“Yule Kahaba Mkuu” Akaribia Kuuawa Kwake
“Hao watamchukia yule kahaba, nao watamfanya kuwa mkiwa na uchi, watamla nyama yake, watamteketeza kabisa kwa moto.”—Ufu. 17:16.
1, 2. Mungu anawapa watumishi wake habari gani, na wa sababu gani?
MUUMBA, Yehova Mungu, anajua kwa usahihi kabisa yale yatakayotukia katika wakati ujao. Yeye Ndiye “[atangazaye] mwisho tangu mwanzo.” (Isa. 46:10) Kwa kuwa yeye ni “mkamilifu wa maarifa,” anayajua mambo yote hata yale madogo madogo juu ya “mwisho” wa hii taratibu ya mambo katika wakati wa “dhiki kubwa” inayokuja. (Ayubu 37:16; Mt. 24:21) Kwa sababu yeye ni Mungu wa upendo, anafunua mambo hata haya madogo madogo ya kutosha kwa wale wanaomtumikia kwa ushikamanifu ili wapate kuarifiwa ifaavyo, wajengwe na kulindwa. Biblia inasema hivi: “Bwana [Yehova] hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.”—Amosi 3:7.
2 Hivyo, Mungu huwapa watumishi wake wanyenyekevu maarifa ya pekee wasiyo nayo wengine. Ni kama vile alivyosema Mtume Paulo: “Wenye kuitawala dunia hii hawaijui hata mmoja . . . lakini Mungu ametufunulia sisi kwa [roho]. Maana [roho] huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu.” (1 Kor. 2:8-10) Wakiwa na maarifa hayo kimbele waliyopewa na Yehova, watumishi wake wametayarishwa—kwa kweli, wameagizwa na Mungu—watangaze ulimwenguni pote onyo la kukaribia kwa mwisho wa taratibu hii, pamoja na ujumbe wenye kufariji wa taratibu mpya.—Mt. 24:14.
3. Je! watumishi wa Yehova watajua wakati ile “dhiki kubwa” imeanza hasa?
3 Kwa kuwa Yehova huwapa watumishi wake washikamanifu maarifa kimbele juu ya mwisho wa hii taratibu mpya, je! hiyo inatia ndani habari itakayowawezesha kufahamu wakati hiyo “dhiki kubwa” imeanza kweli kweli? Ndiyo. Ushuhuda huo ni upi? Inahusiana na kutekelezwa kwa hukumu ya Mungu juu ya yule anayeitwa na Biblia “Babeli Mkuu, mama wa makahaba na machukizo ya nchi.” (Ufunuo 17:5) Na tayari, ndiyo, hivi sasa, mambo fulani yanatukia yanayotayarisha njia ya kutekelezwa kwa hukumu hiyo!
4. Ni kwa sababu gani ni jambo lenye kusaidia kujua yale yaliyoupata Babeli wa kale?
4 Ni nani huyo kahaba wa mfano wa Maandiko? Inaweza kusemwaje kwamba matukio yanayoongoza kwenye uharibifu wake tayari yanatukia? Twaweza kujifunza mengi juu ya mambo hayo kwa kuangalia Babeli mwingine, ile milki ya ulimwengu yenye nguvu ya zaidi ya miaka elfu mbili iliyopita. Yale yaliyoupata Babeli wa kale ni zaidi ya historia tu. Ni ulinganifu wenye kutokeza wa kiunabii wa yale yatakayompata huyo “kahaba mkuu” wa siku zetu.—Ufu. 17:1.
“BABELI MKUBWA” WA KALE
5. Ni kwa sababu gani Nebukadreza alielekea kuwa na sababu ya kujisifu?
5 “[Je!] mji huu sio Babeli mkubwa nilioujenga mimi, uwe kao langu la kifalme, kwa uwezo wa nguvu zangu, ili uwe utukufu wa enzi yangu?” (Dan. 4:30) Ndivyo alivyojisifu mfalme wa Babeli, Nebukadreza, zaidi ya karne sita kabla ya Wakati wa Kawaida. Ilielekea kwamba Nebukadreza alikuwa na sababu nzuri za kujisifu, kwa kuwa Babeli ulikuwa ndio mji wenye nguvu zaidi katika wakati wake, makao makuu ya milki yenye nguvu zaidi ambayo ulimwengu ulikuwa haujapata kuona namna yake kufikia wakati huo. Mji huo uliokuwa mkubwa sana ulielekea kuwa usioweza kushindwa, kwa kuwa ulikuwa umezingirwa kwa kuta mbili zenye nguvu. Vilevile ulikuwa na chanzo cha kujipatia maji chenye kutegemeka— ule Mto Frati—uliopitia katikati ya mji huo. Kandokando ya mto huo, ndani ya mji, kulikuwako kuta zenye nguvu zenye malango ambayo yangeweza kufungwa kuzuia ye yote asiyetakikana asiingie.
