Yonathani—“Mwanamume Mmoja Katika Elfu”
MFALME Sulemani mwenye hekima alisema: “Mwanamume mmoja katika elfu nimemwona.” (Mhubiri 7:28) Hiyo inaonyesha ni jambo haba kumwona mtu anayefaa. Ni wachache wanaotokeza wakiwa na adili bora. Mtu mmoja aliyetokeza hivyo alikuwa Yonathani (Yonatana), mwana wa Mfalme Sauli. Yeye alikuwa shujaa, mshikamanifu na asiye na choyo. Kama kuna mtu awaye yote ambaye angekuwa na haki ya kushindwa na maono ya wivu, uadui au ya kuwa na kijicho, angalikuwa ni Yonathani (Yonatana). Walakini yeye alionyesha shauku nyingi na ushikamanifu kwa mtu yule yule ambaye watu wenye kukosa wema wangemwona kuwa tisho baya sana la cheo chao.
Mapema katika utawala wa babake, Yonathani alijipatia sifa kuwa shujaa hodari. Akiwa na wanaume elfu moja wasio na silaha za kutosha, alishinda ngome ya askari Wafilisti katika Geba. (1 Samweli 13:1-3) Wakati huo lazima Yonathani awe alikuwa mwenye umri wa miaka angaa 20, kwa kuwa hicho ndicho kilichokuwa kiwango cha chini cha umri kwa askari-jeshi Waisraeli.—Hesabu 1:3.
Baadaye, kwa msaada wa Mungu, Yonathani pamoja na mchukua-silaha wake aliua adui Wafilisti karibu 20. Tendo hilo lilitolea Waisraeli njia ya kuwashinda adui zao. Wakati wa shughuli hiyo, pasipo kujua Yonathani alipuza kiapo cha ujinga cha babaye. Ili Sauli atekeleze kikamilifu kiapo chake, ilihitaji Yonathani auawe. Yonathani hakujikunyata kwa woga bali alimwambia hivi babaye: “Tazama, imenipasa kufa.” Hata hivyo, watu walimkomboa Yonathani kwa kuwa walitambua kwamba Yehova alikuwa amekuwa pamoja naye.—1 Samweli 14:1-45.
Ilikuwa karibu miaka 20 baadaye Daudi alipoliua jitu la Ufilisti, Goliathi. Tendo la ushujaa la Daudi, ambalo lilitekelezwa kwa imani kamili kwa uwezo wa Yehova wa kuokoa, liliugusa sana moyo wa Yonathani. Biblia inaripoti hivi: “Nafsi ya Yonatana iliambatana na nafsi ya Daudi, Yonatana akamupenda kama nafsi yake mwenyewe.” (1 Samweli 18:1, ZSB) Ukiwa wonyesho wa urafiki wake, Yonathani alimpa Daudi mavazi yake, upanga wake, upinde wake na mshipi wake.—1 Samweli 18:4.
Baadaye Daudi alipoonyesha kuwa ni shujaa kwa kuongoza vikosi vya Israeli kwenye pigano pamoja na Wafilisti, wanawake waliwalaki washindi waliokuwa wakirudi kwa wimbo na kwa dansi. Waliimba hivi: “Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake.” (1 Samweli 18:5-7) Jambo hilo lilimchochea Sauli awe na wivu mwingi zaidi, naye akaanza kumtuhumu (kumshuku) Daudi sana. Aliposhindwa katika jaribio la kumwua Daudi kwa mkuki, baadaye Sauli alikubali kumpa Mikali bintiye ili waoane, mradi tu Daudi atoe uthibitisho wa kwamba amewaua Wafilisti adui 100. Sauli alikuwa anasadiki kabisa kwamba Daudi akifanya jambo hilo angeangukia mikono ya adui. Hata hivyo, Daudi alirudi akiwa na govi 200 za Wafilisti—uthibitisho wa kwamba alikuwa ameua hesabu hiyo. Jambo hilo lilifanya Sauli azidi kumwogopa Daudi na kumchukia.—1 Samweli 18:8-29.
