Kitabu Cha Biblia Namba 26—Yeremia
Mwandikaji: Yeremia
Mahali Kilipoandikiwa: Yuda na Misri
Uandikaji Ulikamilishwa: 580 K.W.K.
Wakati Uliohusishwa: 647–580 K.W.K.
1. Yeremia alipewa utume lini na nani?
NABII Yeremia aliishi katika nyakati zenye hatari na mchafuko. Alipewa utume na Yehova katika mwaka 647 K.W.K., mwaka wa 13 wa utawala wa Mfalme Yosia wa Yuda mwenye kuhofu Mungu. Wakati wa nyumba ya Yehova kutengeneza kulikoharibika, kitabu cha Sheria ya Yehova kilipatikana akasomewa mfalme. Alifanya kazi kwa bidii aitekeleze, lakini zaidi ambayo angeweza kufanya ni kugeuza kwa muda tu kule kukengeuka kwenye ibada ya sanamu. Manase babu yake Yosia, aliyekuwa ametawala kwa miaka 55, na baba yake Amoni, aliyekuwa ameuawa baada ya utawala wa miaka 2 tu, wote wawili walikuwa wametenda kiuovu. Walikuwa wametia moyo watu kushiriki karamu chafu za ulafi na ulevi na sherehe za kuchukiza sana, hata wakawa na desturi ya kumchomea ubani “malkia wa mbinguni” na kuitolea dhabihu za kibinadamu miungu ya kishetani. Manase alikuwa amejaza Yerusalemu damu isiyo na hatia.—Yer. 1:2; 44:19; 2 Fal. 21:6, 16, 19-23; 23:26, 27.
2. Kazi ya Yeremia ilikuwa nini, na kutoa kwake unabii kulihusu miaka gani yenye matukio mengi?
2 Yeremia hakuwa na kazi rahisi. Yeye alipaswa kutumika akiwa nabii wa Yehova katika kutabiri kufanywa ukiwa kwa Yuda na Yerusalemu, kuchomwa kwa hekalu la Yehova lenye fahari, na kutekwa kwa watu wake—misiba ambayo karibu isiwe ya kuaminika! Kutoa kwake unabii katika Yerusalemu kulipasa kuendelea miaka 40, wakati wa tawala za Wafalme wabaya Yehoahazi, Yehoyakimu, Yehoyakini (Konia), na Sedekia. (Yer. 1:2, 3) Baadaye, katika Misri, alipaswa kutoa unabii kuhusu ibada za sanamu za wakimbizi wa Kiyahudi huko. Kitabu chake kilikamilishwa katika 580 K.W.K. Kwa hiyo wakati unaohusishwa na Yeremia ni kipindi chenye matukio mengi cha miaka 67.—52:31.
3. (a) Kukubaliwa na uasilia wa kitabu cha Yeremia vilithibitishwaje katika nyakati za Kiebrania? (b) Ni ushuhuda gani zaidi juu ya hilo unaopatikana katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo?
3 Katika Kiebrania jina la nabii huyo na kitabu chake ni Yir·meyahʹ au Yir·meya’hu, maana yake, yawezekana ni, “Yehova Hukweza; au, Yehova Hulegeza [yawezekana kutoka kwenye tumbo la uzazi].” Kitabu hicho huonekana katika orodha zote za Maandiko ya Kiebrania, na kuwa kwacho sehemu ya maandiko hukubaliwa kwa ujumla. Utimizo wenye kutokeza wa hesabu fulani ya unabii mbalimbali wakati wa maisha ya Yeremia mwenyewe hushuhudia kikamili juu ya uasilia wacho. Zaidi ya hayo, Yeremia arejezewa mara kadhaa kwa jina katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo. (Mt. 2:17, 18; 16:14; 27:9) Kwamba Yesu alikuwa amejifunza kitabu cha Yeremia yaonyeshwa wazi na kuunganisha kwake lugha ya Yeremia 7:11 na ile ya Isaya 56:7 wakati aliposafisha hekalu. (Mk. 11:17; Luka 19:46) Kwa sababu ya ujasiri na moyo mkuu wa Yesu, watu fulani hata walimdhania yeye kuwa Yeremia. (Mt. 16:13, 14) Unabii wa Yeremia wa agano jipya (Yer. 31:31-34) warejezewa na Paulo kwenye Waebrania 8:8-12 na 10:16, 17. Paulo anukuu Yeremia 9:24 kwa kusema: “Yeye aonaye fahari na aone fahari juu ya Bwana [Yehova, NW].” (1 Kor. 1:31) Kwenye Ufunuo 18:21 kuna matumizi yenye nguvu hata zaidi ya kielezi cha Yeremia (Yer. 51:63, 64) cha anguko la Babuloni.
4. Akiolojia yaungaje mkono maandishi hayo?
4 Vitu vilivyopatikana vya akiolojia (uchimbuzi wa vitu vya kale) pia huunga mkono maandishi yaliyomo katika Yeremia. Kwa kielelezo, maandishi mamoja ya matukio ya Kibabuloni yaeleza juu ya kutekwa kwa Yerusalemu na Nebukadreza katika 617 K.W.K., alipombamba mfalme (Yehoyakimu) na kuweka mmoja aliyemchagua (Sedekia).—24:1; 29:1, 2; 37:1.a
5. (a) Ni nini yanayojulikana kuhusu Yeremia mwenyewe? (b) Ni nini kinachoweza kusemwa juu ya mtindo wake wa kuandika?