6. Babeli ulijulikana sana kwa sababu ya kitu gani?
6 Ijapokuwa Babeli ulikuwa na nguvu nyingi za kijeshi, ulijulikana zaidi kwa sababu nyingine: Ulikuwa ndio makao makuu ya ibada ya uongo katika ulimwengu huo wa kale. Inasemekana kwamba mabaki ya zaidi ya mahekalu 53 yamevumbuliwa katika magofu ya mji huo. Kitabu The World Book Encyclopedia chasema hivi: “Hata hivyo, Wababeli hawakuacha miungu ya kale, kwa hiyo idadi ya miungu waliokuwa wakiabudu iliongezeka ikafikia maelfu. Kulikuwako miungu ya kiume na miungu ya kike walinzi kwa kila mji pamoja na miungu iliyofananisha vitu kama vile jua, mwezi, na nyota, hali ya hewa, mazao, mito, na nchi.” Uvutano wa dini ya Babeli ulikuwa mkubwa sana hivi kwamba baada ya wakati kupita hata ulikuwa na matokeo juu ya Jumuiya ya Wakristo. Mpaka hivi leo, imani za dini ya uongo na mazoea ya Babeli ya baada ya Gharika zaweza kuonekana katika karibu dini zote za ulimwengu huu.—Mwa. 11:1-9.
7. (a) Kosa lenye kuiletea Babeli kifo lilikuwa kosa gani? (b) Yehova angefanya nini kwake?
7 Walakini, Babeli wa siku za Nebukadreza ulikuwa na kosa lenye kuleta mauti. Ulikuwa adui mwenye shingo ngumu na wa muda mrefu wa Mungu wa kweli, Yehova, na wa watu wake. Vilevile, ulikuwa na mazoea ya kumwaga damu nyingi isiyo na hatia. Biblia yasema hivi: “Si kwamba Babeli ulisababisha tu kuanguka kwa Israeli, bali pia katika Babeli waliouawa wa dunia yote wameanguka.” (Yer. 51:49, NW) Kwa sababu hiyo, Yehova alisema hivi: “Na Babeli, huo utukufu wa falme, uzuri wa kiburi cha Wakaldayo, utakuwa kama Sodoma na Gomora hapo Mungu alipoiangamiza. . . . Wakati wake u karibu kufika, na siku zake hazitaongezeka. Unabii huo uliandikwa na Isaya wapata mwaka wa 732 K.W.K. (Isa. 13:19-22) Karne moja hivi baadaye, Yeremia alisema hivi: “Kwa sababu ya ghadhabu ya [Yehova] haitakaliwa na mtu, bali itakuwa ukiwa mtupu; kila mtu apitaye karibu na Babeli atashangaa, atazomea kwa sababu ya mapigo yake yote.” Ndiyo, ule “Babeli mkubwa” ulioelekea kutoshindika “[ungekuwa] magofu, makao ya mbwa-mwitu, . . . pasipo mtu wa kukaa huko.”—Yer. 50:13; 51:37.
8. Ni mambo gani mengi yaliyotolewa kuhusu namna ambavyo Babeli ungeanguka?
8 Sasa Babeli ungeangukaje? Yehova aliwapa Isaya na Yeremia baadhi ya mambo ya kujulisha. Isaya aliandika kwamba Yehova ndiye “[aviambiaye] vilindi, Kauka, nami nitaikausha mito yako.” (Isa. 44:27) Isaya aliendelea kusema hivi: “Haya ndiyo [Yehova] amwambiayo Koreshi, masihi wake, ambaye nimemshika mkono wake wa kuume, ili kutiisha mataifa mbele yake, nami nitalegeza viuno vya wafalme; ili kufungua milango mbele yake, hata malango hayatafungwa.” Yeremia alitabiri hivi: “Mashujaa wa Babeli wameacha kupigana. . . . Ushujaa wao umewapungukia; wamekuwa kama wanawake.” (Yer. 51:30) Kwa hiyo mto wenye kulinda Babeli, Frati, “ungekauka”; kiongozi ambaye Yehova alimwita jina muda mrefu kabla hajazaliwa, “Koreshi,” ndiye angekuwa mshindi; malango kandokando ya mto ‘hayangefungwa’; nayo majeshi ya Babeli ‘yangeacha kupigana.’
