Vijana Wauliza . . .
Ni Nini Siri ya Kuchagua Nguo Zifaazo?
MIKE ajua jinsi ya kuchagua mavazi bora—na jinsi ya kuyapata kwa bei nzuri. Nyakati fulani washiriki wa jamaa yake hata humwomba akawanunulie! Katika safari moja ya ununuzi, alichagua mavazi ya mama yake, ya dada yake aliyeolewa, na mpwa wa kike mwenye miaka minane—ya saizi ifaayo na staili walizotaka! Alipokuwa akifanya hivyo, alijichagulia joho la kuogea kwa robo ya bei ya kawaida. Kwa Mike, hiki hakikuwa kibarua kigumu bali raha halisi.
Labda wewe huna shauku ya Mike kwa ajili ya ununuzi. Lakini kama vijana walio wengi, labda wewe wataka kuonekana vizuri kabisa shuleni, kazini, na mchezoni. Tatizo ni kwamba, uhakika tu wa kwamba staili fulani hufikiriwa kuwa ya kisasa miongoni mwa vijana haimaanishi yafaa kuvaliwa, wala kununua “mtindo wa kisasa” siko kwa lazima utumizi bora zaidi wa pesa zako. Kwa hiyo, kwa kuchukulia kwamba wazazi wako wanakuruhusu uwe na uhuru wa kuchagua nguo zako mwenyewe, hapa pana vidokezi vichache juu ya jinsi ya kuchagua na kununua nguo zifaazo.
Kuchagua “Vazi” Lifaalo
Kwanza, acheni tuondolee mbali wazo la kwamba nguo ni nguo hata iweje. Wewe unasonga mbele katika umri, na matazamio ya kutafuta riziki na kutegemeza jamaa yanajongelea mbele yako. Njia yako ya kuvaa itaathiri si matazamio yako ya kuajiriwa kazi tu bali pia jinsi utaonwa na kutendewa na wengine. La maana zaidi, sisi Wakristo ‘hatupaswi kuwa tukijipendeza wenyewe,’ bali twapaswa kuhangaikia jinsi kitu kile tufanyacho—au tuvaacho—kitaathiri wengine.—Warumi 15:1.
Mithali 25:20 yanena juu ya mtu “avuaye nguo wakati wa baridi.” Ni jambo lisilofaa kama nini! Kwa njia sawa na hiyo haifai kuvaa vazi la kistaili ambalo halifai pindi ile. Mwigizaji katika mchezo wa jukwaani huchagua kwa uangalifu vazi la kufaa sehemu yake. Na katika maisha halisi, mara nyingi sehemu ambazo sisi hushiriki hutaka “mavalio” tofauti. Kwa kielelezo, je! unaenda ukahojiwe kuhusu kazi? Basi huenda suti ya kibiashara ikawa ndilo vazi lifaalo. Je! unaenda shuleni? Basi huenda ukataka kuwa na mtazamo wa kikawaida tu hata hivyo ulio nadhifu.
Millie, mmoja wa Mashahidi wa Yehova, alihudhuria shule ambako jeuri ilikuwako kwa wingi. Kuvaa kana kwamba anaenda kwenye mkutano wa Kikristo kungalifanya atokeze mno. Kwa hiyo msichana huyo alivaa surualijini yenye kiasi wakati wa saa za shule, kwa maana ilikubaliwa kwenye shule yao. Lakini kwa kuwa yeye alijihusisha katika kazi ya elimu ya Biblia baada ya masomo, alienda akiwa na rinda refu. Kubadilika kwa shughuli kwataka mavazi yabadilishwe.
Vijana miongoni mwa Mashahidi wa Yehova hufikiria kihususa mavazi yao kwenye mikutano ya Kikristo na katika kazi yao ya kuhubiri peupe. Kwa kielelezo, surualijini na viatu vya michezo, ambavyo huenda vikatumika vema kabisa shuleni, havifai wakati wa ibada rasmi; huondoa ustahili wa dai la mtu kuwa ni mhudumu wa Mungu.—Linganisha 2 Wakorintho 6:3.