5 Tuna wasifu kamili zaidi wa Yeremia kuliko wowote wa manabii wengineo wa kale isipokuwa Musa. Yeremia afunua mengi juu yake mwenyewe, hisia zake, na hisia-moyo zake, ikionyesha kwa uthabiti ujasiri na moyo mkuu, pamoja na unyenyekevu na wororo wa moyo. Yeye hakuwa nabii tu bali pia kuhani, mjumlishaji wa Andiko, na mwanahistoria sahihi. Kwa kuzaliwa yeye alikuwa mwana wa kuhani Hilkia wa Anathothi, jiji la kikuhani katika nchi iliyokuwa kaskazini mwa Yerusalemu, “katika nchi ya Benyamini.” (1:1) Mtindo wa uandishi wa Yeremia ni wazi, wa moja kwa moja, na wenye kueleweka rahisi. Vielezi na picha za kufananisha ni tele, na kitabu hiki ni jumla ya nathari (maandishi ya kawaida) na ushairi.
YALIYOMO KATIKA YEREMIA
6. Habari inayozungumzwa na unabii huo imepangwaje?
6 Habari yenyewe imepangwa si kulingana na tarehe ya matukio bali kwa kulingana na habari inayozungumzwa. Kwa hiyo, simulizi linafanya mabadiliko mengi kuhusu wakati na hali zenye kuzunguka. Mwishowe, kufanywa ukiwa kwa Yerusalemu na Yuda kwaelezwa kwa urefu ulio wazi katika sura ya 52. Hiyo haionyeshi tu utimizo wa mwingi wa unabii bali pia yaeleza hali zinazozunguka kitabu cha Maombolezo, kinachofuatia.
7. Yeremia alikuwaje nabii, naye Yehova ampaje uhakika tena?
7 Yehova ampa Yeremia utume (1:1-19). Je! Yeremia alipewa utume kwa sababu alitaka kuwa nabii au kwa sababu alitoka katika familia ya kikuhani? Yehova mwenyewe aeleza: “Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.” Huo ni mgawo kutoka kwa Yehova. Je! Yeremia ana nia ya kwenda? Kwa unyenyekevu atoa udhuru huu, “Mimi ni mtoto.” Yehova amhakikishia hivi: “Tazama, nimetia maneno yangu kinywani mwako; angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung’oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.” Yeremia hapaswi kuogopa. “Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, asema BWANA [Yehova, NW], ili nikuokoe.”—1:5, 6, 9, 10, 19.
8. (a) Yerusalemu limekosa kuwa jaminifu katika nini? (b) Yehova ataletaje msiba?
8 Yerusalemu, mke asiye mwaminifu (2:1–6:30). Neno la Yehova laletea Yeremia ujumbe gani? Yerusalemu limesahau upendo walo wa kwanza. Limemwacha Yehova, Chanzo cha maji ya uhai, na kufanya umalaya pamoja na miungu migeni. Kutoka kwa mzabibu mwekundu mwema sana, limebadilishwa likawa “mche usiofaa wa mzabibu-mwitu.” (2:21) Marinda yalo yamepakwa damu ya nafsi za maskini wasio na hatia. Hata Israeli malaya imethibitika kuwa yenye uadilifu zaidi ya Yuda. Mungu atoa wito kwa wana hao walioasi warejee kwa sababu yeye ndiye mume mwenyewe wao. Lakini wao wamekuwa kama mke mwenye hiana. Waweza kurejea kama wakiondoa vitu vyao vyenye kuchukiza sana na kutahiri mioyo yao. “Inueni ishara kuelekea Sayuni,” kwa maana Yehova ataleta msiba kutoka kaskazini. (4:6, NW) Anguko baada ya anguko! Kama simba kutoka kwenye kichaka chake, kama upepo wenye kukausha ngozi kupitia jangwani, kama tufani iliyo kama magari ya vita, ndivyo mtekelezaji wa Yehova atakavyokuja.
9. (a) Yeremia ana neno gani kwa ajili ya Yerusalemu lenye shingo ngumu? (b) Vilio vyao vya amani vina faida gani?
9 Nenda ukipita-pita katika Yerusalemu. Waona nini? Kuvunja sheria na ukosefu wa uaminifu peke yake! Watu wamemkana Yehova, na neno Lake kinywani mwa Yeremia lazima liwe kama moto wa kuwateketeza kama vipande vya mbao. Sawa na ambavyo wamemwacha Yehova ili wakatumikie mungu wa kigeni, ndivyo Yeye atakavyowafanya watumikie wageni katika bara la kigeni. Wenye shingo ngumu hao! Wana macho lakini hawawezi kuona, na masikio lakini hawawezi kusikia. Ni vibaya kama nini! Manabii na makuhani kwa kweli watoa unabii usio wa kweli, “na watu wangu wanapenda mambo yawe hivyo,” asema Yehova. (5:31) Msiba wakaribia kutoka kaskazini, hata hivyo “tangu aliye mdogo hata aliye mkubwa miongoni mwao, kila mmoja ni mtamanifu [ajifanyia mwenyewe faida isiyo ya haki, NW].” Wanasema, “[Kuna, NW] Amani, [kuna, NW] Amani, wala hapana amani.” (6:13, 14) Lakini ghafula mharibifu atafika. Yehova amefanya Yeremia kuwa mtahini (mjaribu) vyuma miongoni mwao, lakini kilichopo tu ni kutu na fedha iliyokataliwa. Wao ni wabaya kwa ujumla.