Walakini Yonathani hakuruhusu chuki yenye wivu ya babaye iharibu urafiki wake pamoja na Daudi. Sauli aliposema wazi tamaa yake ya kutaka Daudi auawe, Yonathani aliingilia jambo hilo na akafaulu kumfanya babaye aahidi hatamwua rafiki yake. Hata hivyo, baadaye, Daudi alilazimishwa akimbie asiuawe, kwa kuwa kwa mara nyingine Sauli alimtupia mkuki. Vilevile mfalme huyo aliwapeleka wanaume wakalinde nyumbani mwa Daudi wakati wa usiku, wakiwa na agizo la kumwua asubuhi. Usiku huo Daudi alifaulu kutoroka kupitia dirisha moja la nyumba yake.—1 Samweli 19:1-12.
Hapo baadaye Yonathani alishirikiana na Daudi katika jitihada ya kuamua jinsi babaye Yonathani alivyokuwa anamwona rafikiye. Sauli alighadhibika na akamkemea mwanawe kwa maneno haya: “Wewe, mwana wa mke mkaidi, asi, je! mimi sijui ya kuwa umemchagua huyo mwana Yese, kwa aibu yako mwenyewe, na kwa aibu ya uchi wa mama yako. Maana wakati mwana wa Yese akiwa hai juu ya nchi, wewe hutafanikiwa, wala ufalme wako. Basi, sasa peleka, ukamlete kwangu maana hakika yake atakufa huyu.” Yonathani alipopinga, babaye aliyeghadhibika alimtupia mkuki.—1 Samweli 20:1-33.
Baada ya hayo, Yonathani alikutana na Daudi, katika mahali walipokuwa wametangulia kupanga. Wanaume hao wawili walithibitisha kwa mara nyingine urafiki wao na ushikamanifu wao. (1 Samweli 20:35-42) Ni jambo la kutokeza hakika kwamba urafiki huo ulikuwapo na uliendelea. Yonathani ndiye aliyeelekea kuwa mrithi wa kiti cha enzi na alijua kwamba hatimaye ufalme ungekuwa mikononi mwa Daudi. Pamoja na hayo, yeye alikuwa mkubwa wa Daudi kwa karibu miaka 30. Hata hivyo Yonathani alifurahia mafanikio ya Daudi na kulia pamoja naye katika mateso yake. Bila shaka urafiki wa Yonathani ulimsaidia Daudi aendeleze heshima iliyomstahili mfalme ili asitumie nafasi za kumdhuru. Sauli alipokuwa akimfuatia Daudi pasipo huruma, Yonathani alipata nafasi ya kumtia nguvu rafiki yake. Kuhusu pindi moja, tunasoma hivi: “Ndipo Yonathani, mwana wa Sauli, akainuka, akamwendea Daudi huko Horeshi, akamtia nguvu mkono wake katika Mungu. Akamwambia, Usiogope, kwa maana mkono wa Sauli, babangu, hautakupata; na wewe utakuwa mfalme juu ya Israeli; na mimi nitakuwa wa pili wako; ndivyo ajuavyo hata Sauli, babangu.”—1 Samweli 23:16, 17.
Yonathani alikuwa mtu bora kama nini kwa kuridhika na kuchukua nafasi ya pili katika ufalme huo! Kujitoa huko kusiko na choyo kuliwezekana kwa sababu Yonathani alimkubali Daudi kuwa chaguo la Yehova la kupewa ufalme na alimpenda kwa ajili ya sifa zake njema.
Hata hivyo, Yonathani hakuwa wa pili katika ufalme huo bali alikufa pamoja na babaye kwenye pigano. (1 Samweli 31:2) Kifo cha Sauli na Yonathani kilimfanya Daudi atokeze wimbo wa maombolezo, unaoitwa “Ule Upinde.” Hapo kwanza, wimbo huo wa maombolezo ulikuwa sehemu ya mkusanyo wa mashairi, nyimbo na maandishi mengine yaliyojumuishwa kuwa kitabu cha Yashari. Halafu “Ule Upinde” uliandikwa katika maandishi yaliyoongozwa na Mungu ya 2 Samweli. Mtungo huo ulipasa kufundishwa wana wa Yuda.—2 Samweli 1:17-27.
Tunapokifikiria kifungo bora sana cha urafiki kilichokuwa kati ya Daudi na Yonathani, tunaweza kuthamini mara moja sababu ya Daudi kusema kama alivyosema katika “Ule Upinde.” Yeye aliomboleza hivi: “Nimesikitika kwa ajili yako, Yonathani, ndugu yangu, ulikuwa ukinipendeza sana; upendo wako kwangu ulikuwa wa ajabu, kupita upendo wa wanawake.” (2 Samweli 1:26) Kweli kweli, Yonathani alikuwa “mwanamume mmoja katika elfu.”