Kukabiliana na Hasara
“TUMEKUWA TUKITEMBEA TANGU ASUBUHI. TUNATOROKA ILI KUJIOKOA. HAKUNA MAJI YA KUNYWA, HAKUNA CHAKULA. NYUMBA ZOTE ZIMEHARIBIWA.”—HARJIVAN, MWOKOKAJI WA TETEMEKO LA ARDHI HUKO INDIA, LENYE UKUBWA WA 7.9 KWENYE KIPIMO CHA RICHTER.
Tetemeko la ardhi huogopesha sana. Mwanamke mmoja aliyeokoka tetemeko la ardhi mwaka wa 1999 huko Taiwan anasema hivi: “Vitabu viliniangukia kutoka kwenye kabati la mbao lenye kimo cha meta 2.5 ambalo lilikuwa kando ya kitanda changu. Kofia mpya ya kujikinga wakati wa kuendesha pikipiki ilianguka kando tu ya kichwa changu kitandani.” Yeye aongezea hivi: “Kofia hiyo ingeniua badala ya kunikinga.”
Maisha Baada ya Tetemeko
Kuokoka tetemeko la ardhi ni jambo la kuogopesha, lakini huo ndio mwanzo tu. Saa chache baada ya tetemeko la ardhi kutokea, wafanyakazi wa kutoa msaada hujaribu kwa ujasiri kuwapata na kuwatibu watu waliojeruhiwa. Mara nyingi, wao hufanya hivyo hata kukiwa na hatari ya kutokea kwa tetemeko jingine la ardhi. “Tunahitaji kuwa waangalifu sana,” ndivyo alivyosema mwanamume mmoja aliyetaka kufukua nyumba zilizofunikwa kwa udongo mwingi sana baada ya tetemeko kutokea hivi majuzi huko El Salvador. “Ardhi ikitikisika tena kwa ghafula, udongo utaporomoka.”
Nyakati nyingine watu hujitoa mhanga ili kuwaokoa watu walioathiriwa. Kwa mfano, tetemeko kubwa la ardhi lilipotokea nchini India mapema katika mwaka wa 2001, Manu, mzee mmoja ambaye sasa anaishi nchini Marekani, alirudi kwenye nchi yake ya asili. Yeye aliwaza hivi: “Ni lazima niende ili nisaidie familia yangu na kila mtu anayeteseka.” Manu alipata hali mbaya sana katika maeneo aliyotembelea. Hata hivyo, alisema hivi: ‘Watu walikuwa na ujasiri mwingi sana.’ Mwandishi mmoja wa habari alisema hivi: “Watu wote niliowajua walichanga chochote walichokuwa nacho—ujira wa siku moja, juma moja, au wa mwezi mmoja, fedha fulani walizokuwa wameweka akibani au msaada wowote ambao wangeweza kutoa.”
Bila shaka, japo ni vigumu kuondoa vifusi na kuwatibu waliojeruhiwa, ni vigumu zaidi kuwasaidia watu ambao wameathiriwa kwa muda mfupi na tukio la kuogopesha kuishi kama hapo awali. Mfikirie Delores, mwanamke mmoja ambaye nyumba yake iliharibiwa na tetemeko la ardhi nchini El Salvador. Anasema hivi: “Tukio hili ni baya sana kuliko vita. Angalau wakati wa vita tulikuwa na nyumba.”
Kama ilivyosemwa katika makala yetu ya kwanza, japo watu walioathiriwa wanahitaji vitu vya kimwili, wanahitaji pia kufarijiwa. Kwa mfano, tetemeko la ardhi lilipoharibu jiji la Armenia lililoko magharibi mwa Kolombia mapema katika mwaka wa 1999, zaidi ya watu elfu moja walikufa, na wengine wengi walishtuka na kufadhaika. Roberto Estefan, daktari wa magonjwa ya akili ambaye nyumba yake iliharibiwa wakati wa msiba huo, alisema hivi: ‘Kokote uendako, watu wanaomba msaada. Ninapokwenda kula kwenye mkahawa, watu wengi wanaonisalimu wananieleza huzuni yao na jinsi wanavyoshindwa kulala.’