Thamani ya Kuvaa Kizamani
Falsafa ya kijana Rudy kuhusu nguo huenda ikakushangaza. Mvulana huyo asema hivi: “Mimi napenda aina ya nguo ambazo watu wamekuwa wakivaa kwa miaka 50 iliyopita.” Je! ni kuwa na mitindo ovyo ya kikale? Hata kidogo. Rudy alikuwa amejifunza kwamba ingawa ‘tamasha ya ulimwengu huu inabadilika,’ staili za msingi hubadilika mara chache. (1 Wakorintho 7:31, NW) Kawaida yake ni kwamba: Usivae chochote ambacho ni kimamboleo sana hivi kwamba karibuni kitakuwa kimambokale! “Kwa njia hii, sikuzote unakuwa katika staili,” Rudy ashauri.
Wastadi waafikiana juu ya hilo. Kwa kielelezo, Mshauri Amelia Fatt asema kwamba mishono ya kizamani ni “akiba bora.” Haiwi ya kikale upesi kwa sababu haionekani kuwa na mwundo hususa sana. Manufaa ya ziada ni kwamba kwa kawaida huwa rahisi zaidi kuratibu staili za kizamani na mavao yako mengine.
Staili fulani za ki-siku-hizi haziwafai Wakristo. Nyingine hupendeza. Ikiwa wazazi wako hukubali, ukiona kwamba kitu fulani cha kistaili si kwamba chaonekana vizuri tu ukikivaa bali pia chapatana na mavazi yako mengine, huenda ikafaa ufikirie kukivaa. Lakini tahadhari usiwe mtumwa wa mitindo! Carole Jackson mshauri juu ya mitindo aonelea hivi: “Ukifuata mielekeo ya mitindo ili uwe ‘mmamboleo,’ hata wakati ambapo mwelekeo wa sasa haukufai wewe, unajidanganya mwenyewe.”
Kuna faida nyingine za kuwa wa kizamani katika mavazi. Wanawake fulani vijana huona kwamba kufanya hivyo huvunja moyo kusumbuliwa kingono shuleni na mahali pa kazi. Zaidi ya hilo, kijana ambaye hushikamana na staili ambazo zimekuwapo muda wote ataelekea zaidi kuonwa na wengine kuwa mkomavu, mwenye imara, wala si mwenye kutupwatupwa huku na huku na kila upepo wa mvalio na mtindo.
Kwa kielelezo, Tammy ni mwanamke kijana anayetumikia akiwa mwevanjeli wa wakati wote. Ingawa kawaida ya mahali aishipo ni kuvaa mavazi mafupi sana, yeye asema, “Urefu ambao hunistarehesha mimi ni chini ya goti kidogo.” Hiyo yalingana na kiasi cha Kikristo. (1 Timotheo 2:9) Bila shaka, viwango vya kiasi vyatofautiana sehemu zote za ulimwengu. Na ukiwa na shaka kama staili fulani yafaa au sivyo, ongea na mzazi au rafiki mwenye umri mkubwa zaidi.
Ununuzi wa Kuvutia
“Kwa mwelekezo stadi endesha vita yako,” yashauri Biblia kwenye Mithali 20:18, NW. Mwelekezo stadi watakwa hata katika mambo ya kimwili kama ununuzi. Kwa kielelezo, je! wewe una ugumu kupata nguo zenye kukuongezea uvutio? Waweza kupata mwelekezo stadi kwa kwenda kwenye maktaba ya watu wote na kufanya utafiti fulani! Kuna vitabu na makala ambazo zaweza kukusaidia utumie mishono, rangi, na staili tofauti za nguo ili zisawazishe matatizo ya umbo la uso, urefu wa shingo, umbo la mwili, na kadhalika.
Namna gani ubora wa mavazi ununuayo? Ingawa Yesu Kristo alikuwa maskini sana kimwili alipokuwa duniani, kwa wazi alivaa vazi la ubora wa juu sana hivi kwamba wenye kumwua walipiga kura kuhusu nani angelitwaa! (Yohana 19:23, 24) Vivyo hivyo, wewe wapaswa ujitahidi kushikamana na mavazi yenye ubora, hata ikiwa pesa zako ni kidogo na walazimika kuweka akiba kabla ya kununua. Baada ya muda mrefu, vazi bora la gharama kubwa zaidi ambalo utatumia kwa miaka mingi huenda likawa la bei rahisi kuliko “vazi la bei ya chini linalokaa” muda mfupi.