10. Ni kwa nini lazima Yerusalemu likutane na hali ile ile iliyopata Shilo na Efraimu?
10 Onyo kwamba hekalu si ulinzi hata kidogo (7:1–10:25). Neno la Yehova lamjia Yeremia, naye apaswa kupiga mbiu kwenye lango la hekalu. Msikie akipaaza sauti kwa wale wanaoingia: ‘Mwajivunia hekalu la Yehova, lakini nyinyi mwafanyaje? Mwaonea yatima na mjane, mwamwaga damu isiyo na hatia, mwatembea kufuatia miungu mingine, mwaiba, mwaua, mwafanya uzinzi, mwaapa ubandia, na kutolea Baali dhabihu! Wanafiki! Mmefanya nyumba ya Yehova kuwa “pango la wanyang’anyi.” Kumbukeni aliyofanya Yehova kule Shilo. Yeye atafanya lilo hilo kwa nyumba yenu, Ee Yuda, naye atawatupa nje, sawa na alivyotupa nje Efraimu (Israeli) kuelekea kaskazini.’—Yer. 7:4-11; 1 Sam. 2:12-14; 3:11-14; 4:12-22.
11. Kwa nini Yuda imepita kiwango cha kuombewa?
11 Yuda imepita kiwango cha kuombewa. Hata watu wanatengeneza keki (mikate) ili wazidhabihu kwa “malkia wa mbinguni”! Kweli kweli, “taifa hili ndilo lisilosikiliza sauti ya BWANA [Yehova, NW], Mungu wao, wala kupokea mafundisho [nidhamu, NW]; uaminifu umepotea.” (Yer. 7:18, 28) Yuda imeweka vitu vya kuchukiza sana katika nyumba ya Yehova na imeteketeza wana na mabinti wayo kwenye sehemu za juu za Tofethi katika bonde la Hinomu. Tazama! litaitwa “Bonde la Machinjo,” na miili yao iliyokufa itakuwa chakula cha nyuni na mnyama. (7:32) Shangwe na mshangilio lazima vikome katika Yuda na Yerusalemu.
12. Badala ya amani, ni nini kitakachopata Yuda na miungu yayo iliyojifanyia?
12 Walikuwa wakitazamia amani na maponyo, lakini tazama, ogofyo! Mtawanyo, kumalizwa, na maombolezo vitatokezwa na shingo ngumu yao. ‘Yehova ndiye Mungu aliye hai na Mfalme wa milele.’ Kwa habari ya miungu ambayo haikufanya mbingu na dunia, hamna roho ndani yayo. Hiyo ni ubatili na kazi ya mzaha, nayo itaangamia. (10:10-15) Yehova atawatupa wakaaji wa dunia. Sikiliza! Kishindo kikubwa kutoka bara la kaskazini ambacho kitafanya ukiwa majiji ya Yuda. Nabii huyo akiri: ‘Kuelekeza mwendo wake si katika uwezo wa mwanadamu,’ naye asali asahihishwe ili asiangamizwe.—10:23.
13. Ni kwa nini Yeremia anakatazwa kusali kwa ajili ya Yuda, na Yehova anatiaje nguvu Yeremia katika saa ya hatari?
13 Wavunja-agano walaaniwa (11:1–12:17). Yuda imekosa kutii maneno ya agano layo na Yehova. Haifai kitu kwa watu kuitisha msaada. Yeremia hapaswi kusali kwa ajili ya Yuda, kwa maana Yehova “amewasha moto” juu ya mzeituni huu ambao wakati mmoja ulikuwa wenye majani mengi mabichi. (11:16) Raia wenzi wa Yeremia wa Anathothi wafanyapo njama ya kumharibu, nabii huyo ageukia Yehova kwa ajili ya nguvu na msaada. Yehova aahidi kisasi juu ya Anathothi. Yeremia auliza, “Mbona njia ya wabaya inasitawi?” Yehova amhakikishia hivi: ‘Mimi nitang’oa na kuangamiza taifa hilo lisilotii.’—12:1, 17.
14. (a) Yehova ajulisha kwamba Yerusalemu haliwezi kubadilika na kwamba hukumu juu yalo haiwezi kubadilishwa kwa vielezi gani? (b) Ni nini tokeo la Yeremia kula maneno ya Yehova?
14 Yerusalemu haliwezi kubadilika na lazima liangamizwe (13:1–15:21). Yeremia akumbusha jinsi Yehova alivyomwamuru afunge mshipi wa kitani kwenye viuno vyake na kisha aufiche kwenye jabali kando ya Frati. Yeremia alipokuja kuufukua, ulikuwa umeharibika. “Haukufaa tena kwa lo lote.” Kwa njia hiyo Yehova akatolea kielezi azimio lake la kuharibu “kiburi cha Yuda, na kiburi kikuu cha Yerusalemu.” (13:7, 9) Atawaponda pamoja katika ulevi wao, kama nyungu kubwa zilizojazwa divai. “Je! Mkushi aweza kuibadili ngozi yake, au chui madoa-doa yake?” (13:23) Vivyo hivyo, Yerusalemu haliwezi kubadilika. Yeremia hapaswi kusali kwa ajili ya watu hawa. Hata kama Musa na Samweli wangekuja mbele za Yehova ili kuwatetea, hangesikiliza, kwa maana ameazimia kuharibu Yerusalemu. Yehova amtia nguvu Yeremia kuelekeana na wenye kumsuta. Yeremia apata na kula maneno ya Yehova, tokeo likawa ni ‘furaha na shangwe ya moyo.’ (15:16) Si wakati wa kufanya mzaha wa kupoteza wakati, bali wa kutumaini Yehova, ambaye ameahidi kufanya Yeremia kuwa ukuta ulioimarishwa wa shaba kuelekeana na watu hao.