Kama Dakt. Estefan anavyofahamu, watu wengi hufadhaika sana baada ya kuokoka tetemeko la ardhi. Mwanamke mmoja aliyejitolea kusaidia kujenga kambi ya msaada alisema kwamba wafanyakazi fulani hawataki kwenda kazini kwani wanaamini kwamba watakufa hivi karibuni.
Kuwasaidia Watu Waliofadhaika
Majanga yanapotokea, Mashahidi wa Yehova huwasaidia waokokaji kimwili, kiroho na kihisia. Kwa mfano, mara tu baada ya tetemeko la ardhi lililotajwa awali kutokea huko Kolombia, ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova nchini humo ilianzisha halmashauri ya dharura kwenye eneo hilo. Maelfu ya Mashahidi kutoka sehemu zote za nchi hiyo walichanga chakula na fedha. Punde baadaye, tani 70 hivi za chakula zilitumwa kwenye eneo lililokumbwa na msiba.
Mara nyingi, watu wanahitaji sana msaada wa kiroho. Asubuhi moja baada ya tetemeko la ardhi kutokea huko Kolombia, Shahidi mmoja wa Yehova katika eneo hilo alimwona mwanamke aliyeonekana kuwa mwenye huzuni nyingi akitembea katika barabara moja ya jiji la Armenia lililokumbwa na msiba huo. Alimwendea mwanamke huyo na kumpa trakti yenye kichwa Kuna Tumaini Gani kwa Wapendwa Waliokufa?a
Mwanamke huyo alienda na trakti hiyo nyumbani na akaisoma kwa uangalifu. Baadaye, Shahidi mwingine wa Yehova alipomtembelea nyumbani kwake, mwanamke huyo alichochewa kusimulia mambo yaliyompata. Tetemeko hilo la ardhi lilikuwa limeharibu nyumba zake kadhaa katika jiji hilo ambazo zilikuwa zinamletea fedha nyingi. Sasa alikuwa ametumbukia katika umaskini. Lakini aliathiriwa hata zaidi. Tetemeko hilo lilibomoa nyumba yake ambamo yeye na mwanawe mwenye umri wa miaka 25 waliishi, na kumwua mwana huyo. Mwanamke huyo alimweleza Shahidi huyo kwamba hapo awali hakupendezwa kamwe na dini lakini sasa alikuwa na maswali mengi. Trakti hiyo ilikuwa imempa tumaini. Punde baadaye, alianza kujifunza Biblia.
Mashahidi wa Yehova wanasadiki kwamba kuna wakati ambapo wanadamu hawataathiriwa tena na misiba ya asili, kutia ndani matetemeko ya ardhi. Makala inayofuata itaonyesha ni kwa nini wanaamini hivyo.
[Maelezo ya Chini]
a Iliyochapishwa na Mashahidi wa Yehova.
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
JITAYARISHE!
◼ Hakikisha kwamba tanki za maji moto zimefungwa imara na kwamba vitu vizito viko sakafuni au kwenye rafu za chini.
◼ Wafundishe watu wa familia yako jinsi ya kuzima kabisa umeme, gesi, na kufunga maji.
◼ Weka kizima-moto na kisanduku cha huduma ya kwanza nyumbani mwako.
◼ Uwe na redio ndogo ya mawasiliano yenye betri mpya nyumbani.
