‘Wafanya Kazi Wema Nyumbani’
PAULO, mtume wa Yesu Kristo, wakati mmoja alisihi wanawake wazee wa Kikristo waweke mfano mwema kwa dada zao vijana wa kiroho. Kati ya mambo mengine, hiyo ingeongoza wanawake vijana wawe ‘wafanya kazi nyumbani.’—Tito 2:3-5.
Usemi ‘wafanya kazi nyumbani’ wamaanisha nini kwako? Akijibu ulizo hilo, mwanamke kijana wa Kikristo alisema: “Naona kuwa ‘wafanya kazi nyumbani’ kwatia mambo mengi ndani. Kwa wazi, kungemaanisha kuweka nyumba yako malidadi na safi. Lakini, pia, kungetia ndani kufanya kazi kuangalia jamaa yako, hata wawe na vyakula vizuri na mavazi yanayofaa. Kwa usemi mwepesi sana, maana yake ni kwamba yeye [‘mfanya kazi nyumbani’] apaswa kufuata maelezo ya mke na mama mwema yaliyo katika Mithali 31:10-31.” Mwanamke mzee wa Kikristo alisema usemi ‘wafanya kazi nyumbani’ ulimkumbusha kisehemu kile kile cha kitabu cha Biblia cha Mithali.
Humo twapata ‘maneno fulani ya mfalme Lemueli,’ na labda ni ya Sulemani. Maelezo hayo juu ya “mke hodari” yalitegemea “wosia ambao mama yake alimpa kumsahihisha.” (Mit. 31:1, NW) Lakini maneno haya hayaonyeshi hekima ya kibinadamu tu, kwa maana yaliongozwa yaandikwe kwa njia ya kimungu. Kwa hiyo, yanayosemwa hapa yanaonyesha maoni ya Mungu na bila shaka yanastahili kufikiriwa kwa uangalifu na wanawake wa Kikristo wanaotaka kuwa ‘wafanya kazi wema nyumbani.’
UBORA WA “MKE HODARI”
Kwanza, Mfalme Lemueli azungumza ubora wa mke mwema. Basi, ubora wa uwekevu wa mke mtunza nyumba ni nini? Karibuni, idara moja ya usimamizi wa usalama wa jamii ya watu iitwayo United States Social Security Administration ilijaribu kuamua hilo kwa kutegemea mishahara ya nchi hiyo ya kazi kama za uyaya na upishi. Kulingana na mambo ya hakika na tarakimu zilizoelezwa kuwa “za kiasi sana,” thamani kuu zaidi ya mke mtunza nyumba hufikiwa kati ya umri wa miaka 25 na 29, na wakati huo ubora wake wa uwekevu wa vitu kila mwaka ulihesabiwa kwamba huwa $6,417 (shilingi 52,362.72 au 3208Z). Bila shaka, wengine wameshangaa yawezekanaje kuamua thamani ya mke mtunza nyumba, kwa maana kuna usemi wa zamani usemao, “Mwanamume aweza kufanya kazi mwaka hata mwaka, lakini kazi ya mwanamke haifanyiki kamwe.”
Hata ikiwa mtu hakubaliani na tarakimu wala usemi huo, hakuna shaka kwamba mke mwema apaswa kuthaminiwa sana. Mfalme Lemueli alisema hivi: “Mke hodari nani awezaye kumpata? Thamani yake yapita sana ile ya marijani. Katika yeye moyo wa mwenyeji wake [mumewe] umetumaini, na hakuna faida inayokosekana. Amemthawabisha kwa mema, wala si kwa mabaya, siku zote za maisha yake.” (Mit. 31:10-12, NW) Naam, “mke hodari” ni mwenye thamani zaidi kuliko vitu vya mapambo vinavyothaminiwa sana ambavyo mafundi hutengeneza kutokana na marijani yenye rangi za kupendeza yatolewayo baharini. Yeye ni mwenye kutumainika, pia, na hufanyia mumewe mema maisha yote wanayoishi pamoja. Lakini kazi zake ni nini?
KAZI ZAKE ZA NYUMBANI
Mfalme Lemueli alieleza habari za “mke hodari” wa Israeli ya kale. Walakini, wanawake wa Kikristo wa leo wanaweza kufaidi kwa kuchunguza hali zao na kuzilinganisha na kazi njema hizo za mke. Ikiwa una Biblia karibu, sababu gani usisome Mithali 31:10-31 sasa hivi? Basi, na turudi nyuma tuchunguze shughuli za “mke hodari.”
