Jinsi Vita Huwaharibu Watoto
HILO pigano, ambalo lilikuwa mojawapo ya vita vingi vya wenyewe kwa wenyewe vya Sierra Leone, lilitukia mapema katika mwaka wa 1995. Vita ilipokwisha, Tenneh mwenye umri wa miaka minne, ambaye wazazi wake tayari walikuwa wamekufa vitani, alikuwa amelala chini akiwa amejeruhiwa. Risasi ilikuwa imekwama katika kichwa chake, nyuma ya jicho lake la kulia, na kulikuwa na hatari ya risasi hiyo kutokeza ambukizo ambalo lingeenea hadi katika ubongo wake na kumwua.
Miezi 16 baadaye, wenzi fulani wa ndoa Waingereza walifaulu kumsafirisha Tenneh hadi Uingereza akafanyiwe upasuaji. Kikundi cha madaktari-wapasuaji waliondoa hiyo risasi, na watu wakafurahi kwamba upasuaji huo ulifanikiwa, na kwamba uhai mchanga ulikuwa umeokolewa. Lakini, shangilio hilo halikuzidi kwa sababu ya kujua kwamba Tenneh alibaki yatima ambaye hakupaswa kamwe kupigwa risasi.
Silaha, Njaa, na Maradhi
Ingawa Tenneh alipigwa risasi kimakosa, kwa kuongezeka watoto hulengwa badala ya kupigwa kimakosa. Mizozo ya kikabila ifyatukapo, haitoshi kuua watu wazima; watoto wa maadui huonwa kuwa maadui wa wakati ujao. Kama alivyotaja mfafanuzi wa kisiasa nchini Rwanda mwaka wa 1994 katika tangazo la redio: “Ili kuua panya wakubwa, ni lazima uue panya wadogo.”
Hata hivyo, wengi wa watoto ambao hufa vitani hawafi kutokana na mabomu wala risasi bali hufa kwa njaa kali au ugonjwa. Kwa kielelezo, katika vita vya Afrika, ukosefu wa chakula na huduma za afya umesababisha vifo mara 20 kuliko vifo vitokezwavyo na mapigano yenyewe. Kuzuiwa kwa vifaa muhimu ni mbinu ambayo vita imetumia kikatili katika nyakati za kisasa. Majeshi yametawanya mabomu ya kutegwa chini ya ardhi katika maeneo makubwa yenye mashamba ya mazao ya kilimo, yameharibu maghala ya nafaka na mifumo ya kupelekea maji, na kukamata vifaa vya kutuliza. Hayo pia yamebomoa vituo vya afya, yakiwatawanya wafanyakazi wa afya.
Mbinu kama hizo huwaathiri watoto zaidi. Kwa kielelezo, kati ya miaka ya 1980 na 1988, watoto waliokufa kutokana na mambo yahusikayo na vita walikuwa 330,000 nchini Angola na 490,000 nchini Msumbiji.
Hakuna Makao, Hakuna Familia
Vita hutokeza mayatima kwa kuua wazazi, lakini vita pia hufanya hivyo kwa kuvunjavunja familia. Ulimwenguni pote, watu wapatao milioni 53 wametoroka makwao kwa sababu ya tisho la kutokea kwa ujeuri. Hiyo ni karibu mtu 1 kwa kila watu 115 duniani! Angalau nusu ni watoto. Katika kutoroka kwa hofu, mara nyingi watoto hutengana na wazazi wao.
Kutokana na mapigano nchini Rwanda, watoto 114,000 walikuwa wametenganishwa na wazazi wao kufikia mwishoni mwa 1994. Kulingana na uchunguzi mmoja wa 1995, mtoto 1 kati ya kila 5 nchini Angola alipatwa na mambo ayo hayo. Kwa watoto wengi, hasa walio wachanga sana, usumbufu wa kutokuwa na wazazi husononesha zaidi kuliko mvurugo wenyewe wa vita.