9. Ni kwa sababu gani sana sana karamu ya Belshaza ilikuwa yenye kumchukiza Yehova?
9 Katika Oktoba 5/6 mwaka 539 K.W.K. unabii huo ulitimizwa barabara. Usiku huo, mfalme wa Babeli mwenye kiburi, Belshaza alifanya karamu kwa ajili ya wakuu elfu moja na wengine. Akiufanya wakati huo kuwa sikukuu ya kidini ili kumkufuru Yehova, alileta vyombo vitakatifu ambavyo Nebukadreza alikuwa ameviteka kutoka katika hekalu huko Yerusalemu katika mwaka 607 K.W.K. Wakitumia vyombo hivyo vilivyokuwa vikitumiwa hapo kwanza na watu wa Mungu katika utumishi wa Yehova, Belshaza na wengine, kutia na wake wa mfalme na masuria, walikunywa kwa kuisifu miungu yao ya uongo.—Dan. 5:1-4.
10. Mwandiko wa mkono uliokuwa juu ya ukuta ulikuwa nini, naye Belshaza alitendaje kwa sababu ya mwandiko huo wa mkono?
10 Hata hivyo, Yehova hangeendelea kudhihakiwa! Wakati ulikuwa umefika wa yeye kuchukua hatua! “Saa iyo hiyo vikatokea vidole vya mkono wa mwanadamu, vikaandika katika chokaa ya ukuta wa nyumba ya enzi ya mfalme, . . . naye mfalme akakiona kitanga cha ule mkono ulioandika.” (Dan. 5:5) Belshaza aliogopeshwa sana na jambo hilo aliloona hivi kwamba “magoti yake yenyewe yalikuwa yakigongana.” (Dan. 5:6, NW) Kwa ujasiri, Danieli akafasiria mfalme mwandiko huo wa mkono kutoka kwa Mungu, akisema: “Mungu ameuhesabu ufalme wako na kuukomesha. . . . Umepimwa katika mizani nawe umeonekana kuwa umepunguka. . . . Ufalme wako umegawanyika, nao wamepewa Wamedi na Waajemi.”—Dan. 5:26-28.
11. Unabii wa Biblia kuhusu Babeli ulitimizwaje kutia na mambo madogo madogo ya unabii huo?
11 Nje ya kuta za Babeli, majeshi ya Kiajemi yakiongozwa na Koreshi Mkuu, yakishirikiana na yale ya Wamedi ya Dario, yaliuzingira mji huo. Huku Wababeli wakijifurahisha karamu yao ya kidini ya uasherati yenye kukufuru Mungu, wakijiona kuwa salama chini ya ulinzi wa miungu yao na nguvu za kijeshi, Koreshi alikuwa akitumia werevu mkubwa wa kivita. Katika upande wa kaskazini wa Babeli, mafundi wake walichimba mtaro ukingoni mwa Mto Frati, wakaugeuza kwingine hivi kwamba maji yake hayakutelemka kuelekea kusini kupitia katikati ya mji huo. Upesi kina cha maji ya mto huo katika na kuzunguka Babeli kilianza kupungua. Baada ya muda mfupi tu, maji yalikuwa yameenda chini sana hivi kwamba majeshi yaliyokuwa yakiongozwa na Koreshi yaliweza kuingia ndani ya mto huo kutoka upande wa kaskazini na wa kusini na kuufuata kuelekea katikati ya Babeli. Jambo la kushangaza ni kwamba, malango yaliyokuwa kandokando ya mto ndani ya mji yalikuwa yameachwa wazi na Wababeli wasiokuwa na habari yo yote au waliokuwa wamelewa. Yakiwa na nguvu nyingi sana, majeshi ya Koreshi yakaingia Babeli. “Usiku uo huo Belshaza, mfalme wa Wakaldayo akauawa.” (Dan. 5:30) “Babeli mkubwa” ukawa umeanguka—katika usiku mmoja tu! Lilikuwa jambo la kushangaza kama nini, wala si kwa Wababeli tu, bali pia kwa mataifa yote yaliyokuwa yakiizunguka! Mwisho wake ulikuwa umefika kama vile tu watumishi wa Yehova walivyokuwa wametabiri. Na baada ya muda kupita Babeli ukaja kuwa “magofu,” “ukiwa mtupu,” “pasipo mtu wa kukaa huko.”
