Dawa za Kulevya
Maana: Kuna maana mbalimbali za neno “dawa.” Katika sehemu hii, tutazungumzia dawa za kulevya, ambazo si vyakula, bali ni vitu vinavyobadili tabia ambavyo havionwi kuwa vya lazima kitiba. Watu huvitumia kujaribu kuepuka matatizo ya maisha, ili kupata hisia kama ya ndoto, au hali ya kuhisi vizuri au kusisimuka.
Je, kwa kweli Biblia inakataza kutumia dawa za kulevya ili kupata raha?
Biblia haitaji kwa jina vitu kama heroini, kokeini, LSD, PCP, bangi, na tumbaku. Lakini inatoa miongozo inayohitajiwa ili tujue jambo la kufanya na la kuepuka ili tumpendeze Mungu. Vivyo hivyo, Biblia haisemi kwamba ni kosa kutumia bunduki kumuua mtu, lakini inakataza uuaji.
Luka 10:25-27: “‘Nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?’ . . . ‘“Lazima umpende Yehova Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa nafsi yako yote na kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yote,” na, “jirani yako kama wewe mwenyewe.”’” (Je, kweli mtu anampenda Mungu kwa nafsi yake yote na akili yake yote ikiwa anatenda mambo yanayofupisha maisha yake bila sababu na kufanya akili zake zipumbazike? Je, anampenda jirani yake ikiwa anawaibia wengine ili aendeleze tabia yake ya kutumia dawa za kulevya?)
2 Kor. 7:1: “Kwa kuwa tuna ahadi hizi [za Yehova kuwa Mungu na Baba yetu], acheni tujisafishe wenyewe kila unajisi wa mwili na roho, tukiukamilisha utakatifu katika kumwogopa Mungu.” (Lakini je, tunaweza kutarajia kukubaliwa na Mungu ikiwa tunafanya kimakusudi mambo yanayochafua miili yetu?)
Tito 2:11, 12: “Fadhili zisizostahiliwa za Mungu zinazowaletea watu wa namna zote wokovu zimeonyeshwa, zikitufundisha kukataa kabisa kutomwogopa Mungu na tamaa za kilimwengu na tuishi kwa utimamu wa akili na uadilifu na ujitoaji-kimungu katikati ya mfumo wa mambo wa sasa.” (Je, kutumia dawa za kulevya zinazoharibu uamuzi wa mtu au zinazofanya mtu ashindwe kujizuia kunapatana na shauri hilo?)
Gal. 5:19-21: “Sasa matendo ya mwili ni wazi, nayo ni . . . mazoea ya kuwasiliana na pepo, . . . karamu za kupindukia, na mambo kama hayo. . . . Wale walio na mazoea ya kufanya mambo ya namna hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.” (Maana halisi ya neno la Kigiriki phar·ma·kiʹa, linalotafsiriwa hapa “mazoea ya kuwasiliana na pepo,” ni “matumizi ya dawa za kulevya.” Ikitoa maelezo kuhusu neno hilo la Kigiriki, An Expository Dictionary of New Testament Words, ya W. E. Vine inasema hivi: “Katika uchawi, matumizi ya dawa za kulevya, ziwe ni nyepesi au kali, kwa ujumla yalifuatana na utamkaji wa maneno ya uganga na kuomba nguvu za uchawi, pamoja na uandalizi wa hirizi mbalimbali, talasimu, n.k., zinazodaiwa zimekusudiwa kumlinda mwombaji au mgonjwa asifuatwe na nguvu za roho waovu, lakini ambazo kwa kweli zimekusudiwa kumvutia mwombaji kwa uwezo wa kifumbo na nguvu za mchawi.” [London, 1940, Buku la 4, uku. 51, 52] Hali kadhalika leo, wengi wanaotumia dawa za kulevya wanajitia katika mazoea ya kuwasiliana na pepo au wanashirikiana na wale wanaowasiliana na pepo, kwa sababu akili iliyo tupu au mtu anayeona au kusikia vitu visivyokuwako huwa rahisi kupagawa na roho waovu. Linganisha na Luka 11:24-26.)
Tito 3:1: “Wajitiishe na kuzitii serikali na mamlaka zikiwa watawala.” (Katika nchi nyingi, kuwa na dawa fulani za kulevya au kuzitumia ni kuvunja sheria.)
