“Vita Si Yenu Bali Ni ya Mungu”
KAMA ILIVYOSIMULIWA NA W. GLEN HOW
Katika miongo sita iliyopita, Mashahidi wa Yehova wameshtakiwa mahakamani mara nyingi huko Kanada. Wanasheria wameshuhudia ushindi wa kesi zao. Hivi majuzi Shirika la Marekani la Wanasheria wa Mashtaka lilinitunukia Tuzo la Wakili Jasiri kwa sababu ya fungu nililotimiza katika baadhi ya kesi hizo. Katika sherehe ya kutuzwa, ilielezwa kwamba kesi zilizowakabili Mashahidi wa Yehova “zilitimiza fungu muhimu sana katika kuzuia serikali kuvuka mipaka . . . , kwa kuwa kesi hizo zilitetea sheria ya haki za binadamu inayotambuliwa na mahakama, ambayo ililinda uhuru wa Wakanada wote.” Acheni niwaeleze mambo yaliyohusika katika baadhi ya kesi hizo na jinsi nilivyopata kuwa mwanasheria na Shahidi wa Yehova.
MNAMO mwaka wa 1924, George Rix, Mwanafunzi wa Biblia, kama Mashahidi wa Yehova walivyoitwa wakati huo, aliwatembelea wazazi wangu katika Toronto, Kanada. Mama yangu, Bessie How, mwenye mwili mdogo, alimwalika ili wazungumze. Nilikuwa na umri wa miaka mitano, na ndugu yangu, Joe, alikuwa na umri wa miaka mitatu.
Punde si punde mama alianza kuhudhuria mikutano ya Wanafunzi wa Biblia huko Toronto. Akawa painia au mhudumu wa wakati wote mwaka wa 1929, na kuendelea na upainia hadi 1969, alipomaliza mwendo wake wa kidunia. Aliwasaidia wengi kupata ujuzi wa kweli ya Biblia na kutuwekea kielelezo bora kwa ajili ya bidii na kutochoka kwake katika huduma.
Baba yangu, Frank How, alikuwa mtu mnyamavu ambaye mwanzoni alipinga utendaji wa kidini wa Mama yangu. Hata hivyo, kwa busara mama aliwaalika waangalizi wasafirio, kama vile George Young, waje kuzungumza naye. Baada ya muda, mtazamo wa Baba ulibadilika. Alipoona namna kweli ilivyosaidia familia yake, aliwaunga mkono sana ingawa hakuwahi kuwa Shahidi.
Kuamua Kumtumikia Mungu
Nilifuzu shule ya sekondari mnamo mwaka wa 1936. Sikupendezwa sana na mambo ya kiroho wakati wa ujana. Ulikuwa wakati wa ule Mshuko Mkubwa wa Kiuchumi, na hakukuwa na mataraja ya kupata kazi. Kwa hiyo nilijiunga na Chuo Kikuu cha Toronto. Nikaamua kujiunga na chuo cha sheria mwaka wa 1940. Mama hakushangazwa na uamuzi huo. Nilipokuwa mtoto, aliniambia hivi kwa hasira: “Mtoto huyu mtundu ni mbishi sana! Huenda atakuwa mwanasheria!”
Katika Julai 4, 1940, kabla tu ya kuanza kwenda kwenye chuo cha sheria, serikali ya Kanada iliwapiga marufuku Mashahidi wa Yehova pasipo onyo. Jambo hilo lilibadili maisha yangu. Nilipoona wenye mamlaka serikalini wakishambulia tengenezo dogo sana la watu wanyenyekevu wasio na hatia, nilisadiki kwamba Mashahidi wa Yehova walikuwa wafuasi wa kweli wa Yesu. Sawa na alivyotabiri, walikuwa “vitu vya kuchukiwa na mataifa yote kwa sababu ya jina [lake].” (Mathayo 24:9) Niliazimia kumtumikia Mungu Mwenye Nguvu anayeliongoza tengenezo hilo. Nilionyesha wakfu wangu kwa Yehova Mungu kwa kubatizwa katika maji, Februari 10, 1941.
