Je! Ilifaa Nijitahidi Kushinda Watu Wote?
Mawazo ya Bingwa wa Mbio katika Michezo ya Olympics
MIAKA mingi nilikuwa nimetamani wakati huu ufike, nishindane katika Michezo ya Olympics. Ilikuwa Jumamosi, Oktoba 17, 1964, siku ya nane ya Michezo hiyo katika Tokyo, Japan.
Kila kimojawapo viti 75,000 katika National Stadium kilikuwa kimekaliwa. Ilionekana barabara za Tokyo zilikuwa hazina watu—karibu kila mtu alikuwa akitazama televisheni. Wakati ulikuwa umefika wa mbio ya mwisho ya kufyatuka mita 200.
Nilijipanga katika mistari ya kuanzia mbio nikiwa pamoja na wapiga mbio wengine saba. Kila mmoja wetu alikuwa amefaulu asiondolewe siku zilizotangulia katika mbio za kujaribu watakaoingia katika mashindano ya mwisho. Sisi ndio tuliokuwa wenye mwendo wa kasi kupita wanadamu wote katika mbio za urefu huo.
Moyo ulinidunda sana, si kwa sababu ya kutazamwa na mamilioni ya watu tu. Nilishikwa na utukuzo wa taifa. Michezo hiyo ilianza kuwa ya kushindana sana kati ya Warusi na Waamerika. Habari zilivuma kila siku ulimwenguni pote juu ya nishani ilizoshinda kila nchi. Shule zetu, mameya (wakuu wa miji) wetu, magavana, na hata rais alitupelekea simu za barua kutukumbusha kwamba tulikuwa tukishindania nchi yetu, na kwamba nchi yetu ndiyo bora.
Magazeti pia yalitukaza, yakahesabu nishani tulizopaswa kushinda. Walitufanya tuone kama kwamba kushinda kulikuwa jambo la kufa au kupona, kama kwamba nchi ingepoteza heshima yake tukishindwa. Kwa kweli, Kokichi Tsuburaya, mpiga mbio Mjapan wa mbio ya marathon (maili 26) alijiua baada ya kushindwa. Kabla hajajiua aliandika kibarua kidogo kusema pole kwa sababu ya ‘kukosa’ kushindia nchi yake.
Kwa hiyo nikaanza kufikiri hivi: ‘Siwezi kuaibisha nchi yangu. Nitaona aibu nyingi kuwarudia nyumbani nikishindwa.’ Mimi ndimi niliyekuwa bingwa wa rekodi ya ulimwengu ya mita 200, kwa hiyo walinitazamia nishinde.
Weusi pia walinikaza kwa sababu walitaka kujulikana. Niliambiwa mara nyingi jinsi weusi wengine walivyoshindwa wakaaibisha watu wetu. Kwa hiyo sasa ilikuwa lazima nishindie weusi wa Amerika. Weusi wengine walichochea tususie Michezo, kuonyesha Amerika kwamba isingeweza kushinda bila ya sisi weusi kuwamo.
Lakini hasa nilifikiria jamaa na rafiki zangu. Sikutaka kuwaaibisha. Mimi nilikuwa dume lao. Waliniunga mkono; walinishangilia. Mimi niliposhinda, wao walishinda. Niliposhindwa, wao walishindwa. Labda utaelewa vizuri zaidi nikikueleza kifupi hali zangu za maisha.
Naanza Kuwa Mashuhuri
Nilikulia Detroit, Michigan, nikiwa wa tisa kati ya watoto kumi na mmoja. Kadiri nikumbukavyo, mama na baba walikuwa wametengana. Mama alifanya kazi saa nyingi nyumbani akijaribu kutupatia riziki.
Sikuzote mimi nilikuwa mwanamichezo. Kwa kuwa ilikuwa vigumu kwangu kusoma na kuandika, lilikuwa jambo la maana sana kwangu kuwa mtoto mwenye mbio zaidi au mchezaji bora; lilikuwa jambo bora maishani.
Katika shule ya masomo ya juu, baada ya muda mfupi tu nikawa hodari katika michezo. Miaka mitatu—1959, 1960 na 1961—niliingizwa katika kikoa cha shule zote za Amerika za masomo ya juu. Mbio ya yadi 220 ndiyo niliyoijua zaidi. Nilichaguliwa pia niwe katika vikoa (timu) vya taifa zima katika mpira wa namna ya rugby na basketball kwa miaka miwili.