15. (a) Nyakati hizo ni zenye uzito jinsi gani, na Yehova anatia mkazo huo kwa amri gani? (b) Watu watakujaje kujua jina la Yehova, na ni kwa nini dhambi yao haimdanganyi?
15 Yehova atapeleka wavuvi na wawindaji (16:1–17:27). Kwa sababu ya ukiwa unaokaribia, Yehova aamuru Yeremia hivi: “Wewe hutaoa mke, wala hutakuwa na wana wala binti mahali hapa.” (16:2) Si wakati wa kuomboleza wala kula karamu pamoja na watu hao, kwa maana Yehova yu karibu kuwatupa kutoka kwenye bara hilo. Kisha Yehova aahidi pia kupeleka ‘wavuvi wawavue na wawindaji wawawinde,’ na kwa yeye kutimiza yote hayo, “watajua ya kuwa jina [lake] ni YEHOVA.” (16:16, 21) Dhambi ya Yuda imechongwa kwenye mioyo ya watu kwa kalamu ya chuma, ndiyo, kwa ncha ya almasi. “Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha,” lakini Yehova aweza kuuchunguza moyo. Hakuna anayeweza kumdanganya. Wale wenye kuasi imani ‘wameacha kisima cha maji yaliyo hai, Yehova.’ (17:9, 13) Kama Yuda haitatakasa siku ya Sabato, Yehova atakula kwa moto malango na minara yayo.
16. Yehova atoa kielezi gani kupitia mfinyanzi na vyombo vyake vya udongo?
16 Mfinyanzi na udongo (18:1–19:15). Yehova amwamuru Yeremia aende kwenye nyumba ya mfinyanzi. Huko aona jinsi mfinyanzi arudishapo chombo cha udongo kilichoharibika, na kukifanya kuwa chombo kingine kama apendavyo. Kisha Yehova ajulisha rasmi kuwa ndiye Mfinyanzi wa nyumba ya Israeli, mwenye uwezo kamili wa kubomoa au kujenga. Kisha, amwambia Yeremia atwae nyungu ya mfinyanzi aende kwenye Bonde la Hinomu na huko ajulishe rasmi msiba kutoka kwa Yehova kwa sababu watu wamepajaza mahali hapo na damu isiyo na hatia, wakiteketeza wana wao katika moto kuwa matoleo mazima ya kuteketezwa kwa Baali. Lazima Yeremia avunje nyungu hiyo kuwa wonyesho wa Yehova kuvunja Yerusalemu na watu wa Yuda.
17. Yeremia apatwa na jambo gani gumu, lakini je! hilo linamnyamazisha?
17 Hakuna kuacha chini ya mnyanyaso (20:1-18). Kwa kuudhiwa na kule kuhubiri kwa ujasiri kwa Yeremia, msimamizi wa hekalu Pashuri amtia Yeremia katika mikatale usiku kucha. Afunguliwapo, Yeremia atabiri kutekwa na kifo cha Pashuri katika Babuloni. Akiwa amehuzunishwa na dhihaka na suto aliloelekezewa, Yeremia atafakari kuacha. Hata hivyo, hawezi kukaa kimya. Neno la Yehova laja kuwa ‘katika moyo wake kama moto uwakao, uliofungwa ndani ya mifupa yake,’ hata alazimika kunena. Ingawa alaani siku ya kuzaliwa kwake, apaaza sauti hivi: “Mwimbieni BWANA [Yehova, NW]; msifuni BWANA [Yehova, NW]; kwa maana ameiponya roho [nafsi, NW] ya mhitaji katika mikono ya watu watendao maovu.”—20:9, 13.
18. Yeremia ajulisha Sedekia juu ya nini?
18 Ghadhabu ya Yehova juu ya watawala (21:1–22:30). Katika kujibu swali kutoka kwa Sedekia, Yeremia amjulisha juu ya hasira kali ya Yehova juu ya jiji hilo: Mfalme wa Babuloni atalizingira, nalo litaharibiwa kwa tauni, upanga, njaa kali, na moto. Shalumu (Yehoahazi) atafia uhamishoni, Yehoyakimu atazikwa kama punda wa kiume, na mwana wake Konia (Yehoyakini) atavurumishwa kutoka Yuda akafie Babuloni.
19. Yeremia atabiri nini juu ya “Chipukizi la haki,” na nini kinachotolewa kielezi na vile vikapu viwili vya tini?
19 Tumaini katika “Chipukizi la haki” (23:1–24:10). Yehova aahidi wachungaji halisi watachukua mahali pa wachungaji bandia na “Chipukizi la haki” la kisiki cha Daudi, mfalme ambaye ‘atamiliki, atatenda kwa hekima, naye atafanya hukumu na haki katika nchi.’ Jina lake ni nani? “Jina lake atakaloitwa ni hili, BWANA [Yehova, NW] ni haki yetu.” Atakusanya baki lililotawanywa. (23:5, 6) Kama manabii wangesimama katika kikundi cha Yehova cha usiri, wangalisababisha watu wasikie na kuacha njia yao mbaya. Badala yake, Yehova asema, ‘wanawakosesha watu wangu kwa uwongo wao.’ (23:22, 32) “Tazama, vikapu viwili vya tini.” Yeremia atumia tini nzuri na mbaya kueleleza baki jaminifu likirejea kwenye bara lao kwa kibali cha Mungu na jamii nyingine ikifikia kwenye mwisho wenye msiba.—24:1, 5, 8-10.
