Kitabu Cha Biblia Namba 14—2 Mambo Ya Nyakati
Mwandikaji:Ezra
Mahali Kilipoandikiwa: Yerusalemu (?)
Uandikaji Ulikamilishwa: c. (karibu) 460 K.W.K.
Wakati Uliohusishwa: 1037–537 K.W.K.
1. Ezra alikamilisha Mambo ya Nyakati wakati gani, na akiwa na kusudi gani?
KWA kuwa ni wazi kitabu cha Mambo ya Nyakati cha Kwanza na cha Pili hapo awali vilikuwa kitabu kimoja, hoja zilizotolewa katika sura iliyotangulia juu ya habari za msingi, uandikaji, wakati wa kuandika, kukubaliwa, na uasilia zahusu vitabu vyote viwili. Kulingana na ushuhuda uliotolewa, Ezra alikamilisha kitabu cha Mambo ya Nyakati cha Pili karibu 460 K.W.K., yawezekana katika Yerusalemu. Lilikuwa ni kusudi la Ezra kuhifadhi habari za kihistoria ambazo zilikuwa katika hatari ya kupotea. Msaada wa roho takatifu, pamoja na uwezo wake akiwa mwanahistoria kupata habari za kindani na kuzichanganua, kuliwezesha Ezra kufanya maandishi sahihi na ya kudumu. Alitunza kwa ajili ya wakati ujao yale aliyoona kuwa uhakika wa kihistoria. Kazi ya Ezra ilikuwa ya wakati unaofaa kabisa, kwa kuwa sasa ilikuwa lazima pia kukusanya jumla yote ya maandishi matakatifu ya Kiebrania yaliyokuwa yameandikwa karne nyingi zilizopita.
2. Kwa nini hakuna sababu ya kutilia shaka usahihi wa Mambo ya Nyakati?
2 Wayahudi wa siku ya Ezra walifaidika sana na maandishi ya matukio yaliyopuliziwa na Mungu ya Ezra. Yaliandikwa kwa ajili ya kuwaagiza na kutia moyo kuvumilia. Kupitia faraja ya Maandiko, wangeweza kuwa na tumaini. Wao walikiona kitabu cha Mambo ya Nyakati kuwa chenye kukubalika. Wao walijua kilitumainika. Wangeweza kukichunguza kwa kukilinganisha na maandishi mengine yaliyopuliziwa na Mungu na historia nyingi za kilimwengu zilizotajwa na Ezra. Ingawa waliruhusu historia za kilimwengu zisizopuliziwa na Mungu ziharibike, walihifadhi kwa uangalifu Mambo ya Nyakati. Watafsiri wa Septuagint walitia ndani Mambo ya Nyakati kuwa sehemu ya Biblia ya Kiebrania.
3. Maandiko mengine yanaonyeshaje kwamba Mambo ya Nyakati ni asilia?
3 Yesu Kristo na waandikaji wa Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo walikikubali kuwa ni asilia na kimepuliziwa na Mungu. Bila shaka Yesu alikuwa akifikiria visa kama vilivyoandikwa kwenye 2 Mambo ya Nyakati 24:21 alipolaani vikali Yerusalemu kuwa mwuaji na mpiga kwa mawe manabii na watumishi wa Yehova. (Mt. 23:35; 5:12; 2 Nya. 36:16) Wakati Yakobo aliporejezea Abrahamu kuwa ‘rafiki ya Yehova,’ labda alirejezea usemi wa Ezra kwenye 2 Mambo ya Nyakati 20:7. (Yak. 2:23) Kitabu hicho pia kina unabii mbalimbali uliotimizwa bila kukosea.—2 Nya. 20:17, 24; 21:14-19; 34:23-28; 36:17-20.
4. Ni vitu gani vya akiolojia vilivyopatikana vinavyothibitisha uasilia wa kitabu cha Mambo ya Nyakati cha Pili?
4 Pia akiolojia (uchimbuzi wa vitu vya kale) yathibitisha uasilia wa kitabu cha Mambo ya Nyakati cha Pili. Kuchimba kituo cha Babuloni wa kale kumetokeza mabamba ya udongo yanayohusu kipindi cha utawala wa Nebukadreza, mojapo likitaja “Yaukini, mfalme wa bara la Yahudi,” yaani, “Yehoyakini, mfalme wa bara la Yuda.”a Hilo lafaana na simulizi la Biblia la Yehoyakini akitwaliwa mateka kule Babuloni wakati wa mwaka wa saba wa kutawala kwa Nebukadreza.
5. Ni kipindi gani cha wakati kinachohusishwa katika kitabu cha Mambo ya Nyakati cha Pili, na ni kwa nini historia ya Yuda yaelezwa badala ya ile ya ufalme wa makabila kumi?