Ilikuwa vigumu kwenda chuo kikuu. Lakini sasa vyuo vikuu vilianza kuniomba nivisaidie. Nilikwenda vyuo vingi United States wakajaribu kunishawishi kwa kunitolea zawadi. Kwa hiyo, niliweza kutia pesa mfukoni ingawa jamaa yetu ilikuwa maskini, hata nikaweza kuendesha motokaa ya maana, aina ya Cadillac! Nilipokea leseni yangu ya uendeshaji katika chumba cha kulia cha jumba la pombe, bila hata ya kufanyiwa mtihani wa uendeshaji! Kimojawapo vyuo vikuu vya karibu kilichokuwa kikijaribu kunizoeza ndicho kilichonipangia niipate.
Lakini, mimi nilichagua kwenda Arizona State University, kisha nikawa mashuhuri ulimwenguni bila kupoteza muda, kwa sababu ya kupiga mbio. Mwaka wangu wa pili wa kuwa katika chuo kikuu nilivunja rekodi ya ulimwengu ya kufyatuka katika mbio ya yadi 220. Viongozi wa ulimwengu walitaka kuniona wanisalimu. Nilionana na Nikita Khrushchev huko Moscow. Lakini sikuona furaha halisi kwa kupata sifa wala kwa kusafiri ulimwenguni nikashiriki mashindano ya mbio.
Huko Arizona State nilitendewa vizuri ati kwa sababu nilikuwa mpiga mbio hodari. Watu walikuwa wakinimiminia zawadi—zinazoitwa “viinua-mgongo.” Kwa hiyo nilikuwa na pesa nyakati zote, mavazi mapya na motokaa. Mara nyingi nilipeleka pesa nyumbani nisaidie washiriki wa jamaa yetu. Hakika niliyapenda mapendeleo na sifa nilizopata. Lakini nilijua haikuwa sawa; sisi tulipaswa kuwa wanamichezo wasio wa mshahara. Hata hivyo, mambo yalikwenda hivyo.
UDHALIMU
Ingawa ujuzi wangu ulinipa sifa, mwezi mmoja tu kabla sijakwenda Tokyo nilifukuzwa katika mkahawa kusini ya United States kwa sababu mimi ni mweusi. Bibi aliyenifukuza alinitolea sauti, “Hatutumikii watu wa aina yako hapa.” Usiku ulikuwa umeingia nami sikutaka cho chote isipokuwa mahali pa kulala.
Karibu na wakati uo huo weupe waliua wafanya kazi watatu katika Mississippi. Huko Kusini mbwa walikuwa wakifunguliwa waume weusi ati kwa sababu walitaka elimu bora. Lakini niliposafiri ulimwenguni nilisadiki kwamba udhalimu uko kila mahali. Katika nchi nyingine watu walikatazwa sana uhuru wa kufanya mambo yao wenyewe ambayo mimi niliyafanya United States bila wasiwasi.
Nilihurumia sana watu wenye kutaabika. Lakini ningeweza kufanya nini? Nilijua kwamba tatizo hilo halikutukia United States kwa sababu ya kuwa na rangi mbalimbali tu za watu. Nyakati nyingine weusi walipopata vyeo walitenda weusi wenzao kama walivyotendwa na weupe. Nilitumia akili nikaona sikuwa na la kufanya niondoe hali hiyo, kwa hiyo nikaamua kutojiharibia mataraja yangu kwa kujishughulisha na mambo hayo.
Mambo yote yaliniendea vizuri wakati huo. Nilipokuwa mtoto sisi tulikuwa maskini sana hata nilikwenda kulala nikiwa na njaa, nami sikutaka hivyo tena. Kwa hiyo nikajifunza kuwa namna ya mtu mwenye adabu na upole anayependwa na taratibu hii. Mara nyingi watu waliniambia: ‘Ukishinda tu katika Olympics, usiwe na wasiwasi. Shirika fulani kubwa litakukodi kwa sababu wewe ni dume la Olympics.’ Kwa hiyo niliepuka matata nikitaka kushinda huko Tokyo.
