusini mwa Afrika. Upepo ndio nguvu hasa ambayo hufanya mchanga uwe na miundo mbalimbali. Ingawa huenda marundo fulani yakaonekana kuwa madogo tu, mengine huwa na kimo cha meta 400. Kiasi hicho kikubwa cha mchanga hutusaidia tuelewe usemi huu wa Biblia, “chembe za mchanga zilizo kando ya bahari.” Unatumiwa kuonyesha kitu fulani kisichoweza kuhesabiwa, ambacho ni vigumu kukipima. (Mwanzo 22:17) Sisi hustaajabu mbele za Muumba ambaye aliumba kwa ustadi kingo za mchanga zinazozuia mawimbi ya bahari.
[Picha katika ukurasa wa 9]
Pwani ya machweo ya jua, Ghuba ya Biafra, Kamerun