Jitihada ya Kujenga Handaki
NA MLETA-HABARI ZA AMKENI! KATIKA UINGEREZA
WATU fulani huuona ujenzi wa lile handaki ambalo sasa launganisha Uingereza na Kontinenti ya Ulaya kuwa “mradi mkubwa kupita yote katika Karne hii.”
Katika tendo hili hodari la uhandisi wa ujenzi, wafanyakazi wapatao 15,000 wa Waingereza na Wafaransa walisaidiana na mashine kubwa za kutoboa handaki zilizobandikwa na jina Brigitte, Cathérine, Pascaline, Virginie, na Europa. Wakiwa pamoja wakajenga handaki lililo refu zaidi ulimwenguni lenye kupita chini ya maji, chini ya ule ambao Waingereza huuita Mlangobahari, na Wafaransa la Manche.a Lakini hawakufanikiwa bila magumu na vipingamizi. Wanaume tisa walipoteza maisha zao wakati wa ujenzi huo.
Majaribio Ambayo Hayakufua Dafu
“Ni vigumu kupata miradi mingi yenye kufikiriwa vibaya kwa wingi sana na kwa muda mrefu sana kama ilivyokuwa kuhusu ujenzi wa handaki la reli kati ya Dover na Calais,” akasema kiongozi wa serikali ya Uingereza, Winston Churchill, katika 1936. Katika 1858, wakati Bunge la Uingereza liliposikia dokezo la kujenga handaki chini ya ule Mlangobahari, Mheshimiwa Palmerston asemekana kuwa alishangaa hivi: “Eti nini! Mwathubutu kutuomba tuchangie mradi wa kufupisha umbali ambao tayari twauona kuwa mfupi mno?”
Mapema zaidi, katika 1802, mhandisi Mfaransa wa kuchimba migodi, Albert Mathieu-Favier, alikuwa amedokeza kujenga handaki lenye kumulikwa na taa likiwa na mabomba yanayotokeza juu ya mawimbi ya maji ili vigari vyenye kukokotwa na farasi viwe na nafasi za kuingia hewa. Hata hivyo, mpango huo ulithibitika kuwa usiofaa kiufundi.
Katika 1856 Mfaransa mwingine, mhandisi Thomé de Gamond, alipendekeza ujenzi wa handaki la reli la kuunganisha Ufaransa na Uingereza. Wafaransa walikubali, lakini Waingereza wakasitasita. Bila kukata tamaa, de Gamond akashauriana na William Low, mhandisi Mwingereza wa kuchimba migodi. Halafu, katika 1872, Low na mhandisi mwenzake Sir John Hawkshaw wakaanzisha shirika la kuchanga fedha za kiunzi cha Mlangobahari. Katika 1880, mashine za kutoboa zilizoundwa na Kanali Beaumont zilianza kuchimba handaki kutoka Genge la Shakespeare, karibu na Dover, na kutoka Sangatte katika pwani ya Ufaransa. Baada ya meta 1,000, kazi ilikwama wakati hofu ya uvamizi wa kijeshi ilipoogopesha serikali ya Uingereza ikauacha mradi huo.
Jaribio lililofuata lilitukia katika miaka ya 1920, na handaki la kujaribia lenye meta 130 likachimbwa karibu na Folkestone, Uingereza. Tena hofu ya Waingereza juu ya kuvamiwa ilikomesha kazi hiyo. Katika miaka ya 1970 uchimbaji handaki ulianza tena, lakini ukakoma wakati serikali ya Uingereza ilipoacha kusaidia.
Halafu, mkataba wa Handaki la Mlangobahari ulitiwa sahihi mwaka 1986. Ulipokubaliwa rasmi na nchi zote mbili Ufaransa na Uingereza mwaka uliofuata, hiyo iliruhusu kazi ianze kwa bidii.
Jitihada ya Kifedha
Kikundi cha mashirika ya kibinafsi ya Wafaransa na Waingereza (kijulikanacho kwa ujumla kuwa Handaki-Ulaya) kiliipa Transmanche-Link (TML), ambao ni muungano wa mashirika kumi ya ujenzi, mgawo wa kubuni na kujenga handaki hilo. Serikali ilisisitiza kwamba fedha za kibinafsi ndizo zingelipia mradi wote.
Miaka miwili tu baada ya kazi kuanza, shirika la Handaki-Ulaya lililazimika kurekebisha kadirio la fedha kwa kuziongeza kutoka pauni bilioni 5.23 hadi pauni bilioni 7. Kufikia 1994 fedha zilizotabiriwa kutumiwa kwa mradi huo zilikuwa zimeongezeka kufikia kama pauni bilioni 10.