Kwa kuwa dawa fulani za kulevya huenda zikamsisimua mtu, je, kweli ni hatari sana?
2 Tim. 3:1-5: “Katika siku za mwisho kutakuwa na nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo. Kwa maana watu watakuwa . . . wanaopenda raha badala ya kumpenda Mungu . . . Nawe geukia mbali kutoka kwa hao.” (Ni wazi kwamba Biblia inaonya kuhusu kutamani raha sana hivi kwamba tunaitanguliza maishani badala ya kufuata kanuni za uadilifu za Neno la Mungu na kupata kibali chake.)
Dawa fulani za kulevya hutuliza maumivu na zinaweza kumfanya mtu ahisi ameridhika, lakini hizo pia zinaleta uzoefu mbaya na zinaweza kuua zikitumiwa kupita kiasi. Kunusa viyeyusho fulani kwaweza kusisimua, lakini kwaweza pia kuharibu usemi, kuzuia kuona vizuri, kupoteza utendaji wa misuli, pamoja na kuharibu kabisa ubongo, maini, na figo. Vidonge vya kulevya humfanya mtu ahisi “raha” navyo huonekana kuondoa uchovu, lakini hivyo pia husababisha mtu asione vizuri, asifikiri vizuri, navyo vinaweza kubadili kabisa tabia, na kumfanya mtu atake kujiua.
Namna gani bangi—je, ina madhara? Madaktari fulani wamesema kwamba haina madhara
David Powelson, M.D., aliyekuwa daktari mkuu wa magonjwa ya akili, Cowell Hospital, Chuo Kikuu cha California, Berkeley, wakati mmoja aliunga mkono kuhalalishwa kwa matumizi ya bangi. Baadaye, baada ya uthibitisho zaidi kupatikana, aliandika hivi: “Sasa naamini kwamba bangi ndiyo dawa ya kulevya iliyo hatari zaidi ambayo tunapaswa kushughulika nayo: 1. Mtu anapoitumia mara ya kwanza yeye hudanganyika. Mtumiaji anakuwa na mawazo ya kuhisi raha; haoni kuharibika kwa akili na mwili wake. 2. Kuendelea kuitumia husababisha fikira za udanganyifu. Baada ya mtu kuitumia mfululizo kwa mwaka mmoja mpaka miaka mitatu, fikira potovu huanza kuutawala uwezo wa kufikiri.”—Executive Health Report, Oktoba 1977, uku. 8.
Dakt. Robert L. DuPont, aliyekuwa mkurugenzi wa Taasisi ya Kitaifa ya Dawa za Kulevya nchini Marekani, ambaye zamani alinukuliwa akisema kwamba bangi si hatari sana, alisema hivi juzijuzi: “Suala muhimu ni hatari ya kiafya inayoletwa na mweneo huu [wa kizazi kichanga kutumia bangi], hatari ya angalau aina mbili. Moja ni zile athari za kulewa, kuanzia matokeo hatari ya uendeshaji magari na kutojali chochote. Hatari nyingine ni ile inayohusu mwili tu. Hapa athari zinahusu ugonjwa wa muda mrefu wa mapafu kati ya watumiaji wa bangi na athari mbaya za hormoni, athari za mfumo wa kinga na hata labda ugonjwa wa kansa.”—Montreal Gazette, Machi 22, 1979, uku. 9.
Gazeti Science Digest linatoa maelezo haya: “Mwishowe, huenda uvutaji wa bangi wa kawaida ukapanua mapengo yaliyo kati ya ncha za neva katika ubongo, ambazo ni muhimu katika utendaji wa kumbukumbu, hisia na tabia. Ili neva zitende kazi, ni lazima ziwasiliane.” Kisha, ikieleza matokeo ya uchunguzi unaohusu wanyama, makala hiyo inaendelea kusema hivi: “Athari zilizo wazi zaidi zilionekana katika eneo la utando, linalohusiana na hisia; eneo la vifuko vya ubongo, linalohusiana na kujenga kumbukumbu; na eneo la kinundu cha ubongo, linalodhibiti mienendo fulani ya tabia.”—Machi 1981, uku. 104.
Je, ni vibaya kuvuta bangi kuliko kunywa pombe?