5 Maandishi ya kitabu cha Mambo ya Nyakati cha Pili yafuatisha matukio katika Yuda tangu utawala wa Sulemani, kuanzia 1037 K.W.K., hadi amri ya Koreshi ya 537 K.W.K. ya kujenga upya nyumba ya Yehova katika Yerusalemu. Katika historia hiyo ya miaka 500, ufalme wa makabila kumi unarejezewa wakati tu unapohusika katika mambo ya Yuda, na kuharibiwa kwa ufalme huo wa kaskazini katika 740 K.W.K. hakutajwi hata. Ni kwa nini hivyo? Kwa sababu kuhani Ezra alihangaikia hasa ibada ya Yehova mahali palo palipofaa, nyumba Yake katika Yerusalemu, na ufalme wa ukoo wa Daudi, ambaye Yehova alikuwa amefanya agano Lake naye. Kwa hiyo, Ezra akaza uangalifu kwenye ufalme wa kusini kwa kuunga mkono ibada ya kweli na kwa kutazamia mtawala atoke Yuda.—Mwa. 49:10.
6. Kitabu cha Mambo ya Nyakati cha Pili ni chenye kuimarisha na kusisimua katika njia zipi?
6 Ezra achukua maoni ya kuchangamsha. Kati ya zile sura 36 za kitabu cha Mambo ya Nyakati cha Pili, zile 9 za kwanza zahusu utawala wa Sulemani, na 6 kati yazo kwa ujumla zahusu matayarisho na kuwekwa wakfu kwa nyumba ya Yehova. Maandishi hayo hayataji kukengeuka kwa Sulemani. Zile sura 27 zilizosalia, 14 zahusu wafalme watano ambao kwa msingi walifuata kielelezo cha Daudi cha ujitoaji kamili kwa ibada ya Yehova: Asa, Yehoshafati, Yothamu, Hezekia, na Yosia. Hata katika zile sura nyingine 13, Ezra ni mwangalifu kukazia mambo mema ya wafalme wabaya. Sikuzote akazia matukio yanayohusu kurejeshwa na kuhifadhiwa kwa ibada ya kweli. Yasisimua kama nini!
YALIYOMO KATIKA MAMBO YA NYAKATI CHA PILI
7. Yehova ‘amtukuzaje sana’ Sulemani?
7 Utukufu wa utawala wa Sulemani (1:1–9:31). Kitabu cha Mambo ya Nyakati cha Pili kifunguapo, twaona Sulemani mwana wa Daudi akikua katika nguvu katika ufalme. Yehova yu pamoja naye na aendelea ‘kumtukuza sana.’ Sulemani atoapo dhabihu kule Gibeoni, Yehova amtokea usiku, akisema: “Omba utakalo nikupe.” Sulemani aomba maarifa na hekima ili atawale watu wa Yehova ifaavyo. Kwa sababu ya ulizo hilo lisilo la ubinafsi, Mungu aahidi kumpa Sulemani si hekima na maarifa bali pia mali na utajiri na heshima “kupita walivyokuwa navyo wafalme wote waliokuwa kabla yako, wala baada yako hapatakuwa na mtu atakayekuwa navyo.” Mali inayoingia katika mji huo ni kubwa mno hata kwamba baadaye Sulemani afanya “fedha na dhahabu kuwa kama mawe humo Yerusalemu.”—1:1, 7, 12, 15.
8. Kazi juu ya hekalu yaendeleaje, na ni nini baadhi ya habari zinazohusu ujenzi walo?
8 Sulemani aandika wafanya kazi ngumu ya lazima kwa ajili ya kazi ya ujenzi wa nyumba ya Yehova, na Mfalme Hiramu wa Tiro ashirikiana kwa kupeleka mbao na mfanya kazi hodari. “Katika mwaka wa nne wa kutawala kwake [Sulemani],” jengo laanzishwa, nalo lakamilishwa miaka saba na nusu baadaye, katika 1027 K.W.K. (3:2) Mbele ya hekalu lenyewe ni ukumbi mkubwa unaoinuka mikono 120 (meta 53.4). Nguzo mbili kubwa mno za shaba, moja yenye kuitwa Yakini, maana yake “[Yehova] Na Asimamishe Imara,” na ile nyingine yenye kuitwa Boazi, kwa wazi kumaanisha “Katika Nguvu,” zasimama mbele ya ukumbi. (3:17) Nyumba yenyewe ni ndogo kwa kulinganisha, ikiwa na mikono 60 (meta 26.7) kwa urefu, mikono 30 (meta 13.4) kwa kimo, na mikono 20 (meta 8.9) kwa upana, lakini kuta zayo na paa zafunikwa kwa dhahabu; chumba chayo cha ndani zaidi, Patakatifu Zaidi, penyewe papambwa kwa madoido ya dhahabu. Pia kina makerubi wawili wa dhahabu, mmoja kila upande wa chumba, ambao mabawa yao yanyooka na kukutania katikati.
9. Eleza mapambo na vyombo vya ua na hekalu.
9 Katika ua wa ndani, kuna madhabahu kubwa ya shaba ya mikono 20 ya mraba (meta 9) na mikono 10 (meta 4.5) kwa kimo. Kitu kingine chenye kutokeza katika ua ni bahari ya kusubu (madini iliyoyeyushwa), bakuli kubwa mno la shaba lililokalia migongo ya fahali 12 wa shaba wanaotazama nje, watatu kila upande. Bahari hii yaweza kuingia “bathi elfu tatu” (lita 66,000) za maji, yanayotumiwa na makuhani kujiosha. (4:5) Pia katika ua kuna mabakuli madogo ya shaba kumi yakikalia vichukuzi vya shaba vyenye madoido, na katika maji hayo, vitu vinavyohusiana na sadaka za kuteketezwa husuzwa. Yajazwa kutoka bahari ya kusubu na kusukumwa juu ya magurudumu kokote yanakohitajiwa maji. Kuongezea hayo, kuna vinara vya taa kumi vya dhahabu na vyombo vingine vingi, vingine vya dhahabu na vingine vya shaba, kwa ajili ya ibada ya hekalu.b
