Vipepeo Wazuri Hawa Ni Wenye Sumu?
NA MLETA-HABARI ZA AMKENI! KATIKA AFRIKA KUSINI
JE, UMEPATA kutazama kwa mduwao huku kipepeo akipita kwa kupepea mabawa yake? Je, ulivutiwa na umaridadi wake, umbo lake, na rangi zake? Kipepeo huyo ayuayuapo kutoka ua hadi ua, huonekana ni kama aitamanisha bure hamu yako na kukutania. Ungependa kupata mtazamo wa karibu zaidi, labda hata kupiga picha, lakini yeye haelekei kamwe kusimama kwa muda wa kutosha juu ya ua lolote lile—na sikuzote anapepea-pepea mabawa yake juu na chini. Lakini je, ulijua kwamba baadhi ya viumbe hawa wenye kupendeza huaminiwa kuwa wenye sumu?
Acheni tuwatazame wawili walio katika kurasa hizi—yule maliki (upande wa kulia), akiwa na mabawa yake makubwa meusi na ya chungwa-kahawia na yule liwali (juu), mwenye sura ikaribiayo kufanana kabisa na yule maliki, ingawa kwa kawaida huwa mdogo zaidi. Ni nini huwafanya wao wawe wenye sumu na hiyo hutimiza kusudi gani?
Vipepeo, ambao kuna spishi zaidi ya 15,000, hupita katika hatua nne za ukuzi ili wakawe zile ajabu-mabawa zilizo nyepesi sana tuzionazo katika bustani zetu. Mojapo hatua hizi ni ile ya buu, au kiwavi mkuu. Kiwavi-mkuu-maliki hujilisha lile gugu-maziwa lenye sumu, na hivyo, yeye huwa “kipepeo aliye sumu kikweli, awezaye kuua ndege yeyote amlaye bila kumtapika amtoe,” aandika Tim Walker katika Science News. Sumu hiyo ni kadenolaidi, sumu ya moyo, na kwa hiyo kipepeo huyo “hurudishwa kinywani ikiwa amemezwa.” (The Random House Encyclopedia) Namna gani yule kipepeo-liwali?
Walker ataarifu hivi: “Kwa zaidi ya karne moja, hekima ya kikawaida imeshikilia kwamba mdudu huyu mwenye mabawa ana mwili mzuri sana wa kuliwa uliofichika chini ya zile rangi za kipepeo-maliki mwenye sumu, Danaus plexippus.” Kama vile uwezavyo kuona kutokana na zile picha, wale vipepeo wawili wana umbo linalofanana sana isipokuwa tu ule mstari mweusi wa ndani katika mabawa ya chini ya yule liwali. Katika miaka 100 iliyopita, wanamageuzi wameamini kwamba yule liwali alijigeuza-geuza akawa na umbo la mabawa linalofanana na la yule maliki mwenye sumu katika jitihada ya kuepuka mashambulio ya ndege waliokuwa wamejifunza kukaa mbali na kipepeo huyu mwenye ladha isiyopendeza. Iliaminiwa kwamba, kama si hilo tu, huyo liwali alikuwa mwenye ladha nzuri kwa ndege.
Wachunguzi wamegundua nini majuzi? Walker aandika hivi: “Hata hivyo, uchunguzi mpya waonyesha kwamba yule liwali amewahadaa kwa mafanikio wanasayansi, si ndege. . . . Wanazuolojia wawili wameonyesha kwamba kwa ndege wenye utambuzi, yule liwali aweza kuwa na ladha mbaya sawasawa na yule maliki mwenye madhara.” Lakini kwa nini huyo liwali ana ladha isiyopendeza, hasa kwa kuwa mabuu yake hula mimea-maji isiyo na sumu, si mimea-sumu? Walker aandika hivi: “Hii yadokeza kwamba kwa njia fulani vipepeo-maliwali hujitengenezea kinga yao ya kikemikali.”
Kwa kweli, entomolojia yadokeza kwamba wastadi wangali na mengi ya kujifunza na yawapasa labda wapunguze kutegemea sana ‘hekima yao ya kikawaida.’ Mchambuzi mmoja aliandika hivi juu ya kitabu kimoja cha majuzi kuhusu yule kipepeo-maliki: “Kitabu hiki kizuri ajabu chatuonyesha kwamba kadiri tujifunzavyo mengi zaidi juu ya yule maliki ndivyo ‘tujuavyo’ machache zaidi tukiwa na uhakika.”
Badala ya hivyo, ni kama vile Biblia itaarifuvyo: “Umestahili wewe, Bwana wetu na Mungu wetu, kuupokea utukufu na heshima na uweza; kwa kuwa wewe ndiwe uliyeviumba vitu vyote, na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako, navyo vikaumbwa.”—Ufunuo 4:11, italiki ni zetu.
Ni wazi kwamba mwanadamu angali na mengi ya kujifunza juu ya namna zote za uhai zilizo katika dunia yetu. Kipingamizi kimoja cha msingi cha kutopata ujuzi sahihi ni katao la wanasayansi wengi kukubali kuwako na fungu tendaji la Muumba-Maumbo. Paul Davies, profesa wa fizikia ya kihisabati, aliandika hivi katika kitabu chake The Mind of God: “Hakuna shaka kwamba wanasayansi wengi hupinga kihisia namna yoyote ya [hoja za] mambo yasiyoonekana kimwili. Wao hudharau wazo la kwamba huenda ikawa kuna Mungu, au hata kanuni ya ubuni isiyo na utu au kisababisha-uhai ambacho kingethibitisha uhalisi wa mambo . . . Mimi binafsi siyashiriki madharau yao. . . . Siwezi kuamini kwamba kuwako kwetu katika ulimwengu huu kulitokea kwa ajali tu, aksidenti ya historia, mfyatuko uliojitokeza tu katika ile tamasha kubwa ya matukio ya kianga.”
Mtunga-zaburi Daudi aliandika hivi: “Mpumbavu amesema moyoni, Hakuna Mungu. Wameharibu matendo yao na kuyafanya chukizo.” Kwa upande mwingine, mtu mwenye hekima atamkiri Muumba kwa unyenyekevu, hata kama vile nabii Isaya alivyofanya: “Jehova aliyeziumba hizo mbingu; yeye ni Mwenyiezi Mngu; yeye aliyeifinanga hii dunia na kuifanya; yeye aliyeithubutisha, yeye aliiumba isiwe ukiwa, yeye aliifinanga illi iketiwe ni watu: yeye asema, Mimi ni Jehova.”—Zaburi 14:1; Isaya 45:18, The Old Testament in Swahili (Mombasa).
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Maliki (juu), liwali (ukurasa 16). Tofauti kubwa ni ule mstari mweusi unaopita katika mabawa ya chini ya yule liwali. (Maumbo si ya ukubwa uliopatanishwa na uwiano wa vipimo)