Magonjwa ya Kuambukiza Katika Karne ya 20
TAUNI ya Ulaya ya karne ya 14 haikuongoza kwenye mwisho wa ulimwengu, kama vile wengi walivyokuwa wametabiri. Lakini namna gani kuhusu wakati wetu? Je, magonjwa ya mlipuko na maradhi ya siku yetu yanadokeza kuwa tunaishi katika kile ambacho Biblia huita “siku za mwisho”?—2 Timotheo 3:1.
‘Kwa hakika sivyo,’ waweza kufikiri. Maendeleo ya kitiba na ya kisayansi yamefanya mengi zaidi ili kutusaidia kuelewa na kupigana na maradhi sasa kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya binadamu. Wanasayansi wa kitiba wametokeza namna nyingi za viuavijasumu na chanjo—silaha zenye nguvu dhidi ya maradhi na vijiumbe-maradhi vinavyoyasababisha. Maendeleo katika utunzaji hospitalini na pia katika usafi wa maji, uondoaji wa maji machafu, na utayarishaji wa chakula kumesaidia pia katika pigano dhidi ya maradhi ya kuambukiza.
Miongo michache iliyopita, wengi walifikiri kuwa pigano dhidi ya maradhi ya kuambukiza lilikuwa limekaribia kwisha. Ndui ilikuwa imeng’olewa kabisa, na maradhi mengine yalilengwa ili kung’olewa. Madawa yalitiisha magonjwa mengi kwa matokeo. Wataalamu wa afya walitazamia wakati ujao wakiwa na matumaini mema. Maradhi ya kuambukiza yangeshindwa; ushindi ungefuata ushindi mwingine. Sayansi ya kitiba ingeshinda.
Lakini haikushinda. Leo, maradhi ya kuambukiza yabaki yakiwa kisababishi kikuu cha vifo ulimwenguni, yakiua watu zaidi ya milioni 50 katika mwaka wa 1996 pekee. Mahali pa matumaini mema ya wakati uliopita panachukuliwa na hangaiko lililoongezeka kwa ajili ya wakati ujao. Ripoti ya The World Health Report 1996, iliyotolewa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), yaonya: “Maendeleo mengi yaliyopatikana katika miongo ya karibuni kuelekea kuboresha afya ya kibinadamu sasa yako hatarini. Tunasimama ukingoni mwa tatizo la tufeni pote la maradhi ya kuambukiza. Hakuna nchi iliyo salama.”
Maradhi ya Zamani Yawa ya Kufisha Zaidi
Sababu moja ya hangaiko ni kuwa maradhi yajulikanayo sana, yaliyodhaniwa kuwa yameshindwa, yanarudi tena katika namna zenye kufisha zaidi na zilizo ngumu zaidi kutibu. Kielelezo kimoja ni kifua kikuu, maradhi ambayo yalidhaniwa kuwa karibu kudhibitiwa katika nchi zilizoendelea. Lakini kifua kikuu hakikuisha; sasa kinaua karibu watu milioni tatu kwa mwaka. Ikiwa njia za kudhibiti haziboreshwi, karibu watu milioni 90 wanatarajiwa kuambukizwa maradhi hayo katika miaka ya 1990. Maradhi ya kifua kikuu yanayokinza dawa yanaenea katika nchi nyingi.
Kielelezo kingine cha maradhi yanayotokea tena ni malaria. Miaka 40 iliyopita madaktari walikuwa na matumaini ya kumaliza malaria haraka. Leo maradhi hayo huua karibu watu milioni mbili kila mwaka. Malaria ni maradhi yaliyoenea, au yako kila wakati, katika nchi 90 na yatisha asilimia 40 ya idadi ya watu ulimwenguni. Mbu wanaobeba vimelea vya malaria wamekuwa wakinzani wa dawa za kuua wadudu, na vimelea vyenyewe vimekuwa vikinzani vya madawa sana hivi kwamba madaktari wahofu kwamba aina fulani za malaria huenda ikawa hazitaweza kutibika hivi karibuni.
Maradhi na Umaskini
Maradhi mengine huua bila kukoma ijapokuwa kuna hatua zenye matokeo za kupambana nayo. Kwa kielelezo, fikiria uvimbe wa tando za uti wa mgongo na ubongo. Kuna chanjo za kuzuia uvimbe wa tando za uti wa mgongo na ubongo na madawa ya kuutibu. Maradhi hayo yalitokea katika Kusini ya Sahara katika Afrika mapema katika mwaka wa 1996. Huenda ulisikia machache kuyahusu; lakini, yaliua watu zaidi ya 15,000—hasa watu maskini, hasa watoto.