10. Kwatukia nini wakati Sanduku liletwapo ndani ya Patakatifu Zaidi?
10 Mwishowe, baada ya miaka saba na nusu ya kazi, nyumba ya Yehova yakamilishwa. (1 Fal. 6:1, 38) Siku ya kuzinduliwa kwayo ni wakati wa kuleta kifananishi cha kuwapo kwa Yehova katika chumba cha ndani zaidi cha jengo hilo lenye fahari sana. Makuhani “wakaliingiza sanduku la agano la BWANA [Yehova, NW] mahali pake katika chumba cha ndani cha nyumba, patakatifu pa patakatifu, yaani, chini ya mabawa ya makerubi.” Kisha kwatukia nini? Waimbaji na wacheza muziki Walawi wamsifupo na kushukuru Yehova katika wimbo wa umoja, nyumba hiyo yajawa na wingu, na makuhani hawawezi kusimama wahudumu kwa sababu ‘utukufu wa Yehova’ wajaza nyumba ya Mungu wa kweli. (2 Nya. 5:7, 13, 14) Kwa njia hiyo Yehova aonyesha kibali chake kwa hekalu na kuonyesha kuwapo kwake humo.
11. Ni sala gani anayotoa Sulemani, naye atoa ombi gani?
11 Jukwaa la shaba lenye kimo cha mikono mitatu (meta 1.3) limejengwa kwa ajili ya pindi hiyo, nalo lawekwa katika ua wa ndani zaidi karibu na madhabahu kubwa ya shaba. Katika kikao hicho kilichoinuka, Sulemani aweza kuonwa na umati mkubwa uliokusanyika kwa ajili ya kuwekwa wakfu kwa hekalu. Kufuatia udhihirisho wa kimwujiza wa kuwapo kwa Yehova katika wingu la utukufu, Sulemani asujudu mbele ya umati na kutoa sala yenye kugusa moyo sana ya kutoa shukrani na sifa, inayotia ndani maombi ya unyenyekevu kwa ajili ya msamaha na baraka. Katika umalizio, yeye asihi: “Sasa, Ee Mungu wangu, macho yako yafumbuke, nakusihi, masikio yako yakasikilize maombi yaombwayo mahali hapa. Ee BWANA [Yehova, NW], Mungu, usiurudishe nyuma uso wa masihi wako; uzikumbuke fadhili za Daudi mtumishi wako.”—6:40, 42.
12. Yehova ajibuje sala ya Sulemani, nayo sherehe ya siku 15 yafikia upeo gani wenye furaha?
12 Je! Yehova anasikia sala hii ya Sulemani? Mara tu Sulemani amalizapo kusali, moto washuka chini kutoka mbinguni na kuteketeza sadaka ya kuteketezwa na dhabihu, na ‘utukufu wa Yehova’ wajaza nyumba hiyo. Hilo laongoza watu wote wasujudu kifudifudi na kushukuru Yehova, “kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake ni za milele.” (7:1, 3) Kisha dhabihu kubwa yatolewa kwa Yehova. Karamu hiyo ya juma zima ya wakfu yafuatwa na Karamu ya Kukusanya ya juma zima na sabato ya kujiepusha na kazi. Baada ya sherehe hii ya furaha, yenye kutia nguvu kiroho ya siku 15, Sulemani arejesha watu nyumbani kwao wakiwa na shangwe na wakihisi vema moyoni. (7:10) Yehova pia amependezwa. Athibitisha tena agano la Ufalme kwa Sulemani, akionya wakati ule ule juu ya matokeo mabaya ya ukosefu wa utii.
13. (a) Ni kazi gani ya ujenzi inayofuata ile ya hekalu? (b) Malkia wa Sheba ajielezaje aonapo ufalme wa Sulemani?
13 Sasa Sulemani aendeleza kazi kubwa ya ujenzi katika milki yake yote, akijenga si nyumba ya kifalme kwa ajili yake mwenyewe bali pia majiji yenye ngome, majiji yenye ghala, majiji ya magari-farasi ya vita, na majiji kwa ajili ya wapanda farasi, na pia kila kitu atamanicho kujenga. Ni kipindi cha fanaka na amani tukufu kwa sababu mfalme na watu wote wanafikiria ibada ya Yehova. Hata malkia wa Sheba, kutoka kilometa zaidi ya 1,900, asikia juu ya fanaka na hekima ya Sulemani na kufunga safari hiyo ndefu, yenye kuchosha ajionee mwenyewe. Je! anakatishwa tamaa? Hata kidogo, kwa maana akiri hivi: “Mimi sikuyasadiki maneno yao, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; wala, tazama, ukuu wa hekima yako sikuambiwa nusu; wewe umezidi kuliko habari nilizozisikia. Heri watu wako, na heri hawa watumishi wako.” (9:6, 7) Hakuna wafalme wengine wa dunia wanaompita Sulemani katika utajiri na hekima. Atawala kwa miaka 40 katika Yerusalemu.