Wengine wanasema nilizaliwa nikiwa mpiga mbio, ‘mwenda-mbio hodari zaidi tangu siku za Jesse Owens.’ Lakini acha nikuambie, nilijitahidi sana kuongeza ujuzi wangu. Haikuwa kazi rahisi kuweza kushinda watu wote. Lakini ikiwa ningepata mambo ambayo watu waliniambia ningepata;, nikishinda katika Olympics, niliona ilifaa nijitahidi.
Maisha yangu yote moyo haukuwa umenidunda jinsi ulivyofanya tulipojipanga katika mistari ya kuanzia mbio ya kuamua mshindi katika Olympics.
MATOKEO
Niliinama nikiwa katika Mstari wa Saba. Nilitaka nitumie maarifa niwatangulie wenzangu kabla hatujafikia duara, niwafanye wajitahidi zaidi kunikuta. Hiyo ni kwa sababu mtu akipiga mbio bila kulegeza misuli, hawezi kufaulu sana.
Msimamizi alisema: “Magoti chini. Juu!” Halafu bunduki ikalia: “TWAA!” Niliondoka vizuri. Nilipofikia duara nikawaza: ‘Nimefaulu! Nimewatangulia! Nitashinda.’ Nilikaza macho kwenye mstari wa kumalizia. Nikanyosha miguu nikang’oka. Nilishinda!
Niliona raha kweli kweli. Niliona vitu vyote kama kwamba vilikuwa vikizunguka; nilifurahi weee. Niliweka rekodi mpya ya Olympics, ikasemekana labda ningalivunja rekodi yangu mwenyewe ya ulimwengu kama kusingalikuwa na upepo mbele yetu.
Nilipokuwa nimesimama katika kibao cha ushindi huku wimbo wa taifa la Amerika ukipigwa kushangilia bendera yetu yenye nyota, nilitaka kujivunia nililofanyia nchi yetu. Nilifurahi kushangiliwa na maelfu ya watu. Lakini nilijua huo ulikuwa udanganyifu tu. Kwa sababu watu bado walikuwa na kinyongo cha kutendwa udhalimu sawa na walivyokuwa kabla sijasimama katika kibao cha ushindi.
Nikashangaa: ‘Sasa nitafanyiwa nini baada ya kumaliza mashindano? Wenye kuniunga mkono watafanya nini? Wataniacha? Nitapata kazi ya namna gani?’ Nilifurahi, nikaogopa na kukasirika wakati ule ule mmoja.
Nilipokuwa katika gari kurudia makao ya wanamichezo, Olympic Villages, ndipo nilipoichunguza nishani ya dhahabu kwa mara ya kwanza. Haikuwa nilivyoitazamia kuwa; ilikuwa dola kubwa sana ya fedha, si zaidi ya hapo. Nikajiuliza: ‘Upuzi gani! Miaka yote hiyo nimekuwa nikijitahidi sana nije kupokea kitu hiki?’ Nilikasirika sana, ingawa ningalipaswa kufurahi. Ilikuwa aibu.
Siku chache baadaye nilipiga mbio mita 400 za mwisho katika mbio ya mita 1,600 ya kupokezana vijiti.
Tuliweka rekodi mpya ya Olympics na ulimwengu pia, nikapokea nishani nyingine ya dhahabu. Baada ya kusafiri Australia kushiriki mashindano mengine, nilirudi nyumbani.
Nilivyofanya Baada ya Kupatwa na Magumu
Nilipokuwa katika safari ya kurudi nyumbani nilikaza fikira juu ya maisha mapya ambayo nilikuwa nimeanza kuwa nayo—kutafuta kazi na kukuza jamaa. Lakini kwanza nilikwenda White House (makao rasmi au Ikulu ya rais wa Amerika) pamoja na wanakikoa wenzangu, tukapongezwa na Rais Johnson.
Nilitazamia kufikiria kazi mbalimbali nitakazopewa, kisha nichague mojawapo niliyotaka. Miaka mingi watu walikuwa wakiniambia ndivyo ingekuwa nikishindia nchi yangu katika Olympics. Lakini wapi. Kila mahali nilikokwenda watu hawakunijali ati kwa sababu nilikuwa nimeshinda katika Olympics. Naam, walifurahia kuzungumza habari hizo. Lakini nilipowaomba waniandike kazi, walinidharau kama wanavyodharau mweusi mwingine ye yote, wakiona sikuwafaa. Nilianza kuona uchungu.
