Jinsi Waisraeli Walivyomjaribu Yehova Jangwani
“MSIMJARlBU [Yehova], Mungu wenu,” (Kum. 6:16) Maneno hayo yalisemwa na Musa kwa watu mwishoni mwa kipindi chao cha miaka 40 cha kukaa jangwani. Uzito wa onyo hilo unaonekana wazi tunapokumbuka namna Waisraeli walivyomjaribu Yehova mara nyingi wakati wa safari yao kutoka Mlima Sinai katika nyanda za Moabu, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Hesabu. Wakristo leo wanaweza kufaidika kwa kurudia habari hii, ambayo, hasa, iliandikwa kwa sababu hiyo.—Rum. 15:4; 1 Kor. 10:11.
Kitabu cha Hesabu kilipata jina lake kutokana na tafsiri ya Kigiriki ya Septuagint ya Maandiko ya Kiebrania kupitia kwa tafsiri ya Kilatini (Kirumi) ya Vulgate. Linatokana na uhakika wa kwamba katika Hesabu, sura ya kwanza hadi ya nne na ya 26, tunapata kuhesabiwa kwa watu wa Israeli. Lakini, kwa kufaa hata zaidi, ni mojawapo majina walichokipa Wayahudi, yaani, “jangwani,” msingi wake ukiwa neno la nne katika sura ya kwanza katika Kiebrania.
Ni nani aliyeandika kitabu cha Hesabu? Kuna ushuhuda mwingi katika kitabu chenyewe na katika Maandiko mengine ukionyesha kwamba Musa ndiye aliyekiandika. Tangu zamani sana ilikubaliwa kwamba ndiye aliyekiandika na Wayahudi, na baadaye na Wakristo wa kwanza.
WALIPOKUWA KATIKA MLIMA SINAI
Waisraeli walikuwa wamekuwa chini wa Mlima Sinai kama mwaka mmoja hivi wakati Musa alipowahesabu watu wenye kwenda vitani wa Israeli. Hesabu yao ilikuwa 603,550, ikionyesha kwamba idadi kamili ya taifa hilo ilikuwa kama milioni tatu. Musa aligawia kila kabila sehemu yake katika kambi, kabila la Walawi likiwa katikati pamoja na hema ya kukutanikia. Pia alitoa maagizo juu ya utaratibu wa mwendo katika safari yao, na kwa kweli ni jambo la kupendeza, kwa sababu ya historia ya baadaye ya Israeli, kwamba kabila la Yuda ndilo lililokuwa na watu wengi zaidi na ndilo liliongoza.
Kwa amri ya Mungu Musa alitoa maagizo ya wazi kuhusu kazi za vikundi mbalimbali vya kabila la Walawi. Yehova alichukua kabila hili badala ya wazaliwa wa kwanza ambao walikuwa mali yake kwa kuwa alikuwa amewahifadhi hai wakati alipowaangamiza wazaliwa wa kwanza wa Misri.a
Pia Musa alipokea maagizo juu ya kupiga kambi na kuvunja kambi pamoja na habari nyingine zinazohusu tengenezo. Katika mahali mbalimbali pana sheria juu ya visa vinavyohusu wivu unaotokana na kutokuaminika kwa mke na ile inayohusu nadhiri ya Wanaziri, iliyohusu kuachilia nywele za mtu zikue na kutokula na/au kunywa mazao ya mzabibu. Pia zawadi zilizotolewa na wakuu wa makabila mbalimbali wakati hema ya kukutanikia ilipokuwa ikimalizika kujengwa zimetiwa ndani ya habari hii, ikionyesha namna wakuu hawa walivyokuwa na mali nyingi.
Katika sehemu hii ya kwanza ya kitabu hiki inapatikana baraka inayojulikana sana ambayo Mungu alimwamuru Musa awabariki watu wake: “[Yehova] akubarikie, na kukulinda! [Yehova] akuangazie nuru za uso wake, na kukufadhili; [Yehova] akuinulie uso wake, na kukupa amani.”—Hes. 6:24-26.