20. Yehova atumiaje Babuloni kuwa mtumishi wake, lakini nayo, itapatwa na nini?
20 Ugomvi wa Yehova pamoja na mataifa (25:1-38). Sura hii ni muhtasari wa hukumu zinazotokea kirefu zaidi katika sura za 45-49. Kwa unabii mtatu unaolingana, sasa Yehova atangaza msiba kwa mataifa yote duniani. Kwanza, Nebukadreza atambulishwa kuwa mtumishi wa Yehova wa kufanya ukiwa Yuda na mataifa yenye kuzunguka, “nayo mataifa haya watamtumikia mfalme wa Babeli miaka sabini.” Kisha itakuwa zamu ya Babuloni, nayo itakuwa ‘ukiwa milele.’—25:1-14.
21. Ni nani wapaswao kunywa kikombe cha hasira kali ya Yehova? Kwa tokeo gani?
21 Unabii wa pili ni njozi ya kikombe cha divai cha hasira kali ya Yehova. Yeremia apaswa kutwaa kikombe hiki kwa mataifa, na lazima ‘wakinywe, na kulewa-lewa, na kufanya wazimu’ kwa sababu ya uharibifu wa Yehova ujao juu yao. Kwanza, kwa Yerusalemu na Yuda! Kisha, kusonga hadi Misri, kurejea kwa Ufilisti, ng’ambo ile ya Edomu, kule juu Tiro, kwa mabara ya karibu na mbali, na kwa “wafalme wote wa dunia, wakaao juu ya uso wa dunia; na mfalme wa Sheshaki atakunywa baada yao.” ‘Watakunywa, watapike na kuanguka.’ Hakuna yeyote atakayeachwa.—25:15-29.
22. Kasirani yenye kuwaka moto ya Yehova itaonyeshwa katika msiba gani mkubwa?
22 Katika unabii wa tatu, Yeremia afikia vilele vyenye fahari vya ushairi. “BWANA [Yehova, NW] atanguruma toka juu . . . juu ya wenyeji wote wa dunia.” Sauti, msiba, tufani kubwa! “Na waliouawa na BWANA [Yehova, NW] siku ile watakuwapo, toka upande mmoja wa dunia hata upande wa pili.” Hakuna kuomboleza, hakuna maziko. Watakuwa kama mbolea juu ya ardhi. Wachungaji bandia watachinjwa, pamoja na wenye fahari wa makundi yao. Hakuna cha wao kuponyoka. Sikiliza yowe lao! Yehova mwenyewe “anayaharibu malisho yao . . . kwa sababu ya hasira yake kali.”—25:30-38.
23. (a) Ni njama gani inayofanywa juu ya Yeremia, kinga yake ni nini, na ni vitangulizi gani vinavyorejezewa katika kumwachilia? (b) Yeremia aigizaje utumwa wa Kibabuloni ujao, na ni unabii gani kuhusu Hanania unaotimia?
23 Yeremia aondolewa malawama (26:1–28:17). Watawala na watu wafanya njama ili wamwue Yeremia. Yeremia ajitetea. Ni neno la Yehova alilonena. Wakimwua, wataua mtu asiye na hatia. Uamuzi: hana hatia. Wanaume wazee watokeza vitangulizi vya manabii Mika na Uria katika kuzungumzia mwendo wa Yeremia. Kisha Yehova aamuru Yeremia atengeneze vifungo na nira, na kuviweka juu ya shingo yake, na kisha avitume kwa mataifa yanayozunguka kuwa ishara ya kwamba ni lazima watumikie mfalme wa Babuloni kwa vizazi vitatu vya watawala. Hanania, mmojawapo manabii bandia, apinga Yeremia. Yeye ajulisha rasmi kwamba nira ya Babuloni itavunjika katika muda wa miaka miwili na aonyesha hilo kwa kuvunja ile nira ya mbao. Yehova akazia unabii wake kwa kumwamuru Yeremia atengeneze nira za chuma na kutabiri kwamba Hanania lazima afe mwaka huo. Hanania afa.
24. (a) Yeremia apelekea wahamishwa katika Babuloni ujumbe gani? (b) Yehova atafanya agano jipya pamoja na nani, nalo litathibitikaje kuwa tukufu zaidi ya lile agano la kwanza?
24 Faraja kwa wahamishwa katika Babuloni (29:1–31:40). Yeremia aandikia wahamishwa waliopelekwa Babuloni pamoja na Yekonia (Yehoyakini): Tulieni huko, kwa maana kabla Yehova hajawarejesha, kwaja kipindi cha miaka 70 ya uhamisho. Yehova aamuru Yeremia aandike juu ya kurudi kwao katika kitabu: Yehova atavunja nira yao, na kwa hakika “watamtumikia BWANA [Yehova, NW], Mungu wao, na Daudi, mfalme wao, nitakayemwinua kwa ajili yao.” (30:9) Raheli lazima azuie sauti yake asimwage machozi, kwa maana wana wake “watakuja tena toka nchi ya adui.” (31:16) Na sasa, julisho rasmi lenye kutuliza latolewa na Yehova! Yeye atafanya agano jipya pamoja na nyumba za Yuda na Israeli. Agano tukufu zaidi ya lile walilovunja! Yehova ataandika sheria yake ndani sana ya mioyo yao. “Nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.” Tangu aliye mdogo zaidi hadi aliye mkubwa zaidi, wote watajua Yehova, naye atasamehe kosa lao. (31:31-34) Jiji lao litajengwa kuwa kitu kitakatifu kwa Yehova.
