Bei ya Udanganyifu?
MAFIGO ya Casey Lunsford yalikuwa yanashindwa kufanya kazi. Madaktari walikadiria kwamba mvulana huyo wa miaka mitatu na nusu angeishi miezi mingine mitatu au minne kama asingepachikwa figo nyingine. Wazazi wake, ambao walikuwa Mashahidi wa Yehova, walifanya uamuzi wenye kupendelea upasuaji huo; kwa kweli, baba ya Casey alikuwa achangie mvulana huyo moja la mafigo yake mwenyewe.a Takwa lao moja tu lilikuwa kwamba damu yoyote isitumiwe—Mashahidi wa Yehova hukataa kutiwa damu mishipani kwa sababu za Kimaandiko.—Ona Matendo 15:20.
Akina Lunsford walipanga mipasuo hiyo ifanywe katika hospitali moja ya Texas iliyojulikana kuwa yenye kufanikiwa katika upachikaji wa mafigo bila ya kutia damu mishipani. Lakini hospitali moja kilometa chache tu kutoka nyumbani kwa akina Lunsford katika California ilikuwa tayari kufanya upachikaji huo bila ya kutia damu mishipani. Akina Lunsford walichagua hospitali hiyo ya karibu zaidi.
Katika juma lililotangulia upasuaji huo, wafanya kazi wa hospitali na daktari wa upasuaji wa upachikaji walirudia-rudia kuhakikishia wazazi kwamba hakungekuwako uhitaji wa kutiwa damu mishipani au agizo la mahakama lenye kutoa ruhusa ya kufanya hivyo kinyume cha makatao ya wazazi. Hata hivyo, mara tu baada ya upasuaji, daktari huyo wa upasuaji alipanga kupata agizo la mahakama lenye kulazimisha damu atiwe Casey. Hata alifaulu kufanya mfanya kazi mmoja wa ujamii aondolewe aliposisitiza kwamba wazazi walikuwa na haki ya kujua juu ya agizo lolote la mahakama. Asubuhi ile ya upasuaji, hospitali hiyo ilijaza hati yenye kuomba mahakama agizo la kutia Casey damu mishipani. Hati hiyo ilifanya ionekane kama kwamba Casey alikuwa akivujwa na damu wakati huo kwenye meza ya upasliaji ambapo, kwa kweli, upasuaji ulikuwa haujaanza bado! Saa moja baada ya upasuaji huo, ambao ulikuwa umefanikiwa bila damu, Casey alitiwa damu mishipani.
Akina Lunsford walishtaki daktari huyo wa upasuaji na hospitali hiyo ili wapate ridhaa kwa ajili ya kuvunja haki za kiraia na kwa ajili ya udanganyifu, ushambulizi, na kutokeza huzuni ya moyoni kimakusudi, na kuvunja amana iliyowekwa. Baada ya kesi iliyosikilizwa kwa majuma manne, wasaidizi wa hakimu walizungumza hilo kwa siku mbili na nusu na wakatoa uamuzi dhidi ya daktari huyo wa upasuaji na hospitali hiyo. Waliagizwa walipe akina Lunsford jumla ya $500,000.
Ingawa hakimu aliyesikiliza kesi sasa amepindua uamuzi juu ya kuvunja haki za raia na kuagiza kesi isikilizwe upya kuhusiana na udanganyifu na mashtaka yale mengine, wale wasaidizi 12 wa hakimu walisadikishwa kwamba udanganyifu wa hospitali hiyo na daktari huyo ulistahilisha ridhaa ya $500,000. Mawakili wa familia hiyo wameonyesha kwamba watajaribu kukata rufani ili kuunga mkono uamuzi wa wasaidizi hao wa hakimu.
[Maelezo ya Chini]
a Mashahidi huona mipasuo ya upachikaji kuwa jambo la dhamiri ya kibinafsi.