Pombe ni chakula na mwili huitumia kutoa nishati; mwili huondoa takataka zake. Hata hivyo, daktari mchunguzi wa dawa katika akili alisema: “Bangi ni dawa kali sana ya kulevya, nasi tunapoilinganisha na pombe, tunafanya kosa kubwa sana.” “Tunapoilinganisha chembe kwa chembe, THC [katika bangi] ni kali zaidi mara 10,000 kuliko pombe inayosababisha ulevi mwepesi . . . THC inaondolewa polepole mwilini, na miezi mingi lazima ipite ndipo athari zake ziondoke.” (Executive Health Report, Oktoba 1977, uku. 3.) Muumba anajua jinsi tulivyoumbwa, na Neno lake linamruhusu mtu kutumia pombe kwa kiasi. (Zab. 104:15; 1 Tim. 5:23) Lakini, yeye pia hushutumu vikali kunywa pombe kupita kiasi, kama vile anavyoshutumu ulafi.—Met. 23:20, 21; 1 Kor. 6:9, 10.
Kwa nini Mashahidi wa Yehova wanaona kuvuta sigara kuwa kosa zito sana?
Ni kutoheshimu zawadi ya uhai
Mdo. 17:24, 25: “Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo . . . huwapa watu wote uhai na pumzi na vitu vyote.”
“Kuna uthibitisho mwingi sana unaoonyesha kwamba sigara hufupisha maisha; kama hali zingine za kitiba zilivyothibitishwa, sigara imethibitishwa kabisa kuwa inasababisha jambo hilo.”—Science 80, Septemba/Oktoba, uku. 42.
Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, “watu milioni nne hufa kila mwaka kutokana na magonjwa yanayosababishwa na uvutaji wa sigara, mtu mmoja hufa kila baada ya sekunde nane.” Ripoti hiyo inaendelea kusema: “Tangu mwaka wa 1950 mpaka 2000, watu zaidi ya milioni 60 wamekufa kutokana na uvutaji wa sigara katika nchi zilizoendelea peke yake, wengi kuliko waliokufa katika Vita vya Pili vya Ulimwengu.”—World Health Organization, Fact Sheet No. 221, Aprili 1999.
Aliyekuwa Waziri wa Afya, Elimu, na Jamii, nchini Marekani, Joseph Califano, alisema: “Leo hakuna shaka kwamba kuvuta sigara kwa kweli ni kujiua polepole.”—Scholastic Science World, Machi 20, 1980, uku. 13.
Ni kinyume cha yale ambayo Mungu anataka Wakristo wamtolee
Rom. 12:1: “Nawasihi ninyi kwa huruma za Mungu, akina ndugu, mtoe miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, yenye kukubalika kwa Mungu, utumishi mtakatifu pamoja na nguvu zenu za kufikiri.”
Daktari mkuu wa upasuaji nchini Marekani, C. Everett Koop, alisema: “Uvutaji wa sigara umetambuliwa waziwazi kuwa ndio kisababishi kikuu cha kifo kinachoweza kuzuiwa katika jamii yetu.” (The New York Times, Februari 23, 1982, uku. A1) “Uchunguzi wa kitiba unaonyesha kwamba . . . kwa wastani mvutaji wa sigara hufa miaka mitatu hadi minne mapema kuliko yule asiyevuta. Mtu anayevuta sigara kwa wingi—mtu anayevuta pakiti mbili au zaidi za sigara kila siku—anaweza kufa miaka minane mapema kuliko yule asiyevuta.” (The World Book Encyclopedia, 1984, Buku la 17, uku. 430) Je, inamfaa mtu kuutoa uhai wake kumtumikia Mungu kisha auharibu uhai huo polepole?
“Kuvuta sigara huleta uharibifu mkubwa sana, hasa kwa moyo na mapafu, hivi kwamba tiba nyingine za kinga hazifai kitu ikiwa mtu anavuta sigara.” (Huduma ya Habari ya Chuo Kikuu cha California Kusini, Februari 18, 1982) “Uvutaji wa sigara labda ndicho kisababishi kikubwa zaidi cha afya mbaya ulimwenguni kinachoweza kuzuiwa.” (Dakt. H. Mahler, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni, katika World Health, Februari/Machi 1980, uku. 3) Je, ni jambo linalopatana na akili mtu kujitoa mwenyewe kumtolea Mungu utumishi mtakatifu na kisha aiharibu afya yake kimakusudi?