SAFARI ZA WAISRAELI JANGWANI
Ilikuwa siku ya ishirini ya mwezi wa pili wa mwaka wa pili baada ya kutoka Misri wakati wingi lililokuwa likikaa juu ya hema lilipoanza kuondoka, likionyesha kwamba Israeli ataanza kusafiri. Wakati wa usiku nguzo ya moto ndiyo iliyokuwa ikikaa juu ya hema na kuwaongoza. Israeli alipovunja kambi, Musa alikuwa akisema: “Inuka Ee [Yehova], adui zako na watawanyike; na wakimbie mbele zako hao wakuchukiao.” Na wakati wingu liliposimama, Musa alikuwa akisema: “Uwarudie maelfu kumi ya maelfu ya Israeli.”—Hes. 10:35, 36.
Mwanzoni mwa safari yao jangwani, Waisraeli walijulishwa uzito wa kumjaribu Yehova. Jinsi gani? Kwa sababu mara tu walipovunja kambi watu “walikuwa kama wanung’unikao, wakinena maovu masikioni mwa [Yehova].” (Hes. 11:1) Hii ilimkasirisha sana hata akapeleka moto, ambao ulianza kuwateketeza wengine wa Waisraeli katika mwisho wa kambi. Musa aliwaombea, na Yehova akamsilikiza akakomesha moto huo.—Hes. 11:2.
Kwa kuonekana, baada tu ya hayo mkutano uliochangamana nao uliotoka Misri na Waisraeli ulimjaribu Yehova. Kwa njia gani? Kwa kunung’unika na kulalamika kwa kukosa nyama, samaki, na mboga kama vile matango, matikiti, vitunguu na vitunguu saumu vya kula, lakini wakilazimika kuishi kwa kula mana, chakula kitamu kilichofanana na chakula cha nafaka kilichotolewa kwa mwujiza kila siku isipokuwa siku ya Sabato. Hii ilimfadhaisha Musa sana hata akamlalamikia Yehova hivi: “Je! ni mimi niliyewatungisha mimba watu hawa wote . . . hata ikawa wewe kuniambia, Haya, wachukue kifuani mwako?” Katika kujibu, Yehova alimhakikishia Musa kwamba angewapa Waisraeli nyama. Musa aliuliza ingekuwaje hivyo, akamfanya Yehova ajibu: “Je! mkono wa [Yehova] umepungua urefu wake?” Basi, haukuwa umepungua urefu wake kwa maana Yehova alileta kundi kubwa la kware. Walakini, kwa sababu ya manung’uniko na pupa yao, Yehova aliwapelekea “pigo kuu mno.” Wakajulishwa tena uzito wa kumjaribu Yehova.—Hes. 11:4-33.
Halafu, walikuwa Haruni na Miriamu ndugu na dada wa Musa waliomjaribu Yehova kwa kunung’unikia mamlaka ya Musa. Hii ilimkasirisha Yehova sana, hata akawaonyesha cheo na pendeleo la pekee alilokuwa nalo Musa, lakini akampiga Miriamu kwa ukoma. Musa alimwombea dada yake na hivyo Mungu akafupiza muda wa kufungiwa peke yake ukawa siku saba tu.—Hes. 12:1-15.
Kwa wazi, kwa kutaka sana kujua jinsi Nchi ya Ahadi ilivyokuwa watu wa Musa walimshawishi atume wanaume 12, mmoja kutoka kila kabila la makabila 12, wakapeleleze nchi hiyo. (Kum. 1:22, 23) Walirudi baada ya siku 40 wakiwa na matunda matamu sana, yakishuhudia kwamba Nchi ya Ahadi kweli kweli ilikuwa “yenye wingi wa maziwa na asali.” (Hes. 13:23-27) Walakini, kumi kati ya wapelelezi hao walionyesha watu wa nchi hiyo kuwa wakubwa mno na miji yake kuwa yenye kujengwa kwa nguvu sana hivi kwamba waliwavunja moyo Waisraeli sana hata wakataka kurudia Misri. Wapelelezi wawili waaminifu Yoshua na Kalebu, walishindwa walipojaribu kuzungumza nao na kuwasihi wamtumaini Yehova. Walakini, wakati watu walipozungumza juu ya kuwapiga mawe Musa na Haruni na hao wapelelezi wawili waaminifu, Yehova Mungu aliingilia jambo hilo na kujulisha kwamba angeangamiza taifa hilo lote na kufanyiza jingine kutoka kwa Musa. Lakini, Musa aliwaombea watu wake kama alivyokuwa amefanya hapo mbele, akimkumbusha Yehova kwamba sifa na jina lake zilihusika na yale ambayo yangewapata Waisraeli. Yehova alighairi lakini akaamuru kwamba watu hao wangetanga-tanga jangwani miaka 40, mwaka mmoja kwa kila siku wale wapelelezi waliyopeleleza nchi, mpaka wale wote waliokuwa na umri wa miaka ishirini na zaidi wafe. Wasiohusika na jambo hili walikuwa Yoshua na Kalebu na kabila la Walawi ambalo halikujiunga na uasi huo. Wakiendelea kutokujifunza somo la kutokumjaribu Yehova, Waisraeli walijaribu kuivamia Nchi ya Ahadi ingawa Musa aliwaamuru wasifanye hivyo. Walishindwa vibaya sana—Hes. 14:39-45.