Nilitaka kuanza upainia mara moja. Lakini, Jack Nathan, aliyeelekeza kazi ya kuhubiri katika Kanada akanitia moyo nikamilishe masomo ya sheria. Kwa hiyo nilikamilisha na kufuzu mnamo Mei 1943, kisha nikaanza upainia. Katika Agosti, nilialikwa kutumikia katika ofisi ya tawi ya Watch Tower Society huko Toronto na kushughulikia matatizo ya kisheria yaliyowakabili Mashahidi wa Yehova. Mwezi uliofuata nilipata kibali cha kujiunga na baraza la wanasheria katika Ontario, Kanada.
Kutetea Kisheria Habari Njema
Vita ya Ulimwengu ya Pili ilikuwa imepamba moto, na Mashahidi walikuwa wangali chini ya marafuku katika Kanada. Wanaume na wanawake walikuwa wanatiwa gerezani kwa sababu tu ya kuwa Mashahidi wa Yehova. Watoto walikuwa wakifukuzwa shuleni, hata baadhi yao walihamishwa nyumbani kwao. Kwa sababu walikataa kushiriki namna mbalimbali ya ibada ya kitaifa, kama vile kusalimu bendera au kuimba wimbo wa taifa. Profesa William Kaplan, aliyeandika kitabu kinachoitwa State and Salvation: The Jehovah’s Witnesses and Their Fight for Civil Rights, alisema kwamba “Mashahidi walitukanwa hadharani na kushambuliwa na serikali isiyowavumilia na vikundi vya raia wenye uhasama wa peupe ambao walinaswa katika tamaa na uzalendo wa vita.”
Mashahidi walikuwa wanaomba marufuku yaondolewe bila mafanikio. Ghafula, yaliondolewa katika Oktoba 14, 1943. Lakini, Mashahidi walikuwa wangali gerezani na katika kambi za kazi ngumu, bado watoto walizuiwa kujiunga na shule za umma, na bado shirika la Watch Tower Bible and Tract Society na International Bible Students Association, shirika lililomiliki vifaa vyetu huko Toronto yalipigwa marufuku.
Mwishoni mwa mwaka wa 1943, nilisafiri hadi New York pamoja na Percy Chapman, aliyekuwa mwangalizi wa ofisi ya tawi ya Kanada, ili kufanya mashauri na Nathan Knorr, aliyekuwa msimamizi wa Watch Tower Society wakati huo, na Hayden Covington, naibu-msimamizi na mshauri wa kisheria wa Society. Ndugu Covington alikuwa na ujuzi mwingi sana wa kisheria. Hatimaye alishinda kesi za rufani 36 kati ya 45 katika Mahakama Kuu Zaidi ya Marekani.
Hali ikawa nafuu hatua kwa hatua kwa Mashahidi katika Kanada. Jengo la tawi katika Toronto lilirejeshwa mwaka wa 1944, na waliokuwa wakitumikia humo kabla ya marufuku waliweza kurudi. Mahakama kuu ya jimbo la Ontario ilitangaza mnamo mwaka wa 1945 kwamba watoto hawatalazimishwa kushiriki utendaji wanaokataa kwa kudhamiria. Iliamuru kwamba watoto waliofukuzwa shuleni wakubaliwe tena shuleni. Hatimaye, katika mwaka wa 1946 serikali ya Kanada iliwaachilia huru Mashahidi wote kutoka katika kambi za kazi ngumu. Huku nikielekezwa na Ndugu Covington, nilijifunza kutetea masuala hayo kwa ujasiri na azimio lakini, zaidi ya yote, kwa kumtegemea Yehova.
Pambano la Quebec
Ingawa sasa uhuru wa kidini wa Mashahidi wa Yehova uliheshimiwa katika sehemu nyingi za Kanada, sehemu moja ilikuwa tofauti—jimbo la Kikatoliki la Kifaransa la Quebec. Jimbo hilo lilidhibitiwa moja kwa moja kwa zaidi ya miaka 300 na Kanisa Katoliki. Shule, hospitali, na huduma nyingi za umma ama ziliendeshwa na makasisi au kudhibitiwa nao. Hata kulikuwa na kiti cha kadinali wa Katoliki kando ya kiti cha spika katika bunge la Quebec!
Waziri mkuu na mkuu wa sheria wa Quebec, Maurice Duplessis, alitumia mabavu, na kulingana na mwanahistoria wa Quebec Gérard Pelletier, alitesa jimbo hilo kwa “utawala wa miaka ishirini wa uwongo, ukosefu wa haki, ufisadi, uonevu wa hatua kwa hatua, kuwapotosha watu wenye akili finyu na kutukuza upumbavu.” Duplessis aliimarisha utawala wake wa kisiasa kwa kushirikiana bega kwa bega na Kadinali Mkatoliki Villeneuve.
