Sura 5
Kuzaliwa kwa Yesu—Wapi na Wakati Gani?
MTAWALA wa Milki ya Roma, Kaisaria Augusto, ametunga sheria kwamba kila mtu apaswa kurudi kwenye mji wa kuzaliwa kwake akaandikishwe. Kwa hiyo Yusufu asafiri kwenda mahali alipozaliwa, mji wa Bethlehemu.
Watu wengi wameenda Bethlehemu wakajiandikishe, na mahali peke yake ambapo Yusufu na Mariamu wapata nafasi ya kukaa ni kwenye boma la wanyama wa kufugwa. Humo, mahali ambamo punda na wanyama wengine huwekwa, ndimo Yesu azaliwa. Mariamu amfunga kwa vitambaa na kumlaza katika hori, mahali panapowekwa chakula cha wanyama.
Hakika ulikuwa uongozi wa Mungu kwamba Kaisari Augosto akatunga sheria yake ya kuandikisha. Iliwezesha Yesu azaliwe katika Bethlehemu, mji ambao Maandiko yalikuwa yametabiri zamani ungekuwa mahali pa kuzaliwa kwa mtawala aliyeahidiwa.
Huo ni usiku wa maana kama nini! Kule nje kwenye viwanja vya malisho mwangaza mkali wawaka kuzunguka kikundi cha wachungaji. Ni utukufu wa Yehova! Naye malaika wa Yehova awaambia: ‘Msiogope; kwa kuwa mimi nawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori.’ Ghafula malaika wengine wengi wakatokea na kuimba: “Atukuzwe Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.”
Malaika wanapoondoka, wachungaji waambiana: ‘Na tufunge safari ndefu mpaka Bethlehemu tukaone jambo hili ambalo Yehova ametujulisha.’ Wakafunga safari haraka na kumkuta Yesu mahali pale pale ambapo malaika alisema wangemkuta. Wachungaji hao wanaposimulia mambo ambayo malaika aliwaambia, wote wanaosikia wastaajabu. Mariamu ayatunza maneno hayo yote na kuyaweka moyoni mwake.
Watu wengi leo huamini kwamba Yesu alizaliwa Desemba 25. Lakini Desemba ni wakati wa majira yenye mvua na baridi katika Bethlehemu. Wachungaji hawangekuwa usiku kucha nje kwenye mashamba ya malisho wakiwa na mifugo yao wakati huo wa mwaka. Pia, haielekei kwamba Kaisari Mroma angeamuru watu ambao tayari walikuwa na maelekeo ya kumwasi wafunge safari hiyo wakajiandikishe wakati wa baridi kali. Kwa wazi Yesu alizaliwa wakati fulani mwanzoni mwa vuli ya mwaka. Luka 2:1-20; Mika 5:2.
▪ Kwa nini Yusufu na Mariamu wasafiri kwenda Bethlehemu?
▪ Ni mambo gani ya ajabu yatokea usiku ambao Yesu azaliwa?
▪ Tunajuaje kwamba Yesu hakuzaliwa katika Desemba 25?