Baada ya miezi michache, nilipigiwa simu nikaulizwa kama nilipendezwa na kucheza mchezo namna ya rugby wa kulipwa mshahara. Sikuwa nimeucheza miaka miwili, kwa maana nilikuwa nimetumia wakati wangu nikipiga mbio. Lakini nilitaka sana kazi, kwa hiyo nikakubali. Kikoa The New York Giants kilinichukua, wakadhani naweza kuwafaa kwa sababu ya mwendo wangu wa kupiga mbio.
Kwa kuwa nilikuwa na shida nilijitahidi sana nikaingizwa katika kikoa (timu). Miaka mitatu niliendelea vizuri sana, na kwa muda nikawa mkingaji mkuu. Mwandikaji mmoja wa habari za michezo alisema: “Carr alijiunga na New York Giants akawa mmojawapo wakingaji bora.”
Niliumia goti tukiwa tumebaki na michezo mitatu tu katika msimu wangu wa tatu, kisha mwenye kutuzoeza akasema mwaka wote huo nisingecheza tena. Lakini baadaye daktari alinipigia simu akasema wakufunzi wangu walitaka nicheze. Ubishi ulitokea juu ya jeraha langu, kwa maana mwanzoni mwa mwaka nilileta ubishi katika kikoa juu ya ubaguzi wa rangi.
Kwa hiyo, mwishoni mwa msimu huo niliondolewa katika kikoa hicho niingie kingine. Ilisemekana kwamba nilikuwa mfanya matata asiyependa kucheza akiudhiwa. Nilitendwa vivyo hivyo na kikoa kile kingine nilichoingia. Kwa hiyo nikaamua kuondoka, ingawa mwaka uliotangulia nilikuwa nimechuma $27,000 (shilingi zaidi ya 216,000 au 13.500Z).
NIKAPATA HASARA
Nilijitahidi kupata kazi nzuri, lakini wapi. Mwishowe nilipata hasara baada ya kuwa na viduka vidogo vya kuuzia hamburger (nyama zilizosagwa na kuviringwa kisha zikakaangwa). Nilikasirika sana. Niliona watu walikuwa wakianza kunidharau kwa vile walidhani nilikosa kufaulu kwa sababu sikujitahidi.
Nilidhoofika akili. Sikuwa nikifanikiwa maishani. Nikawa mvuta bangi kila siku, nikiwaza jinsi ningeweza kuwa na maisha bora tena. Mke wangu alitaka kunisaidia asiweze. Niliona jamaa yangu (yenye watoto wawili wakati huo) ingekuwa afadhali mimi nisipokuwapo. Kwa hiyo nikaondoka nyumbani.
Baada ya muda nikawa mfisadi wa kupindukia, nikashirikiana na wenye kupendekeza watu watumie dawa za kulevya na malaya. Nilianza kucheza kamari na kunusa cocaine (namna ya tumbako kali). Kwa kuwa nilikulia katika mtaa wa weusi katika Detroit, niliwajua wengi kati ya watu niliokuwa nikizurura nao. Baada ya muda mfupi wakapanga niwe mmoja wa wenye kupendekeza watu watumie dawa za kulevya.
Baada ya miezi kadha, nilijichunguza. Nikaona nilikuwa nimeingia katika mambo yale yale ambayo niliyachukia sikuzote. Mambo yote yalikuwa mabaya; sikuwa na matumaini mazuri. Sikujua la kufanya. Nilikuwa na Biblia kwa hiyo nikaanza kuisoma, lakini sikuona ubora. Nikaamua kurudi nyumbani.
Kupata Maisha Yenye Manufaa
Mke wangu alikuwa mwenye huruma. Jinsi watoto walivyonitazama ilionyesha walikuwa wamehuzunika nilipokwenda. Nilianza kazi ya kutunza watoto waasi pamoja na baraza ya mji. Lakini baada ya muda mfupi baraza yenye kuniandika kazi ilipungukiwa pesa, ikawa nitaondolewa kazini kwa muda. Kiburi changu kilinifanya nijione mwenye shida tena.
