Maisha na Huduma ya Yesu
Wanafunzi wa Kwanza wa Yesu
BAADA ya kukaa siku 40 jangwani, Yesu anamrudia Yohana aliyembatiza. Anapokaribia, Yohana anapaaza sauti: “Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu! Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Yuaja mtu nyuma yangu, ambaye amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu.” Ingawa Yohana ni mkubwa kwa umri kuliko Yesu binamu yake, Yohana anajua kwamba Yesu alikuwako kabla ya yeye akiwa mtu wa kiroho mbinguni.
Kesho yake Yohana amesimama pamoja na wawili wa wanafunzi wake. Tena, Yesu anapokaribia, yeye anasema: “Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu!” Kusikia hivyo, wanafunzi hao wawili wa Yohana Mbatizi wanamfuata Yesu. Mmoja wao ni Andrea, na inaonekana wazi kwamba yule mwingine ndiye mtu yule yule aliyeandika mambo haya, ambaye pia jina lake lilikuwa Yohana. Yohana huyo, kulingana na dalili, ni binamu ya Yesu pia, kwa kuwa ni mwana wa Salome dada ya Mariamu.
Anapogeuka na kuona Andrea na Yohana wakimfuata, Yesu anauliza: “Mnatafuta nini?”
“Mwalimu, unakaa wapi?” wanamuuliza.
“Njoni, nanyi mtaona,” Yesu anajibu.
Ni karibu saa kumi ya alasiri, nao Andrea na Yohana wanakaa na Yesu muda uliobaki wa siku hiyo. Baadaye Andrea amesisimuka sana hata anafanya haraka kutafuta ndugu yake, anayeitwa Petro. “Tumemwona Masihi,” anamwambia. Halafu anampeleka Petro aliko Yesu. Labda Yohana naye anamtafuta Yakobo ndugu yake wakati ule ule na kumleta aliko Yesu; hata hivyo, Yohana anaondoa habari hizo za kibinafsi katika Injili yake ili asijilinganishe na mwenzake.
Kesho yake, Yesu anamkuta Filipo na kumwalika, akisema: “Nifuate.” Ndipo Filipo anapomkuta Nathanaeli, anayeitwa pia Bartholomayo, asema: “Tumemwona yeye [aliyeandikwa] na Musa katika torati, na manabii, Yesu, mwana wa Yusufu, mtu wa Nazareti.” Nathanieli ana mashaka. “Laweza neno jema kutoka Nazareti?” anauliza.
“Njoo uone,” Filipo amwalika. Wanapomjia Yesu, anamwambia Nathanaeli: “Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwapo chini ya mtini nilikuona.”
Nathanaeli anastaajabu. ‘Mwalimu, wewe ndiwe Mwana wa Mungu, u Mfalme wa Israeli,’ anajibu.
Muda mfupi sana baada ya hapo, Yesu akiwa na wanafunzi wake aliojipatia karibuni anaondoka kwenye bonde la Yordani na kusafiri mpaka Galilaya Yohana 1:29-51.
◆ Wanafunzi wa kwanza wa Yesu walikuwa akina nani?
◆ Petro, na labda Yakobo, walijulishwaje kwa Yesu?
◆ Ni nini kilichosadikisha Nathanaeli kwamba Yesu alikuwa ndiye Mwana wa Mungu?