14. Ni kwa nini Israeli wavuliwa upesi mno utukufu wao?
14 Tawala za Rehoboamu na Abiya (10:1–13:22). Utawala mkali na wa dhuluma wa mwana wa Sulemani, Rehoboamu wachochea makabila kumi ya kaskazini chini ya Yeroboamu yaasi katika 997 K.W.K. Hata hivyo, makuhani na Walawi wa falme zote mbili wasimama upande wa Rehoboamu, wakiweka uaminifu-mshikamanifu kwa agano la Ufalme juu ya utukuzo wa taifa. Upesi Rehoboamu aacha sheria ya Yehova, na Mfalme Shishaki wa Misri avamia, akipenya ndani ya Yerusalemu na kutwaa hazina za nyumba ya Yehova. Inasikitisha kama nini kwamba miaka inayozidi kidogo tu 30 baada ya ujenzi wayo, majengo hayo yaliyopambwa kwa madoido yanyang’anywa utukufu wayo! Sababu ni nini: Taifa hilo ‘limemwasi Yehova.’ Kwa wakati unaofaa Rehoboamu ajinyenyekeza, hivi kwamba Yehova haangamizi kabisa taifa hilo.—12:2.
15. Ni mapigano gani yanayofuata kifo cha Rehoboamu, na kwa nini Yuda wazidi nguvu Israeli?
15 Rehoboamu afapo mmoja wa wana wake 28, Abiya, afanywa mfalme. Utawala wa miaka mitatu wa Abiya ni wenye vita ya umwagaji wa damu pamoja na Israeli kule kaskazini. Yuda wamezongwa kwa wawili juu ya mmoja, vikosi 400,000 juu ya wale 800,000 chini ya Yeroboamu. Wakati wa mapigano makubwa yafutayo, mashujaa wa Israeli wapunguzwa chini ya nusu, na waabudu wa ndama kufikia hesabu ya nusu milioni waangamizwa. Wana wa Yuda wathibitika kuwa hodari zaidi kwa sababu “walimtegemea BWANA [Yehova, NW], Mungu wa baba zao.”—13:18.
16. Yehova ajibuje sala ya Asa yenye uharaka?
16 Mfalme Asa mwenye kuhofu Mungu (14:1–16:14). Mwandamizi wa Abiya awa mwana wake Asa. Asa ni mtetezi wa ibada ya kweli. Afanya kampeni ya kusafisha bara lote ibada ya mfano. Lakini tazama! Yuda yatishwa na kikosi kikubwa mno cha kijeshi cha Waethiopia milioni moja. Asa asali: “Utusaidie, Ee BWANA [Yehova, NW], Mungu wetu; kwa kuwa sisi twakutegemea wewe, na kwa jina lako tumekuja juu ya jamii kubwa hii.” Yehova ajibu kwa kutoa ushindi mkubwa.—14:11.
17. Asa atiwaje moyo afanye badiliko katika ibada kule Yuda, lakini akemewa kwa ajili ya nini?
17 Roho ya Mungu yaja juu ya Azaria amwambie Asa hivi: “BWANA [Yehova, NW] yu pamoja nanyi, mkiwa pamoja naye; nanyi mkimtafuta ataonekana kwenu.” (15:2) Kwa kutiwa moyo sana, Asa atokeza badiliko la ibada katika Yuda, na watu wafanya agano kwamba yeyote ambaye hatatafuta Yehova apaswa kuuawa. Hata hivyo, wakati Baasha, mfalme wa Israeli, ajengapo vizuizi vya kusimamisha mmiminiko wa Waisraeli katika Yuda, Asa afanya kosa zito kwa kukodisha Ben-hadadi, mfalme wa Shamu, apigane na Israeli, badala ya kumtumainia Yehova atoe msaada. Kwa ajili ya hilo Yehova amkemea. Ijapokuwa hilo, moyo wake Asa wathibitika kuwa “mkamilifu siku zake zote.” (15:17) Afa katika mwaka wa 41 wa utawala wake.
18. (a) Yehoshafati ateteaje ibada ya kweli, na matokeo yawa nini? (b) Mwafaka wake wa ndoa karibu uongoze kwenye afa jinsi gani?
18 Utawala mwema wa Yehoshafati (17:1–20:37). Mwana wa Asa Yehoshafati aendelea kupigana na ibada ya mfano na kuzindua kampeni maalumu ya kielimu, kukiwa wafunzi wenye kusafiri katika majiji yote ya Yuda, wakifundisha watu kutoka kitabu cha Sheria ya Yehova. Wakati wa fanaka na amani kubwa wafuata, na “ukuu wake Yehoshafati ukazidi sana.” (17:12) Lakini afanya mwafaka wa ndoa pamoja na Mfalme Ahabu wa Israeli aliye mwovu na ashuka akamsaidie kupigana na mamlaka ya Shamu yenye kukua, akipuuza Mikaya nabii wa Yehova na anusurika wakati Ahabu anapouawa katika pigano kule Ramoth-gileadi. Yehu nabii wa Yehova akemea Yehoshafati kwa ajili ya kujiunga na Ahabu mwovu. Baadaye Yehoshafati aweka waamuzi katika bara lote, naye awaagiza watimize wajibu wao mbalimbali katika hofu ya Mungu.