Mwanzoni mwa miaka ya 1940, kulikuwa na Mashahidi 300 katika Quebec. Wengi wao, kutia ndani ndugu yangu Joe, walikuwa mapainia kutoka sehemu nyingine za Kanada. Kazi ya kuhubiri ilipopamba moto katika Quebec, polisi wa jimbo hilo wakishinikizwa na makasisi, waliwasumbua Mashahidi kwa kuwakamata mara nyingi na kutumia vibaya sheria ndogo za kibiashara kwa utendaji wetu wa kidini.
Nilikuwa nikisafiri kati ya Toronto na Quebec mara nyingi sana hivi kwamba hatimaye nilipewa mgawo wa kuhamia Quebec ili niwasaidie wanasheria wasio Mashahidi waliowakilisha ndugu na dada zetu Wakristo. Kila siku kazi yangu ya kwanza ilikuwa kujua ni wangapi waliokamatwa siku iliyotangulia na kwenda haraka mahakamani ili kushughulikia dhamana. Kwa uzuri, Frank Roncarelli, Shahidi aliyekuwa tajiri, alitoa dhamana katika kesi nyingi.
Toka mwaka wa 1944 hadi 1946, idadi ya walioshtakiwa kwa tuhuma za kukiuka sheria za jimbo iliongezeka kutoka 40 hadi 800! Mbali na mamlaka za serikali kuwashika na kuwanyanyasa Mashahidi bila kukoma, vikundi vya wafanya-ghasia wafidhuli waliwashambulia pia, huku wakichochewa na makasisi Wakatoliki.
Katika Novemba 2 na 3, mwaka wa 1946, mkutano wa pekee wa kushughulikia tatizo hilo ulifanywa huko Montreal. Ndugu Knorr alitoa hotuba ya mwisho, yenye kichwa “Tutafanya Nini?” Wahudhuriaji wote walifurahia jibu lake—alisoma kwa sauti ile trakti ya kihistoria ya Quebec’s Burning Hate for God and Christ and Freedom Is the Shame of All Canada. Ilikuwa trakti moto-moto yenye kurasa nne—ilitaja waziwazi majina, tarehe, na mahali pa ghasia zilizochochewa na makasisi, ukatili wa polisi, visa vya kutiwa mbaroni, na jeuri ya wafanya-ghasia dhidi ya Mashahidi wa Yehova katika Quebec. Ilisambazwa Kanada yote siku 12 tu baadaye.
Baada ya siku chache, Duplessis alitangaza hadharani “vita isiyo na huruma” dhidi ya Mashahidi wa Yehova. Lakini pasipo kujua alitusaidia. Jinsi gani? Kwa kuelekeza kwamba yeyote anayesambaza trakti ya Quebec’s Burning Hate ashtakiwe kwa kosa la uchochezi—kosa zito sana ambalo lingetufikisha kwenye Mahakama Kuu Zaidi ya Kanada kutoka kwa mahakama za Quebec. Duplessis mwenye hasira kali alipuuza tu matokeo hayo. Kisha yeye binafsi akaamuru leseni ya kuuza divai ya Frank Roncarelli ambaye alikuwa mdhamini wetu mkuu, ifutiliwe mbali. Mkahawa wenye faida wa Ndugu Roncarelli katika Montreal ulifungwa baada ya miezi michache kwa sababu ya ukosefu wa divai, naye akafilisika.
Wengi walitiwa mbaroni. Idadi ya walioshtakiwa iliongezeka upesi kutoka 800 hadi 1,600. Wanasheria wengi na mahakimu walilalamika kwamba kesi za Mashahidi wa Yehova zilijaza mahakama za Quebec. Katika kujibu, tulidokeza utatuzi sahili: Acheni polisi washike wahalifu badala ya Wakristo. Kufanya hivyo kutatatua tatizo hilo!
Wanasheria wawili Wayahudi walio jasiri, A. L. Stein wa Montreal na Sam S. Bard wa Quebec City, walitusaidia kwa kututetea katika kesi nyingi, hasa kabla sijapata kibali cha kuwa mshiriki wa baraza la wanasheria katika Quebec mnamo 1949. Pierre Elliott Trudeau, ambaye alikuja kuwa waziri mkuu wa Kanada baadaye, aliandika kwamba Mashahidi wa Yehova katika Quebec walikuwa “wamedhihakiwa, wamenyanyaswa, na kuchukiwa na jamii yetu yote, lakini wamefaulu kupambana kisheria na Kanisa, serikali, taifa, polisi, na maoni ya umma.”