◼ Panga mazoezi ya familia ili kuonyesha utaratibu wa kufuata wakati wa matukio ya dharura, na ukazie uhitaji wa (1) kutulia, (2) kuzima jiko na tanki za maji moto, (3) kusimama mlangoni au kukaa chini ya meza au dawati, na (4) kutokuwa karibu na madirisha, vioo, na mabomba ya kutolea moshi.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]
MATETEMEKO YA ARDHI HUKO ISRAEL
Profesa Amos Nur aliandika kwamba nchi ya Israel ndiyo “imekumbwa na matetemeko mengi ya ardhi kwa muda mrefu duniani.” Hiyo ni kwa sababu sehemu fulani ya Bonde Kuu la Ufa, yaani, ufa unaopita kati ya mabamba ya Mediterania na ya Arabuni, hupita katika nchi ya Israel kuanzia kaskazini hadi kusini.
Kwa kupendeza, wanaakiolojia fulani wanaamini kwamba wahandisi wa kale walitumia mbinu ya pekee ili kupunguza uharibifu unaosababishwa na matetemeko ya ardhi. Wazo hilo lapatana na maelezo ya Biblia kuhusu ujenzi wa Solomoni: “Na behewa kubwa pande zote ilikuwa na safu tatu za mawe ya kuchongwa, na safu moja ya mihimili ya mierezi; mfano wa behewa ya ndani ya nyumba ya BWANA, na ukumbi wa nyumba.” (1 Wafalme 6:36; 7:12, italiki ni zetu.) Uthibitisho wa mbinu hiyo ya kuingiza mihimili ya mbao katika jengo la mawe umepatikana katika sehemu mbalimbali—kutia ndani lango moja huko Megiddo, ambalo inadhaniwa kuwa lilijengwa katika siku za Solomoni au kabla ya hapo. Msomi David M. Rohl anaamini kwamba huenda mihimili hiyo “iliingizwa ili kujaribu kuzuia jengo lisiharibiwe na tetemeko la ardhi.”
[Picha]
Magofu ya tetemeko la ardhi huko Bet Sheʼan, Israel
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]
DAKIKA MBILI ZA KUOGOPESHA SIMULIZI LA MWOKOKAJI MMOJA
Familia yetu ilikuwa inajitayarisha kwa ajili ya arusi ya binamu yangu, huko Ahmadabad, India. Mnamo Januari 26, 2001, niliamshwa na mtikiso mkubwa badala ya kuamshwa na mlio wa saa yangu. Nilisikia kabati za metali zikisongasonga, na nikajua kwamba kulikuwa na hatari. Mjomba wangu alikuwa akisema hivi kwa sauti kubwa, “Tokeni nje ya nyumba!” Tulipokuwa nje tuliona nyumba ikitikisika. Ni kana kwamba kutikisika huko kuliendelea kwa muda mrefu. Lakini kwa kweli, tetemeko hilo lilitukia kwa muda wa dakika mbili tu.
Ilikuwa vigumu sana kukabiliana na hali hiyo ya ghafula. Tulihakikisha kwamba watu wa familia yetu walikuwa salama. Kwa kuwa nyaya za simu na za umeme zilikatika, hatukuweza kujua mara moja hali ya watu wa jamaa yetu katika miji mingine. Baada ya kuwa na wasiwasi kwa muda wa saa moja, tulipata habari kwamba walikuwa salama. Si watu wote walionusurika. Kwa mfano, huko Ahmadabad, zaidi ya majengo mia moja yalianguka, na zaidi ya watu 500 walikufa.
Watu wote walikuwa na wasiwasi kwa majuma kadhaa. Watu walikwenda kulala huku wakiogopa kwamba tetemeko jingine lingetokea, kwa kuwa ilikuwa imetabiriwa hivyo. Watu wengi walipoteza makao, na marekebisho yalifanywa polepole. Yote hayo yalisababishwa na tetemeko la ardhi ambalo tutalikumbuka daima hata ingawa lilitukia kwa muda wa dakika mbili tu. —Limesimuliwa na Samir Saraiya.
[Picha katika ukurasa wa 6, 7]
Mwokokaji wa tetemeko la ardhi lililotokea huko India mnamo Januari 2001 anashika picha ya mama yake ambaye alikufa na sasa mwili wake unateketezwa
[Hisani]
© Randolph Langenbach/UNESCO (www.conservationtech.com)