Wauawa na Mabomu ya Kutegwa Chini ya Ardhi
Ulimwenguni kote mamia ya maelfu ya watoto wamepata kwenda kucheza, kuchunga mifugo, kuokota kuni, au kupanda mimea, na kisha kulipuliwa tu na mabomu yaliyotegwa chini ya ardhi. Mabomu ya kutegwa chini ya ardhi huua watu wapatao 800 kila mwezi. Katika nchi 64 kuna jumla ya mabomu yapatayo milioni 110 yaliyotegwa chini ya ardhi. Kambodia pekee ina mabomu kama hayo yapatayo milioni saba, mawili kwa kila mtoto.
Zaidi ya nchi 40 hutengeneza aina 340 za mabomu ya kutegwa chini ya ardhi yakiwa na maumbo na rangi tofauti-tofauti. Mengine hufanana na mawe, mengine hufanana na mananasi, na bado mengine hufanana na vipepeo wadogo wenye rangi ya kijani ambao hupeperuka polepole kutoka kwenye helikopta, bila kulipuka. Ripoti fulani zadokeza kwamba mabomu fulani ya kutegwa chini ya ardhi, ambayo yametengenezwa yafanane na vichezeo, yamewekwa karibu na shule na viwanja ambako wanawake na watoto watayapata.
Hugharimu karibu dola 3 pekee kutengeneza mabomu ya kutegwa chini ya ardhi ya kuwalipua askari-jeshi, lakini kutafuta na kuondoa bomu chini ya ardhi hugharimu kati ya dola 300 na dola 1,000. Katika mwaka wa 1993 mabomu yapatayo 100,000 yaliyotegwa chini ya ardhi yaliondolewa, lakini milioni mbili mapya yalitegwa. Hayo yote yanangoja kwa subira kuua, bila kutofautisha kati ya askari-jeshi na mtoto, bila kutambua mkataba wa amani, na kuendelea kuwa tendaji kufikia miaka 50.
Mwezi wa Mei 1996, baada ya mazungumzo ya miaka miwili huko Geneva, Uswisi, wazungumzaji wa kimataifa walishindwa kupiga marufuku duniani kote mabomu ya kutegwa chini ya ardhi. Ingawa walipiga marufuku aina fulani za hayo mabomu na kuwekea vikwazo matumizi ya mabomu mengine, marufuku kamili juu ya mabomu ya kutegwa chini ya ardhi haitafikiriwa mpaka kongamano lifuatalo litakapopitia mambo hayo, ambayo imepangiwa kufanywa mwaka wa 2001. Kati ya sasa na wakati huo, mabomu ya kutegwa chini ya ardhi yataua watu wengine 50,000 na kulemaza watu 80,000. Wengi kati ya hao watakuwa watoto.
Kuteswa na Kubakwa
Katika miaka ya majuzi watoto wameteswa, ama kwa kuadhibu wazazi wao ama kwa kutafuta habari kuhusu wazazi wao. Nyakati nyingine, katika ulimwengu mkatili wa mapigano, hakuna sababu inayohitajiwa na watoto huteswa tu ili kujitumbuiza.
Ujeuri wa kingono, kutia ndani kubakwa, ni kawaida vitani. Katika mapigano ya Balkani, ilikuwa sera kuwabaka wasichana matineja na kuwalazimisha kuzaa watoto wa maadui. Vivyo hivyo, nchini Rwanda askari-jeshi walitumia ubakaji kuwa njia ya kuharibu vifungo vya familia. Katika mashambulio fulani karibu kila msichana tineja aliyeokoka shambulio la wanamgambo alibakwa. Wasichana wengi walioshika mimba walikataliwa na familia zao na jumuiya zao. Wasichana fulani waliwatupa watoto wao; wengine walijiua.
Msononeko wa Kihisia-Moyo
Mara nyingi watoto vitani huvumilia mambo makatili zaidi kuliko mambo ambayo watu wazima wanaogopa zaidi. Kwa kielelezo, katika Sarajevo, uchunguzi uliofanyiwa watoto 1,505 ulionyesha kwamba karibu wote walipata kutupiwa makombora. Zaidi ya nusu walifyatuliwa risasi, na thuluthi mbili walijikuta katika hali ambazo walitarajia kuuawa.