25. Uhakika wa kurudishwa kwa Israeli wakaziwaje, nalo neno la Yehova laleta habari gani?
25 Agano la Yehova pamoja na Daudi ni hakika (32:1–34:22). Wakati wa mazingiwa ya mwisho ya Nebukadreza juu ya Yerusalemu, Yeremia yuko kizuizini. Hata hivyo, ikiwa ishara kwamba kwa hakika Yehova atarejesha Israeli, Yeremia anunua shamba katika Anathothi na kuziweka hati hizo za umilikiji ndani ya nyungu. Neno la Yehova sasa laleta habari njema: Yuda na Yerusalemu zitashangilia tena, na Yehova atatimiza agano lake pamoja na Daudi. Lakini wewe, Ee Sedekia, onywa kwamba mfalme wa Babuloni atateketeza mji huu kwa moto na wewe mwenyewe utaenda utumwani hadi Babuloni. Ole kwa wenye watumwa ambao wamekubali kuweka huru watumwa wao lakini wakavunja agano lao!
26. Yehova atoa ahadi gani kwa Warekabi, na kwa nini?
26 Ahadi ya Yehova kwa Rekabu (35:1-19). Katika siku za Mfalme Yehoyakimu, Yehova apeleka Yeremia kwa Warekabi. Wao walifanya kimbilio katika Yerusalemu kwenye karibio la kwanza la Wababuloni. Yeremia awapa divai wanywe. Waikataa kwa sababu ya amri ya babu yao Yonadabu, iliyotolewa miaka 250 mapema. Hakika, ni tofauti kubwa na mwendo wa ukosefu uaminifu wa Yuda! Yehova awaahidi hivi: “Yonadabu, mwana wa Rekabu, hatakosa kuwa na mtu wa kusimama mbele zangu hata milele.”—35:19.
27. Ni nini kinachofanya iwe lazima kuandika upya unabii mbalimbali wa Yeremia?
27 Yeremia aandika upya kitabu (36:1-32). Yehova amwagiza Yeremia aandike maneno yote ya unabii wake kufikia hapo. Yeremia ampa Baruku imla ya hayo, ambaye kisha ayasoma kwa sauti kubwa katika nyumba ya Yehova katika siku ya kufunga. Mfalme Yehoyakimu aagiza kunjo hilo liletwe na, asikiapo sehemu moja, airarua kwa kasirani na kuitumbukiza ndani ya moto. Aamuru Yeremia na Baruku wakamatwe, lakini Yehova awaficha na kumwambia Yeremia aandike nakili ya kunjo hilo.
28. (a) Ni unabii gani mbalimbali wenye udumifu ambao Yeremia atoa? (b) Mwendo wa Ebed-meleki watofautianaje na ule wa wakuu?
28 Siku za mwisho za Yerusalemu (37:1–39:18). Maandishi yarejesha kwenye utawala wa Sedekia. Mfalme auliza Yeremia asali kwa Yehova kwa niaba ya Yuda. Nabii huyo akataa, akisema lazima Yerusalemu liangamizwe. Yeremia ajaribu kwenda Anathothi lakini ashikwa kuwa ni mtoro, apigwa, na kufungwa gerezani siku nyingi. Ndipo Sedekia apeleka ujumbe aletwe. Je! kuna neno kutoka kwa Yehova? Hakika lipo! “Utatiwa katika mikono ya mfalme wa Babeli!” (37:17) Kwa kutiwa kasirani na matabiri yenye kuendelea ya Yeremia juu ya maangamizi, wakuu wamtupa ndani ya shimo lenye tope. Ebed-meleki yule Mwethiopia, towashi katika nyumba ya mfalme, amtetea kwa fadhili, hivi kwamba Yeremia aponyolewa na kifo chenye kuotea, lakini abaki kizuizini katika Ua wa Mlinzi. Kwa mara nyingine Sedekia amwita Yeremia mbele yake, kumbe aambiwa: ‘Jisalimishe kwa mfalme wa Babuloni au ukabiliwe na utekwa na uharibifu wa Yerusalemu!’—38:17, 18.
29. Ni msiba gani unaopata sasa Yerusalemu, lakini yawaje kwa Yeremia na Ebed-meleki?
29 Mazingiwa ya Yerusalemu yachukua miezi 18, na kisha jiji hilo lapenywa katika mwaka wa 11 wa Sedekia. Mfalme atoroka pamoja na jeshi lake lakini atwaliwa. Wana wake na wakuu wake wachinjwa mbele ya macho yake, naye apofushwa na kupelekwa Babuloni akiwa amefungwa pingu. Jiji lateketezwa na kufanywa magofu, na wote isipokuwa watu wachache maskini wapelekwa uhamishoni Babuloni. Kwa amri ya Nebukadreza, Yeremia aachiliwa kutoka kwenye ua. Kabla ya kufunguliwa kwake amwambia Ebed-meleki juu ya ahadi ya Yehova ya kumwokoa, ‘kwa sababu alitumaini Yehova.’—39:18.
30. Watu wanaosalia wanashindwaje kutii ushauri wa Yeremia, na ni hukumu gani ya maangamizi anayojulisha Yeremia katika Misri?
