Mnyanyaso wa Kidini Huko Georgia Utaendelea Hadi Lini?
KUANZIA PWANI YA BAHARI NYEUSI yenye joto la wastani hadi Milima ya Caucasus, kuna mandhari maridadi kotekote nchini Georgia. Eneo hilo lililoko kwenye mpaka wa Ulaya na Asia lina milima, misitu, mito yenye kutiririka kwa kasi, na mabonde yenye miti na mimea mingi. Tbilisi, jiji kuu la Georgia, ni jiji la pilikapilika na lina majengo ya makumbusho ya kale na majengo ya kisasa. Lakini jambo linalovutia hasa nchini Georgia ni watu wake walio wakarimu na walio na familia zilizoungana.
Watu wa Georgia wamekandamizwa tangu zamani. Nchi yao imevamiwa na Waroma, Waajemi, Waarabu, Waturuki, Warusi, Wamongolia, watu wa Byzantium, na wengineo. Imekadiriwa kwamba jiji la Tbilisi limeharibiwa mara 29!a Hata hivyo, watu wa Georgia bado wanapenda maisha, sanaa, kuimba, na kucheza dansi. Wanajulikana pia kuwa wavumilivu.
Hata hivyo, watu wengine wa Georgia hawafanyi hivyo tena. Kwa muda wa miaka miwili iliyopita, watu wachache wa Georgia wameharibu sifa nzuri ya nchi yao kwa kuwashambulia mamia ya wananchi wenzao. Washambuliaji wenye ghasia wamewapiga wanaume, wanawake, na watoto na hata wazee na walemavu, wasio na hatia. Washambuliaji wamewapiga watu hao na kuwajeruhi vibaya nyusoni na vichwani kwa rungu zenye misumari na za chuma. Kwa nini wananchi wengine wa Georgia wenye amani wanapigwa sana? Kwa sababu wao ni Mashahidi wa Yehova—jamii ya Kikristo ambayo imekuwapo Georgia hata kabla ya wengi wa washambuliaji hao kuzaliwa.
Mashutumu na Mashambulio
Ijapokuwa kuna uhuru wa dini nchini Georgia, Mashahidi wa Yehova wamenyang’anywa vichapo vyao mara nyingi. Mnamo Aprili 1999, maafisa wa forodha walisema kwamba vichapo vingeweza kuingizwa nchini tu kwa kibali cha askofu mkuu wa Kanisa Othodoksi la Georgia.b Mwezi uliofuata, kanisa hilo lilitajwa tena—wakati huo, katika Mahakama ya Wilaya ya Isani-Samgori huko Georgia. Guram Sharadze, mwakilishi wa mbunge na kiongozi wa kikundi cha kisiasa cha “Georgia Juu!,” alifungua kesi ya kufuta usajili wa mashirika yanayotumiwa na Mashahidi wa Yehova. Aliwashtaki Mashahidi wa Yehova kuwa watu hatari wasiopenda taifa lao. Mashtaka ya Sharadze yaliungwa mkono na nani? Waraka wa kesi hiyo uliambatanishwa na barua kutoka kwa karani wa Askofu Mkuu wa Kanisa Othodoksi la Georgia Nzima.
Katika Mei 20, 1999, serikali ya Georgia ilitia sahihi Mkataba wa Ulaya wa Kulinda Uhuru na Haki za Binadamu. Hivyo, serikali ya Georgia ilijiwajibisha kufuata vifungu vya mkataba huo. Kifungu cha 10 cha mkataba huo kinasema: “Kila mtu ana uhuru wa kusema. Uhuru huo unatia ndani haki ya kila mtu ya kuwa na maoni yake na kupokea na kusambaza habari na maoni katika nchi yoyote ile bila kuzuiwa na mamlaka.” Je, mkataba huo uliwazuia wapinzani wa Mashahidi wa Yehova wasijaribu tena kupiga marufuku vichapo vya kidini? Hata kidogo!
