SURA YA 6
Mtoto Aliyeahidiwa
YESU ATAHIRIWA NA BAADAYE APELEKWA HEKALUNI
Yosefu na Maria wanabaki Bethlehemu badala ya kurudi Nazareti. Wanamtahiri Yesu akiwa na umri wa siku nane kama Sheria ya Mungu kwa Waisraeli inavyoamuru. (Mambo ya Walawi 12:2, 3) Pia kulingana na desturi, mtoto wa kiume hupewa jina siku hiyo. Wanampa mwana wao jina Yesu, kama malaika Gabrieli alivyoelekeza.
Zaidi ya mwezi mmoja unapita, na Yesu ana umri wa siku 40. Wazazi wake watampeleka wapi sasa? Watapanda naye kwenda katika hekalu huko Yerusalemu, ambalo liko kilomita chache kutoka mahali wanapoishi. Sheria inasema siku 40 baada ya mtoto mvulana kuzaliwa, mama yake alipaswa kutoa toleo la utakaso hekaluni.—Mambo ya Walawi 12:4-7.
Maria anafanya hivyo. Anatoa ndege wawili wadogo, wakiwa toleo lake. Jambo hilo linaonyesha hali ya kiuchumi ya Yosefu na Maria. Kulingana na Sheria, walipaswa kutoa kondoo dume mchanga na ndege mmoja. Lakini ikiwa mama hangeweza kupata kondoo, angetoa njiwa-tetere wawili au hua wawili. Hivyo ndivyo anavyofanya Maria.
Wakiwa hekaluni, mwanaume fulani mwenye umri mkubwa anawakaribia Yosefu na Maria. Jina lake ni Simeoni. Mungu amemfunulia kwamba kabla hajafa, atamwona Kristo, au Masihi aliyeahidiwa na Yehova. Siku hiyo Simeoni anaongozwa na roho takatifu kwenda hekaluni, ambako anawakuta Yosefu na Maria na mtoto wao mchanga. Simeoni anambeba mtoto huyo mikononi mwake.
Akiwa amembeba Yesu, Simeoni anamshukuru Mungu, akisema: “Sasa, Bwana Mwenye Enzi Kuu, unaruhusu mtumwa wako aende kwa amani kulingana na tangazo lako, kwa sababu macho yangu yameona njia yako ya kuleta wokovu ambayo umetayarisha machoni pa watu wote, nuru ya kuondoa kitambaa kwa mataifa na utukufu wa watu wako Israeli.”—Luka 2:29-32.
Yosefu na Maria wanashangaa kusikia hivyo. Simeoni anawabariki na kumwambia Maria kwamba mwana wake “amewekwa rasmi kwa ajili ya kuanguka na kuinuka tena kwa wengi katika Israeli” na kwamba huzuni itamchoma Maria kama upanga mkali.—Luka 2:34.
Pia, siku hiyo kuna mtu mwingine. Ni Ana, nabii wa kike mwenye umri wa miaka 84. Kwa kweli, yeye hakosi kamwe kwenda hekaluni. Saa hiyohiyo, anawajia Yosefu, Maria, na mtoto Yesu. Anaanza kumshukuru Mungu na kuzungumza kumhusu Yesu kwa wote watakaosikiliza.
Unaweza kuwazia jinsi Yosefu na Maria wanavyoshangilia matukio hayo hekaluni! Kwa hakika, mambo hayo yote yanawathibitishia kwamba mwana wao ni Yule Aliyeahidiwa na Mungu.