19. Kwenye upeo wa utawala wa Yehoshafati, pigano lathibitikaje kuwa la Mungu?
19 Sasa wafikia upeo wa utawala wa Yehoshafati. Vikosi vilivyoungana vya Moabu, Amoni, na mkoa wa milima-milima wa Seiri vyainuka juu ya Yuda kwa nguvu nyingi mno. Wavuvumuka katika nyika ya En-gedi. Hofu yapiga taifa. Yehoshafati na Yuda wote, “pamoja na wadogo wao, na wake zao, na watoto wao,” wasimama mbele ya Yehova na kumtafuta katika sala. Roho ya Yehova yaja juu ya Yahazieli Mlawi, ambaye aitia kusanyiko hilo hivi: “Sikieni, Yuda wote, nanyi mkaao Yerusalemu, na wewe mfalme Yehoshafati; BWANA [Yehova, NW] awaambia hivi, Msiogope, wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili; kwani vita si yenu bali ni ya Mungu. Kesho shukeni juu yao.” ‘Yehova atakuwa pamoja nanyi.’ Wakirauka mapema asubuhi, Yuda wapiga hatua wakiongozwa na waimbaji Walawi. Yehoshafati awatia moyo hivi: “Mwaminini BWANA [Yehova, NW] . . . waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa.” Waimbaji watukuza Yehova kwa shangwe, “kwa maana fadhili zake ni za milele.” (20:13, 15-17, 20, 21) Yehova adhihirisha fadhili zake za upendo katika njia ya ajabu, akivizia majeshi hayo yenye kuvamia hivi kwamba wauana wao kwa wao. Wakifika kwenye mnara wa mlinzi katika nyika, Wayudea wenye kuhimidi waona maiti tu. Kweli kweli, pigano ni la Yehova! Hadi mwisho wa utawala wake wa miaka 25, Yehoshafati aendelea kutembea kwa uaminifu mbele ya Yehova.
20. Ni maafa gani yanayokuwako katika utawala wa Yehoramu?
20 Tawala mbaya za Yehoramu, Ahazia, na Athalia (21:1–23:21). Yehoramu mwana wa Yehoshafati aanza vibaya kwa kuua nduguze wote. Hata hivyo, Yehova amwacha hai kwa sababu ya agano Lake pamoja na Daudi. Edomu waanza kuasi. Kutoka mahali fulani Eliya apeleka barua, ikionya Yehoramu kwamba Yehova atapiga dharuba nyumba yake kwa pigo kubwa na kwamba atakufa vibaya mno. (21:12-15) Kwa kutimiza unabii huo, Wafilisti na Waarabu wavamia na kupora Yerusalemu, na mfalme huyo auawa na maradhi ya kuchukiza sana ya matumbo, baada ya utawala wa miaka minane.
21. Ni mambo gani mabaya yanayotokezwa na utawala wa Athalia katika Yuda, lakini Yehoyada afauluje kurejesha kiti cha enzi cha Daudi?
21 Ahazia (Yehoahazi) mwana pekee aliye hai wa Yehoramu, awa mwandamizi wake, lakini avutwa kwenye ubaya na mama yake Athalia, binti ya Ahabu na Yezebeli. Utawala wake wakatizwa baada ya mwaka mmoja na ufyekaji wa Yehu wa nyumba ya Ahabu. Hilo litokeapo, Athalia awaua wajukuu wake na kunyakua kiti cha enzi. Hata hivyo, mmoja wa wana wa Ahazia abaki hai. Yeye ni Yehoashi mwenye mwaka mmoja, anayefichwa hadi katika nyumba ya Yehova na Yehoshabeathi shangazi yake. Athalia atawala kwa miaka sita, na kisha mume wa Yehoshabeathi, kuhani mkuu Yehoyada, kwa moyo mkuu atwaa Yehoashi mchanga na kuamuru itangazwe kuwa yeye ni mfalme, akiwa mmoja wa “wana wa Daudi.” Akifika kwenye nyumba ya Yehova, Athalia ararua mavazi yake na kulia, “Fitina! fitina!” Lakini wapi. Yehoyada aamuru atupwe nje ya hekalu na kuuawa.—23:3, 13-15.
22. Ni jinsi gani utawala wa Yehoashi unavyoanza vizuri lakini kumalizika vibaya?
22 Tawala za Yehoashi, Amazia, na Uzia zaanza vizuri lakini zamalizika vibaya (24:1–26:23). Yehoashi atawala kwa miaka 40, na maadamu Yehoyada yu hai ili amvutie kwa mema, afanya yaliyo haki. Hata apendezwa na nyumba ya Yehova na airekebisha upya. Hata hivyo, Yehoyada afapo, Yehoashi avutwa na wakuu wa Yuda ageuke kutoka kwa ibada ya Yehova ili atumikie nguzo takatifu na sanamu. Roho ya Mungu ichocheapo Zekaria mwana wa Yehoyada akemee mfalme huyo, Yehoashi aamuru nabii huyo apigwe kwa mawe hadi kufa. Upesi baadaye kikosi kidogo cha kijeshi cha Washami chavamia, na jeshi kubwa zaidi la Yudea lashindwa kukifukuza kwa sababu “wamemwacha BWANA [Yehova, NW] Mungu wa baba zao.” (24:24) Sasa watumishi wa Yehoashi mwenyewe wainuka na kumwua.