Katika Juni 21, 1999, mwakilishi wa Askofu Mkuu wa Georgia Nzima alimwandikia afisa mkuu wa forodha barua, na kusisitiza kwamba “usambazaji wa vichapo vya kidini vya kigeni upigwe marufuku.” Isitoshe, Giorgi Andriadze, mwakilishi wa Kanisa Othodoksi la Georgia, alitangaza kwamba Mashahidi wa Yehova ni watu hatari na inafaa wapigwe marufuku. Mashutumu hayo hayakuambulia patupu. Watu wanaoshikilia dini kupindukia, waliokuwa wameteketeza vichapo vya Mashahidi wa Yehova hapo awali, waliposikia mashutumu hayo walijua kwamba wangeweza kuwashambulia Mashahidi bila kuadhibiwa. Waliwashambulia tena Jumapili, Oktoba 17, 1999.
Washambuliaji Hawajaadhibiwa
Mashahidi wa Yehova 120 huko Tbilisi—wanaume, wanawake, na watoto—walikuwa kwenye mkutano wa kidini Jumapili hiyo. Ghafula, Vasili Mkalavishvili, aliyeachishwa upadre katika Kanisa Othodoksi, na wafuasi wake 200 walivamia mkutano huo.c Waliwazingira Mashahidi hao na kuwapiga tena na tena kwa rungu zao za mbao na misalaba ya chuma. Washambuliaji wanne walishika mikono na shingo ya Shahidi mmoja. Wakainamisha kichwa chake na kuanza kumnyoa, huku wale washambuliaji wengine wakicheka. Washambuliaji hao wenye ghasia walipoondoka hatimaye, Mashahidi 16 walipelekwa hospitalini. Mwanamume mmoja alivunjika mbavu tatu. Baadaye, Shahidi mwingine, mwanamke mwenye umri wa miaka 40 anayeitwa Phati, alisema hivi: “Walianza kunipigia kelele, na mmoja wao alinipiga kwa nguvu. Alinipiga uso na macho. Nilijaribu kujikinga kwa mikono yangu, huku damu ikitiririka katikati ya vidole vyangu.” Mtu huyo katili alipoacha kumpiga Phati, jicho lake la kushoto lilikuwa limepofuka. Jicho la Phati halijapona hadi leo.
Rais Eduard Shevardnadze alishutumu shambulio hilo baya lililoonyeshwa kwenye televisheni. Kesho yake alisema hivi: “Ninashutumu shambulio hilo, na mamlaka zinazotekeleza sheria zinapaswa kufungua kesi ya uhalifu.” Kwa kuwa kiongozi wa ghasia hiyo na washambuliaji wengine walirekodiwa kwenye video ingekuwa rahisi kuwapata na hatia. Hata hivyo, miaka miwili imepita na hakuna hata mmoja kati ya washambuliaji hao ambaye amehukumiwa.
Mashambulio Yamezidi
Haishangazi kwamba washambuliaji walizidisha mashambulio walipoona kwamba serikali na makanisa hayakuchukua hatua yoyote. Kwa sababu hawakuhukumiwa, washambuliaji walizidi kuwaibia, kuwachapa, na kuwapiga mateke Mashahidi wa Yehova wakiwa nyumbani kwao, barabarani, na kwenye mahali pa ibada. Zaidi ya mashambulio 80 yaliyorekodiwa yalifanywa kati ya Oktoba 1999 na Agosti 2001, na zaidi ya Mashahidi wa Yehova 1,000 waliathiriwa. Hata hivyo, katika Februari 9, 2001, mwendesha mashtaka wa jiji la Tbilisi aliwaambia waandishi wa habari kwamba Vasili Mkalavishvili “bado anachunguzwa.” Jambo la kusikitisha ni kwamba, mamlaka ya Georgia bado inaruhusu wapinzani wa Mashahidi wa Yehova hadi leo hii kufanya matendo ya uhalifu yanayosababishwa na chuki.—Soma sanduku “Mashambulio Yanaendelea.”