Mke wangu aliniruhusu niuze mali fulani tuliyokuwa nayo kisha tukatumia pesa tulizopata kuanza biashara ya kutangaza bidhaa. Mfanya biashara mwenzangu alikuwa mchoraji hodari sana, nami nilifanya kazi ya kutangazia watu bidhaa. Watu walinijua wakaniheshimu, na baada ya muda mfupi nikawa nikienda New York kuona wanunuzi. Biashara ilisitawi.
Niliporudi kutoka kazini siku moja, mke wangu aliniuliza kama ingefaa ajifunze Biblia na Mashahidi wa Yehova. Nikamwuliza, “Sababu?” Akasema kwamba wazazi wa mmojawapo wanafunzi wake (alikuwa mwalimu wa shule ya msingi) alikuwa amempa kitabu Kweli Iongozayo kwenye Uzima wa Milele. Mwalimu mwingine alikuwa amemwambia pia kwamba akitaka kujua lo lote kuhusu Biblia, yampasa awaulize Mashahidi wa Yehova.
Siku chache kabla ya hapo tulikuwa tumezungumza habari za dini mbalimbali, maana kivulana wetu alikaribia kwenda shule nasi tuliona ni jambo la maana apate masomo ya dini. Laki hatukufikiria Mashahidi wa Yehova. Habari pekee nilizojua juu yao ni kwamba walikuwa wanadini hoi. Lakini, mimi niliona ni sawa tu mke wangu ajifunze nao akitaka.
Nilifanya kazi mchana kutwa na usiku kucha, lakini ilipowezekana niwe nyumbani mke wangu alinitajia mambo aliyokuwa akijifunza. Juma moja hivi, baadaye, mume wa mwanamke aliyekuwa akijifunza na mke wangu alinitembelea.
JAMBO LA KUFIKIRIA
Alinieleza jinsi ambavyo dunia ingeweza kuwa mahali pazuri ajabu watu wakiishi pamoja kwa amani. Nikakubaliana naye. Halafu akasema “Je! si ni wazi kwamba Mungu Mwenye Nguvu Zote siye anayeleta hali mbaya ulimwenguni leo?”
Nilishangazwa na hilo. “Ikiwa si Mungu, ni nani basi?” Nilitaka kujua.
Akasema, “Shetani Ibilisi.” Lililonishangaza ni kwamba alifungua Biblia akanionyesha. Wakorintho wa Pili 4:4 yasema: “Mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.”
Shahidi akanieleza kwamba Shetani ndiye “mungu wa dunia hii.” Niliona ukweli wa jambo hilo aliponionyesha udhalimu mbaya sana ambao unatendwa ulimwenguni pote. Shahidi akatia mkazo kwamba huu ni ulimwengu wa Shetani naye ndiye anayeongoza watu wake. Jambo hilo likanisaidia kufahamu andiko jingine nililoonyeshwa. Yesu Kristo alisema: “Mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje.”—Yohana 12:31.
Ni wazi kwamba wanadamu hawawezi kumwondolea mbali mtu huyo wa kiroho mwenye nguvu Shetani Ibilisi. Lakini Mungu aweza, Shahidi akanieleza. Atafanya hivyo, ili kutimiza kusudi lake la kufanya dunia iwe yenye amani kwa kutawalwa na Ufalme wake. Jambo hilo lilisikika kuwa la akili. Lilikuwa jambo la kufikiria.
NASAIDIWA KUFANYA UAMUZI UFAAO
Shahidi alinirudia mara nyingi, naye aliponikuta nyumbani tulizungumza tena habari za Biblia. Nikaanza kuamini niliyokuwa nikijifunza kwa maana yalitolewa mle mle ndani ya Neno la Mungu. Kwa mfano, sikujua kwamba Mungu ana jina. Na hali mumo humo ndani ya Biblia, katika Zaburi 83:18, yaelezwa kwamba jina lake ni YEHOVA. Nilifurahia kujifunza mambo hayo.
Lakini nilianza kusumbuka nilipofikiria kwamba Biblia yasema Shetani ndiye mungu wa ulimwengu huu. Lililonisumbua zaidi ni kufikiria kwamba yasema wafuasi wa Kristo si sehemu wa ulimwengu. (Yohana 17:14-16) Sababu moja ni kwamba nilikuwa katika siasa, kwa maana mtangaza bidhaa mmoja aliyekuwa mweusi mwenzangu alikuwa akigombea cheo cha meya (mkuu wa mji) katika Detroit.