23. Ni kigezo gani cha ukosefu wa uaminifu anachofuata Amazia?
23 Amazia awa mwandamizi wa babaye, Yehoashi. Aanza utawala wake wa miaka 29 vizuri lakini baadaye apoteza kibali cha Yehova kwa sababu aweka na kuabudu sanamu za Waedomi. “Mungu amekusudia kukuangamiza,” nabii wa Yehova amwonya. (25:16) Hata hivyo, Amazia awa mwenye majivuno na ataka vita na Israeli kule kaskazini. Kulingana na neno la Mungu, apatwa na ushinde wenye kuaibisha mikononi mwa Waisraeli. Baada ya ushinde huo, wala-njama wainuka na kumwua.
24. Nguvu za Uzia zawaje udhaifu wake, na tokeo lawa nini?
24 Uzia, mwana wa Amazia afuata nyayo za baba yake. Atawala vizuri kwa sehemu kubwa ya ile miaka 52, akipata kujulikana sana kuwa stadi wa kijeshi, kuwa mjenzi wa minara, na kuwa ‘mpenda ukulima.’ (26:10) Apatia jeshi lake silaha na mitambo. Hata hivyo, nguvu zake zawa ndio udhaifu wake. Awa mwenye kiburi na ajitanguliza kuchukua wajibu wa kikuhani wa kutoa ubani katika hekalu la Yehova. Kwa ajili ya hilo, Yehova ampiga kwa ukoma. Kwa sababu hiyo, alazimika kuishi peke yake, mbali na nyumba ya Yehova na pia mbali na nyumba ya mfalme, ambamo mwana wake Yothamu ahukumu watu mahali pake.
25. Ni kwa nini Yothamu afaulu?
25 Yothamu atumikia Yehova (27:1-9). Tofauti na baba yake, Yothamu ‘havamii hekalu la Yehova.’ Badala yake ‘afanya yaliyo ya adili machoni pa Yehova.’ (27:2) Wakati wa utawala wake wa miaka 16, afanya kazi nyingi ya ujenzi na afanikiwa kukomesha uasi wa Waamoni.
26. Ahazi akwea kufikia vilele gani vya uovu visivyo na kifani?
26 Mfalme Ahazi mwovu (28:1-27). Ahazi mwana wa Yothamu athibitika kuwa mmojawapo wa waovu zaidi kati ya wafalme 21 wa Yudea. Apita kiasi kwa kutoa wana wake mwenyewe kuwa dhabihu za kuteketeza kwa miungu ya kikafiri. Kwa sababu hiyo, Yehova amwacha mikononi mwa majeshi ya Shamu, Israeli, Edomu, na Ufilisti. Kwa hiyo Yehova anyenyekeza Yuda kwa sababu Ahazi ‘afanyia Yuda aibu, na kumwasi Yehova.’ (28:19) Akiharibika zaidi na zaidi, Ahazi atoa dhabihu kwa miungu ya Washami kwa sababu Washami wathibitika kuwa hodari zaidi yake katika pigano. Afunga milango ya nyumba ya Yehova na mahali pa ibada ya Yehova aweka ibada ya miungu ya makafiri. Hatimaye, utawala wa Ahazi wamalizika baada ya miaka 16.
27. Hezekia aonyeshaje bidii kwa ajili ya ibada ya Yehova?
27 Mfalme Hezekia mwaminifu (29:1–32:33). Hezekia, mwana wa Ahazi, atawala kwa miaka 29 katika Yerusalemu. Kitendo chake cha kwanza ni kufungua tena na kutengeneza ilikoharibika milango ya nyumba ya Yehova. Kisha akusanya makuhani na Walawi na kuwapa maagizo wasafishe hekalu na kulitakasa kwa ajili ya utumishi wa Yehova. Ajulisha rasmi kwamba ataka kufanya agano pamoja na Yehova ili ageuze kasirani Yake yenye kuwaka. Ibada ya Yehova yaanzwa tena kwa njia tukufu.
28. Ni karamu gani kubwa sana anayofanya Hezekia katika Yerusalemu, na watu waonyeshaje shangwe yao?
28 Sherehe ya Kupitwa kubwa mno imepangwa, lakini kwa kuwa hakuna wakati wa kuitayarisha katika mwezi wa kwanza, uandalizi (mpango) fulani wa Sheria watumiwa, nayo yasherehekewa katika mwezi wa pili wa mwaka wa kwanza wa utawala wa Hezekia. (2 Nya. 30:2, 3; Hes. 9:10, 11) Mfalme aalika si Yuda wote pekee bali pia Israeli pia wahudhurie, na ingawa wengine katika Efraimu, Manase, na Zebuloni wadhihaki mwaliko huo, wengine wajinyenyekeza na kuja Yerusalemu pamoja na Yuda wote. Kufuatia sherehe ya Kupitwa hiyo, Sikukuu ya Keki (Mikate) Zisizotiwa Chachu yafanywa. Jinsi ilivyo karamu yenye shangwe ya siku saba! Kwa kweli ni yenye kujenga sana hata kwamba kundi lote larefusha karamu hiyo siku nyingine saba. Kuna “furaha kuu katika Yerusalemu; kwa sababu tangu siku za Sulemani mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli, hayajakuwako mambo kama hayo huko Yerusalemu.” (2 Nya. 30:26) Watu hao waliorejehswa kiroho wafuatilia shughuli ya kuangamiza ibada ya sanamu katika Yuda na Israeli, naye Hezekia, kwa upande wake, arejesha michango ya kimwili kwa ajili ya Walawi na utumishi mbalimbali wa hekalu.