Maambukizo ya sehemu ya chini ya njia ya kupumulia, kutia ndani nimonia, huua watu milioni nne kila mwaka, wengi wao wakiwa watoto. Surua huua watoto milioni moja kwa mwaka, na kifaduro huua wengine 355,000 zaidi. Vingi vya vifo hivi pia vingeweza kuzuiwa kwa chanjo zisizo ghali.
Watoto wapatao elfu nane hufa kila siku kutokana na ukosefu wa maji mwilini unaosababishwa na kuhara. Karibu vifo hivi vyote vingeweza kuzuiwa kwa kuwa na njia inayofaa ya kuondolea maji machafu au kwa maji safi ya kunywa au kwa kuwapa maji yenye chumvi na sukari.
Vingi vya vifo hivi hutukia katika nchi zinazoendelea, ambapo umaskini ni mwingi. Karibu watu milioni 800—sehemu kubwa ya idadi ya watu ulimwenguni—hawawezi kupata utunzi wa kiafya. Ripoti ya The World Health Report 1995 ilitaarifu: “Muuaji mkubwa zaidi ulimwenguni na kisababishi kikuu zaidi cha afya mbaya na kuteseka duniani pote kimeorodheshwa karibu na mwisho wa Uainishaji wa Kimataifa wa Maradhi. Kimepewa jina Z59.5—ufukara.”
Maradhi Mapya Yaliyotambulika
Bado maradhi mengine ni mageni, yakitambulika tu hivi majuzi. Shirika la WHO hivi majuzi lilitaarifu: “Katika miaka 20 iliyopita, angalau maradhi mapya 30 yametokea kutisha afya ya mamia ya mamilioni ya watu. Mengi ya maradhi hayana tiba, ponyo au chanjo na uwezekano wa kuyazuia au kuyadhibiti ni mdogo.”
Kwa kielelezo, fikiria HIV na UKIMWI. Karibu miaka 15 tu iliyopita hayakuwa yakijulikana, sasa yataabisha watu katika kila kontinenti. Kwa sasa, karibu watu wazima milioni 20 wameambukizwa na HIV, na zaidi ya milioni 4.5 wameshikwa na UKIMWI. Kulingana na ripoti ya Human Development Report 1996, sasa UKIMWI ni kisababishi kinachoongoza cha vifo vya watu wazima walio na umri wa chini ya miaka 45 katika Ulaya na Amerika Kaskazini. Ulimwenguni pote, watu wapatao 6,000 wanaambukizwa kila siku—mmoja kwa kila sekunde 15. Makadirio ya wakati ujao yadokeza kwamba idadi ya visa vya UKIMWI itaendelea kuongezeka kwa haraka. Kufikia mwaka wa 2010, matarajio ya maisha katika mataifa ya Afrika na Asia yaliyoathiriwa zaidi na UKIMWI yanatarajiwa kupungua kufikia miaka 25, kulingana na shirika moja la msaada la Marekani.
Je, UKIMWI ni maradhi ya kipekee, au mlipuko wa magonjwa mengine waweza kutokea na kusababisha maangamizi kama hayo au hata mabaya zaidi? Shirika la WHO lajibu: “Bila shaka, maradhi ambayo sasa hayajulikani lakini yenye uwezekano wa kuwa UKIMWI wa kesho waotea.”
Mambo Yanayopendelea Vijiumbe-Maradhi
Kwa nini wataalamu wa afya wanahofia milipuko ya magonjwa ya baadaye? Sababu moja ni ukuzi wa majiji. Miaka mia moja iliyopita, ni karibu asilimia 15 tu ya idadi ya watu ulimwenguni iliyoishi katika majiji. Hata hivyo, yakadiriwa kuwa kufikia mwaka wa 2010, zaidi ya nusu ya watu wa ulimwengu wataishi katika sehemu za mjini, hasa katika majiji makubwa sana ya mataifa ambayo hayajaendelea.
Visababishi vya magonjwa hunawiri katika sehemu zenye msongamano wa watu. Ikiwa jiji lina nyumba nzuri na pia mifumo ya kutosha ya kuondoshea maji machafu na mifumo ya maji na utunzaji mzuri wa afya, hatari ya magonjwa ya mlipuko inapunguka. Lakini majiji yanayokua haraka zaidi ni yale yaliyo katika nchi maskini. Majiji mengine yana choo kimoja kwa kila watu 750 au zaidi. Sehemu nyinginezo za mjini pia zinakosa nyumba nzuri na maji salama ya kunywa na pia huduma za kitiba. Mahali ambapo mamia ya maelfu ya watu wanaishi wakiwa wamesongamana na penye uchafu, uwezekano wa maradhi kuenea ni wa juu sana.
