Kuutazama Ulimwengu
Uchafuzi na Kansa ya Utoto
Baada ya kuchanganua uchunguzi wa miaka 27 wa watoto 22,400 Waingereza, kikundi cha watafiti wa magonjwa ya kipuku kilipata kwamba vijana waliozaliwa katika eneo la kilometa tano kutoka kwenye chanzo cha uchafuzi walikuwa hatarini zaidi kwa asilimia 20 ya kupatwa na lukemia na kansa nyinginezo za watoto kuliko watoto wengine. Kupatwa na vichafuzi vya hewani ndiko “njia inayoelekea kuwa kubwa zaidi” isababishayo ongezeko la visa vya kansa za watoto, laripoti The Times la London. Vichafuzi vyenye kuhusika vyaonekana kuwa moshi wa petroli au mvuke wa kemikali zenye kaboni utolewao na viwanda kama vile vya kusafisha mafuta, viwanda vya magari, vituo vya nguvu zisizo za nyukilia, viwanda vya chuma na viwanda vya saruji. Uchunguzi huo uliripoti pia kwamba miongoni mwa watoto waliozaliwa katika eneo la kilometa nne kutoka barabarani na reli, kulikuwa na ongezeko la vifo kwa sababu ya kansa. Fueli za petroli na diseli zaelekea zinachangia, wadai waandishi wa hiyo ripoti.
Dini Katika Brazili
Uchunguzi wa hivi majuzi waonyesha kwamba “asilimia 99 ya Wabrazili huamini katika Mungu,” yaripoti ENI Bulletin. Kulingana na uchunguzi huo wa karibu watu 2,000, asilimia 72 walidai kuwa Wakatoliki, asilimia 11 walisema walikuwa Waprotestanti, na asilimia 9 hawakudai kuwa wa dini yoyote. Wale wengine walifuata dini za Kibrazili na zenye kuchanga mambo ya Kiafrika na ya Kibrazili. “Walipoulizwa ikiwa walienda kwenye kanisa au jengo la kidini katika mwisho-juma uliotangulia, asilimia 57 walisema hawakuenda,” yasema ENI. Ni asilimia 44 tu huamini katika adhabu ya milele. Ijapokuwa asilimia 69 ya Wabrazili huamini katika mbingu, ni asilimia 32 pekee wanaotarajia kwenda huko.
Ni Nani Ashikiliaye Kifaa cha Kudhibiti Televisheni?
Katika Italia, watafiti kwenye EURISPES (Taasisi ya Uchunguzi wa Kisiasa, Kiuchumi na Kijamii) hivi karibuni walichapisha matokeo ya uchunguzi wa mazoea ya kutazama televisheni. Karibu familia 2,000 za Waitalia zilihojiwa. Miongoni mwa maswali mengine, waliulizwa ni nani katika familia ambaye anaelekea sana kushikilia na kuendesha kifaa cha kudhibiti televisheni, kilichobandikwa jina na makala ya gazeti la habari kuwa fimbo ya mamlaka ya siku ya kisasa katika familia. Katika visa vingi baba alitajwa kuwa mwenye kudhibiti. Watoto walikuwa namba mbili wakiwa wafanya-maamuzi kwa habari ya kubadilisha vipindi. Mama akawa wa mwisho katika shindano la nguvu la kushikilia kifaa cha kudhibiti televisheni katika familia.
Ngono za Ujana
Kulingana na gazeti la habari la Nigeria Weekend Concord, uchunguzi wa hivi majuzi ulipata kwamba “Vijana wa Nigeria ni miongoni mwa walio watendaji kingono zaidi ulimwenguni.” Asilimia 68 hivi ya wavulana na asilimia 43 ya wasichana walio na umri wa kati ya miaka 14 hadi 19 walikiri kwamba walipata kufanya ngono “muda mfupi baada ya mwanzo wa kubalehe.” Hili limeongoza kwenye mimba nyingi zisizotakiwa. Uchunguzi tofauti waonyesha kwamba “asilimia 71 ya vifo vyote vya wanawake wachanga walio [na umri wa] chini ya miaka 19 katika Nigeria vilihusiana na matatizo ya utoaji-mimba,” lasema Concord.
Tatizo la Kunawa Mikono
Makala ya hivi majuzi katika gazeti la habari la kitiba la Kifaransa Le Quotidien du Médecin ilikazia mwelekeo wenye kutia wasiwasi unaoonekana kuongezeka—kutonawa mikono kabla ya kula au baada ya kwenda choo. Kulingana na Dakt. Frédéric Saldmann, kukosa huu usafi wa kiafya wa kibinafsi ulio sahili, huleta hatari kubwa za kiafya na kwaelekea kuwa tatizo lililoenea. Makala hiyo inataja uchunguzi mmoja ambao bakuli za njugu karanga katika baa za Uingereza zilipatikana zikiwa na dalili za mkojo kutoka kwa vyanzo tofauti 12. Uchunguzi mwingine katika shule ya Marekani ulifunua kwamba kunawa mikono kwa ukawaida kulikosimamiwa na mwalimu kulipunguza idadi ya watoto wakosao kuhudhuria shule kwa sababu ya matatizo ya umeng’enyaji kwa asilimia 51 na wale wakosao kuhudhuria kwa sababu ya matatizo ya kupumua kwa asilimia 23. Makala hiyo yamalizia kwa kukazia umaana wa kufundisha watoto kanuni za msingi kama hizo za usafi wa kiafya tangu utoto sana.