Baada ya kuandika mambo yaliyohusiana na ibada ya Waisraeli, Musa anasema juu ya Waisraeli fulani—Kora, Dathan na Abiramu—waliomjaribu Yehova kwa kumwasi Musa. Yehova alimwangamiza Kora kwa moto na wengine kwa kufanya ardhi ifunuke, ikiwameza waasi hao pamoja na jamaa zao na mali zao.
Badala ya kujifunza jambo lo lote kutokana na wonyesho huu wenye kuogofya wa hukumu za Yehova, Waisraeli walizinung’unikia na kuzilalamikia. Kwa kuendelea kumjaribu Yehova hivyo aliwapelekea pigo lililowaaangamiza Waisraeli 14,700. Ndipo, ili aonyeshe kabisa kwamba alikuwa amelichagua kabila la Walawi kama lilivyowakilishwa na Musa na Haruni, Yehova aliwafanya kila mmoja wa wakuu wa makabila walete fimbo kwenye hema ziletwe mbele za Yehova. Siku iliyofuata Yehova alionyesha ni kabila gani alilokuwa amelichagua kwa kufanya fimbo ya Haruni ichipuke, na kuchanua maua na hata kuzaa malozi mabivu.—Hes. 16:1—17:11.
Baada ya kuandika maagizo ya Yehova kuhusu kazi za makuhani na njia zao za kupata riziki na kuhusu mipango ya kuwatakasa watu na unajisi, Musa anaeleza juu ya wakati mwingine Waisraeli walipomjaribu Yehova. Wakati huu walinung’unika na kulalamika kwa sababu hawakuwa na maji. Yehova alitoa maji kwa mwujiza. Lakini kwa sababu Musa alipatwa na hasira na akakosa kumtukuza Yehova kwa maji, Mungu aliamuru kwamba Musa na Haruni hawataingia katika Nchi ya Ahadi. Msiba mkubwa namna gani!—Hes. 20:1-13.
Alipoondoka Kadeshi, Israeli alifika Mlima Hori, alipofia Haruni na mwanawe Eleazari alitawazwa kama kuhani mkuu. Waisraeli walipoendelea kutanga-tanga jangwani walinung’unika tena juu ya kuchoshwa na safari zao na juu ya chakula cha mana ambacho waliishi kwacho. Wakati huu Yehova aliwaadhibu kwa kuwatumia pigo la nyoka wabaya sana. Watu wakatubu. Musa akawaombea, naye Yehova akamwagiza Musa afanyize nyoka wa shaba na kuiweka juu ya mti. Wale wote walioumwa na nyoka na kutazama mti huo walipona badala ya kufa.—Hes. 21:4-9.
