Tiro—Ulikuwa Mji Wenye Hila
NI MIJI michache ya ulimwengu wa kale iliyokuwa na hila kama Tiro. Miji ya jirani za Israeli haikudai kuwa rafiki za waabudu wa Yehova Mungu. Lakini, kwa muda fulani Tiro ilikuwa tofauti sana.
Kwa mfano, Hiramu mfalme wa Tiro alikuwa rafiki ya wafalme Wayudea, Daudi na Sulemani. Alisaidia Sulemani kwa kumpa vifaa na watu wa kumjengea Yehova hekalu lenye fahari katika Yerusalemu. (1 Fal. 5:2-6; 2 Nya. 2:3-10) Baadaye, Hiramu na Sulemani walikuwa na shughuli ya kupelekeana vitu kwa merikebu. Sulemani alikuwa amejenga merikebu nyingi katika Ezion-geberi, Ghuba la Akaba. Merikebu hizo zilisimamiwa na mwungano wa watumishi wa Sulemani na mabaharia hodari waliotumwa na Hiramu.—1 Fal. 9:26-28.
Lakini Tiro haikuendelea kuwa rafiki ya watu wa Mungu wa agano, Israeli. Tiro ilitumia hila na mwishowe ikajiunga na adui za Israeli. Mtunga zaburi aliyeongozwa na Mungu alisema: “Juu ya watu [wa Mungu] wanapanga mipango ya ujanja; wanatunga hila juu ya wale ambao unawalinda. Wanasema, ‘Njoni, twendeni tukaliharibu taifa lao; jina la Israeli na lisikumbukwe tena!’ Naam, wanafanya shauri kwa akili moja, nao wamejiunga wakushambulie wewe: Hema za Edomu na Waishmaeli, Moabu na watu wa Hagari, Gebali na Amoni na Amaleki, Filistia pamoja na wakaaji wa Tiro.”—Zab. 83:4-8, New American Bible (Kiingereza).
Tiro ilifanya hila kiasi cha kuuza watumwa Waisraeli kwa Wagiriki na Waedomu katika masoko yake. Kwa kuwa hakuna Maandiko yanayoonyesha kwamba Tiro na Israeli zilipigana, pengine watumwa waliouzwa walikuwa wamechukuliwa mateka na mataifa mengine halafu wakaingia mikononi mwa wafanya biashara Watiro. Au, pengine Waisraeli watoro waliokimbilia Tiro walifanywa watumwa na Watiro.
Kwa sababu ya hila ya Tiro, Yehova alitumia manabii wake kuutangazia mji huo na wakaaji wake msiba. Tunasoma hivi: “Nitawarudishia malipo yenu juu ya vichwa vyenu wenyewe. Kwa kuwa . . . watoto wa Yuda na watoto wa Yerusalemu mmewauzia Wayunani.” (Yoeli 3:4-6) “Haya ndiyo asemayo [Yehova]; Kwa makosa matatu ya Tiro, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wameitia kabila nzima katika mikono ya Edomu, wala hawakulikumbuka agano la udugu; lakini nitapeleka moto juu ya ukuta wa Tiro, nao utayateketeza majumba yake.” (Amosi 1:9, 10) Maneno hayo ya unabii yalitimizwa kidogo kidogo karne zilipoendelea kupita.
MAZINGIWA YA NEBUKADREZA
Mfalme Nebukadreza wa Babeli alianza kuzingira Tiro muda fulani baada ya Yerusalemu na hekalu lake tukufu kuharibiwa. Kulingana na mwanahistoria Myahudi Yosefo wa karne ya kwanza, mazingiwa yaliendelea muda wa miaka kumi na mitatu. Wakati wa mazingiwa hayo yenye kuchosha, vichwa vya askari vikawa na “upara” kwa sababu ya kusuguliwa na chapeo zao, na mabega yao ‘yakaambuliwa ngozi’ kwa sababu ya kuchukua vifaa vya ujenzi wa mazingiwa. Lakini, ingawa walijitahidi hivyo, Ezekieli 29:18 inasema hivi: “[Nebukadreza] alikuwa hana mshahara uliotoka Tiro, wala yeye wala jeshi lake, kwa huduma ile aliyohudumu juu yake.”
Historia ya kilimwengu haionyeshi matokeo ya mazingiwa yaliyofanywa na Wababeli. Lakini, kulingana na maelezo ya unabii yaliyo katika kitabu cha Ezekieli, tunajifunza kwamba Watiro wengi waliuawa na kunyang’anywa mali zao. (Eze. 26:7-12) Basi, ni wazi kwamba Wababeli hawakupata “mshahara” wa jitihada zao kwa sababu hawakupata walichotazamia kupata. Vitu walivyoteka havikuwa vingi kama walivyotazamia. Labda hiyo ni kwa sababu mji wa bara peke yake ndio ulioshambuliwa, lakini ule mwingine wa kisiwani, uliokuwa mwendo mfupi kutoka pwani, ukaokoka.
Inaonekana kwamba Tiro ulipona pigo ulilopigwa na Wababeli. Wakati Waisraeli waliporudia Yuda na Yerusalemu baada ya kutoka uhamishoni Babeli, Watiro waliwapa mbao za mierezi kutoka Lebanoni ili kujenga upya hekalu la Yehova katika Yerusalemu. (Ezra 3:7) Miaka mingi baadaye, wakati wa Nehemia, wafanya biashara Watiro waliishi Yerusalemu na kuuza samaki na namna namna za vitu vingine katika mji huo.—Neh. 13:16.
