Sura 107
Kielezi cha Karamu ya Ndoa
KWA njia ya vielezi viwili, Yesu amefichua waandishi na wakuu wa makuhani, nao wataka kumuua. Lakini Yesu angali hajamaliza mambo nao. Yeye aendelea kuwaambia kielezi kingine zaidi, akisema:
“Ufalme wa mbingu umekuwa kama mtu, mfalme, aliyefanya karamu ya ndoa kwa ajili ya mwana wake. Naye akatuma watumwa wake wakaite wale walioalikwa kwenye karamu ya ndoa, lakini wao hawakuwa na nia ya kuja.”
Yehova Mungu ndiye Mfalme ambaye atayarisha karamu ya ndoa kwa ajili ya Mwana wake, Yesu Kristo. Hatimaye, bibi-arusi wa wafuasi wapakwa-mafuta 144,000 wataungana na Yesu mbinguni. Raia za Mfalme ni watu wa Israeli, ambao, walipoingizwa ndani ya agano la Sheria katika 1513 K.W.K., walipokea fursa ya kuwa “ufalme wa makuhani.” Hivyo, katika pindi hiyo, hapo mwanzoni walitolewa mwaliko wa karamu ya ndoa.
Hata hivyo, wito wa kwanza kwa wale walioalikwa haukupelekwa mpaka vuli ya 29 W.K., wakati Yesu na wanafunzi wake (watumwa wa mfalme) walipoanza kazi yao ya kuhubiri Ufalme. Lakini Waisraeli wa asili waliopokea wito huu uliotolewa na watumwa hao kuanzia 29 W.K. hadi 33 W.K. hawakuwa na nia ya kuja. Kwa hiyo Mungu alilipa fursa nyingine taifa hilo la waalikwa, kama vile Yesu asimuliavyo:
“Tena akatuma watumwa wengine, akisema, ‘Ambieni wale walioalikwa: “Tazameni! Mimi nimetayarisha mlo wangu mkuu, ng’ombe ndume wangu na wanyama waliononeshwa wamechinjwa, na mambo yote yako tayari. Njoni kwenye karamu ya ndoa.”’” Wito huu wa pili na wa mwisho kwa wale walioalikwa ulianza katika Pentekoste 33 W.K., wakati roho takatifu ilipomiminwa juu ya wafuasi wa Yesu. Wito huu uliendelea mpaka 36 W.K.
Hata hivyo, walio wengi wa Waisraeli walikataa wito huo pia kwa madharau. “Bila kujali wakaenda zao,” Yesu asema, “mmoja kwenye shamba lake mwenyewe, mwingine kwenye shughuli yake ya kibiashara; lakini wale wengine, wakiwashika watumwa wake, waliwatenda kwa ufidhuli na kuwaua.” “Lakini,” Yesu aendelea, “mfalme akawa na hasira kuu, naye akapeleka majeshi yake na kuharibu wauaji hao na kuchoma jiji lao.” Hilo lilitukia katika 70 W.K., Yerusalemu ulipoteketezwa na kuharibiwa kabisa na Waroma, na wauaji hao wakauawa.
Halafu Yesu aeleza ilivyotukia wakati uo huo: “Ndipo [mfalme] akasema kwa watumwa wake, ‘Karamu ya ndoa iko tayari kweli kweli, lakini wale walioalikwa hawakustahiki. Kwa hiyo endeni kwenye barabara zinazoongoza nje ya jiji, na mtu yeyote mmpataye mwalikeni kwenye karamu ya ndoa.’” Watumwa wakafanya hivyo, na “chumba cha sherehe za arusi kikajaa wale wenye kuegemea kwenye meza.”
Kazi hii ya kukusanya wageni kutoka kwenye barabara zilizo nje ya jiji la walioalikwa ilianza katika 36 W.K. Ofisa wa kijeshi Mroma Kornelio na jamaa yake walikuwa ndio wa kwanza kukusanywa wakiwa watu wasiotahiriwa wasio Wayahudi. Mkusanyo wa hawa wasio Wayahudi, wote wakiwa ni wenye kuchukua nafasi za wale ambao hapo mwanzoni waliukataa wito, umeendelea ukaingia katika karne ya 20.
Ni katika karne ya 20 kwamba chumba cha sherehe ya arusi kimepata kujazwa. Yesu asimulia jambo linalotukia wakati huo, akisema: “Mfalme alipokuja ndani ili akague wageni alitupa jicho akaona mtu mmoja asiyevikwa vazi la ndoa. Kwa hiyo yeye akasema kwake, ‘Jamaa, wewe uliingiaje humu bila kuwa na vazi la ndoa?’ Akaduwaa. Ndipo mfalme akasema kwa watumishi wake, ‘Mfungeni mkono na mguu mmtupe nje ndani ya giza lililo nje. Huko ndiko kutakakokuwa kulia kwake machozi na kusaga meno kwake.’”
Mtu huyo asiye na vazi la ndoa afananisha Wakristo wa mwigizo tu wa Jumuiya ya Wakristo. Mungu hajapata kamwe kuwatambua hao kuwa wenye kitambulisho kifaacho cha kuwa Waisraeli wa kiroho. Mungu hakuwapaka mafuta kamwe kwa roho takatifu wawe warithi wa Ufalme. Kwa hiyo wao watupwa nje ndani ya giza ambamo watapatwa na uharibifu.
Yesu amalizia kielezi chake kwa kusema: “Kwa maana kuna wengi walioalikwa, lakini wachache waliochaguliwa.” Ndiyo, kuna wengi walioalikwa kutoka taifa la Israeli wawe washirika wa bibi-arusi wa Kristo, lakini ni Waisraeli wachache tu wa asili waliochaguliwa. Walio wengi wa wale wageni 144,000 ambao hupokea thawabu ya kimbingu huthibitika kuwa ni watu wasio Waisraeli. Mathayo 22:1-14; Kutoka 19:1-6; Ufunuo 14:1-3, NW.
▪ Wale walioalikwa kwenye karamu ya arusi hapo mwanzoni ni nani, nao walitolewa mwaliko huo wakati gani?
▪ Wito wapelekwa lini mara ya kwanza kwa wale walioalikwa, na ni nani watumwa wenye kutumiwa kuutoa?
▪ Wito wa pili watolewa lini, na ni nani ambao waalikwa baadaye?
▪ Ni nani wanaofananishwa na yule mtu asiye na vazi la arusi?
▪ Ni nani wale wengi walioitwa, na wale wachache waliochaguliwa?