29. Yehova athawabishaje tumaini imara la Hezekia katika Yeye?
29 Kisha Senakeribu mfalme wa Ashuru avamia Yuda na kutisha Yerusalemu. Hezekia awa na moyo mkuu, aganga kinga za jiji, na kukaidi dhihaka za adui. Akitumaini kikamili Yehova, aendelea kusali kwa ajili ya msaada. Kwa kitendo kikubwa Yehova ajibu sala hiyo ya imani. Yeye achukua hatua ya kupeleka “malaika aliyewakatia mbali mashujaa wote, na majemadari, na maakida, matuoni mwa mfalme wa Ashuru.” (32:21) Senakeribu arejea nyumbani kwa aibu. Hata miungu yake haiwezi kumsaidia kujiondolea aibu, kwa maana baadaye auawa kwenye madhabahu na wana wake mwenyewe. (2 Fal. 19:7) Kwa mwujiza Yehova arefusha maisha ya Hezekia, naye aja kuwa na utajiri na utukufu mwingi, Yuda wote wakimheshimu wakati wa kifo chake.
30. (a) Manase arudia uovu gani, lakini nini kinachofuata toba yake? (b) Ni nini kinachotia alama ya utawala mfupi wa Amoni?
30 Manase na Amoni watawala kwa uovu (33:1-25). Manase mwana wa Hezekia arudia mwendo mwovu wa babu yake Ahazi, akiondoa wema wote uliotimizwa wakati wa utawala wa Hezekia. Ajenga mahali pa juu, asimamisha nguzo takatifu, na hata atoa wana wake dhabihu kwa miungu bandia. Mwishowe, Yehova aleta mfalme wa Ashuru juu ya Yuda, na Manase apelekwa utumwani Babuloni. Kule atubu ukosaji wake. Yehova aonyeshapo rehema kwa kumrejesha kwenye ufalme wake, aazimia kuondolea mbali ibada ya roho waovu na kurejesha dini ya kweli. Hata hivyo, Manase afapo baada ya utawala mrefu wa miaka 55, mwana wake Amoni akwea penye kiti cha enzi na kwa uovu atetea ibada bandia tena. Baada ya miaka miwili, watumishi wake mwenyewe wamwua.
31. Ni nini mambo makuu ya utawala wa moyo mkuu wa Yosia?
31 Utawala wenye moyo mkuu wa Yosia (34:1–35:27). Yosia mchanga, mwana wa Amoni, afanya jaribio la moyo mkuu la kurejesha ibada ya kweli. Aamuru madhabahu za Mabaali na mifano ya kuchongwa ibomolewe, na aganga nyumba ya Yehova, ambamo chapatikana “kitabu cha torati ya BWANA [Yehova, NW] iliyotolewa kwa mkono wa Musa,” bila shaka nakala ya awali. (34:14) Hata hivyo, Yosia mwadilifu aambiwa kwamba msiba utakuja juu ya bara hilo kwa ajili ya ukosefu wa uaminifu ambao tayari umekwisha tokea, lakini si katika siku yake. Katika mwaka wa 18 wa utawala wake, apanga mwadhimisho wenye kutokeza wa Kupitwa. Baada ya utawala wa miaka 31, Yosia afa katika jaribio lisilofaa kitu la kuzuia vikosi vya Kimisri visipite kwenye bara hilo vikielekea Frati.
32. Wafalme wanne wa mwisho waongozaje Yuda kwenye mwisho wenye afa?
32 Yehoahazi, Yehoyakimu, Yehoyakini, Sedekia, na kuachwa ukiwa kwa Yerusalemu (36:1-23). Uovu wa wafalme Wayudea wanne wa mwisho wapeleka upesi taifa kwenye mwisho walo wenye afa. Mwana wa Yosia, Yehoahazi atawala kwa miezi mitatu tu, na kuondolewa na Farao Neko wa Misri. Mahali pake pachukuliwa na ndugu yake Eliakimu, ambaye jina lake labadilishwa kuwa Yehoyakimu, na wakati wa utawala wake Yuda watiishwa na mamlaka mpya ya ulimwengu, Babuloni. (2 Fal. 24:1) Yehoyakimu anapoasi, Nebukadreza akwea Yerusalemu ili kumwadhibu katika 618 K.W.K., lakini Yehoyakimu afa mwaka uo huo, baada ya kutawala miaka 11. Mahali pake pachukuliwa na mwana wake wa miaka 18, Yehoyakini. Baada ya utawala usiofikia miezi mitatu, Yehoyakini asalimu amri ya Nebukadreza na kupelekwa utumwani Babuloni. Nebukadreza sasa aweka penye kiti cha enzi Sedekia, mwana wa tatu wa Yosia, baba mdogo wa Yehoyakini. Sedekia atawala vibaya kwa miaka 11, akikataa ‘kujinyenyekeza mbele ya Yeremia nabii aliponena kwa kinywa cha Yehova.’ (2 Nya. 36:12) Kwa ukosefu mkubwa wa uaminifu, makuhani na watu pia wanajisi nyumba ya Yehova.