Kwanza, tafadhali angalia vile mwanamke huyu anavyopendezwa na mavazi ya jamaa yake. “Hutia mikono yake katika kusokota; na mikono yake huishika pia.” (Mit. 31:19) Kusudi lake ni nini? Mke huyu hodari ajifanyia nyuzi zake mwenyewe za kusokota!
“Hutafuta sufu na kitani,” asema Lemueli, “hufanya kazi yake ya mikono kwa moyo.” (Mst. 13) Kati ya Waebrania mavazi yaliyo mengi yalikuwa yametengenezwa kwa sufu au kitani. Pengine huyu “mke hodari” hununua vitambaa bora zaidi awezavyo kupata kwa bei za chini iwezekanavyo. Halafu anafanya kazi ya kuvitengeneza viwe mavazi mazuri sana ya jamaa yake kwa mikono yenye moyo wa kupenda. Kazi hii yamfurahisha yeye!
Washiriki wa jamaa ya mwanamke huyu wana mavazi maradufu yanayowakinga wakati wa baridi nyingi. Yeye mwenyewe hujipamba mavazi ya bei, ingawa si ya urembo mwingi wala si ya kukosa kiasi. (Linganisha shauri la mtume kwamba wanawake wa Kikristo “wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi.” [1 Tim. 2:9]) Mume wake huvaa mavazi yanayofaa kushirikiana na wanaume wazee, nao hawakosi kuona bidii ya mke wake. Kwa kweli, yeye ametengeneza pia mavazi ya ndani na mishipi anayoweza kuuzia wafanya biashara apate faida.
Lemueli aeleza hivi: “Hawahofii theluji watu wa nyumbani mwake; maana wote wa nyumbani mwake huvikwa nguo nyekundu. Hujifanyia mazulia ya urembo; mavazi yake ni kitani safi na urujuani. Mume wake hujulikana malangoni; aketipo pamoja na wazee wa nchi. Hufanya nguo za kitani na kuziuza; huwapa wafanya biashara mishipi.”—Mist. 21-24.
Mke hodari huwa na bidii iyo hiyo kuipa jamaa chakula kizuri. Kama vile merikebu za wafanya biashara zinavyoleta vifaa kutoka mbali, ndivyo mwanamke huyu anavyotafuta vyakula bora, hata ikiwa lazima akavitoe sehemu za mbali. “Afanana na merikebu za biashara; huleta chakula chake kutoka mbali.”—Mst. 14.
Kawaida ya mwanamke huyu si kulala mpaka jua linapokuwa limewaka sana. Yeye huamka kabla hakujapambazuka, labda aanze kuoka mkate. Nao wanawake vijana walio katika jamaa, hawalalamiki kwa kukosa chakula au mgawo wa kazi. Mke huyu hodari huhakikisha kwamba wana chakula na kazi za kufanya. “Tena huamka, kabla haujaisha usiku; huwapa watu wa nyumbani mwake chakula; na wajakazi [wanawake vijana, NW] wake sehemu zao.”—Mst. 15.
Pande fulani za usimamizi wa nyumba hukabidhiwa kwa mwanamke huyu na mumewe. Yeye hufanya mambo yote haya kwa kibali na uongozi wa mumewe. Kwa mfano, hata ikiwa kipande fulani cha ardhi kinauzwa bei nzuri, mwanamke huyu atakinunua baada ya kufikiri kwa uangalifu tu. Kwa kweli, yeye amekusanya pesa kiasi fulani kumwezesha kununua uwanja, kwa sababu ya bidii na jitihada zake za kufaa. Aweza hata kufanya kazi za nje. Kwa vyo vyote anahakikisha uwanja ulionunuliwa unatumiwa vizuri. Twaambiwa hivi: “Huangalia shamba, akalinunua; kwa mapato ya mikono yake hupanda mizabibu.”—Mst. 16.
