Wewe Unathamini Vile Mungu Anavyokusubiri?
“Bwana . . . huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba.”—2 Pet. 3:9.
1. (a) Kwa sababu gani tunathamini watu wanaotusubiri? (Mit. 25:15) (b) Matokeo yanaweza kuwa nini tusiposubiri wengine?
JE! HATUFURAHI wakati watu wanapotusubiri, wasipotufanyia ukali? Tunathamini wanapofikiria matatizo na hali zetu, wanapotusaidia wawezavyo kwa upole. Maisha leo yana matatizo ya kutosha hata hatupaswi kuongezewa mengine kwa kukazwa na watu wasiosubiri. Tena, kama sisi wenyewe tungekosa subira, maisha hayangefurahika zaidi. Bali, tungekuwa tukiudhi wengine na kufanya iwe vigumu kwao kututendea fadhili. Kutosubiri kwetu kungeweza hata kuumiza watu tunaotegemea watusaidie na kututia moyo.
2, 3. (a) Lazima tusadiki nini ili tuweze kuendelea kuhubiri tunapoona watu wasiomcha Mungu wakifanikiwa? (Zab. 37:1-6; Ebr. 11:6) (b) Mhubiri 8:12, 13 yaonyeshaje kwamba sikuzote ni vizuri zaidi tuwe tukimcha Yehova?
2 Lakini mtu awezaje kuendelea kusubiri anapoona udhalimu na uonezi, wakati watu wasiomcha Mungu wanapoelekea kufanikiwa? Ahitaji imani. Naam, lazima tusadiki kwamba Yehova Mungu atanyosha mambo yote. Hilo lapatana na aliyoona Mfalme Sulemani kisha akaongozwa na Mungu ayaandike: “Ajapokuwa mwenye dhambi amefanya maovu mara mia, akazidisha siku zake; lakini hata hivyo najua hakika ya kwamba haitakuwa heri kwa mwovu, wala hatazidisha siku zake, zilizo kama kivuli; kwa sababu hana kicho mbele za Mungu.”—Mhu. 8:12, 13.
3 Huenda sheria zikafikilizwa kwa ulegevu na huenda wahalifu wakaweza kuponyoka wasiadhibiwe kwa kupotoa sheria fulani. Huenda wasiotii sheria wakadhani wanaponyoka. Lakini, kama Sulemani alivyoonyesha, ubaya wao hauwapi thawabu yo yote. Maisha yao yanapita upesi, “kama kivuli,” wala ujanja wao wote na hila zao haziwarefushii maisha hata kidogo. Kwa upande mwingine, wamchao Mungu hawapati hasara. Wanaendelea kuwa na dhamiri safi, wanatosheka na kufanya wanayojua ni haki, tena wana tumaini la kufufuliwa hata wakifa. Mwishowe, ‘inakuwa heri kwao wamchao Mungu wa kweli.’
4. Wakati wo wote tusumbuliwapo na tunayoona yakiendelea ulimwenguni, yatupasa tukumbuke nini, kama linavyokaziwa katika Mwanzo 6:5, 6 na Habakuki 1:13?
4 Tena, yafaa Wakristo wa kweli wakumbuke kwamba uvunjaji sheria unaowasumbua unamhuzunisha Yehova Mungu pia. Twajua hilo kwa sababu Biblia yaeleza jinsi alivyouona ulimwengu wenye jeuri wa siku za Nuhu. Twasoma hivi: “[Yehova] akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote. [Yehova] akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo.” (Mwa. 6:5, 6) Naam, Yehova alihuzunika kwamba wanadamu walikuwa wamegeuka wakawa wabaya sana hata akalazimika kuwaharibu. Aliudhika sana kwa sababu walitumia vibaya maisha yao na mipango tele aliyowapa waishi. Karne nyingi baadaye, nabii Habakuki aliandika juu ya Yehova hivi: “Wewe uliye na macho safi hata usiweze kuangalia uovu [kwa kuufurahia], wewe usiyeweza kutazama ukaidi [kwa kuukubali].”—Hab. 1:13.