MAANA YAKE KWA SIKU ZETU
12. Mtume Yohana anasema nini juu ya “Babeli Mkuu” katika Ufunuo sura ya 17?
12 Yote hayo yana maana gani kwa siku zetu? Maana kubwa sana. Zaidi ya karne sita baada ya Babeli kuanguka, mtume Yohana aliongozwa kwa roho aandike kitabu cha Ufunuo. Katika kitabu hicho alisema juu ya “Babeli mkuu” mwingine, akamweleza kuwa “mama wa makahaba na machukizo ya nchi.” (Ufu. 17:5) “Ambaye,” akaandika Yohana, “wafalme wa nchi wamezini naye, nao wakaao katika nchi wamelevywa kwa mvinyo ya uasherati wake.”—Ufu. 17:2.
13. (a) Ni kwa sababu gani “Babeli Mkuu” wa kisasa hangeweza kuwa mamlaka nyingine tu ya kisiasa? (b) Ni kwa sababu gani huyo kahaba anaitwa “Babeli Mkuu”?
13 Kwa kuwa wafalme wanasemekana kuwa wanazini naye, inaonekana wazi kwamba huyu “Babeli Mkuu” hawezi kuwa “mfalme” mwingine tu. Kwa kweli anafananisha kitu kile kile kilichomfanya Babeli wa kale kujulikana sana—dini ya uongo. Ndiyo sababu kahaba huyo wa kisasa anachukua jina lile lile la mji huo wa kale. Kwa hakika, mengi ya mafundisho ya kidini ya uongo na mazoea yanayopatikana katika Babeli ya kidini ya kisasa yaweza kufuatiliwa moja kwa moja mpaka Babeli ya kidini ya kale. Hivyo, huyo kahaba “Babeli Mkuu” wa siku zetu anafananisha milki ya dini ya uongo ya ulimwengu ambayo kwa muda wa karne nyingi imefanya uasherati na ulimwengu badala ya kumtumikia Mungu kwa usafi. Vilevile, Ufunuo ukimpa kitambulisho kingine cha kidini, unasema hivi kuhusu yeye: “Kwa kuwa mataifa yote walidanganywa kwa uchawi [dini ya uongo wako].”—Ufu. 18:23.
14. Kuna ufanani gani mwingine kati ya hizo Babeli mbili?
14 Kumbuka kwamba Babeli ya kale ilikuwa adui mwenye shingo ngumu wa Mungu na watu wake, nayo ilimwaga damu kwa wingi sana katika vita vyake vya kujipatia ushindi. Hali moja na hiyo, kwa habari ya Babeli ya kisasa Biblia husema hivi: “Ndani yake ilionekana damu ya manabii, na ya watakatifu, na ya wale wote waliouawa juu ya nchi.” (Ufu. 18:24) Kahaba huyu amekuwa mtesi mkuu wa watu wa Yehova wa kisasa, mashahidi wake. Vilevile, kwa kuunga mkono vita vya mataifa, na kutia watu moyo katika pande zote wauane, ndiye anayeonwa kuwa anasababisha umwagaji wa damu “ya wale wote waliouawa juu ya nchi.”