Vipi polisi? Habari za magazeti, na video zinaonyesha kwamba polisi waliruhusu na kushiriki mashambulio hayo dhidi ya Mashahidi wa Yehova! Kwa mfano, katika Septemba 8, 2000, polisi wenye rungu waliuvamia mkusanyiko wenye amani wa Mashahidi wa Yehova uliohudhuriwa na watu 700 huko Zugdidi. Watu waliojionea mambo hayo walisema kwamba polisi waliofunika nyuso waliwapiga zaidi ya Mashahidi 50. Mwenye uwanja huo alisema kwamba ‘alihuzunishwa sana’ kuona jinsi watoto walivyotishwa wakati makombora matupu ya mzinga yalipofyatuliwa hewani. Polisi walivamia uwanja na kuuteketeza. Hata hivyo, hawajaadhibiwa hadi leo.
Mashambulio maovu kama hayo yametukia mara nyingi (soma sanduku “Polisi Walishiriki”). Kwa hiyo, katika Mei 7, 2001, Kamati ya Umoja wa Mataifa Dhidi ya Mateso ilisema kwamba imefadhaishwa na ‘mateso ya mara kwa mara, na matendo mengine ya kikatili, ya kinyama au ya kuvunjia watu heshima, yanayofanywa na watu walio na wajibu wa kutekeleza sheria huko Georgia. Na imefadhaishwa pia na ukosefu wa kuchunguza mara moja bila ubaguzi matukio mengi sana ambayo yanasemekana yalihusisha mateso.’d Mashahidi wa Yehova wameripoti zaidi ya malalamiko 400 kwa polisi. Lakini, ijapokuwa wakosaji wote wanajulikana, hakuna hata mmoja ambaye amehukumiwa! Mchunguzi wa Malalamiko ya Wananchi wa Georgia, ambaye huchaguliwa na bunge, alisema hivi: “Watu walio na daraka la kuzitetea haki za binadamu ndio wanaozikiuka. Kwa watu hao, haki za binadamu hazina maana yoyote.”
Uamuzi wa Mahakama Kuu Usioeleweka
Kuongezea mashambulio yasiyo halali yaliyofanywa na wafanya-ghasia na polisi, hivi majuzi Mahakama Kuu ya Georgia ilitoa uamuzi uliowapotosha watu kuhusiana na haki za Mashahidi wa Yehova.
Tuanze nyuma kidogo. Mwanasiasa Guram Sharadze alifungua kesi ya kufuta usajili wa mashirika yanayotumiwa na Mashahidi wa Yehova. Kesi yake ilitupiliwa mbali katika Februari 29, 2000. Hata hivyo, Sharadze alikata rufani na akashinda. Kisha Mashahidi wa Yehova wakakata rufani katika Mahakama Kuu. Katika Februari 22, 2001, Mahakama Kuu iliamua kesi dhidi ya Mashahidi eti kwa sababu ya kanuni za kisheria. Mahakama Kuu iliamua kwamba kulingana na Katiba, dini zapasa kusajiliwa kufuatana na sheria ya kusajili mashirika ya kidini, ijapokuwa sheria hiyo haijatungwa bado. Mahakama hiyo iliamua kwamba dini ya Mashahidi wa Yehova ingeweza kusajiliwa kwa njia hiyo pekee. Hata hivyo, mashirika mengine 15 ya kidini yamesajiliwa huko Georgia bila kufuata sheria hiyo.