Mtazamo wa mahakama za Quebec ulidhihirishwa na jinsi ambavyo walimtendea ndugu yangu, Joe. Alishtakiwa kwa kosa la kuvuruga amani. Hakimu wa manispaa Jean Mercier alimhukumu Joe kifungo kikali cha siku 60 gerezani. Kisha, akashindwa kabisa kujizuia, akapaaza sauti akiwa kitini ya kwamba angeliweza angelimfunga Joe kifungo cha maisha gerezani!
Gazeti moja lilisema kwamba Mercier aliwaamuru polisi wa Quebec “wamtie mbaroni mara moja kila Shahidi aliyejulikana au kutuhumiwa.” Zoea hilo lilithibitisha tu ukweli wa mashtaka yaliyokuwa katika trakti yetu ya Quebec’s Burning Hate. Vifuatavyo ni baadhi ya vichwa vilivyokuwa vya kawaida katika magazeti ya sehemu nyingine za Kanada mbali na Quebec: “Enzi za Giza Zarejea Quebec” (The Toronto Star), “Kurudi kwa Mabaraza ya Kuhukumu Wazushi” (The Globe and Mail, Toronto), “Kuzuka Tena kwa Ufashisti Mwovu” (The Gazette, Glace Bay, Nova Scotia).
Kujitetea Dhidi ya Shtaka la Uchochezi
Mnamo 1947, nilimsaidia Bw. Stein katika kesi yetu ya kwanza ya uchochezi, ya Aimé Boucher. Aimé alikuwa amesambaza trakti kadhaa ujiranini. Wakati wa kesi ya Aimé tulithibitisha kwamba trakti ya Quebec’s Burning Hate haikuwa na uwongo wowote bali ililaumu kwa maneno makali ukatili dhidi ya Mashahidi wa Yehova. Tulisema kwamba wale waliotenda ukatili huo hawakushtakiwa. Aimé alipatikana na hatia kwa ajili tu ya kutangaza hadharani ukatili huo. Alishtakiwa kwa kosa moja tu: Kusema kweli lilikuwa kosa la jinai!
Mahakama za Quebec zilitegemea ufasili usio yakini wa miaka 350 iliyopita wa “uchochezi,” ambao ulidokeza kwamba mtu yeyote anayechambua serikali aweza kushtakiwa kwa kosa la jinai. Duplessis pia alitegemea ufasili huo ili kukandamiza wachambuzi wa uongozi wake. Lakini katika mwaka wa 1950 Mahakama Kuu Zaidi ya Kanada ilikubali hoja yetu ya kwamba katika demokrasia ya kisasa, “uchochezi” huhusisha kuchochea jeuri au uasi dhidi ya serikali. Trakti ya Quebec’s Burning Hate haikuwa na uchochezi wa aina hiyo na kwa hiyo ilikuwa njia halali ya kujieleza kwa uhuru. Kwa uamuzi mmoja muhimu, kesi zote 123 za uchochezi zilifutiliwa mbali! Nilijionea binafsi jinsi ambavyo Yehova alitupatia ushindi.
Kupambana na Ukaguzi wa Vichapo
Quebec City lilikuwa na sheria iliyoharamisha usambazaji wa vichapo pasipo kibali cha mkuu wa polisi. Huu ulikuwa ukaguzi wa moja kwa moja na kwa hiyo ulikiuka uhuru wa kidini. Laurier Saumur, aliyekuwa mwangalizi asafiriye wakati huo, alikuwa amefungwa gerezani kwa miezi mitatu na alikabili mashtaka mengine kwa mujibu wa sheria hiyo.
Mnamo mwaka wa 1947 kesi ya madai ilifunguliwa kwa jina la Ndugu Saumur ili kuzuia Quebec City kutumia sheria yake dhidi ya Mashahidi wa Yehova. Mahakama za Quebec City ziliamua dhidi yetu, na tukakata rufani tena katika Mahakama Kuu Zaidi ya Kanada. Katika Oktoba 1953, baada ya siku saba za kusikizwa kwa kesi mbele ya mahakimu tisa wa Mahakama hiyo, ombi letu la amri ya kuzuia Quebec lilikubaliwa. Mahakama ilitambua kwamba kusambazwa hadharani kwa vichapo vya Biblia ni sehemu muhimu ya ibada ya Kikristo ya Mashahidi wa Yehova na hivyo vimelindwa kisheria dhidi ya ukaguzi.