Waweza kusitawishaje jicho la kuona ubora? Jaribu kuangalia-angalia katika maduka ya bei kubwa zaidi yaliyo na utaalamu wa mavazi bora. Pata kujua jinsi nguo nzuri zilivyo kwa kuonekana na kwa kuzigusa. Chasema hivi kitabu Elegance: “Usiongozwe na jina fulani; ni lazima nguo istahili yenyewe . . . Hali yenye uhafifu, hata kama ina chapa gani ya watengenezaji, si ununuzi mzuri wa bei ya chini.” Kiguse kitambaa chenyewe. Kagua ukosi, bitana, na matundu ya vifungo. Tafuta uone kama ina mshoneleo wa kuiimarisha.
Mike (aliyetajwa pale mwanzoni) amesitawisha jicho la kuona ubora. Hivyo, yeye alitambua kwamba joho la kuogea lililopunguzwa bei kwa kweli lilikuwa ununuzi mzuri wa bei ya chini! Hata hivyo, “usitongozwe na ‘vipunguzwabei,’” Amelia Fatt aonya. Sweta moja ya bei kamili iwezayo kuvaliwa na mavazi yako kadhaa huenda ikakutumikia zaidi ya sweta ‘iliyopunguzwa bei,’ isiyolandana na kitu chochote. Mithali 21:5 husema hivi: “Kila mmoja mwenye haraka-haraka kwa uhakika huelekea kwenye shida.” (NW) Epuka kununua uwapo na haraka. Fanya ununuzi wakati ambapo maduka hayakusongamana watu. Ujue mapema unatafuta nini. Kadiri uzidivyo kufikiria aina ya kitambaa, staili, rangi, na bei utakayo, ndivyo utakavyoelekea zaidi kutovutwa fikira kando kununua kitu usichohitaji kweli kweli.
Makarani fulani wa maduka waweza kuwa msaada mkubwa ukitaja mahitaji yako hususa. (Kwa kweli, ni kwa msaada wa bibimwuzaji mmoja kwamba Mike aliweza kuwanunulia nguo washiriki wa kike wa jamaa yake.) Lakini usiache wauzaji wakurairai utende dhidi ya uamuzi wako bora. “Mjinga [asiye na ujuzi, NW] huamini kila neno; bali mwenye busara huangalia sana aendavyo.”—Mithali 14:15.
Uwe umevaa na kujipamba ifaavyo wakati ufanyapo ununuzi. Wawezaje kujua kama jaketi ya suti yaonekana vizuri ukiijaribu juu ya T-shati? Au wawezaje kuamua kama gauni au rinda lakuongezea uvutio ikiwa umevaa viatu vya michezo? Mwandikaji mmoja hata adai kwamba ukiwa umevalia kizembe, wauzaji huelekea “kuchukulia kwamba wewe ni mtu asiyejua sana vinavyovutia na/au huna pesa za kutumia,” nao watakaza fikira juu ya wanunuzi wengine.
Mwisho, huenda ukaona kwamba mara nyingi “afadhali kuwa wawili kuliko mmoja” wakati wa ununuzi. (Mhubiri 4:9) Rafiki au mzazi aweza kukuambia jinsi vazi laonekana kutoka nyuma, kama limelegea mno, limebana mno, au halina kiasi kwa njia fulani nyingine.
Mambo Yaliyo ya Maana Zaidi
Kwenye Wafilipi 1:10, NW, Wakristo wahimizwa ‘wahakikishe mambo yaliyo ya maana zaidi.’ Mambo yaliyo ya maana kweli kweli katika maisha hutegemea kuwa na maarifa juu ya Mungu—si nguo. Kwa kuhuzunisha, huenda vijana fulani wakavaa kwa njia bora kabisa lakini wawe ni wazembe katika uwezo wao wa kufanya julisho la peupe la imani yao.
Kwa hiyo ingawa ni vizuri kuwa mnunuzi stadi na kuonekana mwenye sura nzuri kwa kadiri ambavyo fedha zako zaruhusu, kaza fikira juu ya kuwa Mkristo mkomavu. Jifunze kutimiza daraka hilo, na kuvaa kulingana nalo kutakuja kiasili.
[Picha katika ukurasa wa 18]
Nguo za mitindo-mitindo upesi zinakuwa si za kistaili. Staili za kizamani zinazofaa shughuli mbalimbali huelekea kudumu