Waziri wa Sheria wa Georgia, Mikheil Saakashvili, alisema hivi alipohojiwa kwenye televisheni: “Uamuzi huo unaweza kutiliwa shaka kisheria. Sidhani kwamba Mahakama Kuu iliamua vizuri.” Mwakilishi wa mwenyekiti wa halmashauri ya kisheria ya bunge la Georgia, Zurab Adeishvili, alimwambia mwakilishi wa Shirika la Habari la Keston kwamba alikuwa na “wasiwasi sana” juu ya uamuzi huo kwa kuwa “unawatia moyo watu wanaoshikilia dini kupindukia katika Kanisa letu [la Othodoksi la Georgia] kukandamiza dini ndogo.” Jambo la kusikitisha ni kwamba hangaiko la Adeishvili halikuwa la bure. Siku chache baada ya uamuzi huo kutolewa, Mashahidi wa Yehova walishambuliwa tena. Katika mwaka wa 2001, Mashahidi walishambuliwa na wafanya-ghasia, polisi, na makasisi wa Kanisa Othodoksi katika tarehe zifuatazo: Februari 27, Machi 5, Machi 6, Machi 27, Aprili 1, Aprili 7, Aprili 29, Aprili 30, Mei 7, Mei 20, Juni 8, Juni 17, Julai 11, Agosti 12, Septemba 28, na Septemba 30. Na ujeuri bado unaendelea.
Mnyanyaso ulipoongezeka tena, Mahakama Kuu ilichukua hatua isiyo ya kawaida ya kueleza uamuzi wake hadharani kwa kusema: ‘Jambo la kusikitisha ni kwamba watu wameelewa vibaya uamuzi wa Mahakama Kuu wa kufuta usajili wa Shirika la Mashahidi wa Yehova. Usajili wa mashirika yao ulipofutwa, hiyo haikumaanisha kwamba uhuru wao wa maoni, dhamiri na wa kidini ulizuiwa wala kukandamizwa. Uhuru wao wa kubadili dini, wakiwa mtu mmoja-mmoja au wakiwa pamoja na wengine, peupe au faraghani, haukuzuiwa. Mahakama haijawakataza Mashahidi wasipokee wala wasisambaze habari zinazohusu imani yao. Haikuondoa haki yao ya kukutanika kwa amani.’
Maelfu Huko Georgia Wanashutumu Mnyanyaso
Ijapokuwa maneno hayo ya Mahakama Kuu hayakuwafanya washambuliaji wabadilike, inatia moyo kuona kwamba maelfu ya wananchi huko Georgia wamekwisha shutumu mnyanyaso unaoendelea. Kuanzia Januari 8, 2001, Mashahidi wa Yehova waliomba watu watie sahihi hati inayodai ulinzi kutokana na washambuliaji wenye ghasia na kwamba wale ambao wameshiriki katika mashambulio ya wananchi wa Georgia wafikishwe mahakamani. Katika majuma mawili, wananchi 133,375 kotekote nchini Georgia walitia sahihi hati hiyo. Yaelekea wengi waliotia sahihi walikuwa washiriki wa Kanisa Othodoksi la Georgia kwa kuwa kuna Mashahidi wa Yehova 15,000 tu nchini Georgia. Lakini hati hiyo ilipotea Januari 22, 2001. Ilipotea jinsi gani?
Siku hiyo, mkutano wa waandishi wa habari ulifanywa katika ofisi ya Wakili wa Wananchi wa Georgia, Nana Devdariani, ili hati hiyo itangazwe rasmi. Mkutano ulipokuwa ukiendelea, Vasili Mkalavishvili na watu kumi wengine walivamia ofisi hiyo kwa ghafula ili kuwapokonya hati hiyo yenye sehemu 14. Mwakilishi mmoja wa Taasisi ya Caucasus ya Amani na Demokrasia alijaribu kuilinda hati hiyo, lakini wavamizi hao walimpiga. Wafuasi wa Mkalavishvili waliwanyang’anya wale waliopanga mkutano huo sehemu 12 kati ya zile 14 za hati na kukimbia, huku Mkalavishvili akiropoka matusi. Balozi mmoja wa nchi ya kigeni aliyeona tukio hilo alisema hivi kwa mshangao: “Siwezi kuamini!” Hata hivyo, Mashahidi walipata tena hati hiyo katika Februari 6, 2001, na iliwasilishwa kwa rais wa Georgia mnamo Februari 13.