30 Matukio ya mwisho kule Mispa na katika Misri (40:1–44:30). Yeremia abaki kule Mispa akiwa na Gedalia, ambaye Wababuloni wamemfanya liwali juu ya watu waliosalia. Baada ya miezi miwili Gedalia auawa. Watu watafuta ushauri wa Yeremia, naye awapa neno la Mungu: ‘Yehova atawang’oa nyinyi kutoka bara hili. Msiogope kwa sababu ya mfalme wa Babuloni. Hata hivyo, ikiwa mtateremka Misri, mtakufa!’ Hao waenda Misri, wakichukua Yeremia na Baruku pamoja nao. Kule Tahpenesi katika Misri, Yeremia ajulisha hukumu ya Yehova ya maangamizi: Mfalme wa Babuloni atasimamisha kiti chake cha enzi katika Misri. Ni kazi bure kwa Israeli kuabudu miungu ya Misri na kuanza tena kumtolea dhabihu “malkia wa mbinguni.” Je! wamesahau jinsi Yehova alivyofanya Yerusalemu ukiwa kwa ajili ya ibada yalo ya sanamu? Yehova ataleta msiba juu yao katika bara la Misri, nao hawatarudi Yuda. Ili iwe ishara, Yehova atatia Farao Hofra mwenyewe katika mkono wa maadui wake.
31. Ni uhakikisho gani anaopewa Baruku?
31 Fungu la Baruku (45:1-5). Baruku asononeka kwa kusikia unabii mbalimbali wa Yeremia wa maangamizi unaorudiwa-rudiwa. Yeye aambiwa afikiri kwanza juu ya kazi ya Yehova ya kujenga na kubomoa badala ya ‘kujitafutia mambo makuu.’ (45:5) Yeye ataokolewa katika msiba huo wote.
32. ‘Upanga wa Yehova’ utakuja juu ya nani?
32 Upanga wa Yehova juu ya mataifa (46:1–49:39). Yeremia aeleza juu ya ushindi mbalimbali wa Babuloni juu ya Misri kule Karkameshi na kwingineko. Ingawa mataifa yaangamizwe, Yakobo atabaki lakini hatakosa kuadhibiwa. “Upanga wa BWANA [Yehova, NW]” utakuja juu ya Wafilisti, juu ya Moabu yenye kiburi na Amoni yenye kujivuna, juu ya Edomu na Dameski, Kedari na Hazori. (47:6) Upinde wa Elamu utavunjwa.
33. (a) Ni nini kitakachopata kikombe cha dhahabu, Babuloni? (b) Kwa hiyo, watu wa Mungu wapaswa kutendaje?
33 Upanga wa Yehova juu ya Babuloni (50:1–51:64). Yehova anena kuhusu Babuloni: Yaambie mataifa. Usifiche chochote. Babuloni imetekwa na miungu yayo imeaibishwa. Torokeni kutoka kwake. Nyundo hii ya kufulia ambayo imeponda-ponda mataifa ya dunia yote imevunjwa yenyewe. “Ewe mwenye kiburi,” mwonezi wa Israeli na Yuda waliotekwa, jua kwamba Yehova wa majeshi ni Mkombozi wao. Babuloni itakuwa makao ya wanyama wenye kupiga yowe. “Kama vile vilivyotokea Mungu alipoangusha Sodoma na Gomora . . . kadhalika hapana mtu atakayekaa huko.” (50:31, 40) Babuloni imekuwa kikombe cha dhahabu katika mkono wa Yehova cha kulewesha mataifa, lakini ghafula imeanguka, hivi kwamba yenyewe ikavunjika. Pigeni yowe juu yake, enyi watu. Yehova ameamsha roho ya wafalme wa Umedi kuleta uharibifu wayo. Wanaume hodari wa Babuloni wameacha kupigana. Wamekuwa kama wanawake. Binti ya Babuloni atakanyagiwa chini kuwa mgumu kama sakafu ya kupepetea. ‘Lazima walale usingizi wa milele, wasiamke tena.’ Bahari imeinuka na kufunika Babuloni kwa halaiki ya mawimbi. “Tokeni katikati yake, mkajiokoe nafsi zenu na hasira kali ya BWANA [Yehova, NW].” (51:39, 45) Sikiliza kilio, anguko kubwa la Babuloni! Silaha za vita za Babuloni lazima zivunjwe-vunjwe, kwa maana Yehova ni Mungu wa kisasi. Bila kushindwa atalipa.
34. Ni ishara gani inayotolea kielezi kuanguka kwa Babuloni?
34 Yeremia amwamuru Seraya hivi: ‘Nenda Babuloni na usome kwa sauti kubwa maneno haya ya unabii juu ya Babuloni. Kisha ufunge jiwe kwenye kitabu na kukitupa katika Frati. “Nawe utasema, Hivyo ndivyo utakavyozama Babeli, wala hautazuka tena, kwa sababu ya mabaya yote nitakayoleta juu yake.”—51:61-64.
35. Ni maandishi gani yanayofuata?
35 Maandishi ya kuanguka kwa Yerusalemu (52:1-34). Simulizi hilo lakaribia kufanana kabisa na lile lililotangulia kuzungumzwa kwenye 2 Wafalme 24:18-20; 25:1-21, 27-30.
KWA NINI NI CHENYE MAFAA
36. (a) Ni kielelezo gani cha bidii ya moyo mkuu tunachopata katika Yeremia? (b) Ni katika mambo gani Baruku, Warekabi, na Ebed-meleki pia ni vielelezo vizuri kwetu?