Kwa hiyo, uamuzi wa kesi ya Boucher ulionyesha kwamba mambo waliyosema Mashahidi wa Yehova yalifaa kisheria; lakini uamuzi wa kesi ya Saumur ulidhihirisha namna na mahali yanapopasa kusemwa. Ushindi katika kesi ya Saumur ulifanya kesi 1,100 za mashtaka ya sheria ya Quebec zifutiliwe mbali. Zaidi ya kesi 500 huko Montreal pia zilifutiliwa mbali kwa sababu ya kukosekana kabisa kwa ushahidi. Muda si muda mashtaka yote yalifutiliwa mbali—hakukuwa na mshtakiwa yeyote katika Quebec!
Shambulizi la Mwisho la Duplessis
Duplessis alipokosa sheria yoyote ya kutumia dhidi ya Mashahidi wa Yehova, alitunga sheria mpya bungeni mapema Januari mwaka wa 1954, Mswada nambari 38, ulioitwa na vyombo vya habari ‘sheria dhidi ya Mashahidi wa Yehova.’ Ilitaarifu kwamba yeyote aliyeshuku kwamba mtu fulani alinuia kusema jambo lenye “matusi au lenye kuudhi” angeweza kuwasilisha lalamiko lake bila uthibitisho. Akiwa mkuu wa sheria, Duplessis angeweza kupokea idhini ya kumzuia mshtakiwa kutoa taarifa yoyote hadharani. Mara baada ya kumwekea vikwazo mtu mmoja, washiriki wote wa kanisa analoshirikiana nalo wangezuiwa pia kusema hadharani. Isitoshe, Biblia zote na vichapo vya kidini vya kanisa hilo vingechukuliwa na kuharibiwa, na sehemu zote za ibada zingefungwa hadi kesi hiyo ilipoamuliwa, labda baada ya miaka mingi.
Mswada nambari 38 ulifanana na sheria iliyotungwa katika karne ya 15 wakati wa Baraza la Hispania la Kuhukumu Wazushi chini ya Torquemada. Mshtakiwa na washiriki wake wote walinyimwa haki zote za raia pasipo uthibitisho wa kosa. Kuhusu Mswada nambari 38, vyombo vya habari vilitangaza kwamba polisi wa jimbo hilo walikuwa wameamriwa wafunge Majumba yote ya Ufalme ya Mashahidi wa Yehova na kukusanya na kuharibu Biblia zao na vichapo vingine. Wakikabili tisho hilo la kuogofya, Mashahidi wa Yehova walihamisha vichapo vyao vya kidini vyote kutoka katika jimbo hilo. Hata hivyo, waliendelea na kazi yao ya kuhubiri peupe lakini walitumia nakala zao binafsi za Biblia tu.
Mswada huo ukawa sheria katika Januari 28, 1954. Katika Januari 29, saa tatu asubuhi, nilifika mahakamani ili nifungue madai kwa niaba ya Mashahidi wa Yehova katika jimbo la Quebec, na kuomba mahakama itoe amri ya kukomesha kabisa hiyo sheria kabla Duplessis hajaitekeleza. Hakimu hakutoa amri ya kuikomesha kwa muda kwa sababu Mswada nambari 38 haukuwa umetekelezwa bado. Lakini alisema kwamba endapo serikali itajaribu kuutumia, ningeweza kumfikia ili nipate ulinzi. Kwa hiyo uamuzi wa hakimu huyo ulikomesha sheria hiyo kwa muda, kwa kuwa Duplessis angezuiwa mara moja kujaribu kutumia sheria hiyo!
Juma lililofuata, tulisubiri kuona iwapo polisi wangetekeleza sheria hiyo mpya. Hawakuchukua hatua yoyote! Ili kujua sababu, nilipanga kuwajaribu. Mapainia wawili, Victoria Dougaluk (baadaye aliitwa Steele) na Helen Dougaluk (baadaye aliitwa Simcox), walienda nyumba kwa nyumba wakiwa na vichapo huko Trois-Rivières, alikozaliwa Duplessis. Kwa mara nyingine polisi hawakufanya lolote. Dada hao walipokuwa wakihubiri, nilimtuma Laurier Saumur awapigie simu polisi wa jimbo. Pasipo kujitambulisha, alilalamika kwamba Mashahidi wa Yehova walikuwa wakihubiri na kwamba polisi hawakuwa wakitekeleza sheria mpya ya Duplessis.