Uchunguzi wa watoto 3,000 nchini Rwanda ulipata kwamba asilimia 95 walishuhudia ujeuri na mauaji katika maangamizo hayo ya kijamii, na kwamba karibu asilimia 80 walikuwa wamepoteza jamaa zao. Karibu thuluthi moja walishuhudia ubakaji au shambulizi la kingono na zaidi ya thuluthi moja walikuwa wamewaona watoto wengine wakishiriki katika mauaji na mapigo. Mambo kama hayo huharibu akili na mioyo ya wachanga. Ripoti moja juu ya watoto wenye masumbufu ambayo ilitoka katika ile iliyokuwa Yugoslavia ilisema: “Bado wanakumbuka kisa hicho . . . kikiwafanya wawe na ndoto za kuogofya, kumbukumbu za kila siku za matukio hayo yenye kusumbua, hofu, ukosefu wa usalama na uchungu.” Kufuatia maangamizi hayo ya jamii nchini Rwanda, mwanasaikolojia mmoja katika National Trauma Recovery Centre aliripoti: “Miongoni mwa dalili zinazodhihirishwa na watoto ni ndoto za kuogofya, ugumu wa kukaza fikira, kushuka-moyo na kukosa tumaini kuhusu wakati ujao.”
Watoto Wanaweza Kusaidiwaje?
Watafiti wengi waamini kwamba usumbufu hauishi watoto wafungapo hisia zao na kumbukumbu zao. Mara nyingi kupona huanza mtoto akabilipo kumbukumbu mbaya kwa kuzungumza na mtu mzima mwenye ufahamu na huruma juu ya yaliyotokea. “Mojawapo ya mambo makuu zaidi ni kuwafanya watoto wanaosumbuka sana wajifunue na kuzungumza kwa uhuru,” akasema mfanyakazi mmoja wa kijamii katika Afrika Magharibi.
Msaada mwingine mkubwa wa kuponesha maumivu ya kihisia-moyo ni muungano na tegemezo lenye nguvu la familia na jumuiya. Kama ilivyo na watoto wote, wahasiriwa wa vita wahitaji upendo, uelewevu, na hisia-mwenzi. Lakini, je, kuna sababu ya kweli ya kuamini kwamba kuna tumaini kwa watoto wote la kufurahia wakati ujao mzuri?
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]
Ilifanana na Mpira
Nchini Laos msichana mmoja na ndugu yake walikuwa njiani kulisha nyati. Huyo msichana aliona kitu kilichofanana na mpira katika mtaro. Alikichukua na kumrushia ndugu yake. Kilianguka chini na kulipuka, kikamwua papo hapo.
[Sanduku katika ukurasa wa 9]
Mmoja Tu Kati ya Maelfu
Mapigano yalipozuka katika eneo lake la Angola, Maria, ambaye alikuwa yatima mwenye umri wa miaka 12, alibakwa akashika mimba. Vita ilipozidi, Maria alitoroka, akitembea kilometa 300 kufikia eneo salama, ambapo alienda katika kituo cha watoto waliopoteza makao. Kwa sababu alikuwa mchanga sana, alipata utungu wa mimba mapema, akizaa mtoto kwa matatizo sana kabla ya wakati wake. Mtoto huyo mchanga aliishi kwa majuma mawili pekee. Maria akafa juma moja baadaye. Maria ni mmoja tu kati ya maelfu ya watoto ambao wameteswa na kubakwa katika vita vya majuzi.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]
Akili na Mioyo Zilizoharibiwa
Kadiri ambavyo watoto huathiriwa na ujeuri inatolewa kielezi vizuri na Shabana, wa India mwenye umri wa miaka minane. Aliona umati ukimpiga babake hadi kifo na kisha ukamkata mamake kichwa. Akili yake na moyo wake umebaki bila hisia, ukificha ogofyo lake na upotezo wake. “Siwakosi wazazi wangu,” akasema katika sauti ya chini isiyo na hisia. “Siwazi juu yao.”