5. Kulingana na 2 Petro 3:9, kwa sababu gani Yehova ameonyesha subira?
5 Hata hivyo, Mungu Mwenye Nguvu Zote amesubiri wanadamu waasi. Kwa sababu gani? “Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba.” (2 Pet. 3:9) Angalia kwamba subira ya Mungu imekuwa na kusudi la kufaidi Wakristo, kwa maana mtume Petro aliandikia waamini wenzake maneno haya, “huvumilia kwenu.” Hiyo maana yake nini hasa?
6. Kwa sababu gani inaweza kusemwa kwamba subira ya Yehova imefaidi Wakristo wa kweli?
6 Mtume alikuwa akionyesha kwamba Mungu hakupaswa kudhaniwa amekawia, kama wengine walivyodhani. Uhakika wa kwamba siku ya Yehova ya kisasi haijaja bado wahakikisha kwamba apenda wanadamu, kwamba ataka watu waishi, si wafe. Wakati mmoja Wakristo hawakuwa waamini, kwa hiyo hawakuwa na msimamo anaoukubali. Kama Aliye Juu Zaidi angalifikiliza hukumu yake juu ya ulimwengu wa wasiomcha Yeye wakati huo, wao pia wangalipotelea mbali. Kwa hiyo subira ya Mungu imewezesha Wakristo wapate wokovu, na vilevile inawapa watu wote nafasi ya kupata wokovu. Je! haitupasi kushukuru kwamba imekuwa hivyo?
7. (a) Je! Yehova atasubiri wanadamu wasiotii kwa wakati usiojulikana? (Isa. 55:6, 7; Sef. 2:2, 3) (b) Ni nini kinachohakikisha kwamba tunaishi katika “siku za mwisho”? (c) Kwa sababu gani yatupasa tuonyeshe subira hasa?
7 Bila shaka, karibuni sana Yehova Mungu atazimaliza ‘siku zinazokubalika’ alizowapa walio hai kuingia naye katika uhusiano anaoukubali. (2 Kor. 6:2) Unabii na tarehe za Biblia zaonyesha kwamba “siku za mwisho” za ulimwengu huu usiomcha Mungu zilianza 1914 W.K., zikiwa na ongezeko la uhalifu na jeuri, vita, upungufu wa chakula, matetemeko ya ardhi, hofu na msukosuko. (Marko 13:3-37; Luka 21:7-36; 2 Tim. 3:1-5) Maadamu taratibu hii yaendelea kuwapo katika “siku za mwisho,” lazima Wakristo waendelee kuonyesha subira, wakimtegemea Yehova Mungu amtumie Mwanawe Yesu Kristo kuwaletea faraja. (2 The. 1:6-9) Watafanya hivyo kwa sababu “siku za mwisho” hizi zitaendelea kuwa “nyakati za hatari.”—2 Tim. 3:1.
MANABII NI VIELELEZO VYA SUBIRA
8. Mwanafunzi Yakobo alionyesha mfano wa nani wa subira, na huenda ukatokeza ulizo gani?
8 Kwa hiyo, sasa hasa yatupasa tutiwe moyo na mfano wa subira tuliowekewa na watumishi wa zamani wa Mungu. Mwanafunzi Yakobo aliandika, “Ndugu, watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana wawe mfano wa kustahimili mabaya” (Yak. 5:10) Ni mambo gani hasa yaliyo wapata manabii hawa, na yaliwapata kwa sababu gani?
9. (a) Manabii waliitikiwaje na wananchi wenzao? (b) Kwa sababu gani waliendelea kuwasubiri Waisraeli miaka mingi?