15. Kahaba huyo atapata uharibifu mikononi mwa nani, nao utaendelea kwa muda gani?
15 Kwa sababu “dhambi zake zimefika hata mbinguni,” hukumu ya Mungu juu ya kahaba huyo itakuja kwa haraka sana. (Ufu. 18:5, 21) Biblia yasema kwamba “mapigo yake yatakuja katika siku moja,” kwa hakika, “katika saa moja”! (Ufu. 18:8, 10) Jambo hilo litalingana na lile lililompata mfano wake, Babeli wa kale, ulioanguka katika usiku mmoja! Naye kahaba huyo atapata uharibifu mkononi mwa nani? Yehova ataruhusu sehemu ya kisiasa ambayo imekuwa ikifanya uasherati pamoja na huyo kahaba iwe chombo cha kuleta uharibifu. “Hao watamchukia yule kahaba, nao watamfanya kuwa mkiwa na uchi, watamla nyama yake, watamteketeza kabisa kwa moto.”—Ufu. 17:16.
16. “Maji” ambayo Babeli wa kisasa anaketi juu yake ni nini, nako kuna ulinganifu gani kuhusu jambo hilo na Babeli wa kale?
16 Kuna ulinganifu mwingine kati ya Babeli wa kale na wa kisasa, nao unahusu namna ya kuharibiwa kwao. Babeli wa kale ulikuwa ukiketi juu ya maji, maji halisi ya Mto Frati. Babeli wa kisasa vilevile “[anaketi] juu ya maji mengi,” wasema Ufunuo 17:1. Ni nini maji hayo? Neno la Mungu lajibu hivi: “Yale maji uliyoyaona, hapo aketipo yule kahaba, ni jamaa na makutano na mataifa na lugha.” (Ufu. 17:15) Angalia kwamba kuangushwa kwa Babeli wa kale kulitokea baada tu ya kupungua kwa maji halisi ya Mto Frati. Je! kuna kupungua kama huko kwa maji (wanadamu) ya mfano kutoka chini ya Babeli wa kisasa? Ndiyo, nako kunafanyika mbele ya macho yetu yenyewe!—Ufu. 16:1, 12.
NAMNA HAYO “MAJI MENGI” YANAVYOPUNGUKA
17. Ni katika njia gani yale “maji” ya mfano yaliyo chini ya huyo kahaba yanapungua?
17 Hayo “maji mengi” ya mfano yaliyo chini ya Babeli wa kisasa yanapungukaje? Katika njia ya kwamba watu milioni nyingi, kutia na makumi ya maelfu ya viongozi wa kidini na wafanya kazi wao, wameacha kuunga mkono dini zao, na kuzipunguzia sana nguvu. Sana sana inakuwa hivyo katika Jumuiya ya Wakristo, ambayo ina hatia zaidi kwa kuwa inadai kuwa inamtumikia Mungu na Kristo. Ijapokuwa nyakati nyingine inatajwa kwamba kuna “kufufuliwa” fulani katika dini chache, na sana sana zile zisizo na maongozi thabiti, mara nyingi hilo linakuwa jambo la juujuu tu. Isipokuwa katika visa vichache tu, maelekeo yanaonekana wazi nayo yaweza kuonwa katika maelezo yanayotolewa katika magazeti ya ulimwengu, kama haya yanayofuata:
“Jambo fulani limeipata Jumuiya ya Wakristo. Vionyesho vyote vinaonyesha kwamba tumeingia katika usiku mrefu, mrefu sana nasi hatutatoka ndani yake . . .
“Kuwapo kwenye matokeo kwa Ukristo na Ukatoliki wa Kirumi katika [mambo] ya jamii kumekwisha toweka. Sisi tunashuhudia kifo cha Ukristo uliotengenezwa kijamii na kisiasa.”—Mwandikaji Mkatoliki mwenye kujulika Malachi Martin, katika gazeti Providence “Sunday Journal,” Februari 17, 1980.
“Ukosefu wa mapadre na watawa wa kike katika [nchi za] Magharibi unakaribia kuwa hatari katika taifa baada ya jingine.” “Time,” Agosti 21, 1978.
“Ukristo unarudi nyuma kwa haraka sana . . . wonyesho wa ushirikina wa kuamini kwamba hatuwezi kupata habari zo zote juu ya Mungu, mvurugo, ukosefu wa maarifa. . . . Haingekuwa kupita kiasi kusema kwamba karibu watoto wote hawafahamu maana hasa ya Ukristo.”—London “Times,” Septemba 25, 1978, likitoa maelezo juu ya ripoti kutoka kwa Baraza ya Elimu ya Kanisa la Uingereza.
18, 19. Toa ushuhuda zaidi wa kupungua kwa “maji” hayo.
