Je, Maisha Yako Yameamuliwa Kimbele au Wapatwa na Tukio Tu?
WATU wengi walikufa na wengine wakanusurika kwa sababu maisha yao yaliamuliwa hivyo kimbele,” likatangaza gazeti la International Herald Tribune. Mwaka uliopita, karibu watu 200 walikufa na mamia kujeruhiwa magaidi waliposhambulia ubalozi wa Marekani nchini Kenya na Tanzania. Hata hivyo, “wakati uliwanusuru mabalozi wakuu wa ubalozi,” likasema gazeti hilo.
Mabalozi hawa walinusurika kwa sababu walikuwa wakihudhuria mkutano katika sehemu ya jumba iliyokuwa mbali na mlipuko. Lakini ofisa mmoja wa cheo cha juu wa ubalozi, aliyepaswa kuhudhuria lakini akakosa kuwapo, alikuwa katika sehemu ya jumba iliyokuwa karibu na mlipuko akafa.
“Pia msiba uliompata Arlene Kirk ulikuwa umeamuliwa kimbele,” likataarifu gazeti hilo. Alipokuwa akirejea Kenya kutoka likizoni, Arlene aliamua kutosafiri kwa ndege iliyokuwa imejaa. Hata hivyo, abiria wengine walijitolea kubaki badala yake, hivyo akapata nafasi kwenye ndege hiyo. Basi akarejea kazini kwenye ubalozi siku ile ya mlipuko naye akafa.
Msiba si jambo geni kwa mwanadamu. Lakini, kufafanua msiba si jambo rahisi kamwe. Kwa kawaida, katika aksidenti na misiba mikubwa ulimwenguni pote, watu wengine hufa na wengine hunusurika. Hata hivyo, si nyakati za msiba tu ambazo watu hujiuliza, ‘Kwa nini hili linanipata mimi?’ Hata inapohusu mambo bora maishani, baadhi ya watu huonekana wakiwa na fursa bora zaidi ya wengine. Maisha huonekana yakiwa magumu daima kwa watu wengi, na rahisi kwa wengine. Hivyo, huenda ukauliza, ‘Je, inaweza kuwa kwamba yote haya yalikuwa yamepangwa? Je, maisha yangu yanatawaliwa na dhana ya kwamba tayari nimeamuliwa kimbele mambo yatakayonipata?’
Kutafuta Sababu
Yapata miaka 3,000 iliyopita, mfalme mmoja mwenye hekima aliona mambo yasiyotazamiwa yakitukia. Akaeleza hivi juu ya matukio hayo: “Wakati na tukio lisilotazamiwa huwapata wote.” (Mhubiri 9:11, NW) Nyakati nyingine mambo yasiyotazamiwa hutukia. Hakuna njia yoyote ya kutabiri matukio hayo. Matukio yenye kutokeza, mema na mabaya, kwa kawaida hutegemea wakati.
Hata hivyo, huenda ukawa na maoni sawa na watu ambao badala ya kukubali mambo jinsi yalivyo wanayaona kuwa yamesababishwa na jambo jingine—kuwa matukio hayo yalikuwa yameamuliwa. Itikadi juu ya ajali au tukio lisiloepukika ni mojawapo ya itikadi za kidini za kale zaidi na zilizoenea sana za mwanadamu. Profesa François Jouan, mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Hekaya katika Chuo Kikuu cha Paris, asema: “Hakujawahi kuwa na kizazi au ustaarabu ambao haukuitikadi katika mungu anayeamua matukio ya wakati ujao . . . anayejua mambo yote yasiyofahamika maishani mwetu.” Hiyo ndiyo sababu ni kawaida kusikia watu wakisema: “Wakati wake wa kufa haukuwa umefika” au, “Hivyo ndivyo ilivyopangwa.” Lakini dhana ya kuamuliwa kimbele ni nini?
Kufasili Dhana ya Kuamuliwa Kimbele
Neno la Kiingereza fate (kuamuliwa kimbele) hutokana na neno la Kilatini fatum, limaanishalo “tangazo la kiunabii, uaguzi, au azimio la kimungu.” Ingawa nyakati nyingine kani fulani hudhaniwa kuwa inaamua matukio ya wakati ujao katika njia isiyoepukika na isiyofahamika, kwa kawaida, kani hii hudhaniwa kuwa mungu.
