SURA YA 7
Wanajimu Wamtembelea Yesu
WANAJIMU WAFUATA “NYOTA” KWENDA YERUSALEMU NA KISHA KWA YESU
Watu fulani wanakuja kutoka Mashariki. Ni wanajimu—watu wanaochunguza nyota, wakidai kwamba wakifanya hivyo wanaweza kujua maana ya matukio yanayohusu maisha ya watu. (Isaya 47:13) Wakiwa nyumbani kwao huko Mashariki, waliona “nyota” na kuifuata mamia ya kilomita hadi Yerusalemu, badala ya kwenda Bethlehemu.
Wanajimu hao wanapofika huko, wanauliza: “Yuko wapi yule aliyezaliwa awe mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake tulipokuwa Mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.”—Mathayo 2:1, 2.
Mfalme Herode wa Yerusalemu anasikia jambo hilo, naye anakasirika sana. Basi anawaita wakuu wa makuhani na viongozi wengine wa dini ya Wayahudi na kuwauliza mahali ambapo Kristo anapaswa kuzaliwa. Kulingana na Maandiko, wanajibu: “Katika Bethlehemu.” (Mathayo 2:5; Mika 5:2) Kwa hiyo, Herode anawaita kwa siri wale wanajimu, naye anawaambia: “Nendeni mkamtafute kwa uangalifu huyo mtoto, na baada ya kumpata mniletee habari, ili mimi pia niende kumsujudia.” (Mathayo 2:8) Hata hivyo, kwa kweli Herode anataka kumpata mtoto huyo mchanga ili amuue!
Baada ya wanajimu kuondoka, jambo la kushangaza linatokea. “Nyota” waliyoona walipokuwa Mashariki inawatangulia. Ni wazi kwamba hii sio nyota ya kawaida, bali ilikuwa imeandaliwa ili kuwaongoza. Wanajimu hao wanaifuata hadi inaposimama juu ya nyumba ambayo Yosefu na Maria wanaishi pamoja na mvulana wao.
Wanajimu hao wanapoingia ndani ya nyumba, wanamkuta Maria akiwa na mtoto mdogo—Yesu. Basi, wanajimu hao wanampigia magoti. Nao wanampa zawadi za dhahabu, ubani, na manemane. Baadaye, wanapotaka kurudi kwa Herode, wanaonywa na Mungu katika ndoto kwamba wasifanye hivyo. Kwa hiyo wanarudi nchini kwao kupitia njia nyingine.
Unafikiri ni nani aliyefanya “nyota” hiyo iwaongoze wanajimu? Kumbuka, haikuwaongoza moja kwa moja hadi kwa Yesu huko Bethlehemu. Badala yake iliwaongoza hadi Yerusalemu, ambako walikutana na Mfalme Herode aliyetaka kumuua Yesu. Na angefanya hivyo ikiwa Mungu hangeingilia kati kuwaonya wanajimu hao wasimwonyeshe Herode mahali ambapo Yesu alikuwa. Ni wazi kwamba adui wa Mungu, Shetani, ndiye aliyetaka Yesu auawe, na alitumia njia hiyo kujaribu kutimiza kusudi lake.