Kwa aibu, ofisa huyo msimamizi akasema: “Naam, twajua kwamba sheria hiyo ilipitishwa; lakini siku iliyofuata Mashahidi wa Yehova waliomba mahakama ituzuie kuitekeleza, kwa hiyo hatuwezi kufanya lolote.” Mara moja, tulirejesha vichapo vyetu kwenye jimbo, na katika miaka kumi ya kusikizwa kwa rufani ya kesi yetu, kazi yetu ya kuhubiri iliendelea kwa mafanikio.
Pamoja na kuomba amri ya kukomesha sheria hiyo, tuliomba pia Mswada nambari 38 utangazwe kuwa kinyume cha katiba. Ili kuthibitisha kwamba sheria hiyo ilitungwa dhidi ya Mashahidi wa Yehova hasa, tuliamua kuchukua hatua madhubuti—tulimtumia Duplessis hati ya kumwita mahakamani, iliyombidi ahudhurie na kutoa ushahidi wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo. Nilimhoji kwa saa mbili na nusu. Mara kwa mara nilimwuliza kuhusu tangazo lake la hadharani la “vita isiyo na huruma dhidi ya Mashahidi wa Yehova” na taarifa yake ya kwamba Mswada nambari 38 ungewakomesha Mashahidi wa Yehova katika Quebec. Kwa hasira kali, alinishambulia: “Wewe ni kijana mfidhuli sana!”
“Bw. Duplessis,” nikamjibu, “kama tungekuwa tunazungumzia sifa za watu, singesema mengi kuhusu utu wako. Lakini kwa kuwa tunashughulikia mambo mazito sana, waweza kueleza mahakama kwa nini hukujibu swali la mwisho nililokuuliza.”
Mnamo mwaka wa 1964, niliwasilisha Mswada nambari 38 mbele ya Mahakama Kuu Zaidi ya Kanada. Lakini walikataa kuamua kuhusu kuwa kwake kinyume cha katiba kwa sababu sheria hiyo haikuwahi kutumiwa. Hata hivyo, wakati huo Duplessis alikuwa amekufa, na hakuna mtu aliyejali tena Mswada nambari 38. Haukuwahi kutumiwa dhidi ya Mashahidi wa Yehova wala mtu mwingine yeyote.
Muda mfupi kabla ya kifo chake mnamo 1959, Duplessis aliamriwa na Mahakama Kuu Zaidi ya Kanada amlipe ridhaa Ndugu Roncarelli kwa sababu ya kufuta kwa njia isiyo halali leseni yake ya kuuza divai. Tangu wakati huo wengi wa wakazi wa Quebec wamekuwa na urafiki mno. Kulingana na hesabu ya serikali, idadi ya Mashahidi huko imeongezeka toka 300 mwaka wa 1943 hadi zaidi ya 33,000 leo. Sasa Mashahidi wa Yehova wameorodheshwa kuwa kikundi cha nne cha kidini kwa ukubwa katika jimbo hilo. Mimi sioni ushindi huo wa kisheria au mafanikio ya huduma ya Mashahidi wa Yehova kuwa ushindi wa mwanadamu yeyote. Badala yake, umenithibitishia kwamba Yehova hutoa ushindi, kwa kuwa vita si yetu bali ni yake.—2 Mambo ya Nyakati 20:15.
Kubadilika kwa Hali
Mwaka wa 1954, nilimwoa painia mrembo kutoka Uingereza, Margaret Biegel, na tukafanya upainia pamoja. Niliendelea kushughulikia kesi mahakamani kwa niaba ya Mashahidi wa Yehova katika Kanada na Marekani na kutumika nikiwa mshauri katika baadhi ya kesi huko Ulaya na Australia. Margaret akawa mwandishi wangu na alinitegemeza sana kwa miaka mingi. Mnamo mwaka wa 1984, mimi na Margaret tulirudi katika ofisi ya tawi ya Kanada, na nilisaidia kuanzisha tena Idara ya Sheria. Kwa kusikitisha, Margaret alikufa kutokana na kansa mnamo 1987.
