Nyavu za Kichina za Kuvulia Samaki Ziko India
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA INDIA
MJI wa Kochi, uliokuwa ukiitwa Cochin uko kwenye pwani ya magharibi ya India, umbali wa kilometa 250 kutoka kwenye ncha ya kusini mwa bara Hindi. Nyavu za ajabu za shikizowenza zenye mtindo wa Kichina zimesambaa kwenye kingo za hiyo ghuba ndogo. Zilifikaje huko?
Wachina waliishi kwenye eneo hilo kuanzia karne ya nane W.K. na kuendelea, na yaaminika kwamba wafanya-biashara Wachina kutoka kwa jamii ya kifalme ya Kublai Khan walileta nyavu za aina hiyo mara ya kwanza katika Cochin kabla ya mwaka wa 1400. Kuna samaki wengi ukingoni mwa ghuba kuzunguka Cochin. Hivyo, mashine hizo ndefu za kuvulia samaki zinazoendeshwa na wanadamu zilitumiwa sana kwa zaidi ya karne moja, hadi Waarabu walipowafukuza Wachina.
Nyavu hizo ziliondolewa baada ya Wachina kwenda. Lakini mapema katika karne ya 16, Wareno waliwashinda Waarabu. Kwa wazi, ni Wareno waliorudisha tena nyavu za aina hiyo katika Cochin, walizileta kutoka kwa kisiwa kilichokuwa kikitawaliwa na Wareno cha Macao kusini-mashariki ya China.
Japo mbinu hiyo ni ya kale sana, bado nyavu za Kichina hufanya kazi vizuri zikiwa na muundo uleule wa awali na hufanya kazi kama zamani. Na bado huwaandalia wavuvi wengi riziki na watu wengi chakula. Kwa kweli, wavu mmoja waweza kuvua samaki wa kutosha kulisha kijiji kizima. Lakini mbali na kuvua kwa matokeo, nyavu hizo ni maridadi pia, hasa zing’aapo ajabu katika anga zuri mno wakati wa asubuhi au jioni.
Hufanyaje Kazi?
Nyavu kubwa mno za Kichina huwa na egemeo na uzani wa kusawazisha wavu na samaki waliovuliwa. Wavu huo na fremu ya kuutegemeza huinuliwa juu kutoka majini unapokuwa hautumiwi. Uvuvi huanza mapema alfajiri na huendelea kwa muda wa saa nne au tano. Nyavu hizo hushushwa taratibu majini. Ili kuzishusha, ama wavuvi husawazisha uzito ulio upande mmoja wa mfumo huo wa kusawazisha au kiongozi wa kikundi hicho cha wavuvi hutembea juu ya mhimili mkuu wa wavu. Wavu huachwa majini kwa muda wa dakika 5 hadi 20 kabla ya kuinuliwa taratibu, na kuchota samaki wanaoogelea karibu na ufuo. Kiongozi mwenye ujuzi wa miaka mingi hujua wakati barabara wa kuvuta wavu juu.
Kiongozi atoapo ishara, wavuvi wengine wapatao watano au sita huinua wavu huku wakivuta chini kamba zilizofungiliwa mawe ya kusawazisha. Wavu uinukapo, pembe za wavu huibuka kwanza. Hivyo, wavu wenye samaki huwa na umbo la bakuli. Ni jambo lenye kuwasisimua kama nini wavuvi hao! Baada ya kuvua samaki wengi, wanapigana-pigana makofi mgongoni ili kuonyesha furaha yao. Baadaye samaki hao watanunuliwa na wafanya-biashara, wake wa nyumbani, na watalii wanaozuru mara kwa mara.
Wachina, Waarabu, na Wareno wamekuwapo na kutokomea. Lakini nyavu za Kichina huibuka-ibuka katika ghuba ya Kochi, sawa na zilivyofanya zaidi ya miaka 600 iliyopita.
[Ramani katika ukurasa wa 31]
Kochi
[Hisani]
Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.