Mwanahistoria wa dini Helmer Ringgren aeleza: “Jambo muhimu katika maoni ya kidini ni wazo la kwamba mwisho wa mwanadamu haukosi maana au hautukii tu bali huamuliwa na kani fulani inayotekeleza mapenzi yake au kusudi lake.” Ingawa kwa kawaida wanadamu hudhaniwa kuwa na kiasi fulani cha uwezo wa kubadili matukio, watu wengi hufikiri kwamba wanadamu ni hoi wasiweze kudhibiti matukio. Hivyo ‘wanapatwa tu na yaliyoamuliwa kimbele.’
Kwa muda mrefu wanatheolojia na wanafalsafa wamejaribu kufasili hali ya kuamuliwa kimbele. Kichapo The Encyclopedia of Religion chasema: “Wazo la kuamuliwa kimbele, katika ufafanuzi wowote ule, lugha, au maana, sikuzote lina fumbo fulani la msingi.” Ingawa hivyo wazo la kuwapo kwa mamlaka ya juu zaidi inayodhibiti na kuelekeza mambo ya mwanadamu hudhihirika katika dhana zote. Kani hii hudhaniwa kuwa inaamua kimbele maisha ya mtu mmoja-mmoja na mataifa, ikifanya wakati ujao uwe usioepukika kama wakati uliopita.
Jambo Linaloamua
Je, uwe unaitikadi au huitikadi kwamba maisha yako yameamuliwa kimbele inatokeza tofauti yoyote? “Hali za watu za maisha huathiri sana itikadi zao, na kwa upande mwingine itikadi zao huathiri sana hali zao,” akaandika mwanafalsafa Mwingereza Bertrand Russell.
Kwa kweli, kuitikadi kwamba maisha yetu yameamuliwa kimbele—iwe kweli au si kweli—kwaweza kuathiri jinsi tunavyotenda. Wanapoitikadi kwamba maisha yao yameamuliwa kimbele na miungu, wengi hujiachilia—hata hali zao ziwe mbaya na zenye kukandamiza kwa kadiri gani—kana kwamba maisha yao hayawezi kubadilishwa na chochote. Hivyo, kuitikadi kwamba maisha yako yameamuliwa kimbele huondoa wazo la uwajibikaji.
Kwa upande mwingine, kuitikadi tukio lisiloepukika kumewachochea wengine watende vingine. Kwa kielelezo, wanahistoria husema kwamba ukuzi wa ubepari na mvuvumuko wa kiviwanda ulisababishwa na mambo kadhaa. Miongoni mwa mambo hayo ni itikadi ya kuamuliwa kimbele yatakayompata mtu. Baadhi ya dini za Kiprotestanti zilifundisha kwamba Mungu huamua kimbele watu watakaopata wokovu. Mwanasoshiolojia Mjerumani Max Weber asema hivi: “Swali, Je, mimi ni mmojawapo wa watu walioteuliwa kupata wokovu? lazima liwe lilimsumbua kila mwamini wakati fulani.” Mtu mmoja-mmoja alitaka kujua iwapo yeye alikuwa amebarikiwa na Mungu na hivyo kupangiwa kimbele kupata wokovu. Weber alitoa hoja ya kwamba walifanya hivyo kwa “utendaji wao wa kilimwengu.” Kufanikiwa kibiashara na kukusanya utajiri kulionwa kuwa ishara ya kuwa na upendeleo wa Mungu.
Kuitikadi kwamba maisha yameamuliwa kimbele huwachochea wengine wawe na matendo yanayopita kiasi. Katika vita ya ulimwengu ya pili, marubani wa kujitolea kufa wa Japani waliitikadi kamikaze, au “upepo wa kimungu.” Wazo la kwamba miungu ilikuwa na kusudi na kwamba iliwezekana miungu inatumia wanadamu kutimiza kusudi hilo liliongezea uzito imani ya kidini juu ya kifo chenye kuogofya. Katika mwongo uliopita, kwa kawaida magazeti yalijaa habari juu ya mashambulizi ya kutisha ya walipuaji mabomu wa kujitolea kufa katika Mashariki ya Kati. Nadharia ya kwamba maisha yameamuliwa kimbele huchangia sana “mashambulizi haya ya kidini ya watu waliojitolea kufa,” ensaiklopedia moja yasema.
Lakini kwa nini itikadi juu ya maisha kuamuliwa kimbele imeenea sana? Kuchunguza kwa ufupi chanzo chake kutaandaa jibu.