33. (a) Ule ukiwa wa miaka 70 waanzaje, ‘ili kulitimiza neno la Yehova’? (b) Ni amri gani ya kihistoria imeandikwa katika mistari miwili ya mwisho ya kitabu cha Mambo ya Nyakati cha Pili?
33 Hatimaye, Sedekia aliasi kongwa la Babuloni, na wakati huu Nebukadreza hana rehema. Hasira ya Yehova ni kamili, na hakuna maponyo. Yerusalemu laanguka, hekalu lalo laporwa na kuteketezwa, na waokokaji wa mazingiwa ya miezi 18 wapelekwa utumwani hadi Babuloni. Yuda yaachwa ukiwa. Hivyo, katika mwaka huu wa 607 K.W.K., waanza ukiwa “ili kulitimiza neno la BWANA [Yehova, NW] kwa kinywa cha Yeremia . . . kutimiza miaka sabini.” (36:21) Kisha mwandishi wa matukio hayo aruka pengo hilo la karibu miaka 70 ili aandike katika mistari miwili ya mwisho amri ya kihistoria ya Koreshi katika 537 K.W.K. Watumwa wa Kiyahudi watawekwa huru! Yerusalemu lazima liinuke tena!
KWA NINI NI CHENYE MAFAA
34. Ni nini kinachokaziwa katika uchaguzi wa Ezra wa habari, na hilo lilikuwaje lenye mafaa kwa taifa?
34 Kitabu cha Mambo ya Nyakati cha Pili chaongezea ushuhuda wacho wenye nguvu kwenye ule wa mashahidi wengine kuhusu kipindi hiki chenye matukio mengi, 1037-537 K.W.K. Zaidi ya hayo, chatoa habari ya ziada yenye thamani isiyopatikana katika historia nyinginezo za kimaandiko, kwa kielelezo, kwenye 2 Mambo ya Nyakati sura 19, 20, na 29 hadi 31. Uchaguzi wa Ezra wa habari ulikazia zile sehemu za msingi na za kudumu katika historia ya taifa hilo, kama vile ukuhani na utumishi wayo, hekalu, na agano la Ufalme. Hayo yalikuwa yenye mafaa katika kuunganisha taifa katika tumaini la Mesiya na Ufalme wake.
35. Ni mambo gani ya maana yanayothibitishwa katika mistari ya kumalizia ya kitabu cha Mambo ya Nyakati cha Pili?
35 Mistari ya kufunga ya kitabu cha Mambo ya Nyakati cha Pili (36:17-23) yatoa uthibitisho wenye uhakika wa utimizo wa Yeremia 25:12 na, kuongezea hilo, yaonyesha kwamba miaka 70 kamili lazima ihesabiwe tangu ukiwa kamili wa bara hadi kurejeshwa kwa ibada ya Yehova kule Yerusalemu katika 537 K.W.K. Kwa hiyo ukiwa huo ulianza katika 607 K.W.K.c—Yer. 29:10; 2 Fal. 25:1-26; Ezra 3:1-6.
36. (a) Ni onyo gani lenye nguvu lililomo katika kitabu cha Mambo ya Nyakati cha Pili? (b) Linatiaje nguvu tazamio linalohusu Ufalme?
36 Kitabu cha Mambo ya Nyakati cha Pili kina onyo lenye nguvu kwa wale wanaotembea katika imani ya Kikristo. Wengi sana wa wafalme wa Yuda walianza vizuri lakini wakaingilia njia mbovu. Jinsi maandishi hayo ya kihistoria yanavyoonyesha kwa nguvu sana kwamba kufanikiwa kwategemea uaminifu kwa Mungu! Kwa hiyo twapaswa kutii onyo tusiwe “miongoni mwao wasitao na kupotea, bali [tuwemo] miongoni mwa hao walio na imani ya [kuokoa] roho [nafsi, NW] zetu.” (Ebr. 10:39) Hata Mfalme Hezekia mwaminifu alikuja kuwa mwenye kiburi alipopata nafuu ya ugonjwa wake, na ni kwa sababu tu alijinyenyekeza haraka ndipo aliweza kuepuka ghadhabu ya Yehova. Kitabu cha Mambo ya Nyakati cha Pili chaadhimisha sifa nzuri sana za Yehova na chatukuza jina na enzi kuu yake. Historia yote imetolewa kwa maoni ya ujitoaji kamili kwa Yehova. Kinapokazia pia ukoo wa kifalme wa Yuda, kinatia nguvu tazamio letu la kuona ibada yenye kutakata ikitukuzwa chini ya Ufalme wa milele wa Yesu Kristo, aliye “mwana wa Daudi” mwaminifu-mshikamanifu.—Mt. 1:1; Mdo. 15:16, 17.
[Maelezo ya Chini]
a Insight on the Scriptures, Vol. 1, page 147
b Insight on the Scriptures, Vol. 1, page 750-1; Vol. 2, pages 1076-8.
c Insight on the Scriptures, Vol. 1, page 463; Vol. 2, page 326