36 Unabii huu uliopuliziwa na Mungu kwa ujumla unajenga na ni wenye mafaa. Angalia kielelezo cha moyo mkuu cha nabii huyo mwenyewe. Yeye hakuwa na hofu katika kutangaza ujumbe usiopendwa na wengi kwa watu wasiomcha Mungu. Yeye alidharau ushirikiano na waovu. Yeye alithamini uharaka wa ujumbe wa Yehova, akajitoa mwenyewe kwa moyo wote kwa kazi ya Yehova bila kuacha kamwe. Yeye alipata Neno la Mungu kuwa kama moto katika mifupa yake, nalo lilikuwa mshangilio na shangwe ya moyo wake. (Yer. 15:16-20; 20:8-13) Daima sisi na tuwe wenye bidii hivyo kwa ajili ya neno la Yehova! Pia na tuunge mkono kwa uaminifu-mshikamanifu watumishi wa Mungu, kama alivyofanya Baruku kwa Yeremia. Utii wa moyo mweupe wa Warekabi pia ni kielelezo kizuri sana kwetu, na ndivyo ulivyo ufikirio wa fadhili wa Ebed-meleki kwa ajili ya nabii huyo aliyenyanyaswa.—36:8-19, 32; 35:1-19; 38:7-13; 39:15-18.
37. Mfikirio wa Yeremia watiaje nguvu imani katika uwezo wa Yehova wa unabii?
37 Neno la Yehova lililomjia Yeremia lilitimizwa kwa usahihi wenye kustaajabisha. Hilo bila shaka latia nguvu imani katika uwezo wa Yehova wa unabii. Chukua, kwa kielelezo, utimizo mbalimbali wa unabii ambao Yeremia mwenyewe aliishi akaona, kama vile kutekwa kwa Sedekia na kuharibiwa kwa Yerusalemu (21:3-10; 39:6-9), kuondolewa kwenye kiti cha enzi na kufa katika utekwa kwa Mfalme Shalumu (Yehoahazi) (Yer. 22:11, 12; 2 Fal. 23:30-34; 2 Nya. 36:1-4), kutekwa kwa Mfalme Konia (Yehoyakini) mpaka Babuloni (Yer. 22:24-27; 2 Fal. 24:15, 16), na kifo cha nabii bandia Hanania chini ya mwaka mmoja (Yer. 28:16, 17). Unabii huo wote, na mwingine mwingi, ulitimizwa kama vile Yehova alivyokuwa ametabiri. Manabii wa baadaye na watumishi wa Yehova pia waliona unabii wa Yeremia kuwa wenye mamlaka na wenye mafaa. Kwa kielelezo, Danieli alitambua kutokana na maandishi ya Yeremia kwamba ukiwa wa Yerusalemu lazima uwe miaka 70, na Ezra alielekeza uangalifu kwenye utimizo wa maneno ya Yeremia mwishoni mwa ile miaka 70.—Dan. 9:2; 2 Nya. 36:20, 21; Ezra 1:1; Yer. 25:11, 12; 29:10.
38. (a) Ni agano gani, lililorejezewa na Yesu pia, linalokaziwa katika unabii wa Yeremia? (b) Ni tumaini gani la ufalme linalotangazwa?
38 Katika pindi ile alipoanzisha sherehe ya Chakula cha Jioni cha Bwana pamoja na wanafunzi wake, Yesu alionyesha utimizo wa unabii wa Yeremia kuhusu lile agano jipya. Kwa hiyo, yeye alirejezea “agano jipya katika damu yangu,” ambalo kwalo dhambi zao zilisamehewa na walikusanywa kuwa taifa la kiroho la Yehova. (Luka 22:20; Yer. 31:31-34) Waliozaliwa kwa roho ambao wameingizwa katika agano jipya ndio ambao Kristo aingiza ndani ya agano kwa ajili ya Ufalme, ili watawale pamoja naye katika mbingu. (Luka 22:29; Ufu. 5:9, 10; 20:6) Mrejezo wafanywa kwa Ufalme huo mara kadhaa katika unabii wa Yeremia. Katikati ya laana zote kali za Yerusalemu lisilo na imani, Yeremia alielekeza kwenye mwale huo wa tumaini: “Tazama siku zinakuja, asema BWANA [Yehova, NW], nitakapomchipushia Daudi Chipukizi la haki; naye atamiliki mfalme, atatenda kwa hekima, naye atafanya hukumu na haki katika nchi.” Ndiyo, mfalme aitwaye “BWANA [Yehova, NW] ni haki yetu.”—Yer. 23:5, 6.
39. Kurejea kwa baki kutoka Babuloni, kama ilivyotabiriwa na Yeremia, kwatoa uhakikisho wa nini?
39 Kwa mara nyingine Yeremia anena juu ya kurudishwa: “Bali watamtumikia BWANA [Yehova, NW], Mungu wao, na Daudi mfalme wao, nitakayemwinua kwa ajili yao.” (30:9) Hatimaye, aeleza juu ya neno jema ambalo Yehova amenena kuhusiana na Israeli na Yuda, kwamba “katika siku zile, na wakati ule, [mimi Yehova] nitamchipushia Daudi Chipukizi la haki,” ili kuzidisha mbegu yake na ili kwamba kuwe “mwana wa kumiliki katika kiti chake cha enzi.” (33:15, 21) Kama vile baki lililorejea kutoka Babuloni, ndivyo hakika Ufalme huo wa “Chipukizi” utakavyotekeleza haki na uadilifu katika dunia yote.—Luka 1:32.
[Maelezo ya Chini]
a Insight on the Scriptures, Buku 2, kurasa 326, 480.