Mathayo Sura ya 5-7
5 Alipouona umati, akapanda mlimani; na baada ya kuketi wanafunzi wake wakamjia. 2 Kisha akafungua kinywa chake akaanza kuwafundisha, akisema:
3 “Wenye furaha ni wale wanaotambua uhitaji wao wa kiroho, kwa kuwa Ufalme wa mbinguni ni wao.
4 “Wenye furaha ni wale wanaoomboleza, kwa kuwa watafarijiwa.
5 “Wenye furaha ni wale walio wapole, kwa kuwa watairithi dunia.
6 “Wenye furaha ni wale walio na njaa na kiu ya uadilifu, kwa kuwa watashibishwa.a
7 “Wenye furaha ni wale wenye rehema, kwa kuwa wataonyeshwa rehema.
8 “Wenye furaha ni wale walio safi moyoni, kwa kuwa watamwona Mungu.
9 “Wenye furaha ni wale wanaofanya amani, kwa kuwa wataitwa wana wa Mungu.
10 “Wenye furaha ni wale ambao wameteswa kwa ajili ya uadilifu, kwa kuwa Ufalme wa mbinguni ni wao.
11 “Wenye furaha ni ninyi, watu wanapowashutumu na kuwatesa na kuwasingizia kila aina ya uovu kwa sababu yangu. 12 Furahini na kushangilia sana, kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa maana hivyo ndivyo walivyowatesa manabii waliokuwapo kabla yenu.
13 “Ninyi ndio chumvi ya dunia, lakini chumvi ikipoteza nguvu yake, ladha yake itarudishwaje? Haifai tena, inapaswa kutupwa nje na kukanyagwa-kanyagwa na watu.
14 “Ninyi ndio nuru ya ulimwengu. Jiji lililo mlimani haliwezi kufichwa. 15 Watu hawawashi taa na kuiweka chini ya kikapu bali huiweka kwenye kinara cha taa ili iwaangazie wote walio ndani ya nyumba. 16 Vivyo hivyo, acheni nuru yenu iangaze mbele ya watu, ili waone matendo yenu mema na kumtukuza Baba yenu aliye mbinguni.
17 “Msifikiri nilikuja kuharibu Sheria au Manabii. Sikuja kuharibu, bali kutimiza. 18 Kwa kweli ninawaambia ni rahisi zaidi kwa mbingu na dunia kupitilia mbali, kuliko herufi moja iliyo ndogo zaidi au sehemu yoyote ya herufi kuondolewa katika Sheria mpaka mambo yote yatimie. 19 Kwa hiyo, yeyote anayevunja mojawapo ya amri hizi ndogo na kufundisha wengine kufanya hivyo, ataitwa mdogo kuhusiana na Ufalme wa mbinguni. Lakini yeyote anayeshika na kufundisha amri hizi ataitwa mkubwa kuhusiana na Ufalme wa mbinguni. 20 Kwa maana ninawaambia ikiwa uadilifu wenu hauzidi ule wa waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika Ufalme wa mbinguni.
21 “Mlisikia kwamba zamani watu waliambiwa: ‘Usiue, lakini yeyote anayeua atawajibika mahakamani.’ 22 Hata hivyo, ninawaambia kila mtu anayeendelea kumkasirikia ndugu yake atawajibika mahakamani; na yeyote anayemtukana ndugu yake kwa neno la dharau atawajibika katika Mahakama Kuu; na yeyote anayesema, ‘Wewe mpumbavu usiyefaa kitu!’ atastahili moto wa Gehena.b
23 “Basi, ikiwa unaleta zawadi yako kwenye madhabahu na hapo unakumbuka kwamba ndugu yako ana jambo fulani dhidi yako, 24 iache zawadi yako hapo mbele ya madhabahu, uende zako. Kwanza fanya amani na ndugu yako, kisha urudi na kutoa zawadi yako.
25 “Suluhisha mambo upesi na mtu anayekushtaki, ukiwa naye njiani kwenda mahakamani, ili asikupeleke kwa hakimu, naye hakimu kwa mtumishi wa mahakama, nawe utupwe gerezani. 26 Hakika ninakuambia hutatoka humo mpaka utakapolipa sarafu yako ndogo ya mwisho.