9 Manabii waliona mara nyingi kwamba Waisraeli wenzao hawakutaka kuwasikiliza, waling’ang’ania kuendelea katika njia zao wenyewe za kutotii sheria. Biblia yatoa muhtasari inayofuata juu ya hali iliyokuwa Israeli na Yuda: “[Yehova] aliwashuhudia Israeli, na Yuda, kwa kinywa cha kila nabii, na cha kila mwonaji, akisema, Geukeni, na kuziacha njia zenu mbaya, mkazishike amri zangu na hukumu zangu, sawasawa na ile sheria yote niliyowaamuru baba zenu, nikawapelekea kwa kinywa cha manabii watumishi wangu. Walakini hawakutaka kusikia.” (2 Fal.17:13, 14) Ijapokuwa hawakusikiliza, manabii kama Isaya, Yeremia na Mika walitumikia makumi ya miaka kwa uaminifu. Walitaka sana kuona wananchi wenzao wakiwa na hali njema, maana walifahamu kwamba wenye kuitikia maonyo yao wangeokoka.
10. Manabii walipatwa na mambo ya namna gani wakati wa utawala wa Mfalme Ahabu?
10 Manabii walilazimika kutatua matatizo mengine kwa subira, licha ya kutosikilizwa na watu kwa ujumla. Wengi walitukanwa, wakatendwa vibaya miilini mwao na hata wakauawa. Kwa mfano, wakati wa Mfalme Ahabu Mwisraeli, manabii wote wa Yehova walioweza kukamatwa na Yezebeli mwabudu Baali, aliyekuwa malkia wa mfalme, waliuawa. Wengine mia moja walisaidiwa na Obadia mcha Mungu wakaokoka kwa kujificha mapangoni. (1 Fal. 18:4, 13) Wakati uo huo, Yehova alimlinda nabii wake Eliya asiingie mikononi mwa Ahabu, kwa sababu alikusudia kumpa kazi fulani. (1 Fal. 18:10-12) Lakini Yehova Mungu alimwagiza arudi mle mle nchini aendelee na kazi yake ya unabii. (l Fal. 19:9, 15-18) Wakati mwingine Mfalme Ahabu aliagiza nabii Mikaya wa Yehova atiwe gerezani na kupewa chakula na maji machache tu. Kwa sababu gani? Kwa sababu Mikaya alikuwa ameeleza neno la Yehova kwa njia ya kweli.—1 Fal. 22:26, 27.
11. Yeremia alipatwa na mabaya gani wakati wa miaka yake mingi ya kutoa unabii?
11 Nabii mwingine aliyevumilia mengi ni Yeremia. Watu wa mji wa kwao mwenyewe, Anathothi, walitisha kumwua. (Yer. 11:21) Wakati mmoja kundi la watu wenye ghasia, kutia na makuhani na manabii wa uongo, walimkamata nabii wakatisha kumwua. (Yer. 26:8-11) Biblia yasema kwamba ‘alipigwa’ na Pashuri, msimamizi mkuu wa hekalu. Basi pengine hilo lamaanisha kwamba Pashuri aliagiza watu wampige nabii. Ikiwa mkuu huyo aliwaongoza watu hao wengine wamtende vibaya Yeremia, bila shaka walipata ushujaa wa kumfanyia nabii mizaha, dhihaka na matusi. Halafu, Yeremia alifungwa pingu kama mhalifu usiku kucha. (Yer. 20:2, 3, 7, 8) Alikamatwa kwa kushtakiwa uongo kwamba alikuwa amejiunga na Wakaldayo, ‘akatiwa gerezani’ katika hali mbaya sana hata maisha yake yakawa hatarini. Alimsihi Mfalme Sedekia, naye akaagiza atiwe kizuizini katika Ua wa Mlinzi. (Yer. 37:11-16, 20, 21) Baadaye, Sedekia alikubali wakuu wamchukue Yeremia. Wakuu hao walijaribu kumwua nabii kwa kumtupa katika birika la kinamasi (matope mororo).—Yer. 38:5, 6.