Baada ya mama yangu kufa mwaka wa 1969, ndugu yangu Joe na mkewe, Elsie, wamishonari waliozoezwa wa darasa la tisa la Shule ya Biblia ya Gileadi ya Watchtower, walimchukua baba yangu nyumbani mwao na kumtunza hadi alipokufa miaka 16 baadaye. Kwa sababu ya kujidhabihu kwao, niliweza kuendelea na utumishi wa wakati wote, nami nawashukuru daima kwa sababu hiyo.
Mapambano Zaidi
Miaka baada ya miaka, mapambano ya kisheria ya Mashahidi wa Yehova yamebadilika. Kesi nyingi zilihusu kupata ardhi kwa ajili ya Majumba ya Ufalme na Majumba ya Kusanyiko. Nyingine zilihusisha ubishi kuhusu malezi ya mtoto ambapo wazazi wasio Mashahidi walitumia ushupavu wa kidini ama kupata kibali cha kuwalea ama kuwazuia wazazi Mashahidi kushiriki na watoto wao itikadi na mazoea ya kidini yanayonufaisha.
Mwanasheria Mmarekani, Linda Manning, alizuru ofisi ya tawi ya Kanada mwaka wa 1989 ili kusaidia kwa muda kuhusu mambo ya kisheria. Tulifunga ndoa katika Novemba mwaka huo, na tangu wakati huo tumekuwa tukitumikia pamoja kwa furaha hapa.
Miaka ya 1990, mimi pamoja na John Burns, mwanasheria mwenzi katika ofisi ya Kanada, tulienda Japani kuwasaidia ndugu zetu Wakristo kushinda kesi ya kikatiba iliyohusu uhuru wa mwanafunzi wa kutoshiriki somo la judo na karate lililoamriwa na shule. Tulishinda pia kesi iliyohusu haki ya mtu mzima ya kukataa kutiwa damu mishipani.
Kisha mwaka wa 1995 na 1996, mimi na Linda tulikuwa na pendeleo la kuwa Singapore kwa muda wa miezi mitano kwa sababu ya marufuku na mnyanyaso dhidi ya Mashahidi wa Yehova katika nchi hiyo. Nilitetea wanaume, wanawake na vijana 64 waliokabili makosa ya jinai kwa sababu ya kuhudhuria mikutano ya Kikristo na kuwa na Biblia na vichapo vya kidini. Hatukushinda yoyote ya kesi hizo, lakini tuliona jinsi Yehova alivyowaimarisha watumishi wake waaminifu kuvumilia kwa uaminifu-maadili wakiwa na shangwe.
Tunashukuru kwa Sababu ya Kushiriki
Nikiwa na umri wa miaka 80, ninafurahi kuwa na afya nzuri na kuweza kuendelea kushiriki katika kupambana vita vya kisheria vya watu wa Yehova. Bado ningali tayari kwenda mahakamani na kutetea yaliyo haki. Ni pendeleo langu kuona idadi ya Mashahidi katika Kanada ikiongezeka kutoka 4,000 katika 1940 hadi 111,000 sasa. Watu na matukio hubadilika, lakini Yehova huendelea daima kuwaongoza watu wake, akihakikisha kwamba wanasitawi kiroho.
Je, kuna matatizo? Yako, lakini Neno la Yehova hutuhakikishia hivi: “Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa.” (Isaya 54:17) Nikichunguza zaidi ya miaka 56 niliyotumia katika huduma ya wakati wote ‘nikitetea na kuthibitisha kisheria habari njema,’ naweza kushuhudia jinsi unabii wa Isaya ulivyo wa kweli!—Wafilipi 1:7.
[Picha katika ukurasa wa 19]
Nikiwa na ndugu yangu mdogo na wazazi wetu
[Picha katika ukurasa wa 19]
Hayden Covington, mshauri wa sheria
[Picha katika ukurasa wa 19]
Nikiwa na Nathan Knorr
[Picha katika ukurasa wa 20]
Duplessis akimpigia magoti Kadinali Villeneuve
[Hisani]
Photo by W. R. Edwards
[Picha katika ukurasa wa 20]
Frank Roncarelli
[Hisani]
Courtesy Canada Wide
[Picha katika ukurasa wa 21]
Aimé Boucher
[Picha katika ukurasa wa 24]
Nikiwa na wanasheria wenzi John Burns na mke wangu Linda