Kwa hiyo siku moja nilimwambia Shahidi: “Najua unatia bidii nyingi; unajaribu kunisaidia. Lakini nina shughuli nyingi sana katika kazi yangu mpya ya kutangaza bidhaa, nami sitaki kukusumbua, kukuambia uje usipoweza kunikuta nyumbani.”
Basi, muda mfupi baada ya hayo nikaumia mgongo nikawa katika hali mbaya, na mwishowe nikalazwa hospitali. Wakati huo Mashahidi walikuja kunitembelea, wakaonyesha huruma. Nikawaza: ‘Watu hawa hawanijui. Wanajua kwamba mimi ni mume wa Glenda na basi, lakini wananitendea kiajabu.’ Nilipendezwa na walivyonitendea.
Wakati wote huo nilikuwa nimeona mabadiliko katika mke wangu. Kwa mfano:Binti mdogo wa mmoja wa Mashahidi alikufa, naye mke wangu akamhurumia sana mama yake. Nilimtazama mke wangu nikawaza: ‘Hajapata kutenda hivyo. Sababu gani anapendezwa sana kumpikia mama huyo vyakula na kwenda nyumbani kwake kumsaidia?’ Niliyawaza mambo hayo nilipokuwa nimelala hospitalini.
Wakati uo huo biashara yetu ilikuwa ikifilisika. Ilikuwa imekuwa ya watu wanne, nami nilipaswa kuendesha mambo. Nilipotoka hospitali nilikuta biashara imeharibika sana hata wenzangu wote wakaiacha. Tena, mimi ndimi niliyepata hasara ya pesa.
Nilijua nilivyotaka kuwa—kuweza kupenda watu na kupendwa, na kuwa mwenye furaha. Niliona mabadiliko katika mke wangu, hata mimi nikaamua kubadilika. Kilichoingia sana akilini ni kwamba Shetani ndiye mungu wa taratibu hii, na kwamba nilihitaji msaada niyazuie maongozi yake. Kwa hiyo nilipotoka hospitali, nilimwita shahidi yule yule nikamwambia nataka kujifunza Biblia.
NILIVYOFANYA MABADILIKO
Baada ya funzo langu la kwanza Desemba 1972, nilikwenda Jumba la Ufalme. Kila mtu alifurahi kuniona. Niliona mke wangu akifurahi kwa sababu nilihudhuria. Nakumbuka kwamba mmoja wa wasemaji alitaja kuwa mume ndiye kichwa cha nyumba yake, na yampasa aongoze nyumba. Nikawaza, ‘Mke wangu ndiye amekuwa akifanya hivyo, akijifunza na watoto, akiwapeleka mikutanoni, akisali nao, nami nimekuwa sifanyi jambo lo lote.’
Juma iliyofuata watoto wakawa wagonjwa, kisha mke wangu akasema: “Wewe baki na watoto, ninakwenda mkutanoni.” Hakudhani nilitaka kwenda. Lakini nikamtazama nikamwambia: “Mimi ndimi ninayepaswa kuwa kiongozi wa nyumba. Kwa hiyo wewe baki nyumbani na watoto.”
Alinitazama tu, akashangaa—lakini nadhani alifurahi. Mimi pia nilifurahi, nikaona fahari kidogo kwamba sasa nilikuwa nimeanza kutoa uongozi. Nimekosa kuhudhuria mikutano mara chache sana tangu wakati huo. Imenisaidia kweli kweli nifanye mabadiliko ambayo yameletea jamaa furaha.
