Vipepeo, Mimea na Siafu Wenye Uhusiano Muhimu
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UHOLANZI
KATIKA mwezi wa Julai, vipepeo wenye kuvutia wa Ulaya Magharibi hujua kwamba ni wakati wa kuzaa kizazi kipya cha vipepeo. Ili kutokeza kizazi kipya, vipepeo hao wanahitaji mambo mengi mbali na wenzi. Wanahitaji pia maua yenye rangi ya samawati yanayomea eneo lenye majimaji na siafu wekundu wenye njaa. Kwa nini? Mimea na siafu wanahusikaje katika maisha ya vipepeo hao?
Unaweza kuchunguza uhusiano huo wenye kupendeza wa vitu hivyo vitatu katika Mbuga ya Taifa ya Dwingelderveld iliyoko sehemu ya kaskazini mwa Uholanzi. Katika mbuga hiyo kuna vipepeo hao wengi wa rangi ya samawati. Katika majira ya kuchipua na ya kiangazi maua mengi yenye rangi mbalimbali humea katika mbuga ya Dwingelderveld. Kuna maua ya samawati ya eneo lenye majimaji (gentiani), maua ya mbugani nyekundu hafifu, na maua aina ya yungiyungi ya manjano. Vipepeo hao wa samawati wanapenda hasa maua madogo ya mbugani yenye kuvutia na maua ya samawati ya eneo lenye majimaji. Lakini wanayapenda kwa sababu mbili tofauti. Maua ya mbugani yana umajimaji mtamu mwingi ambao vipepeo wanapenda, na maua ya eneo la majimaji ni mahali pazuri pa kuhifadhia vitu. Lakini vipepeo watahifadhi nini hapo?
Mbinu ya Kuokoka
Baada ya kujamiiana kipepeo wa kike anatafuta ua la eneo lenye majimaji ambalo ni refu kuliko mimea mingine katika sehemu hiyo. Kipepeo anatua kwenye ua hilo na kutaga mayai meupe machache. Baada ya siku nne hadi kumi, mayai hayo huanguliwa, na viwavi wawili hadi sita wanaanza maisha yao kwa kuingia katika chipukizi la ua na kukaa humo. Baada ya kula kwa majuma mawili au matatu mfululizo, viwavi huteremka chini.
Kwa kawaida kiwavi huteremka wakati wa jioni. Jambo hilo ni muhimu, kwa kuwa aina mbili ya siafu wekundu, ambao pia huishi katika mbuga hiyo, hutoka katika viota vyao jioni ili kutafuta chakula. Kiwavi anapoteremka kwenye ua anashuka njiani mwa siafu hao wanaotafuta chakula. Huenda ikaonekana kana kwamba kiwavi anataka kujiua, lakini sivyo ilivyo, hiyo ni mbinu ya kuokoka. Vipi baada ya hapo?
Punde si punde siafu kadhaa hukutana na kiwavi anayelala njiani. Upesi wanamburuta kiwavi hadi kwenye kiota chao. Kiwavi hutendewa kama mgeni wa heshima naye huishi kiotani kwa usalama na raha. Humo mna chakula tele, kufikia majira ya kiangazi yanayofuata mwaka ujao. Kiwavi hali chakula cha aina nyingi, mafunza ya siafu na chakula chake kikuu, chakula ambacho siafu wafanyakazi wametapika. Hata hivyo, siafu pia hupata manufaa kupitia mpango huo. Siafu hukamua kwa ukawaida kiwavi ili wapate ule umajimaji mtamu ambao kiwavi hutokeza. Hata kiwavi anapogeuka kuwa buu, siafu wanaendelea kumkamua ili wapate umajimaji ule mtamu na vilevile umajimaji mwingine ambao siafu hupenda. Hata hivyo kiwavi anapofikia hatua ya kuwa buu uhusiano huo wenye manufaa huelekea kukoma.
Mgeni Amekuwa Mvamizi
Katika hatua ya kuwa kifukofuko, kiwavi anaanza kugeuka kuwa kipepeo. Wakati ambapo kipepeo amekomaa ndani ya kifukofuko, gamba lake linapasuka na kipepeo hutoka. Kwa kawaida jambo hilo hutukia mapema asubuhi. Kwa nini? Kwa sababu siafu hawawi macho sana mapema asubuhi. Na hali ni tofauti wakati huu kuliko wakati kiwavi alipoteremka uani. Kiwavi alipoteremka uani alitaka siafu wamwone, lakini sasa ni afadhali sana siafu wasimwone.