27 “Mlisikia kwamba ilisemwa: ‘Usifanye uzinzi.’ 28 Lakini ninawaambia kila mtu anayeendelea kumtazama mwanamke na kumtamani tayari amefanya uzinzi naye moyoni mwake. 29 Basi, ikiwa jicho lako la kulia linafanya ujikwae, ling’oe na kulitupilia mbali. Kwa maana ni afadhali upoteze kiungo kimoja kuliko mwili wako wote utupwe katika Gehena.c 30 Pia, ikiwa mkono wako wa kulia unakufanya ujikwae, ukate na kuutupilia mbali. Kwa maana ni afadhali upoteze kiungo kimoja kuliko mwili wako wote utupwe katika Gehena.d
31 “Zaidi ya hayo, ilisemwa: ‘Yeyote anayemtaliki mke wake, anapaswa kumpa cheti cha talaka.’ 32 Hata hivyo, ninawaambia kila mtu anayemtaliki mke wake kwa sababu nyingine isipokuwa uasherati,e anamweka katika kishawishi cha kufanya uzinzi, na yeyote anayemwoa mwanamke aliyetalikiwa anafanya uzinzi.
33 “Tena mlisikia kwamba zamani watu waliambiwa: ‘Usikose kutimiza kiapo chako, unapaswa kutimiza nadhiri zako kwa Yehova.’ 34 Hata hivyo, ninawaambia: Msiape kamwe kwa mbingu kwa sababu ni kiti cha ufalme cha Mungu; 35 wala kwa dunia kwa sababu ni mahali pake pa kuwekea miguu; wala kwa Yerusalemu kwa sababu ni jiji la Mfalme mkuu. 36 Usiape kwa kichwa chako kwa sababu huwezi kugeuza unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. 37 Acheni ‘Ndiyo’ yenu imaanishe ndiyo, na ‘Siyo’ yenu, siyo, kwa maana linalozidi hayo linatoka kwa yule mwovu.
38 “Mlisikia kwamba ilisemwa: ‘Jicho kwa jicho na jino kwa jino.’ 39 Hata hivyo, ninawaambia: Msimzuie mtu mwovu, bali yeyote anayekupiga kofi kwenye shavu la kulia, mgeuzie pia shavu la kushoto. 40 Na ikiwa mtu anataka kukupeleka mahakamani ili alichukue vazi lako la ndani, mwachie pia vazi lako la nje; 41 na mtu mwenye mamlaka akikulazimisha uingie katika utumishi wa kilomita moja, nenda naye kilomita mbili. 42 Mpe yule anayekuomba, wala usimpe kisogo yule anayetaka umkopeshe.f
43 “Mlisikia kwamba ilisemwa: ‘Lazima umpende jirani yako na kumchukia adui yako.’ 44 Hata hivyo, ninawaambia: Endeleeni kuwapenda adui zenu na kusali kwa ajili ya wale wanaowatesa ninyi, 45 ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni, kwa kuwa yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, na hunyesha mvua juu ya waadilifu na wasio waadilifu. 46 Kwa maana mkiwapenda wale wanaowapenda, mnapata thawabu gani? Je, wakusanya kodi hawafanyi vivyo hivyo? 47 Na mkiwasalimu ndugu zenu tu, mnafanya jambo gani lisilo la kawaida? Je, watu wa mataifa hawafanyi vivyo hivyo? 48 Basi lazima muwe wakamilifug kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.
6 “Iweni waangalifu msionyeshe uadilifu wenu mbele ya watu ili wawaone; la sivyo hamtapata thawabu kutoka kwa Baba yenu aliye mbinguni. 2 Basi unapotoa zawadi za rehema,h usipige tarumbeta mbele yako kama wanavyofanya wanafiki katika masinagogi na barabarani, ili wasifiwe na watu. Kwa kweli ninawaambia, wanapata thawabu yao kikamili. 3 Lakini wewe, unapotoa zawadi za rehema, usiache mkono wako wa kushoto ujue kile ambacho mkono wako wa kulia unafanya, 4 ili utoe zawadi za rehema kwa siri. Naye Baba yako anayetazama akiwa mahali pa siri atakulipa.
5 “Pia, mnaposali msifanye kama wanafiki, kwa maana wanapenda kusali wakiwa wamesimama katika masinagogi na kwenye kona za barabara kuu ili watu wawaone. Kwa kweli ninawaambia, wanapata thawabu yao kikamili. 6 Lakini unaposali, ingia ndani ya chumba chako faraghani, baada ya kufunga mlango wako, sali kwa Baba yako aliye mahali pa siri. Naye Baba yako anayetazama akiwa mahali pa siri atakulipa. 7 Mnaposali msiseme mambo yaleyale tena na tena, kama vile watu wa mataifa wanavyofanya, kwa maana wao hufikiri watasikiwa kwa kutumia maneno mengi. 8 Kwa hiyo, msiwe kama wao, kwa sababu Baba yenu anajua kile mnachohitaji hata kabla hamjamwomba.