Niliweza kupata kazi niliyokuwa nimetaka sikuzote, ya kuwa mkuu mwenye kutayarishia gazeti fulani mambo ya kutangazwa. Nilikuwa mwenye shughuli—nikawa mtu wa kutembea sana—watu wakanijua nami nikawajua, nikaanza kuona jinsi ambavyo ningeweza kufanya maendeleo. Niliitiwa kazi nyingi za ziada. Lakini mimi nilizidi kwenda mkutanoni, na hilo lilikuwa jambo jema kwa sababu niliyojifunza huko yalibadili maisha yangu kweli kweli. Kwa mfano, nilijua madhara yanayoletwa na dawa za kulevya. Nikawa nimeacha kuzitumia. Lakini nilikuwa bado nikivuta bangi. Sikuona kwamba lilikuwa kosa hasa kufanya hivyo, kwa maana inavutwa na watu wengi sana. Lakini katika mkutano mmoja ilionyeshwa kwamba kuvuta ni kinyume cha Maandiko. Biblia yasema yatupasa “tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho.” Nilielewa wazi kwamba hiyo ilimaanisha niache kuvuta bangi nikitaka kumpendeza Yehova Mungu.—2 Kor. 7:1.
Katika mkutano mwingine ilikaziwa kwamba uzinzi ni mbaya. Biblia yasema: “Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.” (Ebr. 13:4) Kwa hiyo nikaona ilinipasa nifanye mabadiliko makubwa zaidi.
Nilitaka kumpendeza Mungu kwa hiyo nikawa nikimfikia katika sala kumweleza mambo hayo. Ndipo niliposoma jambo fulani katika Mnara wa Mlinzi juu ya uhitaji wa kumweleza Yehova ukweli sikuzote. Kwa hiyo nikamfungulia moyo nikamwambia niliyafurahia mambo mabaya hayo—na hata nilitazamia nafasi ya kuyafanya—lakini sasa, juu ya jambo jinginelo lote, nilitaka kumpendeza yeye kweli kweli. Kwa kumweleza Mungu ukweli huo na kumtegemea anisaidie, niliyaacha mazoea mabaya hayo. Hata haikuwa vigumu kuacha kuvuta bangi kama nilivyodhani.
Nilishangaa kujiona mwenye furaha zaidi. Nilianza kuwa na kusudi katika maisha. Watoto wangu walianza kunitegemea niwaongoze. Sote tulimthamini Yehova na mikutano tuliyohudhuria pamoja. Lilikuwa jambo zuri weee! Niliyafurahia matukio na mabadiliko hayo yaliyokuwa yakinipata mimi na jamaa yangu kuliko kitu kinginecho chote ulimwenguni.
Nilisadiki kwamba tulikuwa tumeipata kweli. Nikadhani kwamba rafiki zangu wote—waliokuwa wamevurugika, huku wakipatwa na matatizo na kuzoea uasherati—wataisikiliza. Lakini hata mmoja hakusikiliza. Walianza kunifanyia mzaha, wakaniita “bwana mhubiri.” “Bwana mhubiri yuaja,” walikuwa wakisema.
Kwa hiyo nikaona kwamba watu hao wa ulimwengu hawakuwa rafiki zangu wa kweli. Mimi nilitaka kuwa na rafiki waliompenda Mungu. Kwa hiyo ili tuonyeshe kwamba tulikuwa tumeweka maisha zetu wakf tumtumikie Yehova, mke wangu na mimi tulibatizwa Mei 20, 1973.
Zaidi ya kitu kinginecho chote, nilithamini zaidi uhusiano wangu mwema na Mungu, na jamaa yangu na Wakristo wenzangu. Ingawa nilikuwa na kazi nzuri yenye mshahara mnono, kazi hiyo iligawanya mapendezi yangu, tena kulikuwa na mashirika mabaya na vishawishi. Nikazidi kulifikiria lile andiko lisemalo: “Mashirika mabaya yanaharibu mazoea mazuri.” (1 Kor. 15:33, NW) Kwa hiyo nikaacha kazi yangu ya kuwa mkuu wa utangazaji wa mambo ya magazeti, ingawa hiyo ndiyo kazi niliyokuwa nimetamani muda mrefu.
TUMEPUNGUKIWA MALI ZA KIMWILI, LAKINI TU MATAJIRI
Shahidi katika kundi letu aliniajiri niwe msaidizi wa mpaka rangi. Sikuchuma pesa nyingi, lakini nilikuwa mwenye furaha. Sikuhangaikia kuwa mtu mashuhuri. Mimi nilitaka kumtumikia, Yehova tu. Nilijua kwamba yeye ni mtu halisi, Mtu wa pekee anayeweza kuondoa udhalimi wote. Ushuhuda wa Biblia, yaani, kutimizwa kwa unabii mbalimbali, na uwezo wa Biblia wa kunyosha maisha za watu, ulinisadikisha kwamba angeweza.