18 Wakati Papa John Paul wa Pili alipozuru Ufaransa katika Mei 1980, gazeti New York Times (Mei 31) lilitoa maelezo hivi: Uvutano wa kanisa unapungua haraka sana katika Ufaransa. Uchunguzi wa hivi karibuni ulifunua kwamba [sehemu ya] 15 kwa mia ya watu ndio walio Wakatoliki wenye kutenda, ijapokuwa 85 kwa mia wanabatizwa kanisani.” Katika Brazil, Askofu Mkuu Luciano Cabral Duarte alisema hivi: “Wakatoliki wetu wanapungukiwa nguvu nao wanaangamia kwa sababu ya ukosefu mkubwa wa nguvu za kiroho.” (Veja, Januari 30, 1980) Huko Nigeria, kiongozi wa kidini wa Kanisa la Presbyteri alikubali hivi: “Leo kanisa linaonekana kuwa limepoteza kitambulisho chake kama mtu aliyepoteza fahamu zake naye anauliza, ‘Mimi ni nani,’ na ‘Nipo hapa kwa sababu gani’?” (Daily Star, Septemba 11, 1978) Huko Ugiriki, gazeti moja lilisema yafuatayo juu ya Kanisa la Orthodoksi la Ugiriki lililoheshimiwa sana hapo kwanza:
‘Leo Kanisa, yaani, viongozi, hasa viongozi wenye vyeo vya juu zaidi, mara nyingi sana linakuwa tundu la kuvunjiana heshima, chanzo cha ujinga na upuzi.
‘Inakuwa hivyo sana hivi kwamba, kwa muda fulani sasa, idadi iliyo kubwa ya Wagiriki inawaona viongozi wengi wa kidini, si kama tengenezo la kiroho lenye kuheshimika, bali kama kundi la wenye kuchochea fitina na wenye kukashifu, wenye kutaka mapinduzi na wenye kutumia wengine kwa faida yao wenyewe, ambao badala ya “kuongoza makundi yao,” wanayachekesha kwa upayukaji na wazimu wao.’—“To Vima,” Oktoba 15, 1978.
19 Kuhusu makao makuu ya Kanisa la Orthodoksi la Mashariki huko Uturuki, gazeti Time hutangaza hivi: “Lile jimbo la askofu la kihistoria lenye maana sana, ambao wakati mmoja lilikuwa makao makuu ya nusu ya ulimwengu wa Kikristo linakufa.” Rabi Mwamerika Alvin Reines anasema hivi kuhusu dini ya Kiyahudi: ‘Dini ya Wayahudi wa Amerika iko katika hali mbaya sana na yenye hatari. Tatizo ni kwamba Wayahudi Waamerika hawakubali mafundisho ya kimapokeo ya dini ya Kiyahudi.’ Huko Uingereza, makanisa mengi sana yamefungwa katika miaka ya karibuni kwa sababu ya upungufu wa hudhurio hivi kwamba mtoaji mmoja wa maelezo katika habari alisema kwamba yamo katika ‘hatari kubwa sana ya kutoweka.’ Huko Ujeremani, uchunguzi ulifunua kwamba ni 17 kwa mia ya Wajeremani walio na umri wa miaka chini ya 35 wanaoamini kuwako kwa Mungu. Katika Japan, wakati watu walipoulizwa, “Je! una dini ya namna fulani?” 60 kwa mia walijibu “Hapana” na wengine 7 kwa mia hawakujibu. Katika nchi baada ya nyingine hali ya dini za ulimwengu huu ni kama vile gazeti The Age la Melbourne, Australia, linavyosema—Kwamba madhehebu yote “yanapatwa na upungufu katika waamini.” Kwa kuwa “upungufu katika waamini,” upungufu wa yale “maji mengi” yanayokaliwa na yule kahaba, unaonekana waziwazi sana ukitokea sasa, je! majeshi yenye kuleta uharibifu yaweza kuwa yakifuata nyuma yakiwa mbali? Hasha.