“Washambuliaji Wote Watafikishwa Mahakamani”
Mashahidi wa Yehova huko Georgia na ulimwenguni pote wanatarajia kwamba Rais Shevardnadze atatenda kulingana na hati hiyo, kwani alishutumu mara nyingi mnyanyaso wa Mashahidi wa Yehova. Kwa mfano, katika Oktoba 18, 1999, rais huyo alisema mashambulio ya Mashahidi wa Yehova yalikuwa ‘mauaji ya halaiki yasiyoweza kuvumilika.’ Katika Oktoba 20, 2000, Rais Shevardnadze alimwandikia mshiriki mmoja wa Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova hivi: “Tutajitahidi tuwezavyo kukomesha ujeuri.” Aliongeza: “Ninataka kuwahakikishia kwamba wenye mamlaka wa Georgia wamewajibika kutetea haki za binadamu na uhuru wa dhamiri.” Tena, katika Novemba 2, 2000, Rais Shevardnadze alisema hivi katika barua iliyotumwa kwa tume ya Usalama na Ushirikiano huko Ulaya: “Jambo hilo [la usajili wa dini ndogo nchini Georgia] limewafadhaisha watu wetu na serikali.” Alihakikishia tume hiyo kwamba “washambuliaji wote watafikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa mashambulio yote na matendo yote ya ujeuri waliyofanya.”
Wachunguzi walio na wasiwasi huko Ulaya na sehemu nyingine ulimwenguni wanatumaini kwamba maneno ya Rais Shevardnadze yatatekelezwa hivi karibuni. Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote huwaombea waamini wenzao wenye ujasiri huko Georgia wanaoendelea kumtumikia Yehova licha ya mnyanyaso mkali.—Zaburi 109:3, 4; Mithali 15:29.
[Maelezo ya Chini]
a Ili upate habari zaidi kuhusu Georgia, soma makala ya “Georgia—Urithi wa Kale Uliohifadhiwa,” katika toleo la Amkeni!, la Januari 22, 1998.
b Hata hivyo, idara ya Forodha iliacha kuwanyang’anya Mashahidi wa Yehova vichapo vyao mwaka wa 2001.
c Vasili Mkalavishvili alifukuzwa kutoka Kanisa Othodoksi la Georgia katikati ya miaka ya 1990 baada ya kuchambua vikali kanisa hilo kwa sababu lilijiunga na Baraza la Makanisa Ulimwenguni. (Kwa sasa Kanisa Othodoksi la Georgia limejitenga na Baraza hilo.) Sasa, Mkalavishvili amejiunga na dini ya Calendarist wa Kale wa Ugiriki inayoongozwa na Askofu Mkuu Cyprian.
d Georgia ni mojawapo ya mataifa 123 yaliyotia sahihi Mkataba wa Umoja wa Mataifa Dhidi ya Mateso na Matendo au Adhabu ya Kikatili, ya Kinyama, au ya Kuvunjia Watu Heshima. Kwa hiyo, serikali ya Georgia imejiwajibisha “kupiga marufuku mateso yote.”
[Blabu katika ukurasa wa 24]
“Washambuliaji wote watafikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa mashambulio yote na matendo yote ya ujeuri waliyofanya.”—Rais wa Georgia, Eduard Shevardnadze, Novemba 2, 2000
[Blabu katika ukurasa wa 24]
‘Tunatumaini kwamba tatizo hilo [la mashambulio ya dini ndogo] litatatuliwa, na watu wote huko Georgia watakuwa na uhuru wa kufuata imani yao ya kidini.’—David Soumbadze, mshauri mkuu wa Ubalozi wa Georgia huko Washington, D.C., Marekani, Julai 3, 2001
[Sanduku/Picha ukurasa wa 20]
MASHAMBULIO YANAENDELEA
Mnyanyaso wa Mashahidi wa Yehova unaendelea kwa sababu wenye mamlaka wa Georgia wameshindwa kuwaadhibu washambuliaji.