Baada ya kutoka kwenye kusanyiko kubwa la Mashahidi wa Yehova mwaka 1973, nilimwambia mke wangu hivi: “Yanipasa kuwa nikipainia sasa (kuhubiri wakati wote).” Kwa kuwa tulikuwa na mali za ziada ambazo tungeweza kuuza, sikuwa na kitu cha kunizuia. Kwa hiyo nikaanza kupainia.
Baada ya muda fulani nikawaza, ‘Tunaweza kusaidia zaidi mahali ambako wahubiri wa Ufalme wanahitajiwa zaidi.’ Wakati huo Fred Cooper, niliyekwenda shule ya masomo ya juu pamoja naye, akanipigia simu akiwa Georgia. Yeye ni mzee katika kundi la huko, na alikuwa amesikia nimekuwa Shahidi. Nikamwambia nilikuwa nikifikiria kwenda kwenye uhitaji mkubwa zaidi. Kwa hiyo mwishowe tukauza nyumba yetu tukahamia Georgia.
Nilifurahia sana kupainia, lakini kwa sababu nilikuwa nikiumwa mgongo na kulikuwa na uhitaji wa kupata kazi niruzuku jamaa, mwishowe nililazimika kuacha kupainia Mei 1975. Lakini, Septemba niliwekwa niwe mzee katika kundi la huko. Tangu wakati huo mke wangu nami tumefundisha sana shule ya msingi tuweze kuwa na pesa za gharama zetu. Ni kweli kwamba hatuna mali nyingi za kimwili, lakini tu matajiri katika njia za maana zaidi.
Kwa mfano, mwanangu hupendezwa na mambo ya kiroho—husoma Biblia na vitabu vyetu vya kutusaidia kujifunza Biblia. Karibu mwaka na nusu uliopita, alipokuwa mwenye umri wa miaka saba, aliniuliza kama angeweza kuingia katika Shule ya Kitheokrasi ya kundi. Nilifurahi sana kwa ndani. Nilipokuwa wa umri wake sikuzote niliwaza mambo ya michezo tu, kuwa bingwa wa michezo. Nami nilijua Peyton angaliweza kuniomba ajiunge na kikoa fulani cha michezo.
JAMBO LILILO NA MANUFAA
Nadhani michezo ni mizuri—ikifanywa bila kupita kiasi chake. Lakini tangu mwanzo inakuwa na udanganyifu. Wanamichezo huabudiwa kuwa watu maalum—na kumbe wao ni nyama na damu tu kama mtu mwingine ye yote. Nao watoto hukazwa washinde michezoni, kwa hiyo inakuwa si michezo tena, bali jambo la kukazania kweli kweli. Ebu angalia madhara yanayopata watoto wanaokazwa wawe washindani bora na hali wengi wao hawawezi kuwa hivyo.
Hata mtu anaposhinda watu wote, bado michezo ni udanganyifu. Kwa sababu gani? Kwa sababu haendelei kushinda nyakati zote, wala hapati uradhi halisi. Baada ya muda fulani kunatokea mabingwa wengine wa kumshinda kisha anasahaulika. Halafu anakata tamaa, anashuka moyo na kuanza kuumwa mwili. Basi ni jambo gani lililo na manufaa?
Badala ya kushindana na wengine uwe bora, unaweza kupata uradhi wa kweli kwa kusaidia wengine na kuwatumikia. Ndivyo Kristo alivyofanya. Alikuja ‘kutumikia, si kutumikiwa.’ (Mt. 20:28) Naam, umoja mwingi unaoletwa katika jamaa na kundi na roho hiyo isiyo ya kichoyo, bali ya kupenda wengine, ndio unaofanya maisha yawe yenye manufaa kweli kweli—kujitahidi kushinda watu wote hakuna manufaa.
[Picha katika ukurasa wa 340]
“Nikapokea nishani nyingine ya dhahabu”
[Picha katika ukurasa wa 341]
“Kikoa The New York Giants kilinichukua”
[Picha katika ukurasa wa 343]
‘Nilianza kujifunza Biblia na jamaa yangu’