12. Yeremia 38:20 na 8:21–9:1 yaeleza kwamba Yeremia alionyeshaje subira?
12 Yeremia kweli alitendwa maovu mengi na wananchi wenzake. Lakini aliendelea kusubiri, asiwaghadhibikie. Kwa mfano, baada ya Mfalme Sedekia kumtia mikononi mwa wakuu waliotaka kumwua, nabii alihangaikia hali njema ya mfalme huyo dhaifu. Yeremia alimsihi hivi: “Uitii sauti ya [Yehova] katika hayo ninayokuambia; ndivyo itakavyokufaa, na nafsi yako utaishi.” (Yer. 38:20) Kabla ya hapo, wakati Yeremia alipokuwa akifikiria hukumu yenye kuogofya ambayo ingeipata Yuda na Yerusalemu, alihuzunika, hakutaka kisasi. Alisema: “Kwa sababu ya maumivu ya binti ya watu wangu nimeumia mimi; nimevaa kaniki; ushangao umenishika. Je! hapana zeri katika Gileadi? huko hakuna tabibu? mbona, basi haijarejea afya ya binti ya watu wangu? Laiti kichwa changu kingekuwa maji, na macho yangu kuwa chemchemi ya machozi, ili nipate kulia mchana na usiku kwa ajili yao waliouawa wa binti ya watu wangu!” (Yer. 8:21–9:1) Lo! jinsi Yeremia alivyowasubiri na kuwapenda watu wake, Waisraeli!
13. Ni nini linaloonyesha kwamba manabii walihuzunishwa na hali walizoona? (Yer. 5:3, 4)
13 Walakini, tusisahau kamwe kwamba Yeremia na manabii wengine waaminifu waliona udhalimu mwingi sana na uonezi uliokuwa ukiendeshwa nchini. Walitaka sana mambo hayo yaondolewe. Kwa mfano, nabii Habakuki alipaza sauti akasema: “Mbona wanionyesha uovu, na kunitazamisha ukaidi? Maana uharibifu na udhalimu u mbele yangu; kuna ugomvi, na mashindano yatokea. Kwa sababu hiyo sheria imelegea, wala hukumu haipatikani; kwa maana watu wabaya huwazunguka wenye haki; kwa sababu hiyo hukumu ikipatikana imepotoka.”—Hab. 1:3, 4.
14. Ingawa manabii waaminifu walitaka sana hali mbaya ziondolewe, hawakufanya nini kwa habari ya Yehova na ujumbe wake? (Yer. 20:9; Mik. 3:8)
14 Hata hivyo, manabii waaminifu hawakuacha tamaa zao za kutaka faraja ziwazuie wasimsubiri Yehova wala ziwazuie wasitangaze ujumbe wake. Maadamu Yehova alikuwa na kusudi la kusubiri, wao walikuwa na nia ya kushutumiwa walipokuwa wakiutangaza ujumbe wake kwa kusema: “Ghairini, ghairini, mkaache njia zenu mbaya; mbona mnataka kufa, Enyi nyumba ya Israeli?”—Eze. 33:11.
TUCHOCHEWE NA MIFANO MYEMA YA WENYE SUBIRA TUCHUKUE HATUA
15. Kwa nini sisi tuna sababu kubwa zaidi ya kusubiri kuliko manabii Waebrania?
15 Hakika, ikiwa manabii Waebrania wa zamani waliweza kusubiri sana hivyo walipokabiliwa na magumu makubwa, sisi tuna sababu kubwa zaidi ya kusubiri. Kwa sababu gani? Kwa sababu sisi tuna mengi zaidi kuliko wao. Manabii walikuwa wakimtazamia Masihi kwa imani, lakini walijua wasingekuwa hai wakati angekuja. Yesu Kristo aliambia Wayahudi hivi: “Amin, nawaambia, Manabii wengi na wenye haki walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi, wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi, wasiyasikie.” (Mt. 13:17) Mambo mengi ambayo manabii walikuwa wakingojea kwa imani yalitimizwa karne nyingi zilizopita. Tena, wengi wanaoishi leo wamejionea wenyewe unabii mwingine ukitimizwa. (Ufu. 6:1-8; 17:8) Kwa kutoa uhai wake uwe dhabihu, Yesu Kristo alihakikisha kabisa kwamba ahadi zote za Mungu zitatimizwa. (2 Kor. 1:20, 21) Kila siku twaona ushuhuda wenye kuonyesha kwamba tunaishi “wakati wa mwisho.” (Dan. 11:40-43; 12:1, 4; Mt. 24:7-14) Kwa hiyo, Yesu atutia moyo hivi: “Changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia.” (Luka 21:28) Naam, karibuni Mwana wa Mungu aliye “MFALME WA WAFALME, NA BWANA WA MABWANA” atachukulia wasiomcha Mungu hatua, aondoe taabu zote na uonezi.—Ufu. 19:11-21.