Jitihada ya Chini ya Ardhi
Kwa kweli lile Handaki la Mlangobahari si moja tu bali ni mahandaki matatu. Katika Desemba 15, 1987, TBM (mashine ya kutoboa handaki) ya kwanza ilianza kazi katika Uingereza, na ile nyingine ya Kifaransa, Brigitte, ikaanza katika Februari 28 mwaka uliofuata. Kazi za mashine hizo ilikuwa kuchimba handaki la kuendeshea kazi lenye kipenyo cha meta 4.8, lililoundwa kwa makusudi ya kushughulikia vifaa vyenye kuharibika na hali za dharura. TBM zilizo kubwa zaidi zilitutuma kupasua miamba ili kufungua mahandaki makuu mawili yenye kusonga mbele, kila moja likiwa na kipenyo cha meta 7.6 yakiisha kutiwa tabaka la ndani.
“Kwenye Genge la Shakespeare, tuliteremka kwenye mwanya mkubwa,” asimulia Paul, aliyefanya kazi katika handaki hilo. “Uliposhuka, ulishikwa na hisia ya baridi, ya kukosa hewa mpaka ulipofika chini, ambako hewa ilikuwa nzito-nzito ikiwa na mivuke ya dizeli kutoka kwenye vyombo vyote vya mashine. Ulipokuwa ukipita katika lile handaki, hali ya hewa ilipata kuwa ya jasho-jasho na yenye joto zaidi.”
Kule chini handakini, jumla ya TBM 11 zilifanya kibarua kigumu. Tatu zilitoboa handaki kuelekea barani kutoka upande wa Genge la Shakespeare hadi pale nje tu ya Folkestone mwisho wa Uingereza. Tatu zaidi zilianza kazi kuelekea baharini chini ya ule Mlangobahari ili kukutana na mashine tatu za Kifaransa zilizoanza kazi kwenye mwanya ulioko Sangatte. TBM mbili zilizobaki zilitoboa yale mahandaki matatu kuelekea barani kutoka hapo hadi kituo kilichoko Coquelles, karibu na Calais.
Brigitte iliendesha kazi kwa kutumia mbinu moja kati ya mbili. Wakati wa kutoboa chokaa yenye mianya, mashine hiyo ilifanya kazi ikiwa imefunikwa kichwa cha kukatia na kiwiliwili ili istahimili msongo wa maji wa kilo 11 kwa kila sentimeta ya mraba, kiasi ambacho ni mara kumi kupita msongo wa kawaida wa hewa ya anga. Lakini ilipomaliza chokaa hiyo ya udongo wenye chokaa, mashine hiyo iliongeza mwendo wayo maradufu. Halafu Brigitte ikafuatilia tabaka hii kati ya meta 25 na 40 chini ya sakafu ya bahari, ikisonga mbele kuelekea iliko ile mashine nyingine ya kutoka upande wa Uingereza.
Kama vile Brigitte, TBM zote zilikuwa kama viwanda vyenye kusonga. Kuanzia kile kichwa cha kukatia chenye kikatio kigumu cha chuma cha tangsteni na kabaidi hadi gari-moshi la nyuma lililo la kuhudumia, mashine iliyo kubwa zaidi ilikuwa kama meta 260! TBM moja yenye vikatio vya kuzunguka mara mbili hadi tatu kwa dakika kupasua mwamba, huku vikisukumwa mbele na visukumi vya pistoni vyenye vishikilio, iliweka rekodi ya kukata meta 426 kwa juma moja, ikiziondoa takataka, na pia kutia tabaka la ndani katika lile shimo.
Kupatanisha Sawasawa
Ili kuiongoza mashine isonge mbele, mwenye kuendesha TBM aliangalia viwambo vya kompyuta na monita za televisheni. Vichunguzi vya setilaiti vilisaidia kupanga hata mambo yale madogo-madogo ya njia hususa ambayo ingefuatwa kabla uchimbaji handaki haujaanza. Keekee nyembamba zilitoboa uso wa mwamba kule mbele zaidi ya meta 150, kutafuta sampuli za udongo wa chokaa ili kujua ni njia ipi ingefuatwa huko mbele. Mwale wa leza wenye kulenga shabaha yenye kuathiriwa na nuru kwa urahisi katika ile mashine ulimwezesha dreva kufuata mwendo sahihi.
Karibu kilometa sita hadi nane kule chini ya Mlangobahari, wachimba-handaki walijenga mapango ya kuvukia ambamo magari-moshi yaweza kuhamishwa kutoka handaki moja la kusafiria hadi lile jingine kutokeapo uhitaji. Kila meta 375, wachimba-handaki wa kutumia mashine ndogondogo walitoboa vipito vya kuunganisha lile handaki la kusafiria na lile la kuhudumia.