Je, hii yamaanisha kuwa magonjwa ya mlipuko ya wakati ujao yatakuwa tu katika majiji makubwa sana yenye umaskini na msongamano wa watu? Jarida Archives of Internal Medicine lajibu: “Kwa hakika twapaswa kuelewa kwamba ufukara kidogo, ukosefu kidogo wa tumaini katika uchumi, na matokeo yake hutokeza uwezekano mkubwa zaidi wa kusitawi kwa maambukizo na kushinda nguvu tekinolojia ya wanadamu wengine wote.”
Si rahisi kuwekea maradhi mipaka yawe mahali pamoja tu. Watu wengi wako mwendoni. Kila siku karibu watu milioni moja huvuka mipaka ya kimataifa. Kila juma watu milioni moja husafiri kati ya nchi tajiri na maskini. Vijiumbe-maradhi vyenye kufisha hufuatana na watu wanapohama. Jarida The Journal of the American Medical Association laonelea “Kutokea kwa maradhi mahali popote lazima sasa kuonekane kama tisho kwa nchi nyingi, na hasa zile ambazo huwa vitovu vya usafiri wa kimataifa.”
Hivyo, yajapokuwa maendeleo ya kitiba ya karne ya 20, magonjwa ya kuambukiza yaendelea kuua watu wengi, na wengi wahofia kuwa mabaya zaidi bado yatakuja wakati ujao. Lakini, Biblia husema nini kuhusu wakati ujao?
[Blabu katika ukurasa wa 4]
Maradhi ya kuambukiza yabaki yakiwa kisababishi kikuu cha vifo ulimwenguni, yakiua zaidi ya watu milioni 50 katika mwaka wa 1996 pekee
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
Kukinza Kiuavijasumu
Maradhi mengi ya kuambukiza yanazidi kuwa magumu kutibu kwa sababu yamekuwa yenye kukinza viuavijasumu. Hutukia hivi: bakteria zinapomwambukiza mtu, huongezeka daima, zikipitisha tabia za kijeni kwa wazao wake. Kwa kila bakteria mpya inayotokea, kuna uwezekano wa mabadiliko—kosa dogo katika kutokeza bakteria mpya ambalo litaipa bakteria hiyo vitabia vipya. Uwezekano wa kwamba bakteria hiyo itaweza kubadilika katika njia itakayoifanya iweze kukinza kiuavijasumu ni ndogo sana. Lakini bakteria huzaana kwa mabilioni, wakati mwingine zikitokeza vizazi vitatu katika muda wa saa moja. Hivyo, lisilotazamiwa hutukia—kila baada ya muda fulani, bakteria moja hutokea ambayo ni vigumu kuiua kwa kiuavijasumu.
Kwa hiyo wakati mtu aliyeambukizwa anapomeza kiuavijasumu, bakteria zisizoweza kukinza humalizwa, na huenda mtu huyo akapata nafuu. Lakini, bakteria zenye kukinza hubaki hai. Ila sasa hazihitaji tena kupigania lishe na nafasi na vijiumbe-maradhi vingine. Ziko huru kuzaana bila kuzuiwa. Kwa kuwa bakteria moja yaweza kuongezeka kufikia bakteria milioni 16 kwa siku moja tu, haupiti muda mrefu na mtu yule anakuwa mgonjwa tena. Hata hivyo, sasa, ameambukizwa na bakteria yenye tabia ya kukinza dawa iliyokusudiwa kuiua. Bakteria hizi zaweza kuwaambukiza watu wengine na baada ya muda zibadilike tena ili ziweze kukinza viuavijasumu vingine.
Makala moja ya mhariri katika jarida Archives of Internal Medicine yataarifu: “Ukuzi wa haraka wa ukinzaji wa bakteria, virusi, kuvu, na vimelea kwa vifaa vyetu vya kitiba vya kisasa hufanya mtu asiwazie ikiwa tutashinda, lakini awazie ni lini tutakaposhindwa katika vita hii ya mwanadamu dhidi ya ulimwengu wa vijiumbe-maradhi.”—Italiki ni zetu.