9 “Basi, salini hivi:
“‘Baba yetu uliye mbinguni, jina lako na litakaswe.i 10 Ufalme wako na uje. Mapenzi yako na yatendeke duniani kama ilivyo mbinguni. 11 Utupatie leo mkate wetu kwa ajili ya siku hii; 12 na utusamehe madeni yetu, kama vile tunavyowasamehe wadeni wetu. 13 Na usituingize katika majaribu, bali utukomboej kutoka kwa yule mwovu.’
14 “Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi pia; 15 lakini msipowasamehe watu makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe makosa yenu.
16 “Mnapofunga, msiwe na nyuso zenye huzuni kama wanafiki, kwa maana wao hukunja nyuso zaok ili watu waone kwamba wanafunga. Kwa kweli ninawaambia, wanapata thawabu yao kikamili. 17 Lakini wewe unapofunga, paka kichwa chako mafuta na unawe uso, 18 ili usionekane kwamba unafunga kwa wanadamu bali kwa Baba yako aliye mahali pa siri. Naye Baba yako anayeona akiwa mahali pa siri atakulipa.
19 “Acheni kujiwekea hazina duniani, ambako nondo na kutu hula na ambako wezi huvunja na kuiba. 20 Badala yake, jiwekeeni hazina mbinguni, ambako hazitaliwa na nondo wala kutu, na ambako wezi hawatavunja na kuiba. 21 Kwa maana mahali ilipo hazina yako, ndipo moyo wako utakapokuwa pia.
22 “Taa ya mwili ni jicho. Basi, ikiwa jicho lako linakazia jambo hususa, mwili wako wote utakuwa mwangavu.l 23 Lakini ikiwa jicho lako lina wivu,a mwili wako wote utakuwa na giza. Ikiwa nuru iliyo ndani yako kwa kweli ni giza, basi giza hilo ni kubwa sana!
24 “Hakuna anayeweza kuwatumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia mmoja na kumpenda mwingine, au atashikamana na mmoja na kumdharau mwingine. Hamwezi kutumikia Mungu na Utajiri.
25 “Kwa hiyo ninawaambia: Acheni kuhangaikia uhai wenu kuhusu kile mtakachokula au kunywa, au juu ya miili yenu kuhusu kile mtakachovaa. Je, uhai si zaidi ya chakula na mwili zaidi ya mavazi? 26 Waangalieni kwa makini ndege wa angani; hawapandi mbegu, hawavuni, wala kukusanya ghalani, na bado Baba yenu wa mbinguni huwalisha. Je, ninyi si wenye thamani kuliko wao? 27 Ni nani kati yenu ambaye kwa kuhangaika anaweza kurefusha uhai wake kwa mkono mmoja? 28 Pia, kwa nini mnahangaika kuhusu mavazi? Jifunzeni kutoka kwa mayungiyungi ya shambani, jinsi yanavyokua; hayafanyi kazi, wala hayasokoti; 29 lakini ninawaambia hata Sulemani katika utukufu wake wote hakupambwa kama maua hayo. 30 Basi, ikiwa Mungu huivika hivyo mimea ya shambani, ambayo ipo hapa leo na kesho hutupwa ndani ya jiko, je, hatawavika vizuri zaidi ninyi wenye imani ndogo? 31 Kwa hiyo msihangaike kamwe na kusema, ‘Tutakula nini?’ au, ‘Tutakunywa nini?’ au, ‘Tutavaa nini?’ 32 Kwa maana mataifa yanatafuta vitu hivi vyote kwa bidii. Baba yenu wa mbinguni anajua kwamba mnahitaji vitu hivi vyote.
33 “Basi, endeleeni kuutafuta kwanza Ufalme na uadilifu wake, nanyi mtaongezewa hivi vitu vingine vyote. 34 Basi, msihangaike kamwe kuhusu kesho, kwa maana kesho itakuwa na mahangaiko yake yenyewe. Kila siku ina matatizo yake ya kutosha.
7 “Acheni kuhukumu ili msihukumiwe; 2 kwa maana kwa hukumu mnayohukumu, mtahukumiwa, na kwa kipimo mnachowapimia watu, ndicho watakachowapimia. 3 Basi, kwa nini unautazama unyasi ulio katika jicho la ndugu yako lakini huoni boriti lililo katika jicho lako mwenyewe? 4 Au unawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Niruhusu niutoe unyasi ulio katika jicho lako,’ na huku tazama! una boriti katika jicho lako? 5 Mnafiki! Kwanza toa boriti katika jicho lako, kisha utaona vizuri jinsi ya kuutoa unyasi katika jicho la ndugu yako.
6 “Msiwape mbwa kitu kitakatifu, wala msiwatupie nguruwe lulu zenu, wasije wakazikanyaga-kanyaga chini ya miguu yao, kisha wageuke na kuwararua ninyi.