Mtazamaji ye yote aweza kuona kwamba mwanamke huyu ni mwenye bidii na hodari. “Hujifunga nguvu viunoni kama mshipi; huitia mikono yake nguvu.” (Mst. 17) Mke mwema huyu haogopi kujitahidi, bali hufanya kazi yake kwa juhudi nyingi. Zaidi ya hilo, “huona kama bidhaa yake ina faida.” Kazi zake ni zenye kufaidi, na aweza kushughulikia sana zile zenye faida nyingi zaidi. Kwa hiyo mwanamke huyu ni mwenye bidii sana hata “taa yake haizimiki usiku.” (Mst. 18) Huenda huu ukawa ni usemi wa mfano wenye kumaanisha kwamba yeye hufanya kazi kwa bidii mpaka inakuwa usiku sana na hata huamka kabla hakujapambazuka aendelee kufanya kazi.
Kwa sababu mwanamke huyu hufanya mambo kwa uhodari na jitihada zake zinathawabisha, anajiona salama naye hana wasiwasi juu ya wakati ujao. Bali, anakuwa na matumaini hakika, anakuwa na akili timamu, na nguvu zinazohitajiwa kuvumilia magumu ya maisha. Kwa kweli, “nguvu na hadhi ndiyo mavazi yake; anaucheka wakati ujao.”—Mst. 25.
Mke hodari hufikiri pia kabla hajasema, naye hasemi maneno yake kwa njia ya kuamuru. Akumbusha mtu juu ya Abigaili, aliyekuwa “mwenye akili njema, mzuri wa uso.” (1 Sam. 25:3) Naam, mke hodari husema kwa upole, awe anasema na watoto, watumishi wake au wengine. Kama mke na mama mwaminifu, anasaidia mume wake kufundisha watoto, na vilevile kuwatia moyo wakubali na kufuata mafundisho mema ya adabu ya baba. Kwa wazi, yeye si mwanamke mwenye kujikalia kitako kwa uvivu. “Hufumbua kinywa chake kwa hekima, na sheria ya wema i katika ulimi wake,” asema Mfalme Lemueli. “Huangalia sana njia za watu wa nyumbani mwake; wala hali chakula cha uvivu.”—Mist. 26, 27.
Mke huyu bora ni mkarimu na mtenda mema kwa watu wasio wa nyumba yake. “Huwakunjulia maskini mikono yake; naam, huwanyoshea wahitaji mikono yake,” akitaka kuwasaidia. (Mst. 20) Mwanamke huyu si mchoyo, bali ni mwenye upendo na ukarimu mwingi.
THAWABU ZA “MKE HODARI”
Kazi za mke hodari ni nyingi. Lakini yeye hupata baraka nyingi na thawabu kwa kazi zake njema. Bidii yake, busara yake, hekima yake na sifa nyingine njema zafanya washiriki wa jamaa yake wapendezwe naye. “Wanawe huondoka na kumwita heri; mumewe naye humsifu, na kusema, Binti za watu wengi wamefanya mema, lakini wewe umewapita wote.” (Mist. 28, 29) Naam, vivulana wa jamaa hiyo wanashukuru kwa kuwa na mama mwema hivyo, naye mumewe anafurahi kuwa na mke bora hivyo.
Mapendezi na urembo wa mwili waweza kumalizwa na ugonjwa na uzee. Lakini mwanamke huyu anao uzuri wa ndani unaodumu kwa sababu amejipa kwa Yehova Mungu na aogopa kwa unyofu kumchukiza. Upendo wake kwa Mungu, pamoja na matendo yake mema, unaletea mke hodari sifa na heshima. Matendo yake mema yasifiwa malangoni, kwenye njama ya mji! Yeye anakumbusha watu juu ya Ruthu, ambaye Boazi alimwambia hivi: “Mji wote pia wa watu wangu wanakujua ya kwamba u mwanamke mwema.”—Ruthu 3:11.
Mke hodari hapati sifa ya wengine bure; anaipata kwa sababu ya “matendo yake.” Yaani, ameifanyia kazi heshima hiyo. Kwa hiyo, anapomaliza maelezo juu ya “mke hodari,” Mfalme Lemueli asema: “Mapendezi huenda yakawa ya uongo, na urembo huenda ukawa wa ubatili; lakini mwanamke amchaye Yehova ndiye hujipatia sifa. Mpe matunda ya mikono yake, uache matendo yake yamsifu hata katika malango.”—Mist. 30, 31, NW.