KATIKA NYANDA ZA MOABU
Baada ya kusafiri zaidi na kuwashinda wafalme wawili waliokuja kupigana vita nao, Sihoni na Ogu, Israeli alifika katika nyanda za Moabu. Kwa kuwaogopa sana Israeli, Balaki, mfalme wa Moabu, alijaribu mara nyingi bila kufaulu kumfanya nabii Balaamu amlaani Israeli. (Hes. 22:1–24:25) Hata hivyo, tunajifunza kutokana na Hesabu 31:15, 16 kwamba Balaam aliwafanya Waisraeli washawishwe na wanawake wa Moabu wenye kuabudu Baali washiriki katika kufanya uasherati na ibada ya sanamu. Kwa sababu ya Israeli kumjaribu hivi, Mungu Aliye Juu Zaidi aliwaangamiza Waisraeli 24,000 kabla Finehasi, mwana wa kuhani mkuu Eleazari, hajazuia pigo hilo kwa kumwua mwanamume Mwisraeli pamoja na mwanamke Mmidiani aliyekuwa akifanya ngono naye.—Hes. 25:1-18
Baada ya kuwahesabu tena wanaume wa Israeli na kuweka kiolezo kuhusu haki za urithi za mabinti, Musa alipewa pendeleo la kuitazama Nchi ya Ahadi akiwa juu ya Mlima Abarimu. Ndipo, kwa amri ya Mungu, Musa akamwagiza Yoshua achukue mahali pake. (Hes. 27:1-23) Baada ya kutoa mambo mengi juu ya aina ya matoleo aliyotaka Yehova atolewe kila siku, kila juma, kila mwezi, na kila mwaka, na kuagiza juu ya kuweka nadhiri, Musa anaandika juu ya kisasi Israeli alichojitwalia juu ya Wamidiani kwa kuwafanya Waisraeli wamtende Yehova dhambi.—Hes. 28:1—31:54.
Wakati ulikuwa unakaribia wa Israeli avuke Yordani akajitwalie Nchi ya Ahadi. Lakini, Makabila ya Reubeni, Gad na nusu ya kabila la Manase waliomba waruhusiwe wakae upande wa mashariki wa Yordani. Kwa nini? Kwa sababu walikuwa na makundi makubwa, na nchi hii ilifaa sana ya kulisha mifugo. Walikubaliwa hivyo kukiwa na sharti la kwamba watasaidia makabila yale mengine tisa na nusu waitiishe nchi iliyokuwa magharibi ya Yordani.
Ni mara ngapi Israeli alihama kutoka mahali pamoja kwenda mahali pengine wakati huo wa miaka 40? Mara 40. (Hes. 33:1-49) Kitabu hicho kinapokaribia mwisho wake, kinaeleza juu ya amri za Yehova za kumaliza kabisa ibada ya uongo katika nchi ya Kanaani; pia juu ya kuweka mipaka ya Nchi ya Ahadi pamoja na jinsi alivyowaweka wakuu kutoka katika kila kabila wawasaidie Yoshua na Eleazari kuhani mkuu katika kugawa nchi kwa kila kabila. Zaidi ya hayo, maagizo yalitolewa kuhusu ile miji 40 ambayo ingepewa kwa Walawi, kwa kuwa wao hawakuwa na urithi katika nchi hiyo, pamoja na miji sita ya Walawi ambayo ingekuwa miji ya makimbilio kwa wauaji wasiokusudia. Sheria za Yehova kuhusu wauaji wa kukusudia na wasiokusudia zilielezwa wazi. Kitabu hicho kinamalizika kwa kutoa amri kuhusu kuolewa kwa warithi wa kike.
Kwa kweli kitabu cha Hesabu kinaonyesha uzito wa kumjaribu Yehova. Hata ingawa taifa la Israeli liliingia Nchi ya Ahadi, kwa kuitimiza ahadi ya Yehova, hakuna wo wote wa wale waliotoka Misri lakini wakaasi walioiingia. Paulo aliwaonya Wakristo vizuri wasifuate mfano wa Waisraeli hao. (1 Kor. 10:8-11) Kama vile “kundi kubwa la watu waliochangamana nao” lilivyoungana na Israeli kutoka Misri, na hatimaye likaingia Nchi ya Ahadi, ndivyo ilivyo leo. “Kundi kubwa” likiwa na tumaini la kidunia limetoka katika Misri ya kisasa, ulimwengu huu wa sasa, na wamejiunga na Waisraeli wa kiroho, wafuasi wa Yesu Kristo waliotiwa mafuta katika safari yao ya kuingia katika taratibu mpya ya mambo. (Ufu. 7:9-14; 11:8; Yohana 15:19) Ikiwa tunatamani sana kuwa na tumaini la kuokoka kuangamizwa kwa hii taratibu mbovu ya mambo iliyopo katika dhiki kuu ijayo, tutahitaji kujiangalia tusije tukamjaribu Yehova Mungu kamwe, kwa kukosa imani.—Zef. 2:3.
[Maelezo ya Chini]
a Ili makabila yaendelee kuwa kumi na mawili kabila la Yusufu liligawanywa katika makabila ya wanawe wawili, Efraimu na Manase.