[Sanduku katika ukurasa wa 7]
Maradhi Fulani Mapya ya Kuambukiza Tangu 1976
Mahali Visa
Vilipotokea
Mwaka Kwanza
Vilivyotambuliwa Jina la Maradhi au Kutambuliwa
1976. Maradhi ya Legionnaires. Marekani
1976. Cryptosporidiosis. Marekani
1976. Homa ya kuvuja damu ya Ebola. Zaire
1977. Virusi ya Hantaan. Korea
1980. Mchochota wa Ini Aina ya D (Delta) Italia
1980. Virusi ya Human T-cell lymphotropic 1 Japani
1981. UKIMWI. Marekani
1982. E. coli O157:H7. Marekani
1986. Bovine spongiform encephalopathy*. Uingereza
1988. Salmonella enteritidis PT4. Uingereza
1989. Mchochota wa Ini Aina ya C. Marekani
1991. Homa ya kuvuja damu ya Venezuela. Venezuela
1992. Vibrio cholerae O139. India
1994. Homa ya kuvuja damu ya Brazili. Brazili
1994. Human and equine morbillivirus. Australia
*Visa vya wanyama pekee.
[Hisani]
Chanzo: WHO
[Sanduku katika ukurasa wa 8]
Maradhi ya Zamani Yarudi Tena
Kifua Kikuu: Zaidi ya watu milioni 30 wanatarajiwa kufa kutokana na kifua kikuu katika mwongo huu. Kwa sababu ya utibabu usiotosha wa maradhi hayo wakati uliopita, kifua kikuu kinachokinza dawa ni tisho la ulimwenguni pote. Bakteria nyinginezo sasa haziathiriwi na dawa ambazo zamani ziliziua bila kushindwa.
Malaria: Maradhi haya huathiri kufikia watu milioni 500 kwa mwaka, yakiua watu milioni 2. Udhibiti umezuiwa na ukosefu wa dawa ama utumizi mbaya wa madawa. Likiwa tokeo, vimelea vya malaria vimekuwa vyenye kukinza madawa ambayo wakati mmoja yaliviua. Kufanya tatizo liwe gumu hata zaidi ni kwamba mbu wamekuwa wenye kukinza dawa za kuua wadudu.
Kipindupindu: Kipindupindu huua watu 120,000 kwa mwaka, hasa katika Afrika, ambapo milipuko hiyo imeenea sana na kwa wingi. Kikiwa hakijulikani kwa miongo mingi katika Amerika Kusini, kipindupindu kiliipata Peru katika 1991 na tangu hapo kikaenea kote katika kontinenti hiyo.
Kidingapopo: Virusi hivi vinavyoenezwa na mbu hutaabisha watu wanaokadiriwa kuwa milioni 20 kila mwaka. Katika 1995 mlipuko mbaya zaidi wa kidingapopo katika Amerika ya Latini na Karibea kwa miaka 15 ulipiga angalau nchi 14 huko. Milipuko ya kidingapopo inaongezeka kwa sababu ya ukuzi wa majiji, kuenea kwa mbu wanaobeba kidingapopo, na kuhama kwa watu wengi walioambukizwa.
Dondakoo: Programu nyingi za chanjo ambazo zilianza miaka 50 iliyopita ziliyafanya maradhi haya yawe nadra sana katika nchi zilizoendelea. Hata hivyo, kuanzia 1990, milipuko ya dondakoo imetokea katika nchi 15 za Ulaya Mashariki na ule uliokuwa Muungano wa Sovieti. Mtu mmoja kati ya wanne waliopata maradhi hayo alikufa. Katika nusu ya kwanza ya 1995, karibu visa 25,000 viliripotiwa.
Tauni yenye mitoki: Katika 1995, angalau visa 1,400 vya tauni ya wanadamu viliripotiwa kwa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO). Katika Marekani na kwingineko, maradhi hayo yameenea katika sehemu ambazo zilikuwa bila tauni kwa miongo mingi.
[Hisani]
Chanzo: WHO
[Picha katika ukurasa wa 5]
Yajapokuwa maendeleo katika utunzi wa kiafya, sayansi ya kitiba imeshindwa kumaliza kuenea kwa maradhi ya kuambukiza
[Hisani]
Picha ya WHO iliyopigwa na J. Abcede
[Picha katika ukurasa wa 7]
Maradhi huenea kwa urahisi watu wakiishi wakiwa wamesongamana sana katika sehemu zenye uchafu
[Picha katika ukurasa wa 8]
Karibu watu milioni 800 katika nchi zinazoendelea hawawezi kupata utunzi wa kiafya