Uchumi Unaokua na Umaskini
Ijapokuwa uchumi wa tufeni pote ulikua kwa asilimia 40 kutoka 1975 hadi 1985, “idadi ya watu maskini ulimwenguni iliongezeka kwa asilimia 17,” yaonelea HCHR News, taarifa rasmi ya habari ya Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu. Leo, katika nchi 89 watu wako katika hali mbaya zaidi za kiuchumi zaidi ya walivyokuwa miaka kumi au zaidi iliyopita. Katika nchi 70 zinazositawi, viwango vya mapato ni vya chini zaidi ya vilivyokuwa miaka 20, na katika visa vingine miaka 30 iliyopita. Ukuzi wa kiuchumi, yamalizia HCHR News, umefaidi tu “nchi zilizo chache.”
Majengo Yaliyo Hatari Katika Italia
Katika karne iliyopita, matetemeko ya dunia yameua zaidi ya watu 120,000 katika Italia. Na bado, karibu Waitalia milioni 25 huishi katika sehemu ambazo “asilimia 64 ya majengo si salama kwa matetemeko ya dunia,” laripoti Corriere della Sera. Miongoni mwa majengo yaliyo hatari ni hospitali, vituo vya zima-moto, na majengo mengineyo ambayo yangalikuwa vituo vya dharura iwapo maafa yangetukia. Wastani wa lire bilioni 7,000 (dola bilioni 4, za Marekani) hutumiwa kila mwaka katika Italia ili kurekebisha madhara yaliyosababishwa na maafa ya jiolojia na viwanda. Mtaalamu mmoja aeleza kwamba “mara nyingi kile kiasi kikubwa sana cha fedha kinachotumiwa baada ya misiba mikubwa . . . kimetumiwa ili kujenga upya [majengo] katika njia ileile isiyo sahihi na katika sehemu zilezile zilizo hatari sana.”
Damu na Ambukizo la HIV
Kwa wale watu karibu milioni 22 walioambukizwa HIV/UKIMWI katika tufe lote, zaidi ya asilimia 90 waishi katika nchi zinazositawi. “Kufikia asilimia 10 ya maambukizo mapya ya HIV katika nchi zinazositawi yanasababishwa na utiaji-damu mishipani,” laripoti Panos, shirika la habari lenye makao huko London. Katika nchi nyingi, akiba za damu si salama kwa sababu upimaji wa HIV katika maabara hautegemeki kikamili. Mathalani, katika Pakistan, chini ya nusu ya benki za damu ndizo zilizo na vifaa vya kugundua HIV. Kama matokeo, asilimia 12 ya maambukizo mapya yote ya HIV yanasababishwa na utiaji-damu mishipani. Tangu visa vya kwanza vya UKIMWI vilivyoripotiwa kwa miaka 15 iliyopita, karibu watu milioni 30 tufeni pote wameambukizwa HIV, virusi inayosababisha maradhi hayo.
Hofu ya Kupindukia Juu ya Mungu
Katika uchunguzi wa hivi majuzi, watoto wa Brazili wanaougua mkazo walihojiwa. Ilionekana kwamba, kulingana na ENI Bulletin, asilimia kubwa ya watoto hupatwa na maumivu makali yanayohusiana na hofu ya kupindukia juu ya Mungu. Ingawa asilimia 25 ya watoto walipatwa na mkazo unaohusiana na matatizo ya familia au kifo cha mtu wa jamaa, asilimia 75 walionyesha ishara za maumivu makali kwa sababu wanamwona Mungu akiwa kama mtu mwenye ghadhabu anayetaka kuadhibu. Uchunguzi huo “ulisihi sana wazazi wafundishe watoto wao kwamba Mungu angewasaidia na angeweza kuwaelewa,” laripoti ENI.
Uwasiliano wa Tembo
Vitunga-mlio vya tembo ni vikubwa sana hivi kwamba kiasi cha mvumo wa mawimbi wanayotokeza ni duru 20 kwa sekunde au chini ya hiyo—chini sana ya uwezo wa binadamu kusikia. Mingurumo kama hiyo ya ndani husafiri mbali, na tembo waweza kuitambua kutoka umbali wa kilometa 1.5. Wanaweza pia kutambulisha sauti 150 tofauti-tofauti wakiitikia ifaavyo ishara za washiriki wa familia na wale walio katika kikundi chao. Kwa kawaida tembo hupuuza sauti za tembo wasiojulikana au wao hukasirika wakizisikia. Baada ya kufanya utafiti wa uchunguzi katika Mbuga ya Kitaifa ya Amboseli, Kenya, mchunguza-tabia za wanyama Dakt. Karen McComb, wa Chuo Kikuu cha Sussex, Uingereza, alieleza kwamba “mfumo mkubwa kama huo wa uwasiliano wa sauti haujaonyeshwa na mamalia mwingine yeyote,” laripoti The Times la London.