7 “Endeleeni kuomba, nanyi mtapewa; endeleeni kutafuta, nanyi mtapata; endeleeni kupiga hodi, nanyi mtafunguliwa; 8 kwa maana kila mtu anayeomba hupokea, na kila mtu anayetafuta hupata, na kila mtu anayepiga hodi, atafunguliwa. 9 Kwa kweli, ni nani miongoni mwenu ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? 10 Au akimwomba samaki, je, atampa nyoka? 11 Kwa hiyo, ingawa ninyi ni waovu, mnajua jinsi ya kuwapa watoto wenu zawadi nzuri, je, Baba yenu aliye mbinguni hatawapa hata zaidi vitu vyema wale wanaomwomba?
12 “Basi, mambo yote mnayotaka watu wawatendee ninyi, lazima ninyi pia mwatendee vivyo hivyo. Kwa kweli, hiyo ndiyo maana ya Sheria na Manabii.
13 “Ingieni kupitia lango jembamba, kwa sababu lango ni pana, na barabara inayoongoza kwenye uharibifu ina nafasi kubwa, na ni wengi wanaoipitia; 14 lakini lango ni jembamba na barabara inayoongoza kwenye uzima ina nafasi ndogo, na ni wachache wanaoipata.
15 “Jihadharini na manabii wa uwongo ambao huja kwenu katika mavazi ya kondoo, lakini ndani wao ni mbwamwitu wakali. 16 Kwa matunda yao mtawatambua. Je, watu huchuma zabibu kwenye miiba au tini kwenye michongoma? 17 Vivyo hivyo, kila mti mzuri huzaa matunda mazuri, lakini kila mti uliooza huzaa matunda mabaya. 18 Mti mzuri hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti uliooza hauwezi kuzaa matunda mazuri. 19 Kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa ndani ya moto. 20 Kwa kweli, mtawatambua watu hao kwa matunda yao.
21 “Si kila mtu anayeniambia, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika Ufalme wa mbinguni, bali yule anayefanya mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni ndiye atakayeingia. 22 Wengi wataniambia siku hiyo: ‘Bwana, Bwana, je, hatukutoa unabii katika jina lako, na kufukuza roho waovu katika jina lako, na kufanya matendo mengi yenye nguvu katika jina lako?’ 23 Ndipo nitakapowaambia: ‘Sikuwajua ninyi kamwe! Ondokeni kwangu, ninyi mnaotenda uasi sheria!’
24 “Kwa hiyo, kila mtu anayesikia haya maneno yangu na kuyatenda ni kama mtu mwenye busara aliyejenga nyumba yake kwenye mwamba. 25 Kisha mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, upepo ukavuma na kuipiga nyumba hiyo, lakini haikuporomoka, kwa maana msingi wake ulikuwa umejengwa kwenye mwamba. 26 Zaidi ya hayo, kila mtu anayesikia haya maneno yangu lakini hayatendi ni kama mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba juu ya mchanga. 27 Kisha mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, upepo ukavuma na kuipiga nyumba hiyo, nayo ikaporomoka na kuharibika kabisa.”
28 Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, umati ukashangazwa na njia yake ya kufundisha, 29 kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye mamlaka, na si kama waandishi wao.
a Au “watatoshelezwa.”
b Mahali pa kuteketezea takataka nje ya Yerusalemu. Neno la Kigiriki linalorejelea Bonde la Hinomu, lililokuwa upande wa kusini magharibi wa jiji la kale la Yerusalemu. Hakuna uthibitisho kwamba wanyama au wanadamu walitupwa katika Gehena ili wateswe au kuchomwa moto wakiwa hai. Kwa hiyo mahali hapo hapangeweza kufananisha mahali pasipoonekana ambapo nafsi za wanadamu zinateswa milele katika moto halisi. Badala yake, Yesu na wanafunzi wake walitumia neno “Gehena” kufananisha adhabu ya milele ya “kifo cha pili,” yaani, maangamizi ya milele, uharibifu.
e Neno la Kigiriki por·neiʹa, linalotumiwa katika Maandiko kurejelea baadhi ya matendo ya ngono yanayokatazwa na Mungu. Yanatia ndani uzinzi, ukahaba, ngono kati ya watu ambao hawajafunga ndoa, ngono kati ya watu wa jinsia moja, na kufanya ngono na wanyama.
f Yaani, umkopeshe bila faida au riba.
g Au, “kamili.”
h Au “unapowapa maskini zawadi.”
i Au “litukuzwe; lionwe kuwa takatifu.”
j Au “utuokoe.”
k Au “hawatunzi sura au mwonekano wao.”
l Au “utajawa na nuru.”
a Tnn., “ni bovu; lina uovu.”