Kwa mfano, katika Januari 22, 2001, Vasili Mkalavishvili, aliyekuwa kasisi wa Kanisa Othodoksi, na wafuasi wake walivamia mkutano wa kidini wa Mashahidi 70, katika eneo la Svanetis Ubani huko Tbilisi. Mashahidi hao walipigwa ngumi, walipigwa mateke, na kugongwa kwa misalaba ya mbao na chuma. Mshambuliaji fulani alimpiga Shahidi mmoja kichwani kwa msalaba mkubwa wa mbao kwa nguvu hivi kwamba msalaba huo ulivunjika. Washambuliaji kadhaa waliwaburuta Mashahidi wengine ndani ya chumba chenye giza na kuwapiga. Mashahidi wazee walilazimishwa kukimbia kati ya foleni ya washambuliaji huku wakipigwa ngumi na kupigwa kwa misalaba. Wanaume wawili walimkimbiza kijana mwenye umri wa miaka 14, kisha wakampiga ngumi na mateke kijana huyo asiyeweza kujitetea. Mshambuliaji mmoja mwenye umri wa miaka 30 alimchapa mvulana mwenye umri wa miaka 12 kichwani akitumia Biblia kubwa ya lugha ya Georgia. Shahidi mwingine alitoka nje ili kuita polisi, lakini alikamatwa. Washambuliaji walimpiga usoni hadi mdomo wake ukajaa damu na akaanza kutapika. Mwishowe, washambuliaji hao wakatili walitawanyika, na hadi leo hii hawajaadhibiwa.
Tena, katika Aprili 30, 2001, wafuasi wa Mkalavishvili walivamia mkutano wa kidini wa kutaniko hilohilo la Mashahidi wa Yehova. Washambuliaji waliwaburuta Mashahidi hao nje na kuwapiga kwa fimbo zenye misumari. Shahidi anayeitwa Tamaz alipata majeraha ya misumari kwenye mikono, mguu wa kushoto, na shavu la kushoto. Isitoshe, Tamaz alipata kidonda kikubwa kichwani kilichohitaji kushonwa. Washambuliaji hao waliharibu pia vyombo vya nyumba, vifaa vya umeme, na kuharibu madirisha yote katika nyumba hiyo walimokutania. Kisha wakateketeza vichapo vilivyochapishwa na Mashahidi wa Yehova. Katika Juni 7, 2001, shirika la haki za binadamu, Human Rights Watch, liliomba habari rasmi kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Georgia, Kakha Targamadze, na Mwendesha Mashtaka wa Georgia, Gia Mepharishvili, juu ya hatua ambazo zimechukuliwa ili kuwashtaki wale waliofanya shambulio hilo na mashambulio mengine ya karibuni. Mpaka leo, hata mshambuliaji mmoja hajafikishwa mahakamani.
[Sanduku katika ukurasa wa 21]
POLISI WALISHIRIKI
Katika Septemba 16, 2000, polisi wa jiji la Marneuli waliweka vizuizi barabarani ili mabasi 19 yaliyosafirisha Mashahidi wa Yehova yasiweze kuwasili mahali pa mkusanyiko wao. Kwenye kizuizi kimoja, abiria mmoja aligongwa kichwani wakati washambuliaji walipoyarushia mawe mabasi yaliyobeba Mashahidi hao. Mashahidi kadhaa walitolewa nje na kupigwa, na abiria wengine wakaibiwa. Lakini, polisi hawakuyazuia mabasi yaliyobeba wafuasi wa Mkalavishvili walioazimia kuharibu uwanja wa mkusanyiko. Washambuliaji hao waliteketeza kilogramu 1,500 za vichapo vya kidini. Polisi waliokuwapo walishiriki kuwapiga Mashahidi.