MAISHA YENYE KIASI
Bila shaka mke hodari alitunza nyumba yake sikuzote ikawa safi, yenye kupendeza. Ingawaje, usafi ulitiliwa mkazo kati ya watu wa Mungu. Kwa mfano, makuhani walikuwa na wajibu wa kuwa safi kimwili na katika sherehe. (Kut. 30:17-21) Nyumba malidadi na safi huthaminiwa na kila mshiriki wa jamaa. Lakini, bila shaka wote wanaweza kusaidia kuiweka hivyo kwa kuwa malidadi wao wenyewe. Kwa upande mwingine, ‘mfanya kazi nyumbani’ mwenye kuwaza atakuwa na hekima kwa kuwa na maoni ya kiasi wala si kutia mkazo mwingi kupita kiasi juu ya unadhifu (usafi) hata mumewe na watoto wake wanajisikia kuwa na woga wa kukalia viti fulani au kutumia meza fulani kwa kusudi linalofaa.
Maisha ya mke hodari yalikuwa ya utendaji wa kiasi. Hakutumia wakati mwingi sana katika shughuli moja hata akakosa kuangalia kazi nyingine za maana. Kwa mfano, alitengeneza mavazi, mengine akayauza kwa bei ya kujipatia faida. Lakini hakuacha kufanikiwa kwake katika shughuli hiyo kumwondoe katika kazi nyingine ya lazima, kama vile kuipa jamaa yake chakula. (Mit. 31:13-15, 21-24) Lo! huo ni mfano mwema kweli kwa ‘wafanya kazi nyumbani’ wa Kikristo.
Watu wengi katika Israeli ya kale walianza kazi ya siku kulipopambazuka na wakaiacha usiku ulipoingia. Mtunga zaburi alisema hivi: “Jua lachomoza . . . Mwanadamu atoka kwenda zake kazini, na kwenye utumishi wake mpaka jioni.” (Zab. 104:22, 23) Lakini kwa wengi—kutia na mke hodari—siku ya kazi huanza kabla ya jua kuchomoza. (Mit. 31:15) Kwa vyo vyote, mume alipoondoka nyumbani kwenda kazini, angeweza kuwa na hakika kwamba mke wake hodari angeangalia vizuri mambo ya nyumbani. Mwishoni mwa siku, hakujisikia akitaka kukaa mbali na nyumbani kwa sababu ya kuwa mahali pasipopendeza, pasipoangaliwa na mke mvivu. Bali, mwenzi-msaidizi wake alikuwa amesawazisha mipango ya kazi zake hata asingekosa kuangalia moja na hivyo alete huzuni.
Kwa hiyo, mume alikuwa na hamu ya kurudia nyumba yake yenye starehe, yenye kutunzwa sawasawa. Humo angeweza kukaa saa nyingi akifurahi pamoja na mkewe hodari mwenye upendo, na watoto wao. Sivyo, mke wake asingekuwa akifanya kazi saa zote. Maisha yenye kiasi yahitaji burudisho. Nyakati nyingine burudisho hilo lingekuwa mazungumzo mazuri, labda pamoja na ucheshi mara kwa mara, kwa maana kuna “wakati wa kucheka.”—Mhu. 3:1, 4.
Kwa sababu mke hodari alisawazisha mipango ya madaraka yake mengi, alikuwa na wakati wa kutenda mema kwa ajili ya maskini na wenye shida. (Mit. 31:20) Vivyo hivyo, ‘wafanya kazi nyumbani’ wa Kikristo wanapanga kazi zao kwa njia itakayowawezesha kuwa na wakati wa kutendea wengine mema, kama wanapowaeleza habari njema za ufalme wa Mungu.—Mt. 24:14.
Wanawake wa Kikristo wanaofuata kwa bidii maelezo yaliyoandikwa kwa uongozi wa kimungu ya Mfalme Lemueli juu ya “mke hodari” hupata furaha na baraka nyingi. Hivyo wanapata uradhi wa kupendelewa na waume zao. (1 Kor. 7:34) Ingawa wao hawafanyi kazi ili wajipatie sifa tu, wanasifiwa na waume zao, watoto wao na wengine. Na la maana zaidi, wanawake wa Kikristo hawa wanakuwa na furaha inayotokana na kumpendeza Yehova Mungu kama ‘wafanya kazi wema nyumbani.’