Kuvuta sigara ni kuvunja takwa la Mungu kwamba tumpende jirani yetu
Yak. 2:8: “Mpende jirani yako kama wewe mwenyewe.”—Linganisha na Mathayo 7:12.
“Uchunguzi uliofanywa hivi karibuni . . . ulifunua kwamba wake wasiovuta sigara ambao waume wao huvuta sigara, kwa wastani hufa miaka minne mapema kuliko wanawake ambao waume wao si wavutaji wa sigara.” (The New York Times, Novemba 22, 1978, uku. C5) “Mwanamke anapovuta sigara akiwa mjamzito anaweza kumsababishia mtoto aliye tumboni kasoro mbaya sana hivi kwamba mtoto huyo anaweza kufa akiwa tumboni, au mara tu baada ya kuzaliwa.” (Family Health, Mei 1979, uku. 8) Mtu ambaye anawatendea washiriki wa familia yake kwa njia hiyo isiyo ya upendo anathibitisha wazi kwamba hajiendeshi kama Mkristo.—Linganisha na 1 Timotheo 5:8.
“Uchunguzi umeonyesha kwamba kwa kuwa mvutaji wa kawaida anavuta sana sigara yake kwa sehemu ndogo tu wakati inapokuwa imewashwa, huenda mtu asiyevuta sigara ambaye ameketi karibu naye akalazimika kuvuta karibu kiasi kilekile cha kaboni monoksidi, lami na nikotini kama yule mvutaji.” (Today’s Health, Aprili 1972, uku. 39) Basi mvutaji wa sigara hampendi mwanadamu mwenzake, na hivyo haonyeshi uthibitisho wa kumpenda Mungu.—Ona 1 Yohana 4:20.
Ikiwa ni kosa kutumia dawa za kulevya, kwa nini Mungu aliumba mimea inayotokeza dawa hizo?
Vitu vinavyotumiwa vibaya kwa kawaida vina matumizi yanayofaa pia. Ndivyo ilivyo na viungo vya uzazi vya mwanadamu. Ndivyo ilivyo na divai. Bangi hutokana na majani makavu na maua ya mbangi, ambao hutokeza nyuzi nzuri za kutengeneza kamba na nguo. Majani ya tumbaku, yanayotumiwa vibaya na wavutaji, yanaweza pia kutumiwa kutengeneza dawa za kuua viini vya ugonjwa na wadudu. Mambo mengi hayajajulikana kuhusu jinsi vitu vingi vilivyo duniani vinavyoweza kutumiwa kwa njia yenye kuleta faida. Hata magugu yana faida katika kuzuia mmomonyoko wa udongo na kutia udongo mbolea wakati ambapo haulimwi.
Mtu anaweza kufanya nini ikiwa amejaribu kuacha kuvuta sigara au kutumia dawa za kulevya lakini hajafanikiwa?
Kwanza, kwa kujifunza Biblia na kutafakari unahitaji kusitawisha tamaa yenye nguvu ya kumpendeza Mungu na kuishi katika mfumo wake mpya wa mambo wenye uadilifu. Ukimkaribia, atakukaribia, naye atakupa msaada unaohitaji.— Yak. 4:8.
Ni muhimu mtu asadiki ubaya wa mazoea hayo na kuyachukia kikweli. (Zab. 97:10) Jambo hilo linaweza kufanywa kwa kurudia mambo ya hakika yaliyoandikwa katika sehemu hii ya kitabu na kutafakari, si juu ya raha za muda za sasa ambazo huenda zikatokana na mazoea hayo, bali juu ya yale yanayompendeza Mungu na jinsi matokeo ya mazoea mabaya yanavyochukiza sana.
Ikiwa unatamani sana kuvuta sigara au kutumia moja kati ya zile dawa nyingine za kulevya, sali kwa Mungu kwa bidii ili akusaidie. (Luka 11:9, 13; linganisha na Wafilipi 4:13.) Fanya hivyo bila kukawia. Pia, chukua Biblia yako na uisome kwa sauti kubwa, au mwendee Mkristo aliyekomaa. Mwambie yanayokupata na umwombe msaada.