Shirika la Caucasus Press liliripoti kwamba Wizara ya Mambo ya Ndani ingechunguza shambulio hilo na “kuchukua hatua zinazofaa.” Wachunguzi wana sababu thabiti kuwashtaki washambuliaji hao. Kifungu cha 25 katika Katiba ya Georgia kinawahakikishia watu wote haki ya kufanya mkusanyiko wa hadharani. Hata hivyo, hakuna hata mshambuliaji mmoja ambaye ameshtakiwa. Miezi mitano baada ya shambulio hilo, shirika la Keston News Service liliripoti kwamba wakili wa Guram Sharadze, kiongozi wa kikundi cha “Georgia Juu!,” alikiri kwamba Sharadze alikuwa amewashawishi wenye mamlaka huko Marneuli na Zugdidi wawazuie Mashahidi wa Yehova wasifanye mikusanyiko yao miwili.
[Sanduku katika ukurasa wa 21]
KATIBA YA GEORGIA INATOA UHAKIKISHO WA ULINZI
Katiba ya Georgia ya Agosti 24, 1995, inatoa uhakikisho wa uhuru wa dini na ulinzi dhidi ya mashambulio ya ukatili, kama inavyoonyeshwa hapa chini:
Kifungu cha 17—(1) Heshima na hadhi ya mtu haipasi kuvunjwa au kuingiliwa. (2) Mateso, matendo au adhabu ya kinyama, ya kikatili au ya kuvunjia watu heshima hayaruhusiwi.
Kifungu cha 19—(1) Kila mtu ana uhuru wa kusema, uhuru wa maoni, uhuru wa dhamiri, uhuru wa dini, na uhuru wa imani. (2) Kumnyanyasa mtu kwa sababu ya maoni, imani, au dini yake kumekatazwa.
Kifungu cha 24—(1) Kila mtu ana haki ya kupokea na kusambaza habari, kusema na kusambaza maoni yake kwa mdomo, kwa maandishi, au kwa njia nyingine yoyote ile.
Kifungu cha 25—(1) Watu wote isipokuwa wanajeshi, polisi, au watu wanaolinda usalama, wana haki ya kufanya mkusanyiko wa hadharani usiolindwa kwa silaha, ndani ya jumba au nje bila kuomba ruhusa.
[Sanduku katika ukurasa wa 22]
ULIMWENGU UNATAZAMA
Watu ulimwenguni pote wana maoni gani kuhusu kushindwa kwa serikali ya Georgia kukomesha kunyanyaswa kwa Mashahidi wa Yehova?
Serikali za Marekani na Uingereza zilisema hivi: ‘Mkutano wa Mashahidi wa Yehova ulivamiwa, watu wengi walitendewa kwa ujeuri na wengine walizuiwa wasihudhurie mkutano huo. Hali hiyo na ukandamizaji wa watu wanaotaka kuabudu kwa uhuru huko Georgia umefadhaisha Ubalozi wa Marekani na Uingereza. Tunataka Serikali ya Georgia ichunguze matukio hayo na iwe macho kutetea uhuru wa dini wa watu wote.’
Mwenyekiti wa baraza lililotumwa kwenye Muungano wa Ulaya-Halmashauri ya Ushirikiano wa Bunge la Georgia, Ursula Schleicher, alisema: “Kwa niaba ya baraza la Bunge la Ulaya ningependa kueleza jinsi nilivyofadhaika niliposikia juu ya shambulio la mwisho kati ya yale mashambulio mengi dhidi ya waandishi wa habari, watetezi wa haki za binadamu, na Mashahidi wa Yehova . . . Ninaona shambulio hilo kuwa shambulio la kufedhehesha dhidi ya haki za msingi ambazo watawala wa Georgia wamejiwajibisha kutetea kwa kuwa wametia sahihi Mkataba wa Ulaya wa Kulinda Uhuru na Haki za Binadamu.”