MAZINGIWA YA ALEKSANDA MKUU
Lakini unabii uliotolewa juu ya Tiro haukuwa umeacha kufanya kazi. Bado mji huo ungenyang’anywa utukufu wake wote. Ili kukazia kwamba Tiro ulikuwa haujatimiziwa kabisa unabii uliotolewa, Yehova Mungu alimwongoza nabii wake Zekaria kusema hivi: “[Yehova] atamwondolea [Tiro] mali zake, naye ataupiga uwezo wake alio nao baharini, naye mwenyewe atateketezwa kwa moto.” (Zek. 9:4) Unabii huo na mwingine uliokuwa umetolewa mapema ulitimizwa kwa njia yenye kushangaza mwaka 332 K.W.K.
Wakati huo ndipo Aleksanda Mkuu wa Makedonia aliposhambulia Mashariki ya Kati, akadai kwamba miji ya Foenikia, pamoja na Tiro, imnyenyekee. Ingawa miji ile mingine ilimtii Aleksanda, Tiro ulikataa kumfungulia malango yake. Wakati huo mji huo ulikuwa katika kisiwa kilichokuwa karibu maili moja na nusu (kilomita 0.8) kutoka bara, nao ulikuwa na maboma ya kuulinda. Sehemu ya ukuta iliyoelekea bara ilikuwa na urefu usiopungua futi 150 (mita 46).
Kwa sababu Aleksanda alionyeshwa shingo ngumu na Tiro, alianza kuuzingira mji huo. Kwa kuwa hakuwa na meli za kuufikia mji huo, aliagiza ule mji wa zamani Tiro, uliokuwa bara, ubomolewe halafu mabaki yake yatumiwe kujenga baharini njia ya kuufikia ule mji wa kisiwani. Katika mwisho ule mwingine wa njia hiyo, uliokuwa na upana wa futi karibu 200 (mita 61), alisimamisha mizinga ya vita na minara. Watiro walitumia meli za kutupa makombora wakaiharibu minara hiyo na hata sehemu za njia iliyojengwa. Aleksanda hakuogopa, bali aliagiza minara hiyo ijengwe tena kisha akapanua njia ile. Alipojua kwamba asingefaulu bila kutumia meli, Aleksanda alikusanya meli nyingi sana kutoka Sidoni, Rodesi, Malusi, Soli, Likia, Makedonia na Kipro. Basi Watiro wakawa hawawezi kuingia baharini vyepesi. Sasa kukawa na uhakika kwamba mji utaanguka.
Aleksanda hakutaka kuendesha mazingiwa muda mrefu, kwa hiyo akaagiza vifaa vyenye kuelea majini vitengenezwe, kisha mitambo mikubwa ya kubomoa mji ikawekwa juu. Ndipo askari wake walipoziendea bandari mbili za Tiro wakabomoa maboma yake.
Tiro ulianguka baada ya kuzingirwa miezi saba. Watiro waliendelea kuzuia askari wa Aleksanda hata baada ya mji kutekwa, kwa hiyo Aleksanda akauteketeza Tiro. Watiro 8,000 walichinjwa, wengine 2,000 wakauawa baadaye ili kulipa kisasi, na 30,000 wakauzwa wawe watumwa.
MWISHO WA UTUKUFU WA TIRO
Ingawa Tiro ulifufuka-fufuka mara kadha baada ya hapo, unabii wa Biblia ulitimizwa juu yake. Leo utukufu uliokuwa Tiro hauko. Mahali hapo pana magofu na kibandari kidogo kinachoitwa Souro. Kuhusu mahali hapo, Encyclopcedia Britannica (1971) kinasema kwamba “hapana maana sana; mwaka 1961 palikuwa na wakaaji karibu 16,483.” (Vol. 22, uku. 452) Basi historia ya Tiro mpaka leo hii inahakikisha kwamba unabii huu ulikuwa wa kweli:
“Mimi [Yehova] ni juu yako, Ee Tiro nami nitaleta mataifa mengi kupigana nawe, kama bahari iinuavyo mawimbi yake. Nao wataziharibu kuta za Tiro, na kuibomoa minara yake; tena nitakwangua hata mavumbi yake yamtoke, na kumfanya kuwa jabali tupu. Naye atakuwa mahali pa kutandazia nyavu za wavuvi kati ya bahari.”—Eze. 26:3-5.
Msiba wa Tiro unaonyesha wazi kwamba Yehova Mungu haoni hila kama kijambo kidogo tu. Jambo hilo linapaswa kutukazia ubora wa kuyajua mapenzi ya Mungu na kushikamana sana naye. Kama vile hatakosa kuadhibu watu kwa sababu ya hila, hivyo ndivyo hatakosa kuwapa thawabu watumishi wenye kushikamana naye. Mtume Paulo aliwaandikia waamini wenzake akawaambia, “Mungu si dhalimu hata aisahau kazi yenu, na pendo lile mlilolidhihirisha kwa jina lake.”—Ebr. 6:10.