16. Twaweza kuonyeshaje kwamba twathamini vile Yehova anavyotusubiri?
16 Je! haitupasi tuisubiri siku kuu hiyo, hasa kwa sababu i karibu sana? Je! haitupasi tutake kusaidia wengi iwezekanavyo waijue njia ya Mungu ya wokovu? Na je! haitupasi kuwa wenye nia ya kusubiri watu wanapotukosea? Ikiwa kweli twathamini kwamba subira ya Mungu imetufanyizia wokovu, tutachochewa mioyoni tufanye hivyo.
TUNDA LENYE THAMANI NYINGI LA SUBIRA
17. Ni mfano gani uliomo katika Yakobo 5:7, 8 unaoonyesha kwamba ni lazima kusubiri ndipo tuweze kuona matunda mema?
17 Twaweza kupata matunda mema tukiendelea kuonyesha subira kwa kuiga manabii waaminifu. Hiyo yaonekana kutokana na aliyoandika mwanafunzi Yakobo: “Kwa hiyo ndugu, vumilieni, hata kuja kwake Bwana. Tazama, mkulima hungoja mazao ya nchi yaliyo ya thamani, huvumilia kwa ajili yake hata yatakapopata mvua ya kwanza na ya mwisho. Nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo yenu.”—Yak. 5:7, 8.
18. Ingawa mkulima hawezi kuharakisha mvua wala ukuzi wa mazao, aweza kufanya nini akitazamia mavuno?
18 Mkulima hawezi kuharakisha mvua wala ukuzi wa mazao yake. Aweza kutimiza kazi yake kwa bidii akitayarisha udongo, kupanda na kupalilia shamba lililolimwa. Lakini hana uwezo wa kunyesha mvua, wala hawezi kubadili kawaida zilizowekwa na Muumba kuhusu ukuzi wa mazao yake. Kungojea kwake katika hali asizoweza kubadili, kungojea kupatana na kawaida za Yehova, kwaitwa ‘kuvumilia’ (kusubiri). Mwishowe, mkulima aendeleapo kufanya awezavyo, mimea inakua na mazao yanapatikana.
19. Subira yahusikaje katika kuzaa matunda, yaani, wanafunzi wa kweli?
19 Ndivyo ilivyo kuhusu Wakristo wa kweli leo. Daraka letu ni kutangazia wengine “habari njema” na kufundisha wanaopendezwa Neno la Mungu. (1 Kor. 9:16; Mt. 28:19, 20) Lakini, hatuwezi kuzaa wala kuharakisha ukuzi wa kiroho kwa werevu wetu wala kwa kujitungia njia zetu. Lazima tumngojee Yehova huku tukitimiza fungu letu kwa subira, kupatana kabisa na Neno lake. Mtume Paulo alionyesha wazi hilo alipoandika: “Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye. Basi yeye apandaye, na yeye atiaye maji ni wamoja, lakini kila mtu atapata thawabu yake mwenyewe sawasawa na taabu yake mwenyewe. Maana sisi tu wafanya kazi pamoja na Mungu.” (1 Kor. 3:6-9) Yehova Mungu hatakosa kutimiza fungu lake. Kwa hiyo, na tufanye kazi naye kwa uaminifu, hivyo tuonyeshe kwamba twathamini vile Yehova anavyotusubiri. Jinsi tutakavyofurahi kuona tulivyopanda na kunywesha maji vikikomaa Kikristo! Naam, yatakuwako mazao, yaani, wanafunzi wa kweli wa Yesu Kristo.
[Picha katika ukurasa wa 300]
Ingawa nabii Yeremia alitaabishwa sana na Waisraeli wenzake, aliendelea kuonyesha subira