Tume ya Usalama na Ushirikiano Marekani huko Ulaya ilimwandikia Rais Shevardnadze barua kuhusu mashambulio ya Mashahidi wa Yehova. Barua hiyo ilisema hivi: “Matukio ya karibuni yanatia wasiwasi kwelikweli, na inahofiwa kwamba serikali ya Georgia imeshindwa kukomesha mashambulio hayo. Hatua isipochukuliwa, wale wanaotaka kuwashambulia washiriki wa dini ndogo watachochewa kuendelea na ghasia zao. Tunatumaini kwamba wewe ukiwa mkuu wa nchi utawawekea watu na maafisa wa Georgia mfano mzuri na kusema wazi juu ya mambo haya mawili: hata mtu awe na maoni gani juu ya dini nyingine, haruhusiwi kamwe kuwatendea wafuasi wa dini hiyo kwa ujeuri; na kwamba wale wanaotenda kwa ujeuri jinsi hivyo—hasa polisi wanaosaidia au kushiriki matendo hayo maovu—watashtakiwa kulingana na sheria.” Barua hiyo ilitiwa sahihi na washiriki saba wa Bunge la Marekani.
Mwenyekiti-mwenzi wa tume ya Usalama na Ushirikiano huko Ulaya aliye Mbunge wa Marekani, Christopher H. Smith, alisema hivi: ‘Kwa nini watawala wa Georgia hawaungi mkono uhuru wa dini na haki za binadamu kama walivyoahidi wangefanya? Kuteketeza vichapo ni ukiukaji wa Mkataba wa Helsinki na kunakumbusha wengine wetu jinsi vitabu vilivyoteketezwa wakati wa utawala wa Nazi.’
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ulaya na Asia ya Kati ya shirika la Human Rights Watch aliandika hivi: “Shirika la Human Rights Watch, limehangaishwa sana na uwezekano wa mashambulio kutokea tena, kwa kuwa serikali ya Georgia imeshindwa kufikisha mahakamani wale ambao wameshambulia dini ndogo mbeleni. Tunakuhimiza ukomeshe mara moja mashambulio hayo na kuwashtaki wenye hatia.”
Ulimwengu unatazama. Je, serikali ya Georgia itatimiza wajibu wake? Sifa nzuri ya Georgia imo hatarini.
[Sanduku katika ukurasa wa 23]
RUFANI KATIKA MAHAKAMA YA ULAYA
Katika Juni 29, 2001, Mashahidi wa Yehova waliwasilisha lalamiko rasmi kwa Mahakama ya Ulaya ya Haki za Binadamu juu ya uzembe wa mashirika ya Georgia yanayopaswa kutekeleza sheria. Walipata jibu siku chache baadaye katika Julai 2, 2001. Msajili wa Mahakama hiyo aliandika kwamba Mkuu wa Idara ya Sheria alionelea kwamba kesi hiyo “ishughulikiwe haraka.”
[Ramani katika ukurasa wa 18]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
URUSI
GEORGIA
BAHARI NYEUSI
UTURUKI
[Picha katika ukurasa wa 18]
MEI 13, 2001 - Nyumba ya familia ya Shamoyan iliteketezwa na mtu kimakusudi
[Picha katika ukurasa wa 18]
JUNI 17, 2001 - Giorgi Baghishvili, alishambuliwa kwa ujeuri wakati washambuliaji wenye ghasia walipouvamia mkutano wa Mashahidi wa Yehova
[Picha katika ukurasa wa 19]
JULAI 11, 2001 - David Salaridze alipigwa kichwani kwa rungu na kupigwa mgongoni na kwenye mbavu alipokuwa akihudhuria mkutano wa Mashahidi wa Yehova
[Picha katika ukurasa wa 23]
JUNI 28, 2000 - Vichapo vya Mashahidi wa Yehova viliteketezwa huko Tbilisi
[Picha katika ukurasa wa 23]
AGOSTI 16, 2000 - Warren Shewfelt, Shahidi wa Yehova wa Kanada, alishambuliwa na mfuasi wa Vasili Mkalavishvili katika mahakama ya Gldani-Nadzaladevi
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]
AP Photo/Shakh Aivazov