Hatimaye siafu wanapokuja kukamua kifukofuko, wanashtuka kumwona kiumbe mgeni mwenye mabawa kiotani, na mara moja wanamshambulia huyo mvamizi. Kiwavi, ambaye amegeuka kuwa kipepeo, anatoka kiotani haraka ajiokoe. Kisha, kipepeo anapanda tawi na siafu wanaacha kumkimbiza.
Anapokuwa mahali salama, kipepeo anatandaza mabawa yake yakauke. Hatimaye, tukio kuu maishani mwake limewadia. Kipepeo anapigapiga mabawa yake na kuruka, baada ya mwaka mmoja hivi tangu aanguliwe. Unamwona kule, akirukaruka mbugani! Baada ya siku chache tu atajamiiana, na punde si punde ataanza kutafuta ua refu la samawati la mbugani. Huo ni wakati wa kufanya matayarisho ya kutokeza kizazi kipya cha vipepeo.
[Sanduku katika ukurasa wa 18]
Kipepeo Hatarini
Makao ya kipepeo wa samawati ni mbuga. Katika Ulaya Magharibi mbuga zinapatikana mahali ambapo watu walikata misitu ya awali mamia ya miaka iliyopita. Zamani za kale, mbuga zenye maua ya zambarau zilikuwa kubwa sana. Sehemu kubwa za nchi za Ubelgiji, Ujerumani, na Uholanzi zilikuwa mbuga. Hata hivyo, sehemu ndogondogo tu ya mbuga ambazo zimetapakaa huku na huku zinabaki siku hizi. Kwa hiyo, vipepeo wa samawati wanapoteza makao yao kwa haraka. Katika muda wa miaka kumi iliyopita, kipepeo huyo ametoweka katika sehemu 57 kati ya makao yake 136 ya asili nchini Uholanzi. Kwa kweli kipepeo huyo yumo hatarini kiasi cha kwamba ameorodheshwa kwenye Orodha ya Ulaya ya Vipepeo Waliomo Hatarini. Orodha hiyo, ambayo imetayarishwa na Baraza la Ulaya, inaorodhesha majina ya vipepeo ambao wamo hatarini.
Ili Mbuga ya Taifa ya Dwingelderveld idumu kuwa makao salama ya kipepeo wa samawati, watunzaji wanajaribu kuihifadhi mbuga hiyo kwa kuchunga mifugo hapo jinsi wafugaji walivyofanya mamia ya miaka iliyopita. Kama zamani za kale, wachungaji wanachunga makundi ya kondoo mbugani, na ng’ombe wanalisha kwenye makonde yenye nyasi ngumu. Ng’ombe na kondoo wanapolisha wanaondoa mimea fulani na kwa njia hiyo mimea mbalimbali ya mbugani inaweza kumea vizuri. (Kwa sasa, kuna jamii 580 za mimea katika mbuga hiyo.) Na kwa sababu hiyo vipepeo wa samawati wa Dwingelderveld wanaongezeka idadi. Mbuga hiyo kubwa ni muhimu kuliko mbuga zote za Ulaya, ni makao mazuri sana kwa vipepeo wote hivi kwamba asilimia 60 ya vipepeo wote wa Uholanzi wanapatikana huko.
[Picha katika ukurasa wa 16]
Kipepeo anataga mayai yake kwenye ua la samawati la eneo lenye majimaji
[Picha katika ukurasa wa 17]
Siafu wanaotunza mabuu
[Hisani]
Siafu kwenye ukurasa 16 na 17: Pictures by David Nash; www.zi.ku.dk/personal/drnash/atta/
[Picha katika ukurasa wa 17]
Ua jekundu hafifu la mbugani
[Picha katika ukurasa wa 17]
Ua la manjano aina ya yungiyungi la eneo lenye majimaji
[Picha katika ukurasa wa 18]
Kondoo na mifugo husaidia kudumisha makao ya kipepeo huyo