Pia walikata vifereji vya kuondoa mkazo wa hewa katika pistoni vyenye kuunganisha yale mahandaki makuu mawili, vikiwa vimejipinda kama duara juu ya lile handaki la kuhudumia. “Ni kama pampu ya kizamani ya kujaza hewa katika baiskeli. Uwekapo kidole-gumba juu ya valvu, waweza kulihisi joto,” Paul aeleza. “Yale magari-moshi pia hutokeza joto jingi. Valvu za pistoni hufunguka kupunguza mkazo na joto la magari-moshi yanayopita.”
Brigitte na ile mashine nyingine kama hiyo ya Uingereza zilisimama tuli zilipokaribiana kwa meta 100. Halafu, kwa tahadhari sana, keekee ikatoboa shimo la kipenyo la sentimeta 4 katika ule udongo wenye chokaa. Katika Desemba 1, 1990, hatua ya mafanikio ilifikiwa kama kilometa 22.3 kutoka Uingereza na kilometa 15.6 kutoka Ufaransa. Wazia jinsi kulivyokuwa na hisia ya kutuliza akili wakati uchunguzi ulipofunua kwamba kosa la kupimanisha yale mahandaki mawili lilikuwa la sentimeta chache tu! Ndipo TBM ya Uingereza ilipoendeshwa kwa kujipinda ili iwe chini upande wa kushoto na upande wa Brigitte. Wachimba-handaki wa kutumia mikono wakaimaliza kazi. Baada ya hapo yale mahandaki ya kusafiria yaliungana, na TBM za Uingereza zikaelekezwa kando zikazikwa chini ya ardhi. Zile za Ufaransa zilibomolewa na kuondolewa katika handaki.
Kazi ya Mfululizo Usiopendeza Lakini ya Haraka
“Sasa kupita katika handaki hilo hakuchangamshi na hakuna msisimko,” asema Paul. “Ni mahali pa mfululizo usiopendeza. Usafiripo kupita katika handaki hilo, hakuna kitu cha kuona isipokuwa mianya ya mara kwa mara iliyo kwenye vifereji na mabomba ya kuondoa mkazo wa hewa.” Mzinduo ulikuwa katika Mei 6, 1994, ingawa kutumiwa kwa handaki hilo na umma kumekawizwa. Hivyo basi, litakuaje?
Ili ujue, utaacha barabara kuu ufikapo Folkestone ama Calais, uingilie kituo kikuu, ulipe nauli (kuanzia pauni 220 [dola 330] hadi pauni 310 [dola 460] kwa kila gari ikitegemea ni majira gani), uendeshe kupitia vituo vya uchunguzi wa forodha na kuteremka chini kwenye jukwaa la magari, uendelee hadi jukwaa la stesheni, na usonge mbele ukapande gari-moshi lililobuniwa kwa njia maalumu, Le Shuttle. Baada ya kama dakika 35 na kilometa 50, waibuka upande mwingine wa ule Mlangobahari. Endesha gari lako kwa kuliacha gari-moshi uende moja-kwa-moja hadi barabara kuu—pito sahili lenye amani likuwezeshalo kuendelea na safari yako haraka. Au baki katika gari-moshi la kwenda London au Paris—kukiwa na tofauti moja—utafika Paris kwa mwendo wa kilometa 290 kwa saa moja na London kwa mwendo wa kilometa 80 kwa saa moja. Gari-moshi la kusafiri moja-kwa-moja kutoka Folkestone hadi London halitakuwa tayari mpaka 2002!
Hata hivyo, ile jitihada ngumu yaendelea. Kungali na mabishano juu ya reli ya usafiri wa kasi ya kuunganisha London na lile Handaki. Basi, usiisahau kazi ya ukakamavu iliyofanywa na zile mashine za TBM. Mojapo, ambayo imewekwa nje ya kituo cha maonyesho ya handaki kule Folkestone, ina ishara isemayo, “Yauzwa—Mmiliki Mmoja Mwangalifu,” naam, ikiwa tayari kwa jitihada nyingine!
[Maelezo ya Chini]
a Lile Handaki la Seikan lenye kuunganisha visiwa vya Honshu na Hokkaido katika Japani ni refu zaidi (kilometa 53.9 likilinganishwa na kilometa 49.4 za Handaki la Mlangobahari), lakini urefu wa chini ya maji ni mfupi kwa kama kilometa 14 kuliko ule wa Handaki la Mlangobahari.
[Ramani katika ukurasa wa 15]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
England
Folkestone
Calais
France
[Picha katika ukurasa wa 15]
Chini: Wafanyakazi wakisherehekea kukamilika kwa handaki la chini ya maji lililo refu zaidi ulimwenguni
Kulia: Mashine moja ya TBM
[Hisani]
Wafanyakazi: Eurotunnel Ph. DEMAIL; TBM: Eurotunnel