20. Ni shauri gani la muhimu linalotolewa na Neno la Mungu kwa wale watu wanaopenda haki?
20 Kuungwa mkono kwa huyo “kahaba mkuu” kunakopungua kunalingana na maelezo ya unabii wa Biblia kuhusu hizi “siku za mwisho” unaposema kwamba watu wangekuwa “wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu; wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake.” Kisha unabii uo huo unasema hivi: “Hao nao ujiepushe nao.” (2 Tim. 3:4, 5) Vivyo hivyo, tangazo lenye kuamsha fikira linaloelekezwa kwa watu wanaopenda haki ambao wamo katika “Babeli Mkuu” wa kisasa ni hili: “Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake.”—Ufu. 18:4.
21. Ni tendo gani la mwisho linalofanya ghadhabu ya Yehova kupanda, kukiwa na matokeo gani?
21 Katika wakati ulio karibu sana sasa, huyo “kahaba mkuu” ataharibiwa kama hukumu yake kutoka kwa Mungu. Kama vile ilivyokuwa kwa Babeli wa kale, kuangushwa kwa haraka sana kwa Babeli wa kisasa litakuwa jambo lenye kushtua sana ulimwengu. (Ufu. 18:9-19) Kuharibiwa kwake ndilo tukio litakaloonyesha kwamba “dhiki kubwa” imeanza. Ndipo, pia, wale wenye kumpinga Mungu watakapogeukia watumishi wa Yehova na kujaribu kuwaponda-ponda. (Eze. 38:16) Walakini Yehova asema hivi kwa washikamanifu wake: “Yeye awagusaye ninyi aigusa mboni ya jicho [langu].” (Zek. 2:8) Hilo lamfanya Mungu achukue hatua mara moja. Yehova asema hivi: “Itakuwa katika siku hiyo, . . . ghadhabu yangu itapanda katika mianzi ya pua yangu. Kwa maana katika wivu wangu, na katika moto wa ghadhabu yangu, [nitanena].” (Eze. 38:18, 19) Akiwaokoa watumishi wake washikamanifu, Mungu awapiga mataifa kwa haraka sana tena kwa nguvu nyingi zenye kuponda-ponda katika “vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi,” Har–Magedoni. Hivyo, adui zote za Mungu na watu wake wanaangamizwa kabisa, na kuisafisha dunia na uovu wote.—Ufu. 16:14,16; Mit. 2:22.
22. Walio washikamanifu kwa Yehova watathawabishwaje?
22 Baada ya Har–Magedoni, ile taratibu mpya nzuri sana yaanza! Wale washikamanifu “[wanaotoka] katika dhiki ile iliyo kuu,” wanathawabishwa. “Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao. Naye atafuta kila chozi katika macho yao wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.”—Ufu. 21:3, 4.
23. (a) Ni kwa sababu gani inatupasa tujipe moyo yajapokuwapo magumu ya leo? (b) Twapaswa kuwasihi wale wanaotafuta kweli wafanye nini?
23 Kwa hiyo jipeni moyo, enyi nyote mpendao haki! Jueni kwamba siku zake “yule kahaba mkuu,” na za watawala wa kisiasa wenye kuonea wa taratibu hii ya mambo, zimehesabiwa na kwamba karibuni sana Yehova atawaondolea mbali. Kwa kuwa ‘Mungu hawezi kusema uongo, iweni na uhakika kwamba atawatimizieni tumaini lenu la kuishi milele katika paradiso ya taratibu mpya ambamo kila siku “[mtajifurahisha] kwa wingi wa amani.” (Tito 1:2; Zab. 37:11) Kwa wakati huu, tumieni kwa faida zenu mipango yote ya Yehova mjitie nguvu kiroho kwa ajili ya siku zenye magumu zinazokuja karibuni tu. Mnapofanya hivyo, kwa upendo wafikirieni wengine ambao huenda bado wakawa wanaona “njaa na kiu ya haki. Mwasihi wachukue mioyoni mwao shauri hili la Biblia: “Mtafuteni [Yehova, enyi watu,] maadamu anapatikana, mwiteni, maadamu yu karibu.”-—Mt. 5:6; Isa. 55:6. —Kutoka The Watchtower Oct. 15, 1980.
[Picha katika ukurasa wa 15]
Babeli wa kale uliketi juu ya maji Ya Mto Frati
[Picha katika ukurasa wa 17]
Kupungua kwa maji ya Mto Frati kulitayarishia majeshi ya adui njia yaingie Babeli na kuuangusha
Kupungua kwa maji (watu) ya mfano chini ya